read

Sura Ya Tisini Na Nane: Al-Bayyina

Imeshuka Makka Ina Aya 8 Imesemekana imeshuka Madina na ikasemekana imeshuka Makka.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

لَمْ يَكُنِ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَالْمُشْرِكِينَ مُنْفَكِّينَ حَتَّىٰ تَأْتِيَهُمُ الْبَيِّنَةُ{1}

Hawakuwa waliokufuru mion­goni mwa Watu wa Kitabu na washirikina ni wenye kuachana na walio nayo mpaka iwajie hoja.

رَسُولٌ مِنَ اللَّهِ يَتْلُو صُحُفًا مُطَهَّرَةً {2}

Mtume atokaye kwa Mwenyezi Mungu awasomee kurasa zili­zotakaswa.

فِيهَا كُتُبٌ قَيِّمَةٌ {3}

Ndani yake mna vitabu vilivy­onyooka.

وَمَا تَفَرَّقَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ إِلَّا مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَةُ {4}

Wala hawakufarikiana waliopewa Kitabu ila baada ya kuwajia hoja.

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ {5}

Nao hawakuamrishwa ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe wanyoofu, na wasimamishe Swala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Dini iliyonyooka.

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَالْمُشْرِكِينَ فِي نَارِ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ أُولَٰئِكَ هُمْ شَرُّ الْبَرِيَّةِ {6}

Hakika waliokufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu na washirikina watakua katika Moto wa Jahannamu wadumu milele humo. Hao ndio viumbe waovu.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَٰئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ {7}

Hakika walioamini na waka­ tenda mema hao ndio bora wa viumbe.

جَزَاؤُهُمْ عِنْدَ رَبِّهِمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۖ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ۚ ذَٰلِكَ لِمَنْ خَشِيَ رَبَّهُ {8}

Malipo yao kwa Mola wao Mlezi ni Bustani za milele, zip­itiwazo na mito chini yake. Wakae humo milele. Mwenyezi Mungu yuko radhi nao, na wao wako radhi naye. Haya ni kwa anayemuogopa Mola wake.

Maana

Hawakuwa waliokufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu na washirik­ina ni wenye kuachana na walio nayo mpaka iwajie hoja.

Makusudio ya watu wa Kitabu ni mayahudi na wanaswara, na washirikina ni waabudu masanamu katika waarabu. Watu wa Kitabu walikuwa wame­soma katika vitabu vyao kwamba Mwenyezi Mungu atapeleka Mtume atakayeongoza kwenye haki. Vile vile washirkina walimsikia Nabii huyu.

Yakawa makundi mawili haya ni kama mfano wa maelewano ya kutumwa Nabii aliyeahidiwa. Mara nyingi ikitokea uhasama baina ya watu wa Kitabu na washirikina, kila kundi likidai lina haki; kisha wanaafikiana kumngojea Nabii aje awaaamue na kwamba akija watamwamini na wata­fuata hukumu yake. Huyo ndiye aliyekusudiwa kuwa ni hoja aliyoibainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kauli yake:

Mtume atokaye kwa Mwenyezi Mungu awasomee kurasa zilizo­takaswa, Ndani yake mna vitabu viliyonyooka.

Makusudio ya Mtume hapa ni Muhammad (s.a.w.); na kurasa ni Qur’an, na ni nyingi kwa kuzingatia Sura zake au kurasa zake. Zilizotakaswa maana yake ni zilizotakaswa na ubatilifu na kupotolewa.
Na makusudio ya vitabu ni kuwa Qur’an ndani yake mna ubainifu mwingi wa aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu katika vitabu vya mbinguni vilivy­otangulia kama vitabu vya Ibrahim, Tawrat, Injil na Zaburi, bali mna ubainifu wa yote yaliyoteremshiwa manabii, ukiwemo mwongozo na misingi ya dini. Makusudio ya kunyooka ni kuwa kwenye njia ya haki.

Maana ni kuwa Muhammad (s.a.w.) alipokuja na Qur’an ambayo ndani yake mna ubainifu wa kila kitu, washirikina na watu wa Kitabu walimpin­ga, na wakavunja ahadi waliyoiweka kuwa watahukumiwa na Nabii aliyeahidiwa.

Wala hawakufarikiana waliopewa Kitabu ila baada ya kuwajia hoja.

Hoja hii iliwajia watu wa Kitabu kupitia kwenye ndimi za manabii wao. Kwa hiyo makusudio ya hoja hii sio ile ya Aya iliyotangulia. Maana ni kuwa watu wa Kitabu waliendelea na upotevu kwa kupinga kwao mwito wa Muhammad (s.a.w.), aliyewajia na hoja waziwazi, kama walivyoende­lea na usafihi na upotevu baada ya manabii wao kuwajia na dalili na hoja.

Na hilo ni kwamba mayahudi waligawanyika kwenye vikundi baada ya kujiwa na Musa, vile vile wanaswara wakagawanyika baada ya Isa. Tofauti sio kuwa ilisababishwa na kutojua dini; isipokuwa hawaa na manufaa ndiyo yaliyowafarikisha.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 4 (3:105) na Juz. 25 (45:17).

Nao hawakuamrishwa ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kum­takasia Dini, wawe wanyoofu, na wasimamishe Swala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Dini iliyonyooka.

Neno unyoofu tumelitoa kwenye neno ‘hunafaa’, lenye maana ya kuwa na msimamo wa haki kwa kuepuka kila batili. Maana ni kuwa watu wa Kitabu walifarikiana katika dini yao pamoja na kuwa dini ya Mwenyezi Mungu ni moja na iko wazi, nayo ni kumfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu peke yake, msimamo wa haki na uongofu, kusimamisha swala na kutoa Zaka. Hii ndio dini ya mbinguni iliyonyooka kwenye njia ya sawa; sasa zimetoka wapi idadi za dini mataifa na madhehebu?

Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Haya ndio anayowasikitikia Mwenyezi Mungu watu wa Kitabu. Je, na sisi tusemeje kuhusu hali yetu? Si Kitabu chetu kinatusikitikia kwa kukushudia ubaya wetu katika kufarikiana kwetu kwenye dini, baada ya kuwa makundi na tukaijaza dini bid’a na uzushi? Tazama Juz. 1 (2:111-113) kifungu cha ‘Waislamu vile vile wanakufurishana.’

Hakika waliokufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu na washirikina watakua katika Moto wa Jahannamu wadumu milele humo. Hao ndio viumbe waovu.

Makusudio ya makafiri hapa ni kila mwenye kuipinga haki iliyo na dalili; ni sawa aipinge kwa inadi baada ya kuijua au kukataa kuitafuta haki na kuichunguza pamoja na dalili zake.

Maulama wa kiislamu wameafikiana kuwa asiyejua na akazembea kuitafuta haki, hukumu yake ni sawa na anayeijua kisha akaiacha kwa makusudi. Hakuna shaka kwamba mwenye kuipinga bila ya sababu za kutosha, huyo ni mshari zaidi katika watu wa ardhini; sawa na aliyemfanyia washirika Mwenyezi Mungu. Hakuna malipo ya huyu na yule isipokuwa fedheha na adhabu.

Hakika walioamini na wakatenda mema, yaani walioiamini haki na wakatenda kwa mujibu wa imani yao, hao ndio bora wa viumbe.

Kila mwenye kuitafuta haki na akaitumia kwa njia ya haki bila ya kuogopa lawama, basi hakuna yeyote aliye bora kumshinda; isipokuwa aliyechag­uliwa na Mwenyezi Mungu kufikisha risala yake na kumwamini na wahyi wake.

Malipo yao kwa Mola wao Mlezi ni Bustani za milele, zipitiwazo na mito chini yake. Wakae humo milele. Mwenyezi Mungu yuko radhi nao, na wao wako radhi naye.

Amewaridhia kwa vile walifanya kwa mujibu wa radhi yake, ndio akawali­pa miliki ya daima; na wao wako radhi naye kwa neema alizowamiminia.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (5:119) na Juz. 11 (9:100).

Hayo ni kwa anayemwogopa Mola wake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemwandalia malipo mema yule anayem­wogopa Mwingi wa rehema, na akawa mkwelii. Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amekusudia kwa matamshi matukufu, kuondoa fikra mbovu iliyoenea, kwamba kiasi cha imani tu ya kurithi kutoka kwa wazazi na kujua baadhi ya dhahiri za hukumu na kutekeleza baadhi ya ibada huwa inatosha kumfanya mtu apate aliy­owaamdalia Mwenyezi Mungu waumini; hata kama moyo umejaa chuki, hasadi, kiburi na ria; na mdomoni kumejaa uwongo, fitina na uzushi; na moyoni kumejaa utumwa.

Hapana! hatapata malipo mema, kwa sababu moyoni mwake hamkuingia hofu ya Mwenyezi Mungu wala nafsi haikuwa safi. Hilo haliwi ila kwa anayemwogopa Mola wake na akihisi hofu ndani ya moyo wake.