read

Sura Ya Themanini Na Mbili: Al-Infitar

Imeshuka Makka Ina Aya 19.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu

إِذَا السَّمَاءُ انْفَطَرَتْ {1}

Mbingu itakapopasuka.

وَإِذَا الْكَوَاكِبُ انْتَثَرَتْ {2}

Na nyota zitakapopukutika.

وَإِذَا الْبِحَارُ فُجِّرَتْ {3}

Na bahari zitakapopasuliwa.

وَإِذَا الْقُبُورُ بُعْثِرَتْ {4}

Na Makaburi yatakapofukuli­wa.

عَلِمَتْ نَفْسٌ مَا قَدَّمَتْ وَأَخَّرَتْ {5}

Itajua nafsi ilichokitanguliza na ilichokibakisha nyuma.

يَا أَيُّهَا الْإِنْسَانُ مَا غَرَّكَ بِرَبِّكَ الْكَرِيمِ {6}

Ewe Mtu! Nini kilichokughuri na Mola wako mkarimu?

الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ {7}

Aliyekuumba, akakuweka sawa, akakulinganisha?

فِي أَيِّ صُورَةٍ مَا شَاءَ رَكَّبَكَ {8}

Katika sura yoyote aliyopenda amekutengeneza.

كَلَّا بَلْ تُكَذِّبُونَ بِالدِّينِ {9}

Si hivyo! Bali mnakadhibisha malipo.

وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ {10}

Na hakika bila shaka juu yenu kuna walinzi.

كِرَامًا كَاتِبِينَ {11}

Waandishi wenye heshima.

يَعْلَمُونَ مَا تَفْعَلُونَ {12}

Wanaojua mnayoyafanya.

إِنَّ الْأَبْرَارَ لَفِي نَعِيمٍ {13}

Hakika wema watakua katika nema.

وَإِنَّ الْفُجَّارَ لَفِي جَحِيمٍ {14}

Na hakika waovu watakuwa katika moto.

يَصْلَوْنَهَا يَوْمَ الدِّينِ {15}

Watauingia siku ya malipo.

وَمَا هُمْ عَنْهَا بِغَائِبِينَ {16}

Na hawatakuwa mbali nao.

وَمَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ {17}

Na ni lipi lakukujulisha ni ipi siku ya malipo?

ثُمَّ مَا أَدْرَاكَ مَا يَوْمُ الدِّينِ {18}

Kisha ni lipi la kukujulisha ni ipi siku ya malipo?

يَوْمَ لَا تَمْلِكُ نَفْسٌ لِنَفْسٍ شَيْئًا ۖ وَالْأَمْرُ يَوْمَئِذٍ لِلَّهِ {19}

Ni siku ambayo nafsi haitakuwa na mamlaka juu ya nafsi nyingine; Na amri siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu.

Maana

Sura hii, kwa ukamilifu wake ni sawa na sura iliyotangulia, inaonyesha picha ya baadhi ya matukio ya Kiyama na yatakayofuatia baadae, ya his­abu na malipo.

Mbingu itakapopasuka.

Itapasuka na nyota kuanguka, mfano wake ni:

فَإِذَا انْشَقَّتِ السَّمَاءُ فَكَانَتْ وَرْدَةً كَالدِّهَانِ {37}

“Itakapopasuka mbingu ikawa nyekundu kama mafuta.” Juz. 27 (55:37).

Na nyota zitakapopukutika zitawanyike na kuharibika.

Na bahari zitakapopasuliwa.

Mawimbi yatainuka na kuchanganyika mashariki na magharibi. Au maji yake yatafuka moshi na kujitokeza moto kutoka ndani. Tazama mwanzo mwanzo mwa sura iliyo kabla ya hii.

Na Makaburi yatakapofukuliwa.

Neno “kufukuliwa” tumelifasiri kutokana na neno la kiarabu Bu’thira lenye maana ya kukifumua kitu ndani kuwa nje au nje kuwa ndani. Makusudio yake hapa nikwamba Kiyama kitakua tu, hakuna shaka: “Na hakika Mwenyezi Mungu atawafufua walioma makaburini.” Juz. 17 (22:7).

Itajua nafsi ilichokitanguliza na ilichokibakisha nyuma.

Baada ya ufufuo kila mtu atajua kilichofanywa mikono yake, kiwe cha heri au shari, na ilichokiwacha.

Ewe Mtu! Nini kilichokughuri na Mola wako mkarimu aliyekuumba, akakuweka sawa, akakulinganisha?

Kukuweka sawa nikukupa nguvu za dhahiri na batini zilizokufanya uwe mtu kamili. Kukulinganisha ni kujaalia viungo vyako kuwa na uwiano, hakufanya mkono wako mmoja kuwa mrefu na mwingine kuwa mfupi, wala moja ya macho yako kuwa dogo au baadhi ya viungo vyako kuwa vyeusi na vingine kuwa vyeupe n.k.

Wametofautiana kuhusu neno Mkarimu hapa. Wengine wamesema kuwa Mwenyezi Mungu amejisifu kwa ukarimu ili amfundishe mja wake mwenye dhambi jawabu, atakapoulizwa kesho kuhusu dhambi zake aseme: Umenighuri msamaha wako na ukarimu wako.

Sheikh Muhammad Adul amesema kuwa hii ni kuchezea taawili na ni upotevu kwa kuangalia kitabu cha Mwenyezi Mungu. Usawa ni kufasiri ukarimu hapa kwa maana ya utukufu katika sifa zake zote, na kwamba aliye hivyo hatamwacha mja wake, bure bure bila ya swali wala malipo, bali atamuhisabu na kumpa thawabu mwema na kumwadhibu muovu. Kwa hiyo basi inatakikana kwa mtu kutoghurika na dunia na mapambo yake.

Imam Ali (a.s.) ana maneno marefu kuhusiana na Aya hii aliyoyaunganisha pamoja na khutba. Kwa ufupi wa ujumla wake ni kama ifuatavyo:
Ni lipi lililokupa ujasiri ewe mtu mpaka ukamuasi Mola wako na hali wewe unaishi kwenye himaya yake na unaogelea kwenye neema zake? Je, kumekudanga kukupatia wewe neema zake na huku unamtawalisha mwingine asiyekuwa Yeye? Hivi hujui kuwa hii ni fadhila kwako itokayo kwake, na anakupa muda ili urudi kwenye uongofu wako na uache upote­vu wako?

Kwa hiyo basi makusudio ya ukarimu wake Mwenyezi Mungu ni kumpa muda mja wake mwenye dhambi kwamba aharakishe kutubia na kurejea na asighurike na huku kupewa muda bila ya kuadhibiwa haraka.

Katika sura yoyote aliyopenda amekutengeneza.

Baadhi ya wafasiri wamesema yaani hakukufanya nguruwe au punda. Wengine wakasema: Alikuweka kwenye sura kama alivyotaka uwe mrefu au mfupi, mweusi au mweupe. n.k. Tunavyofahamu kutokana na Aya hii ni kuwa: Fikiria ewe mtu katika mpangilio wa maumbile yako ili utambue ukuu wa Mwenyezi Mungu kati­ka kuumba kwake, na kwamba yule aliyekuumba katika umbile zuri anaweza kukurudisha kwenye uhai mara nyingine.

Si hivyo! Bali mnakadhibisha malipo.

Acheni upotevu wenu usiokuwa na chimbuko lolote zaidi ya kukadhibisha ufufuo. Nyinyi mtahisabiwa tu, yale mliyokuwa mkiyafanya.

Na hakika bila shaka juu yenu kuna walinzi, waandishi wenye heshi­ma, wanaojua mnayoyafanya ya kheri au shari wala hakuna linalofichi­ka kwao. Maana ya wenye hishima ni kuwa wao wana nguvu na ni waaminifu katika kutekeleza wajibu wao kwa njia ya ukamilifu.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 25 (43:80).

Ilivyo ni kuwa lililo wajibu kwetu ni kujua tu, kuwa matendo yetu yanahi­fadhiwa na kudhibitiwa. Ama yanahifadhiwa vipi na kwa kitu gani hayo hatuna majukumu nayo.

Hakika wema watakua katika nema na hakika waovu watakuwa kati­ka moto, watauingia siku ya malipo.

Wema ni wale wakweli na wakatenda mema. Malipo yao mbele ya Mola wao ni maghufira na ujira mwema. Waovu ni wale wanaoneza ufisadi katka ardhi na malipo yao ni kuingia motoni.

Na hawatakuwa mbali nao hata kidogo, ni adhabu tu ya kudumu .

Na ni lipi la kukujulisha ni ipi siku ya malipo?

Wewe hujui uhakika wa siku ya malipo. Iko zaidi ya unavyofikira kwa shida na vituko vyake.

Kisha ni lipi la kukujulisha ni ipi siku ya malipo?

Huu ni msisitizo na kuipa uzito siku hiyo.

Ni siku ambayo nafsi haitakuwa na mamlaka juu ya nafsi nyingine.

Hakuna yeyote atakayekuwa na mamlaka ya manufaa wala madhara siku hiyo kwa ajli ya nafsi yake wala ya mwingine.

Na amri siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu.

Yeye ndiye pekee atakayeamuru na kukataza, hakuna mshauri wala mtetezi, bali hakuna muombezi isipokuwa atakayeruhusiwa na Mwenyezi Mungu na akasema kweli.