read

Sura Ya Tisini Na Mmoja: Ash-Shams

Imeshuka Makka Ina Aya 15.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

وَالشَّمْسِ وَضُحَاهَا {1}

Naapa kwa Jua na mwangaza wake!

وَالْقَمَرِ إِذَا تَلَاهَا {2}

Na kwa mwezi unapolifuatia!

وَالنَّهَارِ إِذَا جَلَّاهَا {3}

Na kwa mchana unapolidhi­hirisha!

وَاللَّيْلِ إِذَا يَغْشَاهَا {4}

Na kwa usiku unapolifunika!

وَالسَّمَاءِ وَمَا بَنَاهَا {5}

Na kwa mbingu na kuzijenga kwake!

وَالْأَرْضِ وَمَا طَحَاهَا {6}

Na kwa ardhi na kuitandaza kwake!

وَنَفْسٍ وَمَا سَوَّاهَا {7}

Na kwa nafsi na kuilingan­isha kwake!

فَأَلْهَمَهَا فُجُورَهَا وَتَقْوَاهَا {8}

Akaifahamisha uovu na takua yake.

قَدْ أَفْلَحَ مَنْ زَكَّاهَا {9}

Hakika amefaulu aliyeitakasa.

وَقَدْ خَابَ مَنْ دَسَّاهَا {10}

Na amepata hasara aliyeitweza.

كَذَّبَتْ ثَمُودُ بِطَغْوَاهَا {11}

Thamud walikadhibisha kwa kupituka kwao mipaka.

إِذِ انْبَعَثَ أَشْقَاهَا {12}

Alipofanya haraka muovu wao zaidi.

فَقَالَ لَهُمْ رَسُولُ اللَّهِ نَاقَةَ اللَّهِ وَسُقْيَاهَا {13}

Akawaambia Mtume wa Mwenyezi Mungu: Mhadharini ngamia wa Mwenyezi Mungu na
kiny­waji chake.

فَكَذَّبُوهُ فَعَقَرُوهَا فَدَمْدَمَ عَلَيْهِمْ رَبُّهُمْ بِذَنْبِهِمْ فَسَوَّاهَا {14}

Wakamkadhibisha na wakamchinja Mola wao akawangamiza kwa sababu ya dhambi zao na akaifanya sawa.

وَلَا يَخَافُ عُقْبَاهَا {15}

Wala haogopi mwisho wake.

Maana

Katika Sura hii Mwenyezi mungu (s.w.t.) ameapa kwa mwangaza, giza, nyota za mbingu na mpangilio wake, ardhi na utandao wake na nafsi na maandalizi yake. Ameapa na yote hayo, kwamba mwenye takua ndiye mwenye faida na mwenye hatia ndiye mwenye hasara; ufafanuzi ni huu ufuatao:

Naapa kwa Jua na mwangaza wake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameapa kwa jua liwe limejitokeza au limejificha kwa sababu ni kiumbe adhimu, vile vile ameapa kwa mwangaza wake.

Na kwa mwezi unapolifuatia hilo jua.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameaapa kwa mwezi unapoambatana na mwan­ga wake na wa Jua pale linapokosekana giza baina yake. Hilo linakuwa katika masiku meupe mwezi 13,14 na 15.

Na kwa mchana unapolidhihirisha hilo jua.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaapa kwa mchana ambao unalidhihirisha jua wazi wazi. Lengo la kupa kwa mwanga wa mchana ni kutanabaisha faida zake kubwa ili tumshukuru Mwenyezi Mungu na kumsifu.

Na kwa usiku unapolifunika hilo jua.

Mwenyezi Mungu ameaapa kwa usiku wakati unapofunika mwanga wa jua bila ya kubakia athari yake, si moja kwa moja kama ilivyo kwa mchana, wala kwa mwanga wa mwezi unaotokana na jua.

Na hilo linakuwa katika usiku wa kwanza au wa mwisho au kila mwezi mwan­damo pale ambapo mwezi hauonekani kwa macho au unaonekana kwa udhaifu. Usiku una manufaa kama mchana; miongoni mwa manufaa ya usiku ni utulivu na raha.

Na kwa mbingu na kuzijenga kwake.

Herufi Ma hapa ni ya Masdariya. makusudio ya kujenga ni yaliyomo ndani yake; zikiwemao nyota zinazoelea kwenye falaki zake na kushikama na kwa kuunganishwa na kani mvutano.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 27 (51:47) na (51:6).

Vile vile kwenye Juzuu hii tuliyo nayo (38:12).

Na kwa ardhi na kuitandaza kwake.

Mahali pengine Mwenyezi Mungu anasema: “Na baada ya hapo akaitandika ardhi. (79:30). Kuitandaza na kuitandika yote ni maana moja.

Nafsi Na Usawa Wake

Na kwa nafsi na kuilinganisha kwake .

Nafsi ni kitu ambacho kinamfanya mtu awe mtu na mnyama kuwa mnya­ma Hatujui uhakika hasa wa kitu hiki; bali tunaona athari yake; kama vile kukua, harakati, kusikia, kuona, kuhisi uchungu kwa mtu au mnyama. Pia elimu ya mtu kwa ujumla.

Makusudio ya nafsi hapa ni nafsi ya mtu, kutokana na kauli yale Mwenyezi Mungu Mtukufu. Akaifahamisha uovu na takua yake, kwa sababu uovu na takua ni katika sifa za mtu sio mnyama.

Kwa hiyo maana ya kulinganisha sawa nafsi ya mtu ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.a.w.t) ameiumbia maandalizi kamili ya kufanya heri na shari kwa nguvu sawa; kisha akaikataza shari na akaiamrisha heri. Linalotujulisha kukusudiwa maana haya ni kauli yake Mwenyezi Mungu.

إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا {3}

“Hakika tumemwongoza njia, ama awe ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru.”
Juz 29 (76:3)
.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameumba katika nafsi ya mtu maandalizi ya kufanya uovu na wema kwa pamoja kwa vile mtu anakuwa mtu kwa uhuru wake, utashi wake na uweza wake wa kufanya wema na uovu. Lau upande mmoja ungelizidi mwingine angelikuwa kama unyoya tu kwenye mavumo ya upepo; hastahiki sifa wala shutuma au thawabu na adhabu kutokana na aliyoyafanya na kuyaacha.

Hakika amefaulu aliyeitakasa na amepata hasara aliyeitweza.

Hili ndilo jawabu la kiapo. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.a.w.t) kuapa kwa mwanga, giza mbingu na kujengwa kwake, ardhi na kutandikwa kwake na nafsi na maandalizi yake, baada ya haya sasa anasema kuwa mwenye kuchagua heri badala ya shari. Akaitwaharisha nafsi yake na uchafu wa madhambi, basi huyo atakuwa amefuzu na kupata takua.

Na mwenye kuichagulia shari na akaichafua kwa madhambi na uovu, basi huyo ni mwenye kupata hasara.

Thamud walikadhibisha kwa kupituka kwao mipaka.

Yaani walimkadhibisha mtume wao Swaleh. Thamud ni jina la kabila.
Alipofanya haraka muovu wao zaidi.

Yaani alifanya haraka kumchinja ngamia. Muovu huyu huwa anapigiwa mfano kwa uovu wake tangu maelfu ya miaka.

Akawaambia mtume wa Mwenyezi Mungu mhadharini ngamia wa Mwenyezi Mungu na kinywaji chake.

Mtume wa Mwenyezi Mungu ni Swaleh; ngamia wa Mwenyezi Mungu ni yule ngamia wa muujiza, na kinywaji chake ni ishara ya kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: ”

Akasema:

 هَٰذِهِ نَاقَةٌ لَهَا شِرْبٌ وَلَكُمْ شِرْبُ يَوْمٍ مَعْلُومٍ {155}

وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَظِيمٍ {156}

“Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalum. Wala msimguse kwa ubaya isije ikawashika adhabu ya siku kubwa.”
Juz; 19 (26:155-156)
.

Wakamkadhibisha na wakamchinja. Mola wao akawangamiza kwa sababu ya dhambi zao na akaifanya sawa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema wakamchinja na aliyemchinja ni mmoja tu, kwa vile wao waliridhia kitendo chake, bali walimhimiza hasa; kama alivyosema Mwenyezi Mungu“Basi wakamwita mtu wao akaja akamchin­ja.” Juz.27 (54:29). Maana ya kuifanya sawa ni kuwa alivunja majumba yao wote na hakuna aliyepona katika wao, si mkubwa wala mdogo:

وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْكُمْ خَاصَّةً ۖ {25}

“Na jikingeni na fitna ambayo haitawasibu wale waliodhulumu miongoni mwenu peke yao.”
Juz. 9 (8:25)
.

Wala haogopi mwisho wake.

Wafasiri wengi wamesema maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ali­wangamiza Thamud wala haogopi kuangamia kwao.

Wengine wamesema hapa kuna maneno yaliyotangulia na yaliyokuja nyuma, kukadiria kwake ni. alipofanya haraka muovu wao zaidi; wala hakuhofia mwisho wake, Mtume wa Mwenyezi Mungu akawaambia mhadharini ngamia na kinywaji chake. Inawezekana pia kuwa maana yake ni Mwenyezi Mungu hana wa kumpinga wala kumtaaradhi katika jambo lake.

قُلْ إِنَّ الْأَمْرَ كُلَّهُ لِلَّهِ ۗ {154}

“Waambie mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu.” Juz. 4 (3:154).