read

Sura Ya Tisini Na Tisa: Az-Zilzala

Imeshuka Makka na imesemekana imeshuka Madina Ina Aya 8.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ 

Kwa jina Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kure­hemu.

إِذَا زُلْزِلَتِ الْأَرْضُ زِلْزَالَهَا {1}

Itakapotetemeshwa ardhi huo mtetemeko wake!

وَأَخْرَجَتِ الْأَرْضُ أَثْقَالَهَا {2}

Na ikatoa ardhi mizigo yake!

وَقَالَ الْإِنْسَانُ مَا لَهَا {3}

Na mtu akasema: Ina nini?

يَوْمَئِذٍ تُحَدِّثُ أَخْبَارَهَا {4}

Siku hiyo itahadithia habari zake.

بِأَنَّ رَبَّكَ أَوْحَىٰ لَهَا {5}

Kwa sababu Mola wako ameipa wahyi!

يَوْمَئِذٍ يَصْدُرُ النَّاسُ أَشْتَاتًا لِيُرَوْا أَعْمَالَهُمْ {6}

Siku hiyo watu watatoka kwa mtawanyiko ili wakaonywesh­we vitendo vyao!

فَمَنْ يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ {7}

Basi anayetenda chembe ya wema, atauona!

وَمَنْ يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ {8}

Na anayetenda chembe ya uovu atauona!

Maana

Itakapotetemeshwa ardhi huo mtetemeko wake!

Hii ni kutoa hadhari ya vituko vya siku ya Kiyama ambapo ardhi itagongana na kutingishika kwa mtingishiko mkali. Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ ۚ إِنَّ زَلْزَلَةَ السَّاعَةِ شَيْءٌ عَظِيمٌ {1}

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu. Hakika tetemeko la saa ni jambo kubwa.” Juz. 17 (22:1).

Na ikatoa ardhi mizigo yake!

Itatoa kila kilichomo ndani yake wakiwemo wafu, hazina, madini na maen­deleo.

Na mtu akasema: Ina nini?

Vipi hii ardhi inakwenda bila ya desturi yake? Imetokewa na nini?

Siku hiyo itahadithia habari zake.

Kuhadithia kwa mtu ni kutoa yaliyo katika nafsi yake na kuhadithia kwa ardhi, Siku ya Kiyama, ni kudhihirisha nje yale maajabu yote iliyoyameza wakati wote. Sijui wataalamu wa mambo ya kale watayaona maonyesho haya ya kutisha?

Kwa sababu Mola wako ameipa wahyi!

Kila litakalotokea kwenye ardhi Siku ya Kiyama ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Sheikh Muhammad Abduh anasema: “Hakuna kitakachozuia kuharibika ardhi katika mwisho wa umri wake, kwa kuvunjika jengo lake na kuifanya vumbi linalotifuka.”

Kama kwam­ba anaashiria, kwa kauli yake hii, kwenye mlipuko wa nyuklia kwenye uso wa ardhi na ndani yake, ingawaje haikuwako wakati wake. Kauli yake hii iko karibu sana, kwa sababu umri wa ardhi hauishi kwa kupita nyakati kama ilivyo katika viumbe vingine hai; bali ni kwa kuharibi­ka yote au sehemu zake za msingi.

Siku hiyo watu watatoka kwa mtawanyiko ili wakaonyweshwe viten­do vyao!

Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu ataubadilisha ulimwengu usiokuwa ulimwengu huu na kiumbe wa kwanza atakutana na wa mwisho na wote watakwenda pale kila mmoja aone jaza ya matendo yake.

Basi anayetenda chembe ya wema, atauona! Na anayetenda chembe ya uovu atauona!

Katika Tafsir Arrazi na nyinginezo imesemwa neno dharra, tulilolifasiri kwa maana ya chembe, kuwa lina maana ya mdudu chungu aliye mdogo zaidi ya wengine. Katika kitabu Al-ur’an wal-ilmulhadith cha Nawfal anasema: “Neno dharra ni sehemu ndogo ambayo umbo lake halifiki sehe­mu ya kumi chini ya milimita bilioni moja.” Vile vile imesemwa kuwa dharra haiwezi kuonekana hata kwa hadubini kubwa, isipokuwa inaju­likana kwa athari yake tu.

Maana ni kwamba kila mtu kesho atakuta malipo ya matendo yake kwa Mwenyezi Mungu, yakiwa ni heri basi ni heri na yakiwa nishari basi ni shari, kwa kiasi chochote cha udogo kitakachofikia. Kimsingi ni kuwa malipo ya kitu yanahisabiwa kwa kiwango na kiaina.

Unaweza kuuliza: Je, mumin na kafiri ni sawa katika hilo, au ni kuwa mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu hayatakubaliwa matendo yake ya heri wala kulipwa, hata kama ameyafanya kwa njia ya heri ya ubinadamu?

Jibu: Kila kitu kina hisabu yake. Ikiwa kafiri atafanya heri, ataadhibiwa adhabu ya ukafiri wake na atalipwa matendo ya heri kulingana na vile hiki­ma ya Mwenyezi Mungu itakavyoona; iwe ni kumlipa duniani au kumhafi­fishia adhabu ya Akhera. Tumeyazungumzia maudhui haya kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 4 (3:176­178) kifungu cha ‘Kafiri na amali njema.’

Swali la pili: Aya nyingi zimefahamisha kuwa kufuru inaporomosha matendo yote hata kama yote ni mema?

Baadhi ya maulama wamejibu kuwa maana ya kuporomoka matendo ni kuwa mema ya kafiri yahayamuokoi na adhabu ya kufuru, na wala sio kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hamlipi kabisa hata duniani.