read

Sura Ya Themanini Na Sita: At-Taariq

Imeshuka Makka Ina Aya 17.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

وَالسَّمَاءِ وَالطَّارِقِ {1}

Naapa kwa mbingu na kina­chokuja usiku!

وَمَا أَدْرَاكَ مَا الطَّارِقُ {2}

Ni lipi la kukujulisha nini kinachokuja usiku?

النَّجْمُ الثَّاقِبُ {3}

Ni nyota inayotoboa.

إِنْ كُلُّ نَفْسٍ لَمَّا عَلَيْهَا حَافِظٌ {4}

Hakuna nafsi yoyote ila ina mwenye kuiihifadhi.

فَلْيَنْظُرِ الْإِنْسَانُ مِمَّ خُلِقَ {5}

Basi na atazame mtu ameumb­wa kwa kitu gani?

خُلِقَ مِنْ مَاءٍ دَافِقٍ {6}

Ameumbwa kwa maji yanay­otoka kwa kuchupa.

يَخْرُجُ مِنْ بَيْنِ الصُّلْبِ وَالتَّرَائِبِ {7}

Yanayotoka baina ya uti wa mgongo na kifua.

إِنَّهُ عَلَىٰ رَجْعِهِ لَقَادِرٌ {8}

Hakika yeye ni muweza wa kumrejesha.

يَوْمَ تُبْلَى السَّرَائِرُ {9}

Siku zitakapofunuliwa siri.

فَمَا لَهُ مِنْ قُوَّةٍ وَلَا نَاصِرٍ {10}

Basi hatakuwa na nguvu wala msaidizi.

وَالسَّمَاءِ ذَاتِ الرَّجْعِ {11}

Naapa kwa mbingu yenye marejeo!

وَالْأَرْضِ ذَاتِ الصَّدْعِ {12}

Na kwa ardhi yenye mpa­suko!

إِنَّهُ لَقَوْلٌ فَصْلٌ {13}

Hakika hiyo ni kauli yenye kupambanua.

وَمَا هُوَ بِالْهَزْلِ {14}

Wala si mzaha.

إِنَّهُمْ يَكِيدُونَ كَيْدًا {15}

Hakika wao wanachimba vitimbi,

وَأَكِيدُ كَيْدًا {16}

Nami ninachimba vitimbi.

فَمَهِّلِ الْكَافِرِينَ أَمْهِلْهُمْ رُوَيْدًا {17}

Basi wape muhula makafiri – wape muhula kidogo.

Maana

Naapa kwa mbingu na kinachokuja usiku. Ni lipi la kukujulisha nini kinachokuja usiku? Ni nyota inayotoboa.

Kila kilicho juu yako ni mbingu. Makusudio ya kinachokuja usiku hapa ni nyota kwa sababu haijitokezi isipokuwa usiku. Kutoboa ni kung’aa, kama wanavyolitumia waarabu neno hilo kwa kusema: utoboe moto wako, yaani uwashe uwe na mwanga.

Nyota imepewa sifa hiyo kwa vile mwanga wake unalitoboa giza, kama kwamba giza ni ngozi nyeusi na nyota inaitoboa kwa mwanga wake. eno “ni lipi la kukujulisha” linatambulisha kulikuza jambo na kuliad­himisha. wenyezi Mungu (s.w.t.) ameapa kwa nyota inayong’aa ili kutanabahisha manufaa yake makubwa na kutengenezwa kwake kwa ajabu.

Ama kinachoapiwa, Mwenyezi Mungu (s.w.t.), amekiashiria kwa kusema:

Hakuna nafsi yoyote ila ina mwenye kuiihifadhi kauli zake na vitendo vyake na kudhibiti harakati zake na siri zake, mpaka uishe muda na kuku­tana na Mola wake, hapo itakuta heri iliyoifanya imehudhurisha na shari iliyoifanya pia. Kwa maneno mengine ni:

وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ بِذُنُوبِ عِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا {17}

“Na Mola wako anatosha kuwa ni mwenye habari na mwenye kuona dhambi za waja wake.”
Juz. 15 (17:17)
.

Basi na atazame mtu ameumbwa kwa kitu gani? Ameumbwa kwa maji yanayotoka kwa kuchupa, yanayotoka baina ya uti wa mgongo na kifua.

Maji yanayochupa ni manii. eno uti wa mgongo tumelifasiri kutokana na neno ulb lenye maana ya kila mfupa wenye uti wa mgongo. Kifua limetokana na araib lenye maana sehemu inayovaliwa mkufu kifuani.

Makusudio ya uti wa mgongo hapa ni mwanamume na kifua ni cha mwanamke. Sehemu hizi mbili ndio chimbuko la manii yanayotengeneza mtoto. Ni hivi karibuni tu sayansi imepata mwongozo wa hakika hii iliyokuja kutoka kwenye ulimi wa mwarabu mmoja ambaye hakwenda shule.

Maana ya Aya hizi ni kuwa ewe mtu ukishajua kuwa Mwenyezi Mungu anajua siri yako na dhahiri yako, basi ni juu yako kujiangalia na kufikiria kupatikana kwako.

Umeanza kutokana na tone la manii lililotoka mgongo­ni mwa baba yako na kifua cha mama yako, kisha ukawekwa mahali maki­ni penye utulivu mpaka muda maalum, ukawa katika umbo zuri lililokami­lika lilio na uhai, mhemuko na utambuzi.

Hebu fikiria na uzingatie hayo ili ujue kuwa aliyekuanzisha na kukuongoza anaweza kukurudisha mara ya pili kwenye uhai wako.

Haya ndio maana ya kuli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Hakika yeye ni muweza wa kumrejesha.

Kwa hiyo kuumbwa kwa kwanza ni ushahi­di wa kuumbwa kwa pili.

Siku zitakapofunuliwa siri, basi hatakuwa na nguvu wala msaidizi .

Neno kufunuliwa tumelifasiri kutokana na neno ubla lenye maana ya kufanyiwa mtihani, yaani siri zitafanyiwa mtihani kwa kufichuliwa na kud­hihirishwa.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawafufua watu katika siku ambayo hakutakuwa na sitara au kificho wala mjadala au hoja, wala haku­takuwa na nguvu kwa yeyote kujisaidia yeye mwenyewe au mwinginewe, isipokuwa nguvu ya imani na matendo mema.

Naapa kwa mbingu yenye marejeo! Na kwa ardhi yenye mpasuko!

Marejeo ni maji ya mvua (kwa vile mvua inanyesha na kurejea) na mpa­suko ni mimea (imepasuka kwa kuchipuka mimea). Mwenyezi Mungu ameapa kwa mbingu yenye kumimina maji na kwa ardhi yenye kuleta heri na vyakula.

Hakika hiyo ni kauli yenye kupambanua wala si mzaha.

‘Hiyo’ ni Qur’an nayo ni ukweli sio mchezo na ni haki isiyofikiwa na batili mbele yake wala nyuma yake. Na hii ni kumrudi aliyesema kuwa ni ngano za watu wa kale.

Hakika wao wanachimba vitimbi nami ninachimba vitimbi. Basi wape muhula makafiri, wape muhula kidogo.

Wao ni wale waliomkadhimisha Mtume Mtukufu (s.a.w). Wanachimba vitimbi ni kufanya njama dhidi ya Mtume na waumini. Nami ninachimba vitimbi ni kubatilisha na kuzipangua njama zao.

Maana ni kuwa: Ewe Muhammad! Mimi ninamuotea yule anayejaribu kubatilisha mambo yako kwa njama, ngoja kidogo utaona hizaya na mate-so yatakayowapata.

Umetangulia mfano wake pamoja na Tafsiri katika Juz. 2. (3:54).