read

Sura Ya Tisini Na Tano: At-Tin

Imeshuka Makka Ina Aya 8.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

وَالتِّينِ وَالزَّيْتُونِ {1}

Naapa kwa tini na zaituni!

وَطُورِ سِينِينَ {2}

Na kwa mlima Sinai!

وَهَٰذَا الْبَلَدِ الْأَمِينِ {3}

Na kwa mji huu wenye amani!

لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنْسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ {4}

Hakika tumemuumba mtu katika hali nzuri mno.

ثُمَّ رَدَدْنَاهُ أَسْفَلَ سَافِلِينَ {5}

Kisha tukamrudisha chini ya walio chini!

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَلَهُمْ أَجْرٌ غَيْرُ مَمْنُونٍ {6}

Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema, wana ujira usiokwisha.

فَمَا يُكَذِّبُكَ بَعْدُ بِالدِّينِ {7}

Basi ni kipi baadaye kitaka­chofanya ukadhibishe dini?

أَلَيْسَ اللَّهُ بِأَحْكَمِ الْحَاكِمِينَ {8}

Kwani Mwenyezi Mungu si hakimu bora wa mahakimu wote?

Maana

Naapa kwa tini na zaituni.

Wametofautiana kuhusu makusudio ya tini na zaituni, kwenye kauli nyin­gi. Iliyo mbali zaidi na dhahiri ya tamko na ufahamisho wake, ni ile aliy­oisema Sheikh Muhammad Abduh:

“Tini ni ishara ya Adam na Hawa wakiwa Peponi, ulipofunuka uchi wao walianza kujibandika majani ya mtini na mzaituni kuashiria zama za Nuh na kizazi chake.”

Hatuoni sababu ya kuleta taawili hii, kwa sababu yanayokuja kwenye ufa­hamu ni kuwa tini ni ile ya kawaida tu na zaituni ni ile ile inayokamuliwa mafuta; wala hakuna kizuizi cha kuapa Mwenyezi Mungu kwa chochote anachotaka katika viumbe vyake, na hii ni kwa kukiri kwake yeye mwenyewe Sheikh Muhammad Abduh, na mara nyingi amekuwa akitege­mea yanayokuja haraka akilini katika Aya za Qur’an yenye hikima.

Ama hikima ya kuapia nazo inawezekana kuwa ni kutanabahisha faida ilizo nazo na inawezekana kuwa ni mengineyo. Ni mengi ambayo hatuya­jui.

Na kwa mlima Sinai.
Mlima hapa ni ule ambao Mwenyezi Mungu alizungumza na Musa.

Na kwa mji huu wenye amani, ambao ni Makka iliyo na heshima kwa kuzaliwa Muhammad (s.a.w.) na kuweko nyumba takatifu; mfano wake ni kama “Naapa kwa mji huu.” (90:1).

Hakika tumemuumba mtu katika hali nzuri mno.

Hili ni jawabu la kiapo na ndilo lililokusudiwa katika sura yote. Hali nzuri ni mpangilio na nidhamu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameapa kwa upole wake na ulinzi wake wakati alipomfanya aweko; akaumba mwili wake katika sura ya ajabu na shepu nzuri; na roho yake akaipa nguvu na utashi ambao anaweza kuwapita viumbe wote akitaka; au kuanguka chini kabisa akipotoka na hawa na matamanio yake.

Ikiwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemshughulikia mtu, kwa umuhimu huu na akamuandaa kwenda juu na ukamilifu, basi mtu mwenyewe, ndio anatakikana ajishughulikie yeye mwenyewe wala asipotoke akaacha lile aliloumbiwa nalo, la ukamilifu na uzuri. Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ {64}

“Na akawatia sura, na akazifanya nzuri sura zenu.”Juz. 24 (40:64).

Kisha tukamrudisha chini ya walio chini; yaani huyo mtu kwa kuzinga­tia baadhi sio kila mtu. Makusudio ya chini ya walio chini hapa, ni Jahannam. Lau si mfumo wa maneno tungelisema makusudio ni uzee na ukongwe, lakini kauli yake Mwenyezi Mungu ‘isipokuwa wale walioami­ni na wakatenda mema,’ ni wazi kuwa makusudio ni Jahannam. Maana ni kuwa tumemuumba mtu katika uzuri wa umbo, kimwili na kiro­ho, lakini baadhi au wengi wao wanamuasi Mwenyezi Mungu na kuziku­furu neema zake, ndio akawarudisha kidato cha chini katika Moto.

Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema, wana ujira usiok­wisha; yaani walioamini wakatenda kwa mujibu wa imani yao kwa ikhlasi, wataneemeka Peponi na kudumu humo milele. Kwa Mwenyezi Mungu kuna malipo makubwa.

Umetangulia mfano wake kwa herufi zake katika Juz. 24 (41:8).

Basi ni kipi baadaye kitakachokufanya ukadhibishe dini?

Tamko ni la kuuliza, lakini maana yake ni kukanusha; yaani hakuna kitaka­chokufanya ukadhibishe dini ya Mwenyezi Mungu baada ya kusimama hoja na dalili juu yake, zikiwa ni kuumbwa mtu katika umbo zuri.

Kwani Mwenyezi Mungu si hakimu bora wa mahakimu wote?

Kwanini isiwe hivyo? Yeye ni mpangiliaji bora zaidi ya wote na mwadlifu zaidi kwa kauli na vitendo; naye atamhukumu kwa haki yule atakayemkad­hibisha kwa kiburi na inadi.