read

Sura Ya Tisini: Al-Balad

Imeshuka Makka Ina Aya 20.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.

لَا أُقْسِمُ بِهَٰذَا الْبَلَدِ {1}

Naapa kwa mji huu!

وَأَنْتَ حِلٌّ بِهَٰذَا الْبَلَدِ {2}

Nawe unaukaa mji huu.

وَوَالِدٍ وَمَا وَلَدَ {3}

Na kwa mzazi na alichokizaa!

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنْسَانَ فِي كَبَدٍ {4}

Hakika tumemuumba mtu katika tabu.

أَيَحْسَبُ أَنْ لَنْ يَقْدِرَ عَلَيْهِ أَحَدٌ {5}

Je, anadhani kuwa hapana yeyote atakayemuweza?

يَقُولُ أَهْلَكْتُ مَالًا لُبَدًا {6}

Anasema nimeteketeza chun­gu ya mali.

أَيَحْسَبُ أَنْ لَمْ يَرَهُ أَحَدٌ {7}

Je, anadhani kuwa hapana yeyote anayemuona?

أَلَمْ نَجْعَلْ لَهُ عَيْنَيْنِ {8}

Je, hatukumpa macho mawili?

وَلِسَانًا وَشَفَتَيْنِ {9}

Na ulimi na midomo miwili?

وَهَدَيْنَاهُ النَّجْدَيْنِ {10}

Na tukambanishia njia mbili?

فَلَا اقْتَحَمَ الْعَقَبَةَ {11}

Basi mbona hakujitoma njia nzito.

وَمَا أَدْرَاكَ مَا الْعَقَبَةُ {12}

Nini la kukujulisha ni ipi hiyo njia nzito?

فَكُّ رَقَبَةٍ {13}

Ni kumwacha huru mtumwa;

أَوْ إِطْعَامٌ فِي يَوْمٍ ذِي مَسْغَبَةٍ {14}

Au kumlisha siku ya njaa.

يَتِيمًا ذَا مَقْرَبَةٍ {15}

Yatima aliye na udugu.

أَوْ مِسْكِينًا ذَا مَتْرَبَةٍ {16}

Au maskini hohe hahe.

ثُمَّ كَانَ مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ وَتَوَاصَوْا بِالْمَرْحَمَةِ {17}

Kisha akawa miongoni mwa walioamini na wakatenda mema, wakausiana kusubiri na wakausiana kuhurumiana.

أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ الْمَيْمَنَةِ {18}

Hao ndio watu wa kuliani.

وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِنَا هُمْ أَصْحَابُ الْمَشْأَمَةِ {19}

Na wale waliozikana ishara zetu, hao ndio watu wa kushotoni.

عَلَيْهِمْ نَارٌ مُؤْصَدَةٌ {20}

Juu yao ni moto uliokomewa.

Maana

Naapa kwa mji huu.

Herufi la hapa ni kama ya Juz 27 (52:75) na katika Juzuu hii tuliyo nayo (81:15). Makusudio ya mji hapa ni Makka yenye kutukuzwa kwa nyumba tukufu zaidi iliyowekewa watu, yenye kubarikiwa, na kwa utukufu wa Nabii aliyezaliwa humo na kutumwa kuwa rehema kwa walimwengu.

Nawe unaukaa mji huu.

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad (s.a.w.) kwa hiyo kiapo cha kuapia na Makka kimefungwa na ukaaji wa Mtume hapo, kujulisha kuwa Makka imezidi utukufu kwa kuzaliwa kwake na kukaa kwake.

Sheikh Muhammad Abduh amechagua kauli ya anayesema kuwa neno Hillu hapo ni kwa maana ya kuhalalishiwa; yaani watu wa Makka wali­halalisha kumuudhi Mtume katika mji wa amani, mpaka akalazimika kuu­toka.

Maana haya yenyewe ni sahihi, lakini yako mbali na ufahamisho wa tamko. Kwa sababu linalokuja haraka kwenye ufahamu ni kukaa sio kuhalalishiwa.

Na kwa mzazi na alichokizaa.

Jamaa katika wafasiri wamesema makusudio ya mzazi ni Adam na ali­chokizaa ni kizazi chake; kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hakusema na aliyemzaa, ili kuashria utukufu wa shani wa aliyezaliwa, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Juz:

 وَاللَّهُ أَعْلَمُ بِمَا وَضَعَتْ {36}

“Na Mwenyezi Mungu anajua sana aliyemzaa.” (3:36).

Wengine akiwemo Ibn Abbas, abariy na Sheikh Muhammad Abduh wanasema makusudio ya mzazi na kilichozaliwa ni kila kitu, awe mtu, mnyama au mmea. Kauli hii iko karibu na dhahiri ya tamko kuliko nyingine. Ama lengo la kuapa kwa mzazi na alichokizaa ni kutambulisha kuanzishwa viumbe hai na kukua kwake kutoka umbo moja hadi jingine; kuanzia tone la manii kwa mtu au mnyama na punje kwa miti na mimea mingineyo.

Hakika tumemuumba mtu katika tabu na mashaka.

Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameuumba mtu apambane na mapendeleo yake na matakwa yake pamoja na mapambano ya maisha na shida zake; kisha baada ya hapo apambane na uchungu wa mauti, giza la kaburini na upweke, hatimaye kwenye vituko vya Kiyama na kwenda mbele ya Mola kwa ajili ya hisabu ya aliyoyafanya na kuyatenda.
Je, anadhani kuwa hapana yeyote atakayemuweza?

Anayedhani ni mtu kwa kuzingatia baadhi yake sio wote. Maana ni kuwa baadhi ya watu wanadhani kuwa wana nguvu za kutosha kumzuia yeyote vyovyote atavyokuwa na kusahau kwamba wao ni viumbe dhaifu wanaoumizwa na chawa na kufa kwa kupaliwa; kama asemavyo Imam Ali (a.s).

Anasema nimeteketeza chungu ya mali.

Mfumo wa maneno unafahamisha kuwa anayesema hivyo ni tajiri aliyetoa mali yake kwa kutaka umashuhuri na kuzungumzwa vizuri, huku akijizuia kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu ya heri. Maana ni kuwa akiambiwa mbadhirifu huyu, kwa nini hutoi katika njia ya Mwenyezi Mungu? Atasema nimetoa nyingi sana mpaka inakurubia mali yangu kuisha, lakini sitoi kwa njia mnayonitakia.

Je, anadhani kuwa hapana yeyote anayemuona.

Je, anadhani huyu mwenye kufitiniwa na umashuhuri kwamba Mwenyezi Mungu ameghafilika naye na matendo yake na malengo yake. Kuna hadith isemayo. “Kesho mtu ataulizwa kuhusu mwili wake alivyoutumia na umri wake alivyo umaliza na mali yake alivyoichuma na alivyoitumia.”

Je, hatukumpa macho mawili na ulimi na midomo miwili na tukam­banishia njia mbili?

Katika Tafsir Ar-Razi, kuna maelezo kuwa aliyesema nimeteketeza chun­gu ya mali, vile vile alisema kwa lugha ya maneno au ya kimazingira kuwa ni nani anayenihisabu na mali yangu nikiizuia au nikiitoa? Ndio Mwenyezi mungu (s.w.t) akamjibu. Atakuhisabu yule aliyekupa viungo hivi.

Hii iko karibu sana na hali ilivyo. Vyovyote iwavyo ni kuwa macho maw­ili ni ishara ya neema ya kuona, na ulimi ni neema ya kusema na kubain­isha, na uongofu ni neema ya akili na ufumbuzi.

Makusudio ya njia mbili ni njia ya heri na shari. Kwa akili mtu anajihad­hari na hili na kufuata lile. Anasema kwenye ahjul-balagha: “Inakutosha kuwa una akili, kwamba imekuwekea wazi njia ya kupotea kwako na kuongoka kwako.”

Umetangulia mfano wake katika Juz. 29 (76:3).

Basi mbona hakujitoma njia nzito, nini la kukujulisha ni ipi hiyo njia nzito?

Neno njia nzito tumelitoa kwenye neno Aqaba lenye maana ya njia ngumu kwenye milima. Makusudio yake hapo ni matendo mema, kwa sababu yanahitajia juhudi, subira juu ya mashaka na kudhibiti mapendeleo; hasa kutoa mali katika njia ya heri.

Miongoni mwa matendo mema au yaliyo muhimu ni kumwacha huru mtumwa au kumlisha siku ya njaa yatima aliye na udugu au masikini hohe hahe. Kisha akawa miongoni mwa waliaoamini na wakatenda mema, wakausiana kusubiri na wakausiana kuhurumumiana.

Kuusina kusbiri ni kuusiana waumini kusubri kwenye jihadi ili kuithibitisha haki na kukataa kusalimu amri kwenye batili. Na kuusiana kuhurumian ni kusaidiana na kumpendelea mtu ndugu yake lile analolipen­delea kwa nafsi yake.

Ujumla wa maana nikuwa yule aliyetoa mali yake kwa kutaka umashuhuri, hakupita njia nzito na vikwazo vilivyo baina yake na kuokoka na adhabu na maangamizi, bali yeye ndiye mwenye hasara zaidi na mwingi zaidi wa adhabu.

Lau kama yeye angelitoa katika njia ya Mwenyezi Mungu na akawa katika walioamini na akausiana kusubiri na kuhurumiana, basi angelipituka hiyo njia nzito na kuwa katika amani ya ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Hao ndio watu wa kuliani.
Hao ni hao walioamini wakatoa na kuusiana. Watu wa kuliani ni watu wema ambao kesho watapewa maandishi ya wema na amani kwa mikono yao ya kulia.

Na wale waliozikana ishara zetu hao ndio watu wa kushotoni juu yao ni moto uliokomewa.

Watu wa kushotoni ni watu waovu ambao watapewa maandishi ya uovu na kiza kwa mikono yao ya kushoto na nyuma ya migongo yao, na watawek­wa kwenye Jahannam makundi makundi, wakifika wanafunguliwa milan­go wakishaingia wanafungiwa kwa muda usiokuwa na kikomo.