read

Sura Ya Tisini Na Mbili: Al-Layl

Imeshuka Makka Ina Aya 21.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

وَاللَّيْلِ إِذَا يَغْشَىٰ {1}

Naapa kwa usiku unapofuni­ka!

وَالنَّهَارِ إِذَا تَجَلَّىٰ {2}

Na kwa mchana unapofunuli­wa!

وَمَا خَلَقَ الذَّكَرَ وَالْأُنْثَىٰ {3}

Na kwa kuumba kiume na kike!

إِنَّ سَعْيَكُمْ لَشَتَّىٰ {4}

Hakika mahangaiko yenu ni mbali mbali.

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ {5}

Basi Mwenye kutoa na akawa na takua.

وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَىٰ {6}

Na akalisadikisha jema.

فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَىٰ {7}

Tutamsahilishia wepesi.

وَأَمَّا مَنْ بَخِلَ وَاسْتَغْنَىٰ {8}

Na ama mwenye kufanya ubahili na akatoshelezeka.

وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَىٰ {9}

Na akalikadhibisha jema.

فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَىٰ {10}

Basi tutamsahilishia uzito.

وَمَا يُغْنِي عَنْهُ مَالُهُ إِذَا تَرَدَّىٰ {11}

Itamfaa nini mali yake atakapodidimia?

إِنَّ عَلَيْنَا لَلْهُدَىٰ {12}

Hakika ni juu yetu kuongoza.

وَإِنَّ لَنَا لَلْآخِرَةَ وَالْأُولَىٰ {13}

Hakika ni wetu mwisho na mwanzo.

فَأَنْذَرْتُكُمْ نَارًا تَلَظَّىٰ {14}

Basi ninawaonya na moto unaowaka!

لَا يَصْلَاهَا إِلَّا الْأَشْقَى {15}

Hatauingia isipokuwa muovu mno.

الَّذِي كَذَّبَ وَتَوَلَّىٰ {16}

Ambaye amekadhibisha na kupa mgongo.

وَسَيُجَنَّبُهَا الْأَتْقَى {17}

Na ataepushwa nao mwenye takua.

الَّذِي يُؤْتِي مَالَهُ يَتَزَكَّىٰ {18}

Ambaye anatoa mali yake kwa kujitakasa.

وَمَا لِأَحَدٍ عِنْدَهُ مِنْ نِعْمَةٍ تُجْزَىٰ {19}

Wala hapana yeyote aliyem­fanyia hisani ili alipwe.

إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِ الْأَعْلَىٰ {20}

Isipokuwa ni kwa kutaka radhi ya Mola wake aliye juu kabisa.

وَلَسَوْفَ يَرْضَىٰ {21}

Na hakika ataridhia

Maana

Naapa kwa usiku unapofunika na kwa mchana unapofunuliwa

Kiapo hiki ni kama cha sura iliyopita. Huko tumemebainisha kwamba lengo la kuapa kwa mwanga na giza ni kutanabahisha manufaa yake.

Na kuwa kuumba kiume na kike.

Hii ni kwa kila kiumbe hai; awe mtu, mnyama au mmea. Na kwa kuumba huko ndio kunapatikana kizazi na kuendelea maisha

Hapa kuna maswali yanayojitokeza:

Ni nani aliyefanya kuwe na uhai kwenye ulimwengu huu? Ni nani aliye­andaa uhai kwa wadhifa wa kizazi? Kwa nini anayezaliwa mara anakuwa wa kiume na mara nyingine wa kike, na hali chimbuko lao ni moja tu? Je, mada pofu ndiyo iliyofanya yote haya kwa mpangilio, au ni kwa upande wa sadfu?

Je, ilimu imeweza kugundua kuwa mada moja inakuwa ni sababu ya hali mbali mbali bila ya kuingiliana na vitu vingine? Au tusema ni sadfa? Sadfa nayo ni juhudi ya kushindwa.
Kwa hiyo hakuna jibu lililobaki isipokuwa kuweko mpangiliaji mwenyye ujuzi anayepanga kulingana na hikima ya hali ya juu na nidhamu kamili.

Hakika mahangaiko yenu ni mbali mbali.

Hili ndilo jawabu la kiapo. Maana ni kuwa katika matendo ya mtu kuna ya kheri na ya makosa.

Unaweza kuuliza kuwa kadhia hili ni la kimsingi halihitaji kiapo; kwanini Mwenyezi Mungu (s.w.t) akalisisitiza kwa kiapo?

Jibu: Ndio, nikweli kuwa mahangaiko yenu ni mbali mbali, ni kadhia lililo wazi hilo lenyewe tu, bila ya kuangalia mwisho na natija yake, lakini kama tukiangalia yale yanayofungamana nalo; kama kufanyiwa wepesi mwema na kufanyiwa uzito muovu na mengine mfano wake, hapa itahitajika msisitizo au angalau tuseme hakuna kizuizi cha msisitizo.

Yanayoapiwa hapa ni kuanzia Aya hii tuliyo nayo na zinazofuatia ambazo ni:

Basi Mwenye kutoa katika njia ya heri kwa ajili ya heri na akawa na takua; kwa kujiweka mbali na mambo ya haramu na madhambi. Na akalisadikisha jema yaani akaamini Pepo na Mto, halali na haramu na akafanya kwa mujibu wa imani yake, vinginevyo imani yake itakuwa ni sarabi, kwa sababu imani ni nyezo ya kufikia kwenye lengo na wala sio lengo lenyewe. Basi huyo tutamsahilishia wepesi.

Wametofautiana wafasiri katika maana ya wepesi, kuna anayesema kuwa ni Pepo, mwingine akasema ni heri, na Sheikh Muhammad Abduh akase­ma: “ni mkakati wa kuikamilisha nafsi na kuikuza kwenye ukamilifu.”

Ama sisi tunafasiri wepesi hapa kwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na anayemcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea.” Juz. 28 (65:4) Yaani atampa msaada wake na atampa tawfiki kwenye lile lililo na heri yake na masilahi yake.

Na ama mwenye kufanya ubahili wa kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, na akatoshelezeka kwa mali yake bila ya kutaka msaada wa Mwenyezi Mungu, akaicha Akhera yake kwa dunia yake, Na akalikad­hibisha jema kwa kusema kuwa hakuna Pepo wala Moto wala halali au haramu, basi tutamsahilishia uzito.

Makusudio ya uzito hapo ni kuingia katika uovu na upotovu. Dalili ya kukusudiwa maana haya ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu inay­ofuatia: ‘Atakapodidimia.’

Makusudio ya kufanyiwa wepesi uzito ni kumwacha na hawa yake wala hakatazwi kwa nguvu yale anayojichagulia mwenyewe ya kudidimia na kuangamia.

Itamfaa nini mali yake atakapodidimia?

Pia inawezekana kufasiriwa: Haitafaa mali yake atakapodidimia.

Makusudio ya kudidimia ni kuanguka kwenye shimo la uchafu na maovu.

Muhtasari wa Aya hizi kuanzia: Ama mwenye kutoa, mpaka, atakapo­didimia, ni kwamba desturi ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake ni kubainishia njia mbili, ya wema na ya ufisadi, na kuwapa uwezo wa kufu­ata njia yoyote katika hizo mbili au kuacha yoyote, kisha anamchukulia kila mmoja kwa lile alilojichagulia yeye mwenyewe.

Akiathrika na heri na wema, basi humwingiza kwenye tawfiki yake na msaada wake, na akijich­agulia shari na ufisadi hukaa mbali naye na kumwachia nafsi yake na hawa yake imwongoze kwenye shida na maangamizi.

Hakika ni juu yetu kuongoza.

Hili ni jawabu la swali la kukadiria ambalo vipi Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamwachia muovu na kumwakilishia nafsi yake na hawa yake? Je, hii haipingani na upole wake na rehema yake?

Ndio akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwamba lililo wajibu kwake ni kumpa mja uwezo wa kutenda na akili ya kupambanua kheri na shari, kisha anambainishia, kumwongoza, kumbashiria na kumuonya. Haya yote yamekamilika kwa ukamilifu, nayo ni ukomo wa upole na huruma.

Ama kufanya amali na kuongoka ni juu ya mja mwenyewe peke yake; wala Mwenyezi Mungu hamlazimishi, kwani kulazimisha kunampokonya mtu uhuru na utashi wake, bali hata na utu wake. Kwa sababu mtu ni kwa uhuru wake na matakwa yake.

Neno juu yetu hapo linajulisha wajibu, kinyume na Sheikh Muhammad Abduh na wengineo katika Ashaira. Kwa sababu wajibu ukinasibishwa kwa mtu, maana yake ni kuwa kuna mwingine aliyemwajibishia na kama akiacha kutekeleza ataulizwa. Na ukinasibishwa kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, maana yake ni kuwa yeye mwenyewe amejiwajibishia; yaani kwamba yeye ameahidi na ahadi yake haivunji; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema Juz:

كَتَبَ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ۚ {12}

“Amejilazimishia rehema” 7 (6:12).

Hakika ni wetu mwisho na mwanzo.

Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mfalme wa wafalme, duniani na Akhera wala hana manufaa yoyote kwa twaa ya mtiifu au uasi wa muasi; wala waasi hawatapata pa kuponyokea utawala wake.

Basi ninawaonya na moto unaowaka.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameamrisha akakataza na akahadharisha mwenye kuasi na moto unaowaka ili atubie na kurejea kwa Mola wake.

Hatauingia isipokuwa muovu mno, ambaye amekadhibisha na kupa mgongo.

Imesemekana kuwa muovu mno hapa ni kafiri, Sheikh Muhammad Abduh anasema:” Muovu mno ni yule aliye muovu zaidi ya mwengine.” Usahihi ni kuwa uovu zaidi sio makusudio kwa upande wa kuingia motoni, kwa sababu hakuna muovu yeyote ila atauonja:

فَأَمَّا الَّذِينَ شَقُوا فَفِي النَّارِ لَهُمْ فِيهَا زَفِيرٌ وَشَهِيقٌ {106}

“Ama wale waovu watakuwa motoni watachachatika na kukoroma.” Juz. 12 (11:106).

Tofauti ya muovu na muovu mno iko katika uchungu wa adhabu na shida yake si katika asili ya adhabu. Kwa hiyo itakuwa makusudio ya muovu mno hapa ni yule aliyemuasi Mwenyezi mungu na akaipinga amri yake; ni sawa awe ameipinga kwa vile hamwamini Mwenyezi Mungu na sharia yake, au anamwamini, lakini akazembea na kupuuza.

Hakuna tofauti baina ya wawili hawa, kwa sababu imani ni nyenzo na wala si lengo. Imethibiti kwa nukuu ya Qur’an kwamba mwenye kuamini bila ya maten­do yuko sawa na kafiri. Mwenye Mungu Mtukufu anasema:

 لَا يَنْفَعُ نَفْسًا إِيمَانُهَا لَمْ تَكُنْ آمَنَتْ مِنْ قَبْلُ أَوْ كَسَبَتْ فِي إِيمَانِهَا خَيْرًا ۗ {158} 

“Basi mtu haitamfaa imani yake ambaye hakuamini zamani, au hakuchu­ma kheri kwa
imani yake.” Juz. 8 (6:158).

Na ataepushwa nao mwenye takua.

Maana ya kuepushwa nao ni kujitanibu na sababu zinazopelekea huko; ambazo ni maharimisho ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo makusudio hapa ni mwenye mwenye takua.

Ambaye anatoa mali yake kwa kujitakasa.

Yaani anatoa mali yake katika njia ya kheri ili kuitwaharisha nafsi yake na madhambi na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu; wala hatoi kwa umashuhuri na kujitukuza au kwa biashara na ria.

Wala hapana yeyote aliyemfanyia hisani ili alipwe.

Mara nyingine hisani inakuwa kwa msukumo wa umashuhuri na kujionye­sha, au kwa kulipa hisani uliyofanyiwa; kama kumpa aliyekufanyia wema kwa kumlipa wema wake. Pia inaweza kuwa kutoa ni kwa njia ya nipe nikupe; kama wafanyavyo wanasiasa kwenye miradi ya heri na mingineyo, siku za uchaguzi ili apate kura. Mumin hakusudii hayo wala mengine isipokuwa ni kwa kutaka radhi ya Mola wake aliye juu kabisa, kwa kutaka thawabu zake na kuhofia adhabu yake:

إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّهِ لَا نُرِيدُ مِنْكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا {9}

“Hakika tunawalisha kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu tu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani.” Juz. 29 (76:9).

Na hakika ataridhia.

Mwenyezi Mungu atampa mwenye kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kila analoliridhia na zaidi ya alivyokuwa alifikiria na kutarajia.

Imesemekana kuwa atakayeridhia ni Mwenyezi Mungu sio mwenye takua. Maana ni moja katika makadirio yote mawili, kwa sababu Mwenyezi Mungu akimridhia mja wake na mja naye huwa radhi.

Sheikh Muhammad Abduh anasema kuwa wafasiri wamepokea sababu za kushuka Aya na kwamba Aya hizi zilishuka kwa ajili ya Abu Bakr. Ukipatikana usahihi wa hilo hakuna cha kutuzuia kulisadiki hilo, lakini maana ya Aya bado ni ya ujumla.