read

Sura Ya Tisini Na Sita: Al-A’laq

Imeshuka Makka Ina Aya 19.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ {1}

Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba.

خَلَقَ الْإِنْسَانَ مِنْ عَلَقٍ {2}

Amemuumba mtu kwa pande la damu.

اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ {3}

Soma! Na Mola wako ni Karimu zaidi!

الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ {4}

Ambaye amefundisha kwa kalamu.

عَلَّمَ الْإِنْسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ {5}

Amemfundisha mtu aliyokuwa hayajui

كَلَّا إِنَّ الْإِنْسَانَ لَيَطْغَىٰ {6}

Si hivyo! Hakika mtu bila ya shaka hupituka mipaka.

أَنْ رَآهُ اسْتَغْنَىٰ {7}

Kwa kujiona amejitosheleza.

إِنَّ إِلَىٰ رَبِّكَ الرُّجْعَىٰ {8}

Hakika ni kwa Mola wako marejeo.

أَرَأَيْتَ الَّذِي يَنْهَىٰ {9}

Je, umemwona yule anayemkataza.

عَبْدًا إِذَا صَلَّىٰ {10}

Mja anaposwali?

أَرَأَيْتَ إِنْ كَانَ عَلَى الْهُدَىٰ {11}

Je, umeona kama yuko juu ya uwongofu?

أَوْ أَمَرَ بِالتَّقْوَىٰ {12}

Au anaamrisha takua?

أَرَأَيْتَ إِنْ كَذَّبَ وَتَوَلَّىٰ {13}

Je, umeona kama yeye akikanusha na kurudi nyuma?

أَلَمْ يَعْلَمْ بِأَنَّ اللَّهَ يَرَىٰ {14}

Hajui kwamba Mwenyezi Mungu anaona?

كَلَّا لَئِنْ لَمْ يَنْتَهِ لَنَسْفَعًا بِالنَّاصِيَةِ {15}

Si hivyo! Kama hatakoma, tutamburuza kwa nywele za utosi!

نَاصِيَةٍ كَاذِبَةٍ خَاطِئَةٍ {16}

Utosi wa uwongo, wenye makosa!

فَلْيَدْعُ نَادِيَهُ {17}

Basi na awaite wanachama wenzake!

سَنَدْعُ الزَّبَانِيَةَ {18}

Nasi tutawaita Mazabania!

كَلَّا لَا تُطِعْهُ وَاسْجُدْ وَاقْتَرِبْ ۩ {19}

Si hivyo! Usimtii! Nawe suju­du na ujikurubishe.

Maana

Imesemekana kuwa Sura ya mwanzo kumshukia Mtume ni sura A-lfatiha. Kauli hii inanasibiana na na jina la Sura yenyewe (ufunguzi), lakini kauli hii ni nadra. Ikasemekana kuwa ya kwanza kushuka ni Muddathir. Waliosema hivi ni wachache. Wafasiri wengi, wapokezi na ulama wame­sema ya kwanza iliyoshuka ni mwanzo wa Sura hii tuliyo nayo.

Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Imesihi katika Hadith kwamba mwanzo wa malaika aliyekuwa akimpa wahyi ni pale alipomwambia: Soma kwa jina la Mola wako, mpaka kufikia, amemfundisha mtu asiyoya­jua.”

Vyovyote iwavyo lilio wajibu kwa mwislamu ni kuamini pasi na kuwa na shaka kwamba yote yaliyo katika Qur’an ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wala halazimiki kufanya utafiti wa wakati na tarehe ya kushuka Aya. Ambalo halina shaka ni kuwa wahyi ulimshukia Mtume mtukufu (s.a.w.), akiwa na miaka arubaini katika umri wake mtukufu; na kwamba kabla

yake alikuwa akiamini Mungu mmoja bila ya kumshirikisha na chochote, na hakuwa akitetereka hata kidogo katika kumtegemea kwake. Chimbuko la imani hii ni mambo mawili: Kwanza ni dhati ambayo ni akili yake na umbile lake. Pili urithi wa kutoka kwa babu yake Ibrahim Al-Khalil (a.s.).

Mwenye kufuatilia maisha ya Nabii (s.a.w.) na sera yake, atapata ushahi­di mwingi wa kumwamini Mungu mmoja; miongoni mwayo ni kwamba yeye katu hakuwahi kusujudia sanamu udogoni mwake na ukubwani.

Wapokezi wamenukuu kwamba mmoja wa washirikina siku moja, kabla ya kufikia umri wa utu uzima alimwambia: “Ewe kijana ninakuomba kwa Lata na Uzza uniambie jambo fulani.” Muhammad (s.a.w.) akamwambia: “Usiniombe kwa lata na Uzza: Wallah hakuna kitu ninachokichukia kama hivyo viwili.” Na siku nyingine alitofautiana na mshirikina katika jambo fulani, kabla ya utume. Yule mshirikina akamwambia: “Apa kwa Lata na Uzza,” akasema: “Siapi kwa hao katu na mimi nawapinga.”
Vile vile kauli ya mkewe, Bibi Khadija wakati alipomwelezea yaliompata wakati wa kushukiwa na wahyi: Wallah Mwenyezi Mungu hatakuhizi milele, wewe utaunga udugu, utachukua taabu, utawakaribisha wageni na utasaidia upande wa haki’’. Katika ibara hii ya kihistoria. Wallah Mwenyezi Mungu hatakuhizi, inatuonyesha njia isiyo na mjadala wa fikra ya Mungu mmoja ndani ya familia ya Muhammad kabla ya utume. Tumeyanukuu haya kutoka kitabu Adhahiratul ur’aniyya cha Malik bin Nabiy.

Wakati wowote ule, hata wakati wa wajinga, wamepatikana watu waliomwamini Mungu mmoja kwa msukumo wa akili zao na maumbile yao; miongoni mwao ni Waraqa bin Nawfal, Zaid bin Amr, Uthman bin Al-Huwayrith na wengineo. Tazama Juz. 15 (17: 105-111) kifungu cha ‘Wanyoofu.’ Sasa je, itakuwa ni ajabu kwa bwana wa duniani na Akhera na mtukufu wa viumbe kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho, kuongoka kwa akili yake kwenye Mungu mmoja Mwenye nguvu?

Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba.

Hii ni Aya ya kwanza kushuka katika Qur’an, kama tulivyoashiria. Hilo linatiwa nguvu na amri ya kuanza kwa jina lake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema aliyeumba, bila ya kutaja alichoumba, kwa ajili ya kuenea, kwamba Yeye ni muumba wa vyote. Maulama wa Kiarabu wanasema: Kutotajwa kinachofanywa kunafa­hamisha kuenea kote.

Unaweza kuuliza: Nabii (s.a.w.) alikuwa hasomi wala haandiki, na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anajua hilo, sasa ilikuwaje kumpa amri ya kuso­ma? Hii sio kukalifisha asiloliweza?

Sheikh Muhammad Abduh amejibu swali hili kwa kusema: “Soma kwa jina la Mola wako ni amri ya kimaumbile ya kukiambia kitu ‘kuwa’ na kikawa na wala sio amri ya taklifa; mfano swali na utoe zaka. Tazama Juz. 1 (2:26-27) kifungu cha ‘Kuumba na kuweka sharia.’ Kwa hiyo maana ni: kuwa msomaji hivi sasa, hata kama hapo mwanzo hukua hivyo, kwani Mwenyezi Mungu ambaye ameumba mbingu na ardhi anaweza kukufanya wewe Muhammad kuwa msomaji bila ya kujifundisha kusoma.

Amemuumba mtu kwa pande la damu,

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kutaja kuwa Yeye ni muumba wa kila kitu, hapa amemhusisha mtu, kwa kumtukuza:

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ {70}

“Hakika tumewatukuza wanaadamu.” Juz. 15 (17:70).

Vile vile kutanabahisha uweza wake mkuu ambao umefanya pande la damu liwe mtu huyu wa ajabu jinsi alivyopangiliwa, ili atoe dalili kwa hilo kuweko muumba mwenye uweza:

أَوَلَا يَذْكُرُ الْإِنْسَانُ أَنَّا خَلَقْنَاهُ مِنْ قَبْلُ وَلَمْ يَكُ شَيْئًا {67}

“Je hakumbuki mtu kwamba tulimuumba kabla na hali hakuwa chochote?” Juz. 16 (19:67)

Soma! Na Mola wako ni Karimu zaidi! Ambaye amefundisha kwa kalamu.

Soma, ni kusisitiza amri ya kwanza. Na Mola wako ni karimu… hii ni jumla nyingine; maana yake ni Mwenyezi Mungu ni mkarimu wala haku­na kiwango cha ukarimu wake; kama ulivyo uweza wake na ilimu yake. Hakuna kitu kinachofahamisha zaidi ukarimu na fadhila yake kuliko kuwa yeye amemtoa mtu kutoka chini-pande la damu-hadi juu, kuandika kwa kalamu ambayo ina faida zisizokuwa na idadi; kama vile kuunganisha yaliyopita na yatakayokuja na kuanganisha mashariki ya ardhi na magharibi yake; hasa baada ya kugunduliwa mtambo wa kuchapisha ambao umefanya ilimu ienee hata kwa vipofu wanaosoma kwa herufi zao. Ulimi unatoa yaliyo moyoni, lakini maneno yanakwenda na upepo. Ndio maana ikasemwa kalamu ni naibu wa ulimi na ulimi ni naibu wa kalamu.

Amemfundisha mtu aliyokuwa hayajui.
Mwenyezi Mungu haitii ilimu moyoni isipokuwa anampa mtu akili ambayo ni chimbuko la ilimu. Akili haina mpaka, si kupanda mwezini wala Mars. Vile vile ilimu, huwa inazidi siku baada ya siku bila ya kikomo.

Wafasiri wameafikiana mpaka kufikia hapa kuanzia Aya ya kwanza ndizo Aya za kwanza kushuka na zilishuka mara moja zote. Ama zilizobakia zil­ishuka baadae

Mali Na Kupituka Mipaka

Si hivyo! Hakika mtu bila ya shaka hupituka mipaka, kwa kujiona amejitosheleza.

Mtu hapa ni kwa kuzingatia aghalabu ya watu. Watu wengi wanatoa ushahidi kwa Aya hii kwamba mtu anajikuza na kudhulumu anapomiliki mali na utajiri. Fikra hii wamekwenda nayo jamhuri ya wafasiri. Anasema Arrazi: “Ni Sura ya kwanza inayosifu ilimu na ya mwisho kuishutumu mali.”

Mwenye ajmaul-bayan anasema: “Yaani mtu akijiona hana haja na Mola wake, kwa sababu ya familia yake, mali yake na chakula chake.” Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Yaani pale anapojihisi yeye mwenyewe bila ya kuangalia yaliyo kabla yake, ambayo ni kufundishwa asiyoyajua.”

Tukiangalia mkusanyiko wa Aya mbili hizi, zikiwa ziko kwenye sentesi moja bila ya kitenganisho kati yake, na hapana budi kuwa na mtazamo huu, tukifanya hivyo maana yatakuwa, mtu hupituka mipaka ya sharia pale anapojiona amejitosheleza kielimu na nyenzo zake; kama vifaa vya upelelezi na viwanda na kumdhulumu aliye chini yake kwa nguvu.

Tafsiri hii, mbali ya kutiliwa nguvu na mfumo wa Aya, lakini pia ndio hali halisi ya sasa anayoishi nayo mtu. Wale walio na ilimu wanajaribu kuu­fanya ulimwengu wote uwanyenyekee wao na ukandamizaji wao, baada ya kuielekeza ilimu kuwa ni natija ya vita na viwanda vya silaha; wamekuwa na silaha zinazoweza kuimaliza dunia yote na vilivyomo ndani yake, kwa masaa machache tu.

Hii ndio tafsiri sahihi ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Kwa kujiona ame­jitosheleza.’ Hata hivyo tuna uhakika ulioenea: “Mtu akijitosheleza, huji­faharisha na kuwa na kiburi, na akifukarika hukata tamaa na kuwa mny­onge.” Lakini hakika ya dhati ya kitu ni jambo jingine na ufahamisho wa tamko na mfumo wa maneno ni jambo jingine.

Hakika ni kwa Mola wako marejeo, usighurike na dunia na mapambo yake ewe mpetuka mipaka, wala pia na ilimu na makombora yake au mali na hadaa yake. Kwa sababu nguvu ya haki inasonga kuliko makombora ya nyuklia. Mapinduzi dhidi ya ukandamizaji na utumwa yaliyotokea India, China na kwengineko, yametoa somo kubwa kwa wenye viwanda vya sila­ha katika Amerika; kisha watarudishwa kwa mjuzi wa ghaibu na dhahiri awaambie yale waliyokuwa wakiyafanya.

Je, umemwona yule anayemkataza mja anaposwali?

Hii ni kumkana kila anayekataza mema kwa njia moja au nyingine.

Je, umeona kama yuko juu ya uwongofu? Au anaamrisha takua?

Niambie kuhusu huyo mpotevu ambaye anakataza mema na kuamrisha uovuje, yuko kwenye haki katika makatazo yake na amri yake?

Je, umeona kama yeye akikanusha na kurudi nyuma? Hajui kwamba Mwenyezi Mungu anaona?

Mpotevu huyu ameikanusha haki na akaipinga; hivi haogopi adhabu ya Mwenyezi Mungu ambaye anajua siri yake na dhahiri yake?

Si hivyo! Kama hatakoma, tutamburuza kwa nywele za utosi! Utosi wa uwongo, wenye makosa!

Waarabu walikuwa wakizingatia kuburuta huku kuwa ni upeo wa idhlali na dharau, kwa sababu ni kwa wanyama si kwa watu. Utosi wa uwongo maana yake ni wa mwenye kusema uwongo. Maana ni akome huyu mpote­vu na upotevu wake, vinginevyo tutamkokota kwa utosi wake kwenda kwenye adhabu ya kuungua.

Basi na awaite wanachama wenzake!

Hapa kuna maneno ya kukadiria kuwa mpotevu na awaite watu wa baraza lake wamzuie na adhabu. Makusudio ya wanachama wenzake ni wasaidi­zi wake na jamaa zake; mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُمْ مِنْ دُونِهِ فَلَا يَمْلِكُونَ كَشْفَ الضُّرِّ عَنْكُمْ وَلَا تَحْوِيلًا {56}

“Sema: Waombeni hao mnaodai badala Yake. Hawawezi kuwaondolea madhara wala kuyabadilisha.”Juz. 15 (17:56) .

Nasi tutawaita Mazabania!

Ambao ni malaika wa adhabu. Neno zabania lina asili ya maana ya kusukuma; yaani malaika watawasukuma wapituka mipaka kwenye moto wa Jahannam.

Si hivyo! Usimtii! Nawe sujudu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake, na ujikurubishe kwa Mwenyezi Mungu kwa vitendo vya kheri; bora yake zaidi ni jihadi.

Mafakihi wamezigawanya sijda kwenye vigawanyo vifuatavyo: Sijda ya Swala iliyozoeleka, sijda ya kusahahu inayotokana na ziada au upungufu katika Swala, sijda ya kushukuru, kwa kupata neema au kuondoka balaa na sijda ya kisomo.

Shia Imamiya wameifanya wajibu sijda ya kisomo katika sura 32, 41, 53 na 96 (Sajda, Hamim Sajda, Najm na A’alaq). Zisizokuwa hizo ni sunna.