read

Sura Ya Themanini Na Saba: Al-A’ala

Imeshuka Makka Ina Aya 19.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى {1}

Lisabihi jina la Mola wako aliye mtukufu.

الَّذِي خَلَقَ فَسَوَّىٰ {2}

Ambaye ameumba, na akawe­ka sawa.

وَالَّذِي قَدَّرَ فَهَدَىٰ {3}

Na ambaye amekadiria, na akaongoza.

وَالَّذِي أَخْرَجَ الْمَرْعَىٰ {4}

Na ambaye ameotesha mal­isho.

فَجَعَلَهُ غُثَاءً أَحْوَىٰ {5}

Kisha akayafanya makavu yenye kupiga weusi.

سَنُقْرِئُكَ فَلَا تَنْسَىٰ {6}

Tutakusomesha hutusahau,

إِلَّا مَا شَاءَ اللَّهُ ۚ إِنَّهُ يَعْلَمُ الْجَهْرَ وَمَا يَخْفَىٰ {7}

Ila akipenda Mwenyezi Mungu, Hakika yeye anayajua yaliyo jahara na yaliyofichika.

وَنُيَسِّرُكَ لِلْيُسْرَىٰ {8}

Tutakusomesha hutusahau

فَذَكِّرْ إِنْ نَفَعَتِ الذِّكْرَىٰ {9}

Basi kumbusha, kwani kukumbusha kunafaa.

سَيَذَّكَّرُ مَنْ يَخْشَىٰ {10}

Atakumbuka mwenye kuo­gopa.

وَيَتَجَنَّبُهَا الْأَشْقَى {11}

Na atajiepusha nako muovu.

الَّذِي يَصْلَى النَّارَ الْكُبْرَىٰ {12}

Ambaye ataingia moto ulio mkubwa.

ثُمَّ لَا يَمُوتُ فِيهَا وَلَا يَحْيَىٰ {13}

Kisha hatokufa humo wala hatakuwa hai.

قَدْ أَفْلَحَ مَنْ تَزَكَّىٰ {14}

Hakika amekwisha faulu aliyejitakasa.

وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّىٰ {15}

Na akalitaja jina la Mola wake, na akaswali.

بَلْ تُؤْثِرُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا {16}

Bali mmeathirika na maisha ya dunia!

وَالْآخِرَةُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ {17}

Na akhera ni bora na yenye kubaki zaidi.

إِنَّ هَٰذَا لَفِي الصُّحُفِ الْأُولَىٰ {18}

Hakika haya yamo katika vitabu vya mwanzo.

صُحُفِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ {19}

Vitabu vya Ibrahim na Musa

Maana

Lisabihi jina la Mola wako aliye mtukufu.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume (s.a.w.) na taklifa inawahusu wote. Maana ni kuwa mtakase Mwenyezi Mungu na ushirika na kuwa na mke na mtoto na kila lisilo laikiana na cheo chake na utukufu wake.

Hakuna kitu kinachofahamisha utakaso wa muumba kuliko neno lailaha illallah (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu). Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameamrisha kulitakasa jina na wala sio dhati, kwa vile ukomo wa juhudi ya mtu ni kumjua Mwenyezi Mungu kwa majina yake mazuri na sifa zake kuu, lakini kuijua dhati yake hakuwezi kingia kwenye akili wala fahamu.

Ambaye ameumba na akaweka sawa.

Aliumba alivyoumba akaweka kiwango cha kimo chake, akatia sura alivy­otia sura akazifanya nzuri sura zake.

Na ambaye amekadiria na akaongoza.

Kila kitu amekifanyia lengo na kukisahilishia kwenye lengo hilo. Tafsiri nzuri ya Aya hii ni kauli ya Imam Ali (a.s): “Amekadiria alivyoviumba akakadiria na kuimarisha makadirio yake, na amepanga akaufanya mzuri mpango, na akaelekeza mweleko wake wala hakuvuka mpaka wa ngazi yake au kuzembea kwa kutofikia lengo lake.”

Na ambaye ameotesha malisho kwa ajili ya manufaa na riziki ya wanya­ma.

Kisha akayafanya makavu yenye kupiga weusi.

Kimsingi ni kuwa mimea ina manufaa ikiwa mibichi au mikavu kwa mal­isho ya wanyama. Hapa kuna ishara kuwa kila kilicho hai kitaondoka.

Tutakusomesha hatusahau.

Hii ni habari njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Nabii wake Mtukufu, kwamba Qur’an itamshukia moyoni mwake na kujikita humo, haitampita hata herufi moja. Umetangulia mfano wake katika Juz. 28 (75:17).

Ila akipenda Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu hatamsahahulisha mtume wake chochote katika Qur’an isipokuwa Aya za naskh (za kufuta hukumu.).

Sisi tuko pamoja na wale wasemao kuwa lengo la kuvua huku ni kutana­bahisha kuwa kuhifadhi na kutoshau ni fadhila na takrima kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake na wala sio jambo la lazima. Lau Mwenyezi Mungu (s.w.t.) angelitaka kumsahaulisha Nabii wake angeli­fanya na kisingemshinda chochote. mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

خَالِدِينَ فِيهَا مَا دَامَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ إِلَّا مَا شَاءَ رَبُّكَ ۚ {107}

“Watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipokuwa apen­davyo Mola wako.”
Juz 12 (11:107).

Yaani kubakia milele ni kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu na utashi wake, lau angelitaka kuwatoa kwenye Jahannam asingelimzuia na hilo mzuiaji yoyote.

Hakika yeye anayajua yaliyo jahara na yaliyofichika.

Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu. Hapa ameashiria hilo baada ya kutaja kusahau kwa mtume ili kumwambia Nabii wake mtukufu: Sisi tunajua yaliyo katika nafsi yako kwamba wewe ulikuwa unahofia kisikupite kitu chochote. Hapana, hakuna kitaka­chokupita; kuwa katika amani na utulivu.

Tutakasahilisha yawe mapesi.

Makusudio mepesi ni sharia nyepesi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atakusahilishia njia ya wahyi kwa ishara zake na hukumu zake ili uzihifadhi na kuzifanyia kazi kama anavyotaka Mwenyezi Mungu.

Basi kumbusha, kwani kukumbusha kunafaa.

Hakuna mwenye shaka kwamba kukumbusha ni wajibu hata kama utajua kuwa hakutanufaisha, ili kuondoa visababu na kuleta hoja, vinginevyo kusingelikuwa na hisabu na adhabu. Mwenyezi Mungu Mtume anasema:

رُسُلًا مُبَشِّرِينَ وَمُنْذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ ۚ {165}

“(Ni) Mitume wabashiri, waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya mitume; Juz. 6 (4:165).

Kwa hiyo basi herufi in hapa itakuwa mbali tena mbali sana kuwa ni ya shart (kuifasiri kukumbusha kama kutafaa kukumbusha).

Makusudio hapa ni kubainisha uhalisia; yaani ananufaika na ukumbusho mwenye kutaka uongofu, lakini mwenye kung’ang’ania upotevu hanufaiki na chochote.

Linalofahamisha makusudio ya maana haya ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtume iliyokuja moja kwa moja.

Atakumbuka mwenye kuogopa na atajiepusha nako muovu.

Kwa hiyo ukumbusho unamfaa yule aliyeamshwa na kumwogopa Mwenyezi Mungu wala haupingi isipokuwa muovu aliyepofushwa na matamanio na uovu wake ukamshinda.

Ambaye ataingia moto ulio mkubwa kwa ukali wake na vituko vyake.

Kisha hatokufa humo wala hatakuwa hai.

Tutaifasiri kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ نَارُ جَهَنَّمَ لَا يُقْضَىٰ عَلَيْهِمْ فَيَمُوتُوا وَلَا يُخَفَّفُ عَنْهُمْ مِنْ عَذَابِهَا {36}

“Na wale ambao wamekufuru watakuwa na moto wa Jahannam, hawahukumiwi wakafa wala hawatapunguziwa adhabu yake.” Juz: 22 (35:36).

Sheikh Muhammad Abduh anasema katika kufasiri kumbusha, kwani kukumbusha kunafaa: “Jihadhari na kuhadaika na wayasemayo wale wanovaa vazi la ulama na kudai madai ya wapumbavu kwamba si wajibu kukumbusha kwa vile kukumbusha hakufai wakitoa hoja kwa Aya hii.

“Kama ingelikuwa kweli kauli yao hiyo basi isingelikuwa ni wajibu kukumbusha wakati wowote, kwa sababu hakuna wakati usiokuwa na wapinzani wala kusalimika na wanaomlani Mungu. Wengine wanajitamkia kwa hawaa lakini wanajikinga na woga na kutoa hoja kwa uvivu wao na wanapenda kujipamba machoni mwa watu hata kama wataingia kwenye chuki ya Mwenyezi Mungu.

Hakika amekwisha faulu aliyejitakasa.

Makusudio ya kufaulu hapa ni kuokoka na hasira za Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Kujitakasa ni kujisafisha na dhambi.

Na akalitaja jina la Mola wake na akaswali.

Makusudio ya kutaja hapa ni yale yanayomkurubisha kwenye heri na kumweka mbali na shari. Ama harakati za ulimi tu peke yake sio lengo. Wala hakuna katika amri ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake isipokuwa ni nyenzo ya kufanya heri na kujiweka mbali na shari.

Inatosha kuwa ni dalili ya hakika hii kauli yake Mtume (s.a.w): “Hakika si mengineyo nimetumwa kukamilisha hulka njema” na kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ {107}

“Na hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu.” Juz. 17 (21:107).

Makusudio ya maswali ni swala tano, kwani ndizo nguzo za dini.

Bali mmeathirika na maisha ya dunia.

Hapa ndio inapatikana siri ya mwanzo na mwisho ya kuikataa haki kwa makusudi. Kuwa mtumwa wa dunia na kuing’ang’ania kama mtoto anavy­oling’ang’ania titi la mama yake, kwa hiyo imemuweka mbali na Mwenyezi Mungu na haki na utu.

Na akhera ni bora na yenye kubaki zaidi; bali hakuna heri yoyote kabisa katika dunia ikiwa sio nyenzo ya heri ya akhera. Kwa sababu uamirishaji wa dunia unaharibika, ufalme wake unaondoka na mali yake inaisha.

Amesema kwenye Nahjul-Balagha: “Kila kitu duniani kusikiwa kwake ni kukubwa kuliko kuonekana kwake, na kila kitu Akhera kuonwa kwake ni kukubwa kuliko kusikiwa kwake. Jueni kwamba linalopungua duniani na kuzidi Akhera ni bora kuliko linalopungua Akhera na kuzidi duniani.”

Hakika haya yamo katika vitabu vya mwanzo vitabu vya Ibrahim na Musa.

‘Haya’ ni ishara ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu : “Hakika amek­wisha faulu aliyejitakasa’ maana ni kuwa mwito wa mitume kwa upande wa kiitikadi ni mmoja kwa sababu aliyewatuma ni mmoja na kauli yake ni moja haipingani.

Tofauti zinakuweko kwenye tanzu ambazo zinaenda na wakati.

Maadamu ni hivyo basi wale wanaomwamini Ibrahim kama waarabu na wanaomwamini Musa kama Mayahudi ni juu yao wamwamni Muhammad (s.a.w.); vinginevyo watakuwa ni katika wale wanaoamini msingi mmoja na kuukataa wakati huo huo.