read

Sura Ya Tisini Na Saba: Al-Qadr

Imeshuka Makka Ina Aya 5.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

إِنَّا أَنْزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ {1}

Hakika tumeiteremsha katika Laylatul Qadri.

وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ {2}

Na nini cha kukujulisha nini Laylatul Qadri?

لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِنْ أَلْفِ شَهْرٍ {3}

Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu.

تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِمْ مِنْ كُلِّ أَمْرٍ {4}

Hushuka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo.

سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ {5}

Ni amani huo mpaka mapam­bazuko ya alfajiri.

Maana

Hakika tumeiteremsha katika Laylatul Qadri,

Iliyoteremshwa ni Qur’an kwa kuingia kwake akilini. Laylatulqadr ni usiku mmojawapo katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kutokana na Hadith nyingi, na pia kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa ndani yake Qur’an.” Juz. 2 (2:185). Tukiunganisha Aya hii na hii tuliyo nayo, natija inakuwa laylatulqadr iko ndani ya mwezi wa Ramadhani.

Kauli zimekuwa nyingi kuhusu tarehe ya usiku huo, kutokana na hadith mbali mbali. Kitabu cha Mwenyezi Mungu kimelinyamazia hilo ili kuhimiza kuyashughulikia masiku yote ya Ramadhani kwa ibada, kama ilivyosemekana.

Kuna riwaya ya Imam Jafar As-Swadiq (a.s.) inayosema kuwa muulizaji alimuuliza kuhusiana na huo, akasema: “Utafute kwenye mwezi 19, 21 na 23,” imekuwa desturi kwa Sunni kuuadhimisha kwenye mwezi 27.

Maajabu niliyoyasoma, kuhusu kuuainisha usiku huu, ni yale yaliyoko kwenye kitabu AhkamulQur’an cha Abu Bakr, aliye maarufu kwa jina la Ibn Al-arabi Almua’firi Al-andalusi Almaliki, ninamnukuu: “Huo ni usiku wa 27, kwa sababu maulama wamehisabu herufi za sura mpaka walipofikia neno ‘huo,’ wakakuta ni 27, ndio wakauhukumia hivyo. Hilo ni jambo lililo wazi na baada ya kulijua ni jepesi, wala hawezi kulifuata ila mwenye fikra ya ukweli na mazingatio ya sawa.”

Wala ugwiji huu katika kutafuta natija na huku kujichunga sana katika kufafanua maneno ya Mwenyezi Mungu kuwa ni jambo jipya kwa yule aliyesema akiongezea juu ya fatwa ya Imam Shafi. Kwa kusema: “Haya ni maneno ya ambaye hajaonja ladha ya fiqh.” Vile vile aliyesema akiongezea fatwa ya Imam Abu Hanifa: “Hii ni fiqh dhaifu.” Tazama Kitabu Ahkamul ur’an Juz. 2 chapa ya 331 AH.

Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Laylatulqadr ni usiku wa ibada, kunyenyekea na kukumbuka neema ya haki na dini, lakini waislamu siku hizi wanazungumza yale ambayo Mwenyezi Mungu hayaangalii kwao, na wanasikiliza kitu katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu bila ya kuchunguza yaliyomo wala kuzingatia maana yake; bali kama watasikiliza basi watazingatia sauti tamu tu ya anayesoma Qur’an, nao wana njozi nyingi, kuhusu laylatulqadr, zisizoingia hata kwenye akili za watoto, sikwambii za watu wazima.”

Wametofautiana kuhusu kushuka Qur’an kwamba ilishuka mara moja kwa ujumla au ilishuka kidogo kidogo? Ilivyo ni kuwa ilishuka kidogo kidogo na kwamba maana ya tumeiteremsha katika aylatulqadr ni kuanza kushu­ka kwake kwenye usiku huo. Hayo tumeayazungumza kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 15 (17:106).

Vile vile wametofautiana kuwa kwanini usiku huu ukaitwa laylatulqadr: kuna waliosema kuwa ni usiku wa makadirio, kwa vile Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anakadiria na kugawanya riziki na muda wa kufa baina ya waja wake katika usiku huu. Kuna aliyesema kwamba makusudio ya neno adr hapa ni cheo na heshima, kwa maana ya usiku wa heshima. Kauli hii iko karibu zaidi na neno adr na inatiliwa nguvu na Mwenyezi Mungu alivy­ousifu usiku huu kuwa ni wa Baraka: “Hakika tumekiteremsha katika usiku uliobarikiwa.” Juz. 25 (44:3).

Baraka ni wema na kukua. Hakuna mwenye shaka kuwa utu unakua na kuwa wema kama utaenda na sera ya Qur’an iliyoteremsha kwenye usiku wa heshima.

Na nini cha kukujulisha nini Laylatul Qadri?

Hii ni kuadhimisha shani yake na utukufu wa cheo chake na kwamba hau­fikiriki.

Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu isiyokuwa na laylatulqadr;

vinginevyo ingelazimika kujiweka chini huo wenyewe. Maana yake ni kuwa mwenye kukesha kwenye aylatulqadri ni kama aliyemwabudu Mwenyezi Mungu kwa miezi elfu moja.

Arrazi anasema: “Aya hii ina bishara kuu na tahadhari kubwa. Bishara ni kuwa Mwenyezi Mungu ametaja kuwa usiku huu ni bora lakini hakubain­isha kiwango cha ubora wake.

Hii ni kama kauli ya Mtume (s.a.w.) kwa Ali (as): kupambana Ali na Amru bin Wudd ni bora kuliko amali ya umma wangu mpaka siku ya Kiyama. Hakusema mfano wa amali yake, bali ame­sema ni bora zaidi; kama kwamba anasema: inatosha hii kuwa ni kipimo vilivyo baki ni vya kubahatisha.”

Hushuka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo.

Tafsiri na kauli zimekuwa nyingi kuhusiana na Aya hizi. Kwanza tutataja maana ya misamiati yake kisha ujumla wa maana.

Neno ‘Hushuka,’ hali­hitaji tafsiri, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakutaja hao malika wanashukia wapi huo usiku wa layalatulqadr? Je, wanashukia kwenye ardhi yetu au nyingineyo? Au mahali popote? Roho ni Jibril. Idhini ya Mola ni amri. Kila jambo ni kila kitu mbinguni na ardhini.

Ujumla wa maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika laylatulqadr anawaamuru Malaika washuke mahali fulani kwa ajili ya kila jambo.

Kama tukiulizwa nini maana ya kwa ajili ya kila jambo? Je, ni kupangilia vitu na mkakati wa mwenendo wake, kuudhibiti au mengineyo? Tutajibu: Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi. Sheikh Muhammad Abduh anasema: “makusudio ni kuwa mwanzo wa Mtume (s.a.w.) kushuhudia malaika ilikuwa usiku wa laylatulqadr.” Kauli hii iko mbali na dhahiri ya tamko.

Ni amani huo mpaka mapambazuko ya alfajiri.

Je, makusudio ya amani mpaka mapambuzo inakuwa katika masiku yote ya laylatulqadr, kwamba hakuna shari wala maafa katika usiku wowote wa laylatulqadr, au amani mpaka mapambuzoko ilikuwa maalum tu ya usiku ulioshukia Qur’an kwenye moyo wa Mtume?

Dhahiri, kutokana na ibara ya wafasiri, ni kuenea kwenye masiku yote ya laylatulqadr. Na kwa ibara ya Sheikh Muhammad Abduh ni kuhusika na usiku ule tu, anasema: “Ulikuwa ni usiku uliosalimika na kila shari na adha…Mwenyezi Mungu alimfariji Nabii wake na akamfungulia njia ya uwongofu akampa yale aliyokuwa anamtakia.”