read

Sura Ya Themanini Na Tano: Al-Buruj

Imeshuka Makka. Ina Aya 22.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

وَالسَّمَاءِ ذَاتِ الْبُرُوجِ {1}

Naapa kwa mbingu yenye Buruji!

وَالْيَوْمِ الْمَوْعُودِ {2}

Na kwa siku iliyoahidiwa!

وَشَاهِدٍ وَمَشْهُودٍ {3}

Na kwa shahidi na chenye kushuhudiliwa!

قُتِلَ أَصْحَابُ الْأُخْدُودِ {4}

Wemelaaniwa watu wa mahandaki.

النَّارِ ذَاتِ الْوَقُودِ {5}

Yenye moto wenye kuni nyingi.

إِذْ هُمْ عَلَيْهَا قُعُودٌ {6}

Walipokuwa wamekaa hapo.

وَهُمْ عَلَىٰ مَا يَفْعَلُونَ بِالْمُؤْمِنِينَ شُهُودٌ {7}

Na wao ni mashahidi wa yale walioyoyafanya waumini.

وَمَا نَقَمُوا مِنْهُمْ إِلَّا أَنْ يُؤْمِنُوا بِاللَّهِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ {8}

Na hapana lililowachukiza kwao ila ni kwamba wal­imwamini Mwenyezi Mungu mwenye nguvu mwenye kusifi­wa.

الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَاللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ {9}

Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, na Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kila kitu.

إِنَّ الَّذِينَ فَتَنُوا الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ لَمْ يَتُوبُوا فَلَهُمْ عَذَابُ جَهَنَّمَ وَلَهُمْ عَذَابُ الْحَرِيقِ {10}

Hakika wale waliowafitini waumini wanaume na wau­mini wanawake, kisha wasitubie, basi watapata adhabu ya Jahannam na wat­apata adhabu ya kuungua.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْكَبِيرُ {11}

Hakika waliaomini na waka­tenda mema watapata bustani zipitiwazo na mito chini yake. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

إِنَّ بَطْشَ رَبِّكَ لَشَدِيدٌ {12}

Hakika kamato la Mola wako ni kubwa.

إِنَّهُ هُوَ يُبْدِئُ وَيُعِيدُ {13}

Hakika yeye ndiye anayeanzisha na anayerud­isha.

وَهُوَ الْغَفُورُ الْوَدُودُ {14}

Na yeye ni mwingi wa maghu­fira Mwenye mapenzi.

ذُو الْعَرْشِ الْمَجِيدُ {15}

Mwenye Arsh, Mtukufu.

فَعَّالٌ لِمَا يُرِيدُ {16}

Mwingi wa kutenda alipenda­lo.

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ الْجُنُودِ {17}

Je imekufikia habari ya majeshi?

فِرْعَوْنَ وَثَمُودَ {18}

(Ya) Frauni na Thamudi?

بَلِ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي تَكْذِيبٍ {19}

Lakini waliokufuru wako katika kukadhibisha.

وَاللَّهُ مِنْ وَرَائِهِمْ مُحِيطٌ {20}

Na Mwenyezi Mungu nyuma yao amewazunguka.

بَلْ هُوَ قُرْآنٌ مَجِيدٌ {21}

Bali hiyo ni Qur’an Tukufu.

فِي لَوْحٍ مَحْفُوظٍ {22}

Katika ubao uliohifadhiwa

Maana

Naapa kwa mbingu yenye buruji.

Kila kilicho juu yako ni mbingu. Ama buruji imesemekana ni nyota nyin­gi kubwa kwa sababu kila nyota katika hizo inaonekana kama buruji kubwa.

Imesamekana ni manazili kumi na mbili yaliyo maarufu ambayo ardhi inayapitia katika mzunguko wake wa jua kwa mwaka mmoja, nayo: Punda, Ng’ombe, Mapacha, Kaa, Simba, Mashuke, Mizani, Nge, Mshale, Mbuzi, Kondoo na Samaki.

Ni sawa makusudio yawe ni maana ya kwanza au ya pili au yote pamoja, lakini lengo ni kutanabahisha usanii wa hali ya juu katika nyota na hikima kubwa, ili kutoa dalili kwa hilo kuwa kuna muumba aliye mkuu.

Na kwa siku iliyoahidiwa ambayo ni siku ya Kiyama.

Na kwa shahidi na chenye kushuhudiliwa.

Kauli zimekuwa nyingi na kugongana kuhusiana na maana ya shahidi na chenye kushuhudiliwa. Baadhi ya wafasiri wameishia kwenye kauli 48; 16 zikiwa katika maana ya shahidi na 32 katika chenye kushuhudiliwa!

Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Makusudio ya shahidi ni kila chenye hisia za kushuhudia, na makusudio ya chenye kushuhudiliwa ni chenye kuhisiwa ambacho ushahidi umetokea juu yake.” Ametoa dalili ya kusihi kauli yake kwa mambo mawili:

Kwanza hilo ni hakika dhahiri inayofahamika kutokana na dalii ya tamko.

Pili, kwamba cha kwanza alichoapia nacho Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni nyota za mbingu. Na katika nyota hizi kuna zilizo ghaibu na zina­zoshuhudiwa. Zinazoshuhudiwa ni kuwa nuru ya harakati zake, machim­buko yake na machweo yake, yote yanahisiwa na kushuhudiwa.

Ama zilizo ghaibu ni kuwa hakika yake na nguvu zilizomo ndani yake hazitambuliwi wala kushuhudiwa kwa hisia. Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akaapa kwa siku ya mwisho ambayo ni ghaibu isiyohusiana na kushuhudiwa kwa karibu wala kwa mbali.

Tena Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akaapa kwa shahidi na chenye kushuhudi­wa. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anakuwa ameapa na ulimwengu wote, ni sawa uwe ni wa ghaibu tu, au wakushuhudiwa tu, au wa yote mawili pamoja.

Lengo la hayo ni kuwa waangaliaji waangalie viumbe kwa aina zake zote, wazingatie hikima na nidhamu inayojitokeza na wafanye juhudi kujua yale yaliyo ghaibu na kujificha.

Wemelaaniwa watu wa mahandaki yenye moto wenye kuni nyingi, walipokuwa wamekaa hapo na wao ni mashahidi wa yale walioyoy­afanya waumini.

Mahandaki ni mashimo yanayochimbwa ardhini kwa umbo la msitatili. Watu wake hapa ni makafiri walio na nguvu na utawala. Imesemekana makusudio yake hapa ni Dhunuwasi na watu wake, aliyekuwa mmoja wa wafalme wa Yemen.

Vyovyote watakavyokuwa wenye mahandaki, muhimu ni kuwa Aya hizi zinaashiria watu waasi waliochimba handaki na wakalikokea moto ndani yake uliowaka sana.

Kisha wakawaleta waumini wenye ikhlasi na kuwaonyesha moto. Mwenye kurudi na kuacha dini yake na kuafikiana nao kwenye kufru na maasi basi walimwacha, na mwenye kushikamana na imaani na ikhlasi, walimuunguza; wenyewe wakiwa wamekaa pembeni mwa haandaki wakiangalia huku wakifurahia na kuburudika kwa kuona miili iliyo hai ikiteketea motoni.

Na hapana lililowachukiza kwao ila ni kwamba walimwamini Mwenyezi Mungu mwenye nguvu mwenye kusifiwa. Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, na Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kila kitu.

Hili ndilo kosa lao la kwanza na la mwisho kwao-kuwa wamemwamini Mwenyezi Mungu mfalme wa wafalme Mwenye uweza, Mwenye kushin­da, Mjuzi wa kila kitu na Mwenye kustahiki sifa njema Yeye peke Yake. Mwenye Mungu (s.w.t.) amejisifu kwa sifa hizi kuashiria kuwa waasi hawana pa kumkimbia Mwenyezi Mungu na adhabu yake, mfano wake ni:

 أَتَقْتُلُونَ رَجُلًا أَنْ يَقُولَ رَبِّيَ اللَّهُ {28}

“Mtamuua mtu kwa kusema Mola wangu ni Mwenyezi Mungu”?: Juz. 24 (40:28).

Hakika wale waliowafitini waumini wanaume na waumini wanawake, kisha wasitubie, basi watapata adhabu ya Jahannam na watapata adhabu ya kuungua.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kudokeza juu ya watu wa mahandaki waliojifanya majabari, hapa anawaelezea vigogo wa kikuraishi waliowaud­hi waumini kwa kuwafitini na dini yao au kuwarudisha kwenye ukafiri baada ya imani yao. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewahadharisha na kuwaahidi adhabu kama hawatakoma.

Kuunganisha adhabu ya kumjua na adhabu ya Jahannam ni katika upande wa kuunganisha tafsir na ufafanuzi, kwa lengo la kusisitiza na hadhari, pia kuzidishia kuhofia.

Hakika waliaomini na wakatenda mema watapata bustani zipitiwazo na mito chini yake. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

Umetangulia mfano wake katika Aya kadhaa zilizopita. Imetajwa hapa kutokana na njia ya Qur’an Tukufu, kukutanisha maangamizi ya wenye hatia na kufuzu wenye takua, na neema ya hawa na moto wa wale.

Hakika kamato la Mola wako ni kubwa.

Neno “kamato” tumelifasiri kutokana na neno Batsha lenye maana ya kukamata kwa nguvu. Itakuwaje ikiwa kamato hilo ni kubwa, tena kutoka kwa aliye Jabari wa mbingu na ardhi. Maneno hapa yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa lengo la kuwahadharisha wale ambao wanamuudhi Mtume na wale walioamini pamoja naye.

Hakika yeye ndiye anayeanzisha na anayerudisha.

Mwenye kuwa na uwezo wa kuanza kuumba na kurudisha tena, basi ana uwezo zaidi wa kukamata na kudhibiti waasi.

Na yeye ni mwingi wa maghufira Mwenye mapenzi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alipotaja adhabu kali aliikutanisha na maghufira yake na upole wake, ili waasi warejee kwa toba wala wasikate tamaa na rehema yake. Kwani ghadhabu yake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa wenye dhambi haimzui na huruma zake kwao.

Mwenye Arsh, Mtukufu, yaani Mwenye ufalme na utawala.

Mwingi wa kutenda alipendalo.

Kutaka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kunathibitika kwa mjaradi wa kutaka kwake tu, bila ya kuwa na haja ya kutumia kitu kingine. Imam Ali (as) anasema: “Ni mwenye kufanya sio kwa kutumia vifaa, Mwenye kukadiria sio kwa kuanza kufikiria, Mwenye kutaka bila ya kudhamiria … huliambia analotaka: kuwa, na linakuwa si kwa sauti ya kusikiwa wala kwa mwito unaoitikiwa.”

Hikima yake Mtukufu ilitaka uma zilizotangulia ziangamie zilipowakid­hibisha Mitume, kwa hiyo ikawa ni kama alivyotaka.

Je imekufikia habari ya majeshi ya Firauni na Thamudi?

Hao ni wale ambao Mwenyezi Mungu amewaangamiza kwa kuwakad­hibisha kwao Mitume wao.

Neno “Je” hapo ni la kuthibitisha kama ilivyo katika Juz. 29 (76:1) maana ni umekwishasikia ewe Muhammad na pia kaumu yako wamesikia yaliy­owapitia watu wa Hud ambao ni kaumu ya Swaleh na Firauni na watu wako, jinsi Mwenyezi Mungu alivyomuadhibu walipowakadhibisha Mitume, vile vile Mwenyezi Mungu anaweza kuwaadhibu waliokukad­hibisha wewe wakati wowote anapotaka.

Lakini waliokufuru wako katika kukadhibisha.

Kikundi cha wale waliokufuru, wakiwemo vigogo wa kikuraishi wanaipin­ga haki, si kwa lolote ila ni kwamba wao wanapenda sana kuikadhibisha na kuifanyia inadi popote walipokuwa na watakapokuwa; vinginevyo ni udhuru gani walio nao wa kuipinga haki na hali dalili na ubainifu uko wazi na umejitokeza kama mchana?

Na Mwenyezi Mungu nyuma yao amewazunguka.

Wao wako mikononi mwa Mwenyezi Mungu, anawageuza vyovyote atakavyo na anaweza kuwangamiza wakati wowote anaotaka. Hapa kuna ishara kwamba wao hawataacha kukadhibisha haki mpaka waione adhabu.

Bali hiyo ni Qur’an Tukufu yenye shani kubwa, kwa sababu kila kili­chomo ndani yake ni haki na uadilifu, pamoja na kusimama hoja na dalili. Na hakuna anayeikadhibisha isipokuwa wakosefu wenye hatia.Katika ubao uliohifadhiwa na upotofu na kulindwa na mageuzo na mabadiliko.

Wafasiri wana maneno marefu na mapana kuhusiana na neno “Ubao ulio­hifadhiwa!” sisi hatutaulizwa hakika yake na ilivyo. Waliozama katika ilimu wanaamini ya ghaibu na yaliyofichika kwao na wanajizuia kuy­achambua.