read

Sura Ya Themanini Na Nane: Al-Ghashiya

Imeshuka Makka Ina Aya 26.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ الْغَاشِيَةِ {1}

Je, imekujia habari ya msiba unaofunikiza?

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ خَاشِعَةٌ {2}

Nyuso siku hiyo zitadhalilika.

عَامِلَةٌ نَاصِبَةٌ {3}

Zitatumika na kutabika.

تَصْلَىٰ نَارًا حَامِيَةً {4}

Zitaingia katika moto mkali.

تُسْقَىٰ مِنْ عَيْنٍ آنِيَةٍ {5}

Zitanyweshwa katika chem­chem inayochemka.

لَيْسَ لَهُمْ طَعَامٌ إِلَّا مِنْ ضَرِيعٍ {6}

Hawatakuwa na chakula isipokuwa cha miba.

لَا يُسْمِنُ وَلَا يُغْنِي مِنْ جُوعٍ {7}

Hakinenepeshi wala hakiondoi njaa.

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَاعِمَةٌ {8}

Nyuso siku hiyo zitaneemeka.

لِسَعْيِهَا رَاضِيَةٌ {9}

Zitakuwa radhi kwa mahangaiko yake.

فِي جَنَّةٍ عَالِيَةٍ {10}

Katika Bustani ya juu.

لَا تَسْمَعُ فِيهَا لَاغِيَةً {11}

Hazitasikia humo upuzi.

فِيهَا عَيْنٌ جَارِيَةٌ {12}

Humo mna chemchem inay­otiririka.

فِيهَا سُرُرٌ مَرْفُوعَةٌ {13}

Mna viti vilivyoinuliwa.

وَأَكْوَابٌ مَوْضُوعَةٌ {14}

Na bilauri zilizowekwa.

وَنَمَارِقُ مَصْفُوفَةٌ {15}

Na mito iliyopangwa.

وَزَرَابِيُّ مَبْثُوثَةٌ {16}

Na mazulia yaliyopangwa huku na huko.

أَفَلَا يَنْظُرُونَ إِلَى الْإِبِلِ كَيْفَ خُلِقَتْ {17}

Je, hawamtazami ngamia jinsi alivyoumbwa?

وَإِلَى السَّمَاءِ كَيْفَ رُفِعَتْ {18}

Na mbingu jinsi zilivyoinuli­wa?

وَإِلَى الْجِبَالِ كَيْفَ نُصِبَتْ {19}

Na milima jinsi ilivyosi­mamishwa?

وَإِلَى الْأَرْضِ كَيْفَ سُطِحَتْ {20}

Na ardhi jinsi ilivyotan­dazwa?

فَذَكِّرْ إِنَّمَا أَنْتَ مُذَكِّرٌ {21}

Basi kumbusha hakika wewe ni mkumbashaji tu.

لَسْتَ عَلَيْهِمْ بِمُصَيْطِرٍ {22}

Wewe si mwenye kuwatawalia.

إِلَّا مَنْ تَوَلَّىٰ وَكَفَرَ {23}

Lakini anayerudi nyuma na akakufuru.

فَيُعَذِّبُهُ اللَّهُ الْعَذَابَ الْأَكْبَرَ {24}

Basi Mwenyezi Mungu atamwadhibu adhabu iliyo kubwa sana!

إِنَّ إِلَيْنَا إِيَابَهُمْ {25}

Hakika ni kwetu marejeo yao.

ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا حِسَابَهُمْ {26}

Kisha hakika ni juu yetu his­abu yao.

Maana

Je, imekujia habari ya msiba unaofunikiza.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume (s.a.w), lakini sababu inawaenea wote. Msiba unaofunikiza ni Kiyama. Kimeitwa hivyo kwa sababu kinafunikiza watu kutokana na shida yake na vituko. Vyovyote iwavyo, maana yake ni: Je, unajua kitu kuhusu Kiyama? Watu watakuwa makundi mawili.

Kundi la kwanza ni wale ambao nyuso siku hiyo zitadhalilika.

Athari ya udhalili, hizaya na utwevu itajitokeza kwenye hizo nyuso.

Zitatumika na kutabika.

Maana ni kuwa watu wa nyuso hizi walifanya kazi sana duniani, lakini walifanya kwa ajii ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo hakuna walichopata kutokana na kazi yao hiyo isipokuwa tabu na kuchoka duni­ani, na Akhera ni hasara na adhabu.

Katika Nahjul-balagha anasema: “Mwenye hasara zaidi ya kupunjika na aliyehangaika bure zaidi ni yule aliyeutumia mwili wake kwa juhudi kati­ka kutafuta mali, lakini majaaliwa hayakumsaidia kwenye matakwa yake, akatoka duniani akiwa na masikitiko na akafika Akhera na majukumu yake.”

Zitaingia katika moto mkali; yaani zitachomwa kwenye moto unaowaka.

Zitanyweshwa katika chemchem inayochemka.

Neno la kiarabu lililotumika kuelezea kuchemka, lina maana ya kufikia nyuzi joto za mwisho. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

يَطُوفُونَ بَيْنَهَا وَبَيْنَ حَمِيمٍ آنٍ {44}

“Watakuwa wakizunguka baina ya hiyo na maji ya moto yanayochemka.” Juz. 27 (55:44).

Hawatakuwa na chakula isipokuwa cha miba.

Mweny Kamusi ya Almuhit anasema: neno dharii (tulilolifasiri kwa maana ya miba) ni mmea usiokurubiwa na mnyama kwa ubaya wake.

Vyovyote iwavyo maana ni kuwa ni chakula kibaya. Ni tosha kuwa ni chakula cha watu wa Motoni.

Hakinenepeshi wala hakiondoi njaa;

Yaani hakiondoi dhara wala hakileti manufaa.

Kundi la pili ni: nyuso nyingine siku hiyo zitaneemeka, zenye uangavu na uzuri.

Zitakuwa radhi kwa mahangaiko yake.

Zitaridhia ujira wake Akhera, kutokana na kazi yake duniani.

Katika Bustani ya juu, iliyo tukufu kwa sifa zake zote; mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Basi yeye atakuwa katika maisha ya kuridhia, katika Bustani ya juu.” Juz. 29 (69:21-22).

Hazitasikia humo upuzi, wala maneno yasiyokuwa na maana. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

لَا يَسْمَعُونَ فِيهَا لَغْوًا وَلَا تَأْثِيمًا {25}

“Humo hawatasikia upuzi wala maneno ya dhambi.” Juz. 27 (56-25).

Humo mna chemchem inayotiririka, bustani zipitiwazo na mito chini yake. Mna viti vilivyoinuliwa kuepukana na ardhi.

Na bilauri zilizowekwa pambizoni mwa chemchem, wanazitumia wakita­ka kunywa maji.

Na mito iliyopangwa, ya kuegemea. Na mazulia yaliyopangwa huku na huko.

Kila yaliyoelezwa hapa katika wasifu wa Pepo ni baadhai ya makumi ya Aya zilizopita. Na kila yaliyosmewa au yatakayosemwa katika wasifu wake ni tafsiri na ubainifu wa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنْفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ ۖ {71}

“Vitakuwamo ambavyo nafsi zinavipenda, na macho yanavifurahia.” Juz. 25 (43:71).

Je, hawamtazami ngamia jinsi alivyoumbwa?

Unaweza kuuliza: Kwanini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemuhusu kumta­ja ngamia badala ya wanyama wengine?

Sheikh Muhammad Abduh amejibu kuwa ni mnyama bora na mwenye manufaa zaidi kwa waarabu. Pia ni kiumbe wa ajabu. Kwani pamoja na nguvu zake, lakini anamtii aliye dhaifu; na umbo lake limeandaliwa kube­ba vitu vizito. Huwa anapiga magoti ili abebe, kisha anatembea pole pole na mzigo wake akivumilia kiu, njaa na mengineyo ambayo hayafanani na wanyama wengineo.

Na mbingu jinsi ilivyoinuliwa juu ya ardhi pamoja na nyota zake zenye kumeremeta.

Na milima jinsi ilivyosimamishwa, kuwa vigingi vya ardhi na ikaituliza isitingishike. Lau si milma ardhi ingeliyumba pamoja na watu wake.

Na ardhi jinsi ilivyotandazwa.

Mwenyezi Mungu ameifanya ni tandiko kwa viumbe wake walale humo na watembee. Ilivyo ni kuwa kutandazwa ardhi ni kwa inavyoonekana kwa macho, sio uhalisia wake. Mwenyezi Mungu ameashiria mduara wa ardhi aliposema: “Ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Huuzongazonga usiku kwenye mchana, na Huuzongazonga mchana kwenye usiku.” Juz. 23 (39:5).
Sheikh Muhammad Abduh anasema: Imekuwa vizuri kutajwa ngamia pamoja na mbingu, milima na ardhi, kwa sababu viumbe hivi ndivyo wanavyoviona waarabu katika mabonde yao.

Basi kumbusha hakika wewe ni mkumbashaji tu.

Huu ni ufasaha na uwazi zaidi wa kutaja shughuli ya Mtume - kukum­busha:

 وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ {54}

“Na hapana juu ya mtume ila kufikisha (ujumbe) wazi wazi.” Juz. 18 (24:54).

Wewe si mwenye kuwatawalia, lakini anayerudi nyuma na akakufuru, basi Mwenyezi Mungu atamwadhibu adhabu iliyo kubwa sana. Hakika ni kwetu marejeo yao, kisha hakika ni juu yetu hisabu yao.

Wewe Muhammad si mtawala kwao mpaka uwalazimishe imani, lakini hii haimaanishi kuwa wanaokukadhibisha watachwa burubure. Hapana! wao watarejea kwetu na amali zao na makusudio yao yaliyowekwa rahani, wala hawana malipo isipokuwa adhabu ya fedheha.