read

Sura Ya Themanini Na Mmoja: At-Takwir

Imeshuka Makka Ina Aya 29.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

إِذَا الشَّمْسُ كُوِّرَتْ {1}

Jua litakapokunjwa kunjwa.

وَإِذَا النُّجُومُ انْكَدَرَتْ {2}

Na nyota zitakapoanguka.

وَإِذَا الْجِبَالُ سُيِّرَتْ {3}

Na milima itakapoondolewa.

وَإِذَا الْعِشَارُ عُطِّلَتْ {4}

Na ngamia wenye mimba watakapotupiliwa mbali.

وَإِذَا الْوُحُوشُ حُشِرَتْ {5}

Na wanyama pori watakapokusanywa.

وَإِذَا الْبِحَارُ سُجِّرَتْ {6}

Na bahari zitakapofurika.

وَإِذَا النُّفُوسُ زُوِّجَتْ {7}

Na nafsi zitakapounganishwa.

وَإِذَا الْمَوْءُودَةُ سُئِلَتْ {8}

Na msichana aliyezikwa hai atakapoulizwa.

بِأَيِّ ذَنْبٍ قُتِلَتْ {9}

Ni kwa dhambi gani aliuawa?

وَإِذَا الصُّحُفُ نُشِرَتْ {10}

Na madaftari yatakapoenezwa.

وَإِذَا السَّمَاءُ كُشِطَتْ {11}

Na mbingu itakapotanduliwa.

وَإِذَا الْجَحِيمُ سُعِّرَتْ {12}

Na moto utakapokokwa.

وَإِذَا الْجَنَّةُ أُزْلِفَتْ {13}

Na Pepo itakaposogezwa.

عَلِمَتْ نَفْسٌ مَا أَحْضَرَتْ {14}

Itajua kila nafsi ilichokihud­hurisha.

Aya 1 – 14 : Jua Litakapokunjwa Kunjwa

Maana

Katika Aya hizi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameashiria yatakayotokea Siku ya Kiyama hadi saa ya hisabu; kama ifutavyo:-
Jua litakapokunjwa kunjwa.

Neno kukunjwa tumelifasiri kutokana na neno takwir lenye maana ya kukunja kwa kuviringa, kama kichwa kukiviringa kilemba. Sababu ya kukunjwa kunjwa jua ni uharibifu utakaolipata.

Na nyota zitakapoanguka.

Neno lililotumika ni Inkadar, lenye maana ya kuanguka kichwa chini miguu juu. Makusudio yake hapa ni kuanguka nyota na kutawanyika. Mahali pengine Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

وَإِذَا الْكَوَاكِبُ انْتَثَرَتْ {2}

“Na nyota zitakapopukutika.’’ (82:2).

Na milima itakapoondolewa kutoka sehemu zake na kuwa hewani.

Na ngamia wenye mimba watakapotupiliwa mbali.

Hawa ni mali ya thamani kubwa sana kwa waarabu. Hiki ni kinaya cha shida na vituko vya siku hiyo ambapo mtu atasahau kila kitu.

Na wanyama pori watakapokusanywa.

Watakurupuka kwa hofu. Mwenye Majmaul-Bayan na Razi wanasema kuwa Mwenyezi Mungu atawakusanya wanyama ili walipane visasi. Lakini inavyoeleweka ni kuwa Mwenyezi Mungu hahisabu mpaka akali­fishe, wala hakalifishi mpaka atoe akili. Kwayo hutoa thawabu na kwayo hutoa adhabu. Lau wanyama wangelikuwa na akili wangelijikinga na wanadamu na wangelikuwa sawa nao.

Na bahari zitakapofurika.

Neno kufurika tumelifasiri kutokana na neno sujjira ambalo miongoni mwa maana zake ni kujaa kupita kiasi. Kwa hiyo maana yake ni kuwa maji ya bahari yatafurika huku na huko bila ya kuwa na kizuizi chochote, ikiwa ni natija ya kuharibika ulimwengu mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu: Na bahari zitakapopasuliwa. (82:3).

Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Inawezekana kuwa maana ni kuwa­ka moto, kwa sababu moto ulioko ndani ya ardhi huwa unajitokeza inapopasuka, hapo maji ya bahari yatageuka moshi na kuisha na hakutabakia kitu baharini isipokuwa moto. Imepokewa hadith kuwa bahari ni kifuniko cha Jahannam. Utafiti wa ilimu umethibitisha hilo na kushuhudiwa na volkano na matetemeko ya ardhi.”

Na nafsi zitakapounganishwa na viwiliwili; yaani kila nafsi itarudi kwenye mwili wake wa kwanza ilioachana nao. Na msichana aliyezikwa hai atakapoulizwa, ni kwa dhambi gani ali­uawa? Ili liwe ni tukio gumu kwa yule aliyemzika akiwa hai. Tazama Juz.14 (16:59).

Na madaftari yatakapoenezwa.

Kesho kila mtu atapewa kitabu cha matendo yake yawe ya heri au ya shari. Inawezekana haya kuwa ni kinaya cha kuwa Siku ya Kiyama matendo ya waja yatawadhihirikia kwa ukamilifu, kama yalivyokuwa. Vyovyote iwavyo si wajibu kutafiti uhakika wa madaftari hayo.

Na mbingu itakapotanduliwa; yaani zitaondolewa nyota zilizokuwa zimefunika yaliyo nyuma yake; kama inavyoondolewa ngozi ya mnyama aliyechinjwa na kuonekana nyama iliyokuwa imeifunika.

Na moto utakapokokwa uwake.

Na Pepo itakaposogezwa.
Itasogezewa watu wake na wao wataisogelea, kwa sababu imeandaliwa wao na wao wamejiaanda nayo. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na Pepo italetwa karibu kwa wenye takua, haitakuwa mbali.” Juz. 26 (50:31)

Itajua kila nafsi ilichokihudhurisha.

Hili ndilo jawabu la mambo yote hayo 12 yaliyopita (jawabushart). Maana ni kuwa yatakapotokea hayo yaliyotajwa, kila mtu ataletwa kwa Mola wake akiwa anajua amechukua matendo gani na amejibebea akiba gani, ya heri au ya shari. Imeelezwa katika Nahjul-balagha imesemwa: “Hakika msafiri anayekwenda ‧ kwa Mola wake ‧ kwa kufaulu au kutofaulu anas­tahiki maandalizi bora. Basi jiandalieni masurufu i mkiwa duniani ambayo mtajihifadhi nafsi zenu kwayo.”

فَلَا أُقْسِمُ بِالْخُنَّسِ {15}

Naapa kwa zinazorejea nyuma,

الْجَوَارِ الْكُنَّسِ {16}

Zinazokwenda kwa kujificha.

وَاللَّيْلِ إِذَا عَسْعَسَ {17}

Na kwa usiku unapopungua.

وَالصُّبْحِ إِذَا تَنَفَّسَ {18}

Na asubuhi inapopumua.

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ {19}

Hakika hiyo bila shaka ni kauli ya mjumbe mtukufu.

ذِي قُوَّةٍ عِنْدَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ {20}

Mwenye nguvu, mwenye cheo mbele ya mwenye Arshi.

مُطَاعٍ ثَمَّ أَمِينٍ {21}

Mwenye kutiiwa huko mwaminifu.

وَمَا صَاحِبُكُمْ بِمَجْنُونٍ {22}

Na mwenzenu si mwendawaz­imu.

وَلَقَدْ رَآهُ بِالْأُفُقِ الْمُبِينِ {23}

Hakika alimuona katika upeo ulio wazi.

وَمَا هُوَ عَلَى الْغَيْبِ بِضَنِينٍ {24}

Wala yeye si bakhili kwa mambo ya ghaibu.

وَمَا هُوَ بِقَوْلِ شَيْطَانٍ رَجِيمٍ {25}

Na wala si kauli ya shetani aliyekufukuzwa.

فَأَيْنَ تَذْهَبُونَ {26}

Basi mnakwenda wapi?

إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِلْعَالَمِينَ {27}

Haikuwa hiyo ila ni ukum­busho kwa walimwengu wote.

لِمَنْ شَاءَ مِنْكُمْ أَنْ يَسْتَقِيمَ {28}

Kwa anayetaka katika nyinyi kuwa sawa.

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَنْ يَشَاءَ اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ {29}

Na hamtataka isipokuwa atake Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu.

Aya 15 – 29: Kwenda Nyuma Na Kujificha

Maana

Naapa

Tumetangulia kusema huko nyuma kwamba herufi la hii kwa mujibu wa wafasiri wengi ni ziada ya kiirabu, na kwa wengine ni ya kukanusha, kwa misingi ya kuwa jambo liko wazi halihitajii kiapo.

Natija ya kauli zote mbili ni moja tu. Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Ibara hii inaletwa ikiwa inakusudiwa kuadhimishwa kinachoapiwa, na hakika hakiadhimish­wi kwa kuapiwa kwa sababu chenyewe ni adhimu.”

Kwa zinazorejea nyuma, zinazokwenda kwa kujificha

Makusudio yake hapa ni nyota zote. Imesemekana kuwa ni nyota tano tu: Zebaki, Zuhura, Mars Mushtara na Zohali. Nazo zinakwenda kwa sababu zinazunguka kwenye falaki yake.

Wametofautiana kuwa kwa nini zimepewa sifa ya kurudi nyuma na kuji­ficha?

Sheikh Muhammad Abduh anasema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amezisifu kwa kujificha kwa sababu hazionekani kwenye mwanga wa jua, kama anavyojificha paa kwenye nyumba yake na amezisifu kwa kurejea, kwa vile zinarudi kuonekana baada ya kupotea jua.

Hii inaafikiana na natija ya tafsir ya Tabrasi katika ajmaul-bayan ali­posema, ninamnukuu: “Ni nyota zinazorudi kujificha mchana na kuji­tokeza usiku.

Tofauti baina ya tafsiri mbili nikuwa kwa Mwenye Majmau kurudi ni kuji­ficha na kwa Muhammad Abduh ni kujitokeza, lakini natija ni moja.

Hali yoyote iwayo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameapa kwa nyota kutanabahisha utengenezaji wake kwenye dalili ya uweza wa mtengeneza­ji na hikima yake.

Na kwa usiku unapopungua na asubuhi inapopumua.

Neno kupungua tumelifasiri kutokana na neno A’s-a’s lenye maana ya kuondoka na kurudi. Hiki ni kiapo cha pili, kutoka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuondoka usiku na kuja mchana, kwa sababu ameunganisha kwenye kiapo. Katika kitabu uhawalatu fahmil Asril lil ur’an anasema: “Unasoma Qur’an nayo inaacha mdundo, athari na picha kwenye masikio. Wakati Mwenyezi Mungu anapoapa kwa usiku na mchana anatumia neno A’s-a’s. Hizi herufi nne ndio usiku, kwa kuleta sura ya kila yaliyomo ndani yake. Na asubuhi inapopumua. Hakika mwanga wa alfajiri hapa unaonekana na kusikikika. Hakika wewe unakurubia kusikia sauti mwanana ya ndege na kuwika jogoo.”

Hakika hiyo bila shaka ni kauli ya mjumbe mtukufu mwenye nguvu, mwenye cheo mbele ya mwenye Arshi.

Hiyo ni Qur’an, imefahamika hivyo kutokana na mfumo wa maneno. Mjumbe ni Jibril, Mwenyezi Mungu ameitegemeza Qur’an kwa Jibril kwa vile yeye ndiye anayeichukua na kuinukuu kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.). Mwenye Arshi ni Mwenyezi Mungu. Jibril ana cheo na heshima mbele ya Mwenyezi Mungu, ni mwaminifu wa uteremsho, ana nguvu kulitekeleza hilo na mengineyo katika kazi anazoziwakilisha. Umetangulia mfano wake katika Juz. 27 (53:5-6).

Mwenye kutiiwa huko mwaminifu.

Huko ni ishara ya mahali anakotiiwa Jibril nako ni ulimwengu wa ghaibu ambao haujui hakika yake isipokuwa Mwenyezi Mungu.

Na huyu mwenzenu si mwendawazimu.

Maneno yanaelekezwa kwa vigogo wa kikuraishi, mwenzao ni Muhammad (s.a.w.) ambaye baadhi yao walimbandika uwazimu: “Na walisema:

يَا أَيُّهَا الَّذِي نُزِّلَ عَلَيْهِ الذِّكْرُ إِنَّكَ لَمَجْنُونٌ {6}

“Ewe uliyeteremshiwa ukumbusho! Wewe ni mwendawazimu.” Juz. 14 (15:6).

Mwenyezi Mungu hapa anamwondelea wanayomzulia. Umetangulia mfano wake katika Juz. 29 (68:2).

Hakika alimuona katika upeo ulio wazi.

Mnamwambia Muhammad ni mwendawazimu wakati anawapa habari ya Pepo na Moto? Hapana! Hakika Qur’an ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, alioletewa na Jibril alipomuona kwenye upeo ulio wazi akiwa kwenye sura yake na uhakika wake alivyo, alimuona kiukweli usiokuwa na shaka. Umetangulia mfano wake katika Juz. 27 (53:5-12).

Wala yeye si bakhili kwa mambo ya ghaibu.

Yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) na ghaibu ni Qur’an. Maana ni kuwa Muhammad hakuwa ni mwenye kuificha Qur’an na kunyamazia kuitangaza haki, kwa kuwahofia nyinyi washirikina kumwambia kuwa ni mwendawazimu; bali anaitangaza waziwazi bila ya kuhofia lawama.

Na wala si kauli ya shetani aliyekufukuzwa.

Hii ni kuyarudi madai yao kuwa anayoyasema Mtume yamepuziwa na shetani kwenye ulimi wake. Shetani kweli anaweza kufahamisha uongofu na heri au haki na uadilifu?

Basi mnakwenda wapi kwenye hukumu yenu na upotevu?

Haikuwa hiyo ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote.

Qur’an ni yenye kuamarisha heri na kuikemea shari. Zaidi ya hayo yote ndani yake mna ubainifu wa kila kitu, vipi itakuwa ni kauli ya shetani?

Kwa anayetaka katika nyinyi kuwa sawa.

Qur’an ni uongozi na wema kwa yule mwenye kupendelea uongofu na usawa. Ama mwenye kung’ang’ania upotevu hatanufaika na ukumbusho wala kuathirika na mawaidha.

Na hamtataka isipokuwa atake Mwenyezi Mungu Mola wa wal­imwengu.

Razi anasema Aya hii inafahamisha kuwa mtu ni mwenye kuendeshwa hana hiyari. Lakini anajibiwa kuwa maana ya Aya ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamtakia mja wake kufuata haki na uadilifu, lakini mpin­zani anakataa isipokuwa upotevu tu, wala hawi sawa, ila akilazimishwa na Mwenyezi Mungu na hilo linapingana na uadilifu wa Mwenyezi Mungu na hikima yake.

Kwa maneno mengine ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemuumba mtu akiwa na hiyari, mwenye akili na utashi, na akamtofautisha na mnya­ma kwa hilo. Kutokana na hilo ndio akamkalifisha utiiifu kinyume cha mwenginewe. Lau angelitaka Mwenyezi Mungu angelimnyang’anya mtu utashi wa akili na kumfanya kama mnyama au chini ya mnyama.