read

Sura Ya Tisini Na Tatu: Ad-Dhuha

Imeshuka Makka Ina Aya 11.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

وَالضُّحَىٰ {1}

Naapa kwa Dhuha!

وَاللَّيْلِ إِذَا سَجَىٰ {2}

Na kwa usiku unapotua!

مَا وَدَّعَكَ رَبُّكَ وَمَا قَلَىٰ {3}

Hakukuacha Mola wako wala hakukukasirikia!

وَلَلْآخِرَةُ خَيْرٌ لَكَ مِنَ الْأُولَىٰ {4}

Na hakika mwisho ni bora kwako kuliko mwanzo.

وَلَسَوْفَ يُعْطِيكَ رَبُّكَ فَتَرْضَىٰ {5}

Na Mola wako atakupa utarid­hia.

أَلَمْ يَجِدْكَ يَتِيمًا فَآوَىٰ {6}

Je, hakukukuta ni yatima akakuhifadhi?

وَوَجَدَكَ ضَالًّا فَهَدَىٰ {7}

Na akakukuta umepotea akakuongoa?

وَوَجَدَكَ عَائِلًا فَأَغْنَىٰ {8}

Akakukuta mhitaji akaku­tosheleza?

فَأَمَّا الْيَتِيمَ فَلَا تَقْهَرْ {9}

Ama yatima usimwonee!

وَأَمَّا السَّائِلَ فَلَا تَنْهَرْ {10}

Na ama mwenye kukuomba usimkaripie!

وَأَمَّا بِنِعْمَةِ رَبِّكَ فَحَدِّثْ {11}

Na ama neema ya Mola wako izungumze.

Maana

Naapa kwa Dhuha

Makusudio ya dhuha hapa ni mchana wote, kwa dalili ya mkabala wake na usiku. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameuletea mchana ibara ya dhuha kwa sababu dhuha ni chimbuko la mchana, kwa mujibu wa maelezo ya Razi. Au ni ujana wa mchana kwa maelezo ya Sheikh Muhammad Abduh.

Na kwa usiku unapotua.

Makusudio ya kutua usiku ni kutulia watu wake na kuacha harakati. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameapa na mawili haya kwa sababu ni katika ishara zake kubwa.

Mafakihi wengi wamesema kuwa Nabii (s.a.w) aliswali swala ya dhuha siku ya ushindi wa Makka, nayo ni rakaa mbili kwa baadhi, na wengine wanasema ni zaidi, na ikafanywa Sunna kwa wote.

Shia Imamiya wamesema hakuna kiwango kwa Swala ya Sunna ni Qurbani ya kila mwenye takua, anayetaka ataifanya chache na anayetaka ataifanya nyingi. Kila mtu anaweza kuswali rakaa za kuanzia kila wakati na kila mahali, kwa nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.

Hakukuacha Mola wako wala hakukukasirikia.
Hili ni jawabu la kiapo. Wafasiri na wapokezi wameafikiana kwamba wahyi ulisimama kumfikia Mtume kwa siku kadhaa. Washirikina wakase­ma: Mungu wa Muhamadi amemchukia na Jibril amemkasirikia, ndio akateremsha Mwenyezi Mungu Mtukufu: Hakukuacha Mola wako wala hakukukasirikia.

Maneno ni yale aliyosema: Sheikh Muhammad Abduh: “Kwenye mfumo wa Sura hakuna kinachoashiria hilo. Washirikina walijua wapi vipindi vya wahyi? Isipokuwa Mtume alitamani wahyi baada ya kuonja Utamu wake na kila mwenye kuonja huwa na hamu na shauku na shauku huleta hofu? Kuna Hadithi katika sahih inayosema kuwa Nabii (s.a.w.w) alihuzunikia sana kwa wahyi kuchukua muda.”

Kwa mnasaba huu ninasema kuwa mimi nimesoma kila chapisho la Sheikh Muhammad Abduh nikagundua kuwa heshima ya mtu huyu na umashuhuri wake, hautokani na ilimu yake tu, wala kwa upeo wa uchun­guzi wake; kwani badhi ya wanafunzi wake, kwa ninavyoona mimi, wana upeo na kujua kauli za waliopita na wapya zaidi yake.

Siri pekee ya heshi­ma ya Sheikh huyu iko katika kuitegemea kwake haki, kuifanyia ikhilasi na ujasiri wake wa kuisema wazi wazi; hata kama inapingana na waliopita na wanaokuja. Kwa njia hii ndio maana vilemba viovu vimemkufurisha, lakini historia imemsafisha na kumweka mbele na kuutupa kapuni ule uovu.

Na hakika mwisho ni bora kwako kuliko mwanzo. Na Mola wako atakupa utaridhia.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.). Makusudio ya mwisho hapa ni maisha ya Akhera na mwanzo ni maisha ya dunia kuanzia kushukiwa na wahyi mpaka Siku ya Kiyama. Kwa sababu hakuna Siku yoyote inayopita ila wanazaliwa mamia ya waislamu, kuongezea umma na mataifa yatakayoingia katika dini ya Mwenyezi Mungu. Yote hayo yamepatikana kwa Muhammad na risala ya Muhammad (s.a.w.).

Maana ya Aya ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atakuzidishia fadhila zake ewe Muhammad siku baada ya siku mpaka Siku ya Kiyama. Fauka ya hayo wewe utakuwa na ukuu na utukufu huko Akhera. Je, yanakutosha haya au unataka mengine?

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamtajia Nabii wake mtukufu neema ali­zomneemesha tangu siku yake ya kwanza na kuendelea bila ya kikomo; zifuatazo ni neema kabla ya utume:­

1. Je, hakukukuta ni yatima akakuhifadhi?

Swali hili ni la kuripoti uhalisia; yaani ulikuwa hivyo. Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Nabii (s.a.w.) alikuwa yatima kwa sababu baba yake alikufa Madina akiwa bado yuko tumboni mwa mama yake, akalelewa na babu yake, Abdul-Mutwalib, kwa malezi bora. Kisha babu yake naye aka­fariki akiwa na umri wa miaka minane.

Akalelewa na ami yake, Abu Twalib, kwa wasia wa Abdul-Mutwalib. Alikuwa akimlinda na akimpenda sana hadi ukubwani mwake. Aliendelea kumhami na kumsaidia, baada ya utume, hadi kufariki kwake, ndio Makuraishi wakasubutu kumghasi, baada ya mauti ya ami yake, mpaka akalazimika kuhamia Madina.

Hiyo ndiyo hifadhi ya Mwenyezi Mungu kwa Nabii wake akiwa ni yatima.

2. Na akakukuta umepotea akakuongoa.

Wafasiri wametofautiana kuhusu makusudio ya kupotea hapa. Razi ameishiliza kauli zao ishirini.

Iliyo karibu zaidi na uhalisia ni ile isemayo kuwa Nabii (s.a.w.) alikuwa amedangana kuhusu watu wake, hajui afanye nini kuhusiana na kupotea kwao katika itikadi zao. Pia ufisadi wa matendo yao, ujinga wao na utengano wao.
Akawa hajui atumie njia gani ya kuwaongoza mpaka akashukiwa na wahyi ambao ndani yake mna ubainifu wa kila kitu, mwongozo na rehema. Kwa hiyo upotevu wa Mtume (s.a.w.) ni kudangana kwake jinsi atakavy­owaongoza makafiri, lakini Qur’an ikamwongoza.

3. Akakukuta mhitaji akakutosheleza?

Wapokezi wanasema kuwa Mtume (s.a.w.) hakurithi kutoka kwa baba yake isipokuwa ngamia mmoja na mjakazi, lakini Mwenyezi Mungu alimfanya asiwe mhitaji kwa kutunzwa na ami yake, Abu Twalib, mali ya Khadija na ngawira.

Ama yatima usimwonee na ama mwenye kukuomba usimkaripie.

Ambaye amekuwa yatima anakuwa mtunzaji mzuri wa mafukara na may­atima na kuwashughulikia sana. Hakuna mwenye shaka kwamba hii ni kumfunza kila mwenye kujaribu kuwaonea mayatima au kuwakaripa mafukara; ni kuwa tayari Mtume wa rehema ana hulka adhimu na mwenye kuwahurumia wanyonge.

Na ama neema ya Mola wako izungumze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumsifu. Kuna Hadith tukufu isemayo: “Kuzizungumza neema za Mwenyezi Mungu ni kumshukuru. Imam As-Sadiq (a.s.) anasema kati­ka maana ya Aya hii: “Simulia aliyokupa Mwenyezi Mungu, akakufadhili, akakuruzuku, akakufanyia hisani na akaukuongoza.

Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Maana ya zungumza ni ongeza kuwapa mafukara.” Mwanafunzi wake Al-Maraghi naye akamfuata katika tafsiri hii, lakini iko mbali na dhairi ya tamko na ufahamisho wake. Linalokuja haraka kwenye ufahamu kutokana na neno zungumza ni kuz­izungumza neema za Mwenyezi Mungu kwa kumshukuru na kumsifu.