read

Aya 1 – 4: Anfal Ni Ya Mwenyezi Mungu Na Mtume

Maana

Wanakuuliza juu ya Anfal

Katika Aya hii Mwenye Mungu (s.w.t.) ametaja kwamba watu walimuuliza Mtume (s.a.w.) kuhusu Anfal, wala hakubainisha makusudio yake.

Wameifikiana watu wa elimu ya dini kwamba neno lolote litakalokuja katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadith za Mtume bila ya kuelezwa maana yake, basi litachukuliwa kwenye maana wanayoifahamu watu. Ikiwa watu hawalijui maana yake, zitarudiwa kamusi za lugha.

Kamusi zinasema: Anfal ni ngawira na ziada kwa ujumla bila ya kuyafunga maana yake na ngawira au ziada maalum.

Kwa ajili hiyo ndipo wafasiri wakatofautiana katika makusudio ya Anfal. Je, ni ngawira zote au ni ngawira za Badr tu au ni ngawira nyingine.

Shia Imamia wamesema: “Hakuna sababu ya kutofautiana huku. Kwa sababu imethibiti katika Hadith za Mtume kwa riwaya za Ahlul-bait wa Mtume Muhammad (s.a.w.) kwamba makusudio ya Anfal ni ardhi iliyochukuliwa kwa wasiokuwa waislamu bila vita na ardhi iliyokufa, ni sawa iwe ilikuwa ikimilikiwa kisha akatoweka mmiliki au la. Pia vilele vya milima, mabonde, misitu minene na kila kinachohusika na vita, kwa sharti ya kuwa kisiwe kimechukuliwa kwa mwislamu au mwenye mkataba. Vilevile na mirathi ya asiyekuwa na mrithi.

Haya yanaafikiana na madhehebu ya Malik, kwa sababu wao wamefasiri Anfal kuwa ni kilichochukulia bila ya vita. Hayo yanapatikana katika Kitab Ahkamul Qur’an cha Abu Bakar, maaruf kwa jina la Ibn Arabi Al-Muafiri. Abu Is-haq Al-fairuzbadi, wa madhehebu ya Shafi, anasema:

Anfal ni kutoa ziada Amiri jeshi kwa aliyefanya tendo lililopelekea kushindwa adui; kama vile uchunguzi, kuonyesha njia au ngome n.k.”

Naye Al-Jisas wa madhehebu ya Hanafi anasema: Ni kusema Amiri jeshi: Atakayemuuwa mtu basi vitu vyake ni vyake na atakayepata kitu ni chake.”

Sema Anfal ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume.

Huu ni ubainifu wa mahali pa Anfal, na kwamba ni ya Mwenyezi Mungu, na cha Mwenyezi Mungu ni cha Mtume wake, na cha Mtume wake hutolewa kwa kuinua tamko la Uislam na maslahi ya waislamu. Atachukua kila mwenye haja kiasi cha haja yake. Ufafanuzi umo katika vitabu vya Fiqh, kikiwemo kitabu chetu Fiqhul-Imam Jafar As-Sadiq Juz. 2.

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na msuluhishe mambo baina yenu, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni waumini.

Hii inatambulisha kuwa swahaba walizozana juu ya Anfal, na walipomuuliza Mtume (s.a.w.) aliwaambia, kwa amri itokayo kwa Mwenyezi Mungu, kuwa hiyo ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume, na kwamba ni juu yao kuitoa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala wasigombane juu ya Anfal na mengineyo, waungane wapendane kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kama ilivyo kwa waumini wa kweli.

Kisha Mwenyezi Mungu mtukufu akawafafanulia kwamba waumini wa kweli ni wale wanaosifika na sifa zifuatazo:

1. Hakika waumini ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa hofu.

Hofu inakuwa kwa waumini, kwa sababu ya kukutana kwao na Mwenyezi Mungu,hisabuyakenamalipoyake.Lakiniwaowakatihuohuowanataraji rehema ya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu wao vilevile wanaamini kauli yake Mwenyezi Mungu:

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِنْ رَحْمَةِ اللَّهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ {53}

Enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika yeye ni Mwingi wa kusamehe mwingi wa kurehemu” (39:53).

Na pia kauli ya Mwenyezi Mungu:

كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ۖ {54}

“Mola wenu amejilazimisha rehema” (6:54).

Miongoni mwa aliyoyasema Imam Ali (a.s.) katika kuwasifu waumini: “Wao na pepo ni kama waliyoiona wakiwa ndani wananeemeshwa. Na wao na moto ni kama waliouona, wakiwa ndani wanaadhibiwa”

Anasema mshairi katika kuwasifu: Yalingana hofu na matarajio si kwa kuogopa wala tamanio

2. Na wanaposemewa Aya zake huwazidisha Imani.

Kwa sababu wao na dini yao ni kama vile wameiona ghaibu kwa macho. Bali wanaweza kutilia shaka wanaloliona kwa jicho. Kwa sababu macho mara nyingine hudanganya mtu akadhani mangati ni maji na uvimbe ni shahamu. Lakini kauli yake Mwenyezi Mungu haina shaka hata chembe.

Dini Haioteshi Ngano

3. Na wanamtegemea Mola wao.

Maana ya kutegemea sio tu kusema kwa midomo yetu: Tumemtegemea Mungu, pia sio kuacha visababishi na kuacha kufanya kazi kwa kutegemea mambo yaje yenyewe tu, na sisi tumekaa. Isipokuwa kutegemea ni kuhangaika, kama alivyotuamrisha Mwenyezi Mungu, tukitaraji tawfik kutoka kwake katika kuhangaika kwetu tukiamini kuwa kazi ni sharti la msingi la kutegemea. Na kwamba hiyo ni ibada, na kutii kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِنْ رِزْقِهِ ۖ {15}

Basi tembeeni katika pande zake zote na kuleni katika riziki zake.” (67:15).

Hakika kuamini na kumtegemea Mwenyezi Mungu bila ya kazi hakuwezi kuotesha ngano wala kuponesha mgonjwa; vinginevyo Mwenyezi Mungu asingetuumbia mikono na miguu kwa ajili ya kufanya kazi.

Ndio! Dini ya kweli inaotesha upendo, ikhlas na msimamo, lakini sio mkate na dawa, hata elimu haitupatii chakula wala haitupozi magonjwa; isipokuwa inatufundisha jinsi ya kulima chakula na kutengeneza dawa; kisha haitushughulikii kuwa tutakufa na njaa na magonjwa au hatutakufa.

Dini inatuhimiza kushghulikia maisha yetu. Ndiyo maana inatuhimiza elimu na kufuata njia zake, na inazingatia kuwa kuipuuza ni kosa, kwani kutasababisha madhara na ufisadi.

Elimu nayo inapanga mkakati wa maisha mazuri. Na hayo ndiyo yanayolengwa na Uislamu. Kwa ajili hiyo Uislamu umeamrisha na kuhimiza elimu; sawa na Swaumu na Swala, na ataadhbiwa atakayeitumia elimu kwa unyang’anyi na uchokozi; kama ambavyo ataadhibiwa atakayeiharibu dini kwa manufaa yake ya kiutu.

Kwa ufupi ni kwamba, ikiwa ni sawa kuwa mtu hawezi kuishi kwa mkate peke yake, Vilevile hawezi kuishi kwa Swala peke yake.

4. Ambao wanasimamisha Swala. Na wanatoa katika yale tuliy- owaruzuku.

Sifa zilizotangulia ni za hali ya moyo, na Swala na Zaka ni katika vitendo vya mwili, vyote viwili ni natija ya kumwamini Mwenyezi Mungu na kumhofia na kumtegemea. Mwenye kuacha Swala hahisabiwi kuwa ni katika waumini wa kweli, na dalili ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

Hao kweli ndio waumini. Wao wana vyeo kwa Mola wao, na maghufira na riziki bora.

Hao, ni ishara ya wale waliokusanya sifa tano; waumini wa kweli, ni wale ambao imani yao inaonekana katika vitendo vyao, si katika kauli zao tu. Vyeo mbele ya Mwenyezi Mungu vinatofautiana kufuatana na juhudi na kujitolea mhanga, mwenye cheo cha juu zaidi ni yule ambaye watu wamenufaika naye na akavumilia mengi ili waja wa Mwenyezi Mungu wote waishi katika kivuli cha amani na uadilifu. Maghufira ni kukiuka utelezi; na riziki bora ni pepo.

كَمَا أَخْرَجَكَ رَبُّكَ مِنْ بَيْتِكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّ فَرِيقًا مِنَ الْمُؤْمِنِينَ لَكَارِهُونَ {5}

Kama alivyokutoa Mola wako nyumbani kwako kwa haki, na hakika kundi moja la waumini linachukia.

يُجَادِلُونَكَ فِي الْحَقِّ بَعْدَمَا تَبَيَّنَ كَأَنَّمَا يُسَاقُونَ إِلَى الْمَوْتِ وَهُمْ يَنْظُرُونَ {6}

Wanajadiliana nawe katika haki baada ya kubainika. Kama kwamba wanasukumwa katika mauti na huku wanaona.

وَإِذْ يَعِدُكُمُ اللَّهُ إِحْدَى الطَّائِفَتَيْنِ أَنَّهَا لَكُمْ وَتَوَدُّونَ أَنَّ غَيْرَ ذَاتِ الشَّوْكَةِ تَكُونُ لَكُمْ وَيُرِيدُ اللَّهُ أَنْ يُحِقَّ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ وَيَقْطَعَ دَابِرَ الْكَافِرِينَ {7}

Na alipowaahidi moja ya makundi mawili kuwa ni lenu. Nanyi mkapenda lile lisilo na nguvu ndio liwe lenu. Na Mwenyezi Mungu anataka kuihakikisha haki kwa maneno yake na kuikata mizizi ya makafiri.

لِيُحِقَّ الْحَقَّ وَيُبْطِلَ الْبَاطِلَ وَلَوْ كَرِهَ الْمُجْرِمُونَ {8}

Ili kuihakikisha haki na kuivunja batili; ijapokuwa watachukia wafanyao makosa.