read

Sura Ya Themanini Na Nne: Al-Inshiqaq

Imeshuka Makka Ina Aya 25.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

إِذَا السَّمَاءُ انْشَقَّتْ {1}

Mbingu itakapochanika.

وَأَذِنَتْ لِرَبِّهَا وَحُقَّتْ {2}

Na ikamsikiliza Mola wake na ikafanya ndivyo.

وَإِذَا الْأَرْضُ مُدَّتْ {3}

Na ardhi itakaponyooshwa.

وَأَلْقَتْ مَا فِيهَا وَتَخَلَّتْ {4}

Na ikatupa vilivyo ndani kuwa tupu.

وَأَذِنَتْ لِرَبِّهَا وَحُقَّتْ {5}

Na ikamsikiliza Mola wake na ikifanya ndivyo.

يَا أَيُّهَا الْإِنْسَانُ إِنَّكَ كَادِحٌ إِلَىٰ رَبِّكَ كَدْحًا فَمُلَاقِيهِ {6}

Ewe Mtu! Hakika wewe ni mwenye kufanya bidii kwa Mola wako, basi utamkuta.

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ {7}

Ama atakayepewa daftari lake kwa mkono wake wa kulia.

فَسَوْفَ يُحَاسَبُ حِسَابًا يَسِيرًا {8}

Basi atahisabiwa hisabu nyepesi.

وَيَنْقَلِبُ إِلَىٰ أَهْلِهِ مَسْرُورًا {9}

Na atarudi kwa watu wake mwenye furaha.

وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ وَرَاءَ ظَهْرِهِ {10}

Na ama atakayepewa daftari lake nyuma ya mgongo wake.

فَسَوْفَ يَدْعُو ثُبُورًا {11}

Ataomba maangamizo.

وَيَصْلَىٰ سَعِيرًا {12}

Na atauingia moto.

إِنَّهُ كَانَ فِي أَهْلِهِ مَسْرُورًا {13}

Hakika alikuwa kati ya watu wake ni mwenye furaha.

إِنَّهُ ظَنَّ أَنْ لَنْ يَحُورَ {14}

Hakika yeye alidhani hatare­jea.

بَلَىٰ إِنَّ رَبَّهُ كَانَ بِهِ بَصِيرًا {15}

Kwani? Hakika Mola wake alikuwa akimuona

Aya 1-15: Mbingu Itakapochanika

Maana

Sura hii ni kama sura mbili zilizotangulia (Takwir na Infitar), inabainisha vituko vya siku ya Kiyama na kugawanyika watu, siku ya malipo, kwenye makundi mawili: kundi la peponi na la motoni.

Mbingu itakapochanika.

Mbingu itachanika na kupasuka wakati Mwenyezi Mungu atakapotaka kuuharibu ulimwengu tulio nao.

Na ikamsikiliza Mola wake.

Yaani mbingu itaitikia amri ya Mwenyezi Mungu. Kwa maneno mengine ni kuwa Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila kitu.

Na ikafanya ndivyo, yaani ikafanya inavyotakiwa kufanywa kufuata amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa vile imeumbwa naye na iko mikononi mwake.

Na ardhi itakaponyooshwa.

Kitakaposimama Kiyama ardhi itakosa mshikamano wake na majabali yatang’oka na mengineyo , hapo ardhi itakuwa laini.
Na ikatupa vilivyo ndani, yaani vilivyo ndani ya ardhi wakiwemo wafu na vinginevyo, na kuwa tupu, haina chochote kilichokuwamo.

Na ikamsikiliza Mola wake na ikifanya ndivyo, sawa na ilivyofanya ardhi.

Ewe Mtu! Hakika wewe ni mwenye kufanya bidii kwa Mola wako, basi utamkuta.

Makusudio ya bidii hapa ni mtu anavyojifanyia yeye mwenyewe katika heri au shari. Maana ni kuwa mtu hatakaa milele duniani naye anafanya juhudi kwenda kwa Mola wake na atakutana naye akiwa na matendo yake tu na hakuna kitakachomkutanisha na Mola wake isipokuwa mauti. Maadamu umri unapita na mauti yanakuja, basi mkutano huo uko karibu sana. Kwa hiyo angalie mtu ameandaa nini atakapokutana na Mwenyezi Mungu na hisabu yake?

Ama atakayepewa daftari lake kwa mkono wake wa kulia, basi atahis­abiwa hisabu nyepesi, na atarudi kwa watu wake mwenye furaha.

Kila mwenye kuamini na akatenda mema kesho atapewa maandishi yake kwa mkono wake wa kulia. Makusudioo ya watu wake hapa ni waumini walio wema kama yeye watakapokutana Peponi wakiwa na furaha. Hisabu nyepesi ni ile isiyokuwa na mashaka. Kuna hadithi isemayo: “Mwenye kuihisabu nafsi yake duniani, itakuwa nyepesi kwake hisabu ya akhera.”

Na ama atakayepewa daftari lake nyuma ya mgongo wake, ataomba maangamizo na atauingia moto.

Makusudio ya atakayepewa maandishi yake kwa nyuma ya mgongo wake ni mkosefu mwenye dhambi , angalia katika Juzuu . 18 (25:14).

Unaweza kuuliza! Hapa Mwenye Mungu (s.w.t.) anasema kuwa mkosefu atapewa daftari lake kwa nyuma ya mgongo wake na katika Juzuu 29 (69:25) anasema atapewa kwa mkono wake wa kushoto, sasa kuna wajihi gani wa kuonanisha Aya mbili hizi?

Wafasiri wengi wamejibu kuwa mkono wa kulia wa mwenye hatia uta­fungwa shingoni mwake Siku ya Kiyama na wa kushoto utakua nyuma ya mgongo wake na ndio atapokea nao daftari lake.

Sheikh Muhammad Abduh anasema kuwa kupewa daftari kwa mkono wa kulia, kushoto au nyuma ya mgongo ni kufananisha na kuleta picha ya mtu atakavyo yaona matendo yake siku hiyo. Kuna watu watakapoyaona matendo yao watashangilia na kufurahi. Huku ndiko kupokea kwa mkono wa kulia. Kuna wengine watakapofichuliwa matendo yao watakunja uso na kutamani lau wasingefichuliwa.

Huku ndiko kupokea kwa kushoto au nyuma ya mgongo. Kwa hiyo hakuna haja ya kuoanisha Aya mbili hizi kwa kuzua maana yasiyofanana na kitabu cha Mwenyezi Mungu, kama walivy­ ofanya wafasiri wengi.

Hakika alikuwa kati ya watu wake ni mwenye furaha.

Duniani alipokuwa na watu wake alikuwa akicheza wala hafikiri hisabu na malipo.

Hakika yeye alidhani hatarejea.

Yaani hatarejea kwa Mola wake baada ya mauti, wala hakuna yoyote atakayemsaili na dhambi zake. Kwani? Yeye atarejea tu na kuulizwa hilo halina shaka.

Hakika Mola wake alikuwa akimuona.

Hakikufichika kwake chochote katika kauli zake na vitendo vyake, atahis­abiwa ndivyo, ikiwa ni heri basi ni heri na ikiwa ni shari basi ni shari.

فَلَا أُقْسِمُ بِالشَّفَقِ {16}

Naapa kwa wekundu wa machweo.

وَاللَّيْلِ وَمَا وَسَقَ {17}

Na kwa usiku na unavyoviku­sanya.

وَالْقَمَرِ إِذَا اتَّسَقَ {18}

Na kwa mwezi unapotimia.

لَتَرْكَبُنَّ طَبَقًا عَنْ طَبَقٍ {19}

Bila shaka mtapanda tabaka kwa tabaka!

فَمَا لَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ {20}

Basi wana nini hao hawaami­ni?

وَإِذَا قُرِئَ عَلَيْهِمُ الْقُرْآنُ لَا يَسْجُدُونَ ۩ {21}

Na wanaposomewa Qur’an hawasujudu?

بَلِ الَّذِينَ كَفَرُوا يُكَذِّبُونَ {22}

Bali waliokufuru wanakad­hibisha tu.

وَاللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا يُوعُونَ {23}

Na Mwenyezi Mungu anaya­jua zaidi wanayoyakusanya.

فَبَشِّرْهُمْ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ {24}

Basi wabashirie adhabu chungu!

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ أَجْرٌ غَيْرُ مَمْنُونٍ {25}

Isipokuwa wale walioamni na wakatenda mema, wana ujira usiokatika.

Aya 16-25:Naapa Kwa Wekundu Wa Machweo

Maana

Naapa kwa wekundu wa machweo.

Yametangulia maelezo mara kadhaa kuhusu la Uqsimu. Tazama Juz. 27 (56:75) na Juzu hii tuliyo nayo (81: 15). Wekundu wa machweo ni ule wekundu unaobakia pambizoni mwa mbingu kutokana athari ya kuchwa jua. Pengine lengo la kuapa huku ni kutanabahisha kwenye wakati huu, kwa sababu ni kipindi cha kugura kutoka mchana na taabu zake hadi usiku na raha yake.

Na kwa usiku na unavyovikusanya.

Yaani unavikusanya vilivyotawanyika mchana na kuviweka pamoja ­wanafamlia wanajumuika usiku baada ya kutawanyika mchana. Vile vile majirani na marafiki wanakusanyika usiku kwa mazungumzo.

Sheikh Muhammad Abduh anasema kuwa si siri kwamba yaliyotawanyika mchana yanakusanyika usiku, hata mikono yako miwili unayoinyoosha kwa kazi mchana, unaikusanya pamoja kwenye ubavu wako usiku. Usiku unawakusanya majike na watoto wao na kuwarudisha waliokwenda machungani kwenye mazizi yao.

Na kwa mwezi unapotimia.

Unakamilika na kutimia nuru yake usiku wa 13,14 na 15. Nyusiku hizi zinaitwa nyusiku nyeupe.

Bila shaka mtapanda tabaka kwa tabaka.

Hili ndilo jawabu la kiapo. Maana ni kuwa mtu hana budi kupitia ngazi nyingi, kuanzia tone la manii hadi kilenge na kuanzia utoto hadi ujana, kisha uzee hadi ukongwe na umri dhalili kabisa.

Vile vile anapambana na hali tofauti katika maisha yake kuanzia afya hadi maradhi, utajiri na ufukara na huzuni na furaha. Vile vile maendelo na kurudi nyuma.

Hivi ndivyo inavyofanya dunia kwa watu wake, kutoka hali moja hadi nyingine, mpaka waje wasimamae wote mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hisabu na malipo.

Basi wana nini hao hawaamini, pamoja na kuwa sababu za kuamini haz­ina idadi katika pambizo za mbingu na katika nafsi zao?

Na wanaposomewa Qur’an hawasujudu? Hawakiri wala kusalimu amri.

Sheikh Muhammad Abduh anasema kuwa, usifikirie Qur’an haikugonga nyoyo zao wala kufika sauti yake ndani ya dhamiri zao, bali imefikia kiwango cha kukinaisha, lakini inadi tu ndiyo inayowazuia kuamini chan­zo cha ukadhibishaji, sio uzembe wa dalili, isipokuwa ni uzembe wa mwenye kupewa dalili na upinzani wake.

Bali waliokufuru wanadadhibisa tu! Haki kwa kiburi na inadi na Mwenyezi Mungu anayajua zaidi wanayoyakusanya; yaani malengo wanayoyadhamiria katika nyoyo zao si mengine, isipokuwa kupupia vyeo vyao na chumo lao.

Basi wabashirie adhabu chungu ikiwa ni malipo ya waliyoyatenda.

Isipokuwa wale walioamni na wakatenda mema, wana ujira usiokati­ka.

Maana ya yasiyokatika ni kutoisha wala kupungua wala kusimbuliwa.

Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 24 (41:8).