read

Sura Ya Themanini Na Tisa: Al-Fajr

Imeshuka Makka Ina Aya 30

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

وَالْفَجْرِ {1}

Naapa kwa alfajiri.

وَلَيَالٍ عَشْرٍ {2}

Na kwa masiku kumi.

وَالشَّفْعِ وَالْوَتْرِ {3}

Na kwa shufwa na witiri.

وَاللَّيْلِ إِذَا يَسْرِ {4}

Na kwa usiku unapopita.

هَلْ فِي ذَٰلِكَ قَسَمٌ لِذِي حِجْرٍ {5}

Je, katika hayo mna kiapo kwa Mwenye akili?

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِعَادٍ {6}

Je, hukuona jinsi Mola wako alivyowafanya A’ad?

إِرَمَ ذَاتِ الْعِمَادِ {7}

Wa Iram wenye maguzo?

الَّتِي لَمْ يُخْلَقْ مِثْلُهَا فِي الْبِلَادِ {8}

Ambao hakuumba mfano wake katika miji?

وَثَمُودَ الَّذِينَ جَابُوا الصَّخْرَ بِالْوَادِ {9}

Na Thamud waliopasua maja­bali bondeni?

وَفِرْعَوْنَ ذِي الْأَوْتَادِ {10}

Na Firauni mwenye vigingi?

الَّذِينَ طَغَوْا فِي الْبِلَادِ {11}

Ambao walipituka mipaka katika miji?

فَأَكْثَرُوا فِيهَا الْفَسَادَ {12}

Wakakithirisha humo ufisa­di?

فَصَبَّ عَلَيْهِمْ رَبُّكَ سَوْطَ عَذَابٍ {13}

Basi Mola wako akawami­minia kiboko cha adhabu.

إِنَّ رَبَّكَ لَبِالْمِرْصَادِ {14}

Hakika Mola wako yuko kwenye kuotea.

فَأَمَّا الْإِنْسَانُ إِذَا مَا ابْتَلَاهُ رَبُّهُ فَأَكْرَمَهُ وَنَعَّمَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَكْرَمَنِ {15}

Na ama mtu Mola wake anapomjaribu na akamkir­imu na akamneemesha, huse­ma: Mola wangu amenikir­imu.

وَأَمَّا إِذَا مَا ابْتَلَاهُ فَقَدَرَ عَلَيْهِ رِزْقَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَهَانَنِ {16}

Na anapomjaribu, akam­punguzia riziki yake, husema: Mola wangu amenitweza.

Aya 1-16:Alfajiri Na Masiku Kumi

Maana

Naapa kwa alfajiri, na kwa masiku kumi, na kwa shufwa na witiri na kwa usiku unapopita.

Makusudio ya Alfajiri hapa ni kila alfajiri, kwa kuchukulia dhahiri ya neno. Ama masiku kumi hakuna dhahiri ya kuwa ni masiku maalum, wala haku­na karina inayoweza kutusaidia. kwa ajili hiyo tunayanyamazia yale aliy­oyanyamazia Mwenyezi Mungu.
Ama kauli ya kwamba ni mianzo ya mwezi wa Dhul-hijja (mfunguo tatu) au Muharram (mfunguo nne) au kuwa ni mwisho wa Ramadhani, inahitajia dalili.

Sheikh Muhammad Abduh amejaribu kuainisha kuwa ni kila masiku ya mwanzo wa mwezi na akaelezea kwa urefu, lakini hakuleta hoja ya kuki­naisha.

Mwanafunzi wake Al-Maraghi naye akamuiga kwa kila alilolisema na akanukuu ibara zake pamoja na urefu wake bila ya kuishiria kwenye chim­buko lake, kama ilivyo desturi yake.

Katika kufasiri shufwa na witiri kuna kauli nyingi; iliyo karibu zaidi na dhahiri ya tamko ni ishara ya kuwa ni hisabu na kudhibiti viwango tu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameapa kwa hisabu ili kutanabahisha kwenye faida zake.

Makusudio ya kupita usiku ni kuondoka. Kwa hiyo hapa Mwenyezi Mungu amechanganya viapo viwili: Kutangulia mchana na kuja usiku, kama alivyosema.

وَاللَّيْلِ إِذْ أَدْبَرَ {33}

وَالصُّبْحِ إِذَا أَسْفَرَ {34}

“Na kwa usiku unapokucha na kwa asubuhi inapopambazuka.” Juz. 29 (74:33-34).

Je, katika hayo mna kiapo kwa Mwenye akili?

Swali hili ni kuripoti uhalisia, kwa maana ya kuwa ndivyo ilivyo hivyo kuwa hakika katika hayo mna kiapo kwa mwenye akili. Makusudio ya kuapia hivi ni hoja na dalili, kwa sababu ndani yake kuna uthibitisho wahaki.

Neno akili tumelitoa kwenye neno Hijr lenye maana nyingi; miongoni mwazo ni majumba ya Thamud, na kizuizi cha Al-kaiba. Limetumika neno hilo kwa maana ya akili kwa vile inamzuia mwenye nayo na mambo mengi.

Maana ni kuwa katika vitu alivyoapia navyo Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuna hoja tosha za kuweko Mwenyezi Mungu, uweza wake na hikima yake. Kwa sababu mazingatio na hikima iliyomo inafahamisha hilo kwa utoaji; sawa na unavyofahamisha ukulima kuwako mkulima.

Je, hukuona jinsi Mola wako alivyowafanya A’ad wa Iram wenye maguzo, ambao hakuumba mfano wake katika miji?

A’d ni kaumu ya Hud. Iram ni jina la kabila la A’d kwa kunasibishwa kwa mmoja wa babu yao, aliyeitwa Iram.

Sheikh Muhammad Abduh anasema, makusudio ya maguzo hapa ni magu­zo ya mahema yao au ni kinaya cha nguvu walizo kuwa nazo. Lililo karibu zaidi na usawa ni kuwa makusudio ya maguzo hapa ni majen­go na ngome kwa sababu Mtume wao aliwaambia kwa kutokubaliana nao:

أَتَبْنُونَ بِكُلِّ رِيعٍ آيَةً تَعْبَثُونَ {128}

وَتَتَّخِذُونَ مَصَانِعَ لَعَلَّكُمْ تَخْلُدُونَ {129}

“Je, mnajenga juu ya kila muinuko ishara ya kufanyia upuzi? Na mnajen­ga ngome ili mkae milele?” Juz. 19 (26:128-129).

Naam! Sisi tuko pamoja na Sheikh Muhamad Abduh katika kauli yake hii: “Hapa wafasiri wamepokea hekaya nyingi katika kuleta picha ya Iram wenye maguzo, ambazo ilikuwa ni wajibu ziepushwe na kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Ukiona chochote katika vitabu vyao katika wasifu wa Iram, basi lifumbie jicho lako na ujihadhari na kuchunguza yamepita maelezo kuhusu A’ad na Nabii wao Hud katika Juz. 12 (11:50-56), Juz. 19 (26:123-140) na nyinginezo.

Na Thamud waliopasua majabali bondeni.

Thamud ni kaumu ya Swaleh, kupasua majabali ni ishara ya yaliyosemwa kwenye Aya nyingine isemayo: “Na mnachonga majumba milimani kwa ustadi.” Juz. 19 (26:149).

Na Firauni mwenye vigingi; yaani majengo adhimu, kama ihram (pyra­mids).

Ambao walipituka mipaka katika miji; wakakithirisha humo ufisadi, basi Mola wako akawamiminia kiboko cha adhabu.

Kuanzia neno ambao walipituka mipaka na kuendelea, ni sifa za A’ad, Thamud na Firaun. Mwenyezi Mungu ametaja kiboko kwa sababu kinaashiria kukaririka adhabu; kwani Mwenyezi Mungu aliwaadhibu A’ad kwa upepo, Thamud kwa ukelele na Firauni kwa kuzama majini.

Hakika Mola wako yuko kwenye kuotea.

Hili ni jawabu la kiapo katika mwanzo wa Sura. Imesemekana kuwa jawabu sio hili bali ni la kukadiria, kuwa atawaadhibu wenye hatia. Kwenye makadirio yote mawili natija ni moja.

Maana yako wazi kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anajua makusudio ya waja na vitendo vyao na atawalipa kulingana navyo.

Na ama mtu Mola wake anapomjaribu na akamkirimu na akam­neemesha, husema: Mola wangu amenikirimu. Na anapomjaribu, akampunguzia riziki yake, husema: Mola wangu amenitweza.

Mtu hapa ni jinsi ya mtu yeyote, kumkirimu na kumneemesha ni wasaa wa riziki na kumjaribu ni kumfanyia mtihani. Maana ya kumfanyia mtihani kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) mja wake, ni kumpa sababu za kudhi­hirisha hakika yake; kama utajiri na ufukara. Akishukuru kwa utajiri na kuwa na subira kwa ufukara, atastahiki thawabu. Akikufuru kwa ufukara na akapituka mipka kwa utajiri atastahili adhabu.

Kwa maneno mengine nikuwa mtihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kuweko mgongano ambao utadhihirisha vitendo vya mwema na muovu. Hiyo ni kwa ajili ya maandalizi ya kumlipa wema kwa wema na ubaya kwa ubaya, pamoja na kupatikana hoja.

Hii ni hali ya Mwenyezi Mungu pamoja na mja wake. Ama hali ya mtu mpotevu ni kupima takrima anayoipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu ­riziki ikiwa ni kubwa anadhani kuwa yeye ni katika walio karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, na kwamba hataulizwa kitu wala hataadhibiwa kwa alilolitenda au kulifanya.

Sambamba na walivyokuwa vigogo wa kishrik­ina, walikuwa wakitoa dalili ya kukirimiwa kwao na Mwenyezi Mungu kwa wingi wa mali na kuwa Mwenyezi Mungu amewatweza waumini kwa ufukara.

Na kama Mwenyezi Mungu akimdhikisha mpotevu kwenye riziki yake ili angalau atubie, hudhania kuwa Mwenyezi Mungu amemtweza.

Inatosha kwa mja kuwa ni jeuri kumdhania muumba wake dhana mbaya .

Imepokewa kutoka kwa Imam Ali (a.s.): “Mwislamu akipata dhiki asimtilie shaka Mola wake, bali ajitilie shaka yeye kwa Mola wake mwenye funguo za mambo yote.” Umetangulia mfano wake katika Juz. katika Juz.17 (21:35).

كَلَّا ۖ بَلْ لَا تُكْرِمُونَ الْيَتِيمَ {17}

Si hivyo! bali nyinyi humumkirimu yatima,

وَلَا تَحَاضُّونَ عَلَىٰ طَعَامِ الْمِسْكِينِ {18}

Wala hamuhimizani kulisha masikini;

وَتَأْكُلُونَ التُّرَاثَ أَكْلًا لَمًّا {19}

Na mnakula mirathi kula kwa pupa.

وَتُحِبُّونَ الْمَالَ حُبًّا جَمًّا {20}

Na mnapenda mali kupenda sana.

كَلَّا إِذَا دُكَّتِ الْأَرْضُ دَكًّا دَكًّا {21}

Si hivyo! Ardhi itakapopand­wa pondwa.

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا {22}

Na akaja Mola wako na malaika safu safu.

وَجِيءَ يَوْمَئِذٍ بِجَهَنَّمَ ۚ يَوْمَئِذٍ يَتَذَكَّرُ الْإِنْسَانُ وَأَنَّىٰ لَهُ الذِّكْرَىٰ {23}

Na ikaletwa siku hiyo Jahannam, siku hiyo atakum­buka mtu, lakini kutamfaa nini kukumbuka?

يَقُولُ يَا لَيْتَنِي قَدَّمْتُ لِحَيَاتِي {24}

Atasema: laiti ningeutan­gulizia uhai wangu!

فَيَوْمَئِذٍ لَا يُعَذِّبُ عَذَابَهُ أَحَدٌ {25}

Basi siku hiyo hataadhibu adhabu yake yoyote.

وَلَا يُوثِقُ وَثَاقَهُ أَحَدٌ {26}

Wala hatafunga kufunga kwake yoyote.

يَا أَيَّتُهَا النَّفْسُ الْمُطْمَئِنَّةُ {27}

Ewe nafsi iliyotua!

ارْجِعِي إِلَىٰ رَبِّكِ رَاضِيَةً مَرْضِيَّةً {28}

Rejea kwa Mola wako hali ya kuwa radhi umeridhiwa!

فَادْخُلِي فِي عِبَادِي {29}

Basi ingia katika waja wangu.

وَادْخُلِي جَنَّتِي {30}

Na ingia katika Pepo yangu.

Aya 17-30: Mnapenda Sana Mali

Si hivyo! Karama sio mali mbele ya Mwenyezi Mungu, bali ni kwa takua, wala ufukara si utwevu, isipokuwa ni kwa makusudio na matendo mabaya. Bali nyinyi ni washari zaidi, katika viumbe wa Mwenyezi Mungu, kutokana na sababu zifuatazo:

Humumkirimu yatima; hamuwafanyii wema wakimbizi wasiokuwa na wa kuwahami wala kuwatunza kutoka serikalini wala kwao, na nyinyi hamshughulikii mambo yao.

Hamuhimizani kulisha masikini; yaani hamuhimizani kujitolea kwa ajili ya wasio nacho na kuwatengenezea mambo yao.

Na mnakula mirathi kula kwa pupa: Mirathi ni mali inayogura kutoka kwa maiti kwenda kwa warithi wake. Mali nyingi zinazorithiwa huwa mna haki maalum kwa mwenye kuomba na anayejizuia, lakini warithi wanawanyima wenye haki hiyo.

Na mnapenda mali kupenda sana; iwe mirathi au isiyokuwa mirathi; ya halali au haramu.

Si hivyo! Haitakikanii kwa mtu kuifanyia ubahili mali katika njia ya heri; kwa sababu yeye ataulizwa hilo, siku ardhi itakapopandwa pond­wa.

Kukaririka neno kupondwa ni kufuatana yaani kupondwa baada ya kupondwa. Maana ni kuwa kani mvutano itaondoka siku ya Kiyama. Kwa hiyo sehemu moja itaiponda nyingine na utafululiza mpondano mpaka yaharibike yote yaliyo katika ardhi; ikiwemo milima na majengo.

Umetangulia mfano wake katika Juz. katika Juz. 29 ( 69:14).

Na akaja Mola wako na malaika safu safu.

Kuja Mola wako ni kuja amri yake, kadhaa yake, utukufu wake, hukumu yake na utawala wake. Safu safu yaani safu mbali mbali

Na ikaletwa siku hiyo Jahannam.

Itaonekana waziwazi na kuwa katika ulimwengu wa kuonekana baada ya kuwa katika ulimwengu wa ghaibu.

Siku hiyo atakumbuka mtu, lakini kutamfaa nini kukumbuka. Atasema: Laiti ningeliutangulizia uhai wangu.

Waonyaji na watoa nasaha walimwambia mkosefu mwenye jeuri: fanya kwa ajili ya maisha yako ya Akheraa hapa duniani. Akasema Akhera gani? Ni njozi na mawazo tu! Lakini itakapofika siku ya upambanuzi na kuona mahali pake katika Jahannam atasema: haya ndio maisha yangu ya kubakia na makazi ya daima. Kumbe maisha ya dunia yalikuwa ni ya kupi­ta tu, lakini ningeliyatengenezea ya kubakia kwenye yanayopita. Alisahau Akhera alipokuwa duniani kunakofaa toba na ukumbusho; anakumbuka akiwa akhera kutamfaa nini kumbuka.

Basi siku hiyo hataadhibu adhabu yake yoyote, wala hatafunga kufun­ga kwake yoyote.

Pia imesomwa kwa Maf’ul; kwa maana hataadhibiwa na hatafungwa. Maana ya visomo vyote viwili ni kuwa adhabu mbaya zaidi duniani ni nafuu ikilinganishwa na adhabu ya chini Akhera.

Ewe nafsi iliyotua! Rejea kwa mola wako hali yakuwa radhi umerid­hiwa. Basi ingia katika waja wangu na ingia katika Pepo yangu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja nafsi inayoamrisha uovu ambayo haitulii isipokuwa kwa masilahi yake na hawaa yake, sasa anata­ja nafsi iliyotulia, kuwa ni ile ambayo imemwamini Mwenyezi Mungu, ikasikiliza kwa makini mawaidha yake, ikatumia amri yake na makatazo yake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameibanisha nafsi hii kwa kauli yake:

الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ طُوبَىٰ لَهُمْ وَحُسْنُ مَآبٍ {29}

“Wale ambao wameamini na wakafanya mema, raha ni yao na marejeo mazuri.” Juz. 13 (13-29).

Maana ya kuridhia na kuridhiwa ni kuwa itashukuru ujira wake na nafasi yake mbele ya Mwenyezi Mungu kwa sababu ameyashukuru mahangaiko yake na amali yake.

Sheikh Muhammad Abduh anasema katika maana ya kurejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuingia katika waja wake. “Kurejea kwa Mwenyezi Mungu ni kufananisha takrima kwake; vinginevyo Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi popote tulipo. Na kuingia katika waja wake ni kuwa miongoni mwao. Na waja wanaostahiki kuwa miongoni mwao ni wale wenye takua wenye kutukuzwa.”