read

Sura Ya Tisini Na Nne: Al-Inshirah

Imeshuka Makka Ina Aya 8.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

أَلَمْ نَشْرَحْ لَكَ صَدْرَكَ {1}

Je, hatukukukunjulia kifua chako?

وَوَضَعْنَا عَنْكَ وِزْرَكَ {2}

Na tukakuondolea mzigo wako.

الَّذِي أَنْقَضَ ظَهْرَكَ {3}

Ambao uliuelemeza mgongo wako?

وَرَفَعْنَا لَكَ ذِكْرَكَ {4}

Na tukakunyanyulia utajo wako?

فَإِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا {5}

Basi kwa hakika pamoja na uzito kuna wepesi.

إِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا {6}

Hakika pamoja na uzito kuna wepesi.

فَإِذَا فَرَغْتَ فَانْصَبْ {7}

Basi ukishamaliza jitaabishe.

وَإِلَىٰ رَبِّكَ فَارْغَبْ {8}

Na Mola wako mtake haja.

Maana

Razi anasema: “Imepokewa kutoka kwa Twaus na Umar Bin Abdul-aziz, kwamba Sura hii na Sura Adhuha ni moja na walikuwa wakiisoma katika rakaa moja bila ya kuitenganisha na Bismillah.

Lililowafanya hivyo ni kauli yake Mwenyezi Mungu tukufu: Je, hatukukukunjulia kifua chako? Ni kama inaungana na kauli yake: Je, hakukukuta ni yatima akakuhifadhi?

Mwenye ajamul-bayan anasema: “Wamepokea watu wetu ‧ yaani Shia Imamiya ‧ kuwa hizo ni sura moja kutokana na kufungamana na wamezi­soma pamoja katika rakaa moja, vile vile Sura Fiyl na Quraysh.

Sheikh Almaraghi anasema: “Sura hii ilishuka baada ya Dhuha na ime­fungamana sana nayo.” Mwenye Dhilal anasema: Sura hii imeshuka baada ya Sura Adhuha, kama kwamba inaikamilisha.

Je, hatukukukunjulia kifua chako?

Mtume aliona dhiki sana kutokana na ufisadi wa jamii aliyokuwa akiishi nayo. Akawa hajui afanye nini, huku akitafuta njia ya kuwatengeneza watu wake na kuwaongoza, mpaka aliposhukiwa na Qur’an ikamwangazia njia anayoitaka ‧ kuleta utangamano na wema. Ndipo moyo wake ukatulia na kifua chake kikakunjuka.

Na tukakuondolea mzigo wako, ambao uliuelemeza mgongo wako?

Makusudio ya mzigo unaolemea hapa ni hamu na ghamu yake Mtume kwa ushirikina na upotevu waliokuwa nao watu wake, ndio Mwenyezi Mungu akampa raha Mtume wake kwa Qur’an Tukufu.

Kwa hiyo basi, makusudio ya kukuondolewa mzigo ni sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Je, hatukukukunjulia kifua chako.’ Hakuna tofauti isipokuwa katika mfumo wa maneno na ibara. Lengo ni kuzidisha ufafanuzi na kusisitiza.

Na tukakunyanyulia utajo wako?

Kuna kitu gani cha juu na kitukufu zaidi kuliko kukutanishwa jina la Muhammad na jina la Mwenyezi Mungu na kutiiwa yeye kuwa ndio kuti­iwa Mwenyezi Mungu? Juz. 5 (4:80) na Juz, 22 (33:36).

Basi kwa hakika pamoja na uzito kuna wepesi. Hakika pamoja na uzito kuna wepesi.

Maana yako wazi, ni kuwa baada ya dhiki ni faraji, kwa haraka au kwa kuchelewa. Kwa sababu makusudio ya pamoja hapa ni kusisitiza matu­maini ya kupata wepesi hata kama muda utarefuka, na wala sio kusuhu­biana na kwenda pamoja.

Unaweza kuuliza: Nini makusudio ya kukaririka huku?
Jibu: Hatuoni wajihi wowote zaidi ya kusisitiza kadhia hili katika nafsi na kulimakinisha katika nyoyo, kwani watu wengi wanakuwa na shaka nalo. Ama riwaya inayosema: Uzito mmoja hautashinda wepesi mbili, tume­ichunguza na tukafahamu kuwa wepesi wa kwanza ni kuondokewa na uzito, lakini hatukufahamu wepesi wa pili. Imesemekana kuwa ni thawabu za Akhera, lakini hii ni mbali ya umbali zaidi wa dhahiri ya tamko na mfumo wa Aya, kwa sababu inazungumzia uzito wa dunia na wepesi wake, si Akhera na thawabu zake.

Vile vile imesemekana kuwa uzito wa pili ndio ule ule uzito wa kwanza, kwa sababu zote mbili zina heruf alif na lam ya jinsi, lakini wepesi umerudiwa bila, ya alifu na lam (nakira), na likirudiwa hivyo neno basi makusudio ya kwanza yanakuwa sio ya pili.

Kauli hii kwa hakika, haina mategemzi ya hoja yoyote isipokuwa ni kucheza na matamshi tu, kwa sababu, kwa mfano ukimwambia unayem­dai: ninakudai shilingi mbili naye akasema: unanidai shilingi moja, unanidai shilingi moja, haina maana kuwa amekubali kuwa unamdai shilingi mbili.

Sheikh Muhammad Abduh amejaribu kutofautisha baina ya uzito, sio wepesi, akasema: Makusudio ya uzito wa kwanza ni ule uzito uliozoeleka. Ama uzito wa pili ni wa kiujumla. Sheikh Muhammad Abduh amerefusha na kubainisha ili kuipa nguvu rai yake, lakini hakuleta kitu cha kutuliza nafsi, kwani linalokuja haraka akilini ni kuwa uzito uliotajwa kwanza ndio ule ule uliotajwa mara ya pili, wala hakuna tofauti baina yake.

Swali la pili: Tumeona watu wengi wanaendelea kuwa na uzito hadi mauti; na hili haliafikiani na mtazamo wa Aya hii; sasa je, kuna wajihi gani?

Jibu: Hukumu katika Aya ni ya kiujumla na uaghlabu, sio kuenea na kuchanganya wote. Zaidi ya hayo ni kuwa inaleta matumaini katika nafsi na kuipa msukumo wa kufanya kwa ikhlasi - jambo ambalo linasaidia kushikamana na Mwenyezi Mungu na kumtegemea Yeye tu.

Basi ukishamaliza jitaabishe.

Yaani ewe Muhammad, ukishamaliza kazi ya kutafuta maisha, jitaabishe na ufanye juhudi kwa ajili ya maisha ya Akhera.

Kuna baadhi ya mamluki walioajiriwa kwa ajili ya kueneza fitna katika madhehebu za kiislamu, wamewazulia Shia Imamiya kuwa eti wanafasiri neno fanswab, tulilolifasiri kwa maana ya jitaabashe, kwa maana ya msi­mamishe Ali kuwa khalifa.

Inatosha kuurudi uzushi huu, yale aliyoyasema mwenye ajmaul-bayan, ambaye ni miongoni mwa masheikh wafasiri katika Shia Imamiya, amese­ma katika kufasiri Aya hii, ninamnuku: “Maana ya neno fanswab ni jitaabishe; usijishughulishe na raha.”

Na Mola wako mtake haja.

Usiuelekeze moyo wako kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, wala usimtake msaada yoyote asiyekuwa Yeye. Mtume (s.a.w.) anasema: “Ukiomba muombe Mwenyezi Mungu, ukitaka msaada mtake msaada Mwenyezi Mungu. Jua kwamba lau watu na majini wataungana kukunufaisha na cho­chote, hawawezi kukunufaisha na chochote ila kile alichokuandikia Mwenyezi Mungu na kama wataungana kukudhuru, basi hawawezi kukud­huru ila kwa kile alichokuandikia Mwenyezi Mungu.”