read

Aya 101 – 102: Miji Hiyo Tunakusimulia

Maana

Miji hiyo tunakusimulia baadhi ya habari zake.

Miji hiyo ni ishara ya watu wa miji hiyo ambao ni aina tano: Watu wa Nuh, wa Hud, wa Swaleh, wa Lut na wa Shuaib.
Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Nabii Muhammad (s.a.w.) wakikusudiwa waislamu kupewa habari ya hali za waliopita, ili wazingatie na watahadhari.

Hakika waliwajia Mitume wao kwa ishara zilizo waziwazi, lakini hawakuwa wenye kuamini waliyoyakadhibisha zamani.

Ametaja Razi njia tatu za kutafsiri kipande hiki cha Aya, na Tabrasi naye akazidisha ya nne. Hakuna hata moja waliyoitilia nguvu, na wakamwacha msomaji wa kawaida kwenye mataa; ambapo maana yako wazi yasiyokuwa na undani wowote.

Kwa ufupi ni kuwa watu wa miji hiyo kabla ya kupelekewa Mitume wa Mwenyezi Mungu, walikuwa kwenye shirki na upotevu; na kwamba wao waliendelea katika shirki yao na upotevu baada ya kuwafikia Mitume kwa dalili na miujiza. Na hawakuathirika na chochote, wakawa kama ambao hawakupelekewa mjumbe anayetoa bishara na maonyo. Haya yanafahamishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

Namna hii Mwenyezi Mungu anazipiga muhuri nyoyo za makafiri.

Muhuri hapa ni fumbo la kususuwaa kwa nyoyo zao na kwamba hazijali kupotea kwake wala haitarajiwi kheri yake.

Na hatukuona kwa wengi wao ahadi yoyote.

Hawaamini dini ya Mwenyezi Mungu wala hawalazimiani na chochote kinachohusiana na ubinadamu. Hata hivyo wanayo ahadi moja tu wanayolazimiana nayo wala hawapingani nayo, nayo ni kufuata masilahi na hawaa.

Na hakika tuliwakuta wengi wao ni mafasiki.

Yaaniwamepoteakufuatanjia.

ثُمَّ بَعَثْنَا مِنْ بَعْدِهِمْ مُوسَىٰ بِآيَاتِنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ فَظَلَمُوا بِهَا ۖ فَانْظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ {103}

Kisha baada yao tukamtuma Musa na ishara zetu kwa Firauni na wakuu wake lakini wakazikanusha. Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa wafisadi.

وَقَالَ مُوسَىٰ يَا فِرْعَوْنُ إِنِّي رَسُولٌ مِنْ رَبِّ الْعَالَمِينَ {104}

Akasema Musa: Ewe Firauni! Hakika mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu.

حَقِيقٌ عَلَىٰ أَنْ لَا أَقُولَ عَلَى اللَّهِ إِلَّا الْحَقَّ ۚ قَدْ جِئْتُكُمْ بِبَيِّنَةٍ مِنْ رَبِّكُمْ فَأَرْسِلْ مَعِيَ بَنِي إِسْرَائِيلَ {105}

Yanipasa nisiseme juu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa haki. Nimewajia na dalili wazi itokayo kwa Mola wenu. Basi waache wana wa Israel waende nami.

قَالَ إِنْ كُنْتَ جِئْتَ بِآيَةٍ فَأْتِ بِهَا إِنْ كُنْتَ مِنَ الصَّادِقِينَ {106}

Akasema: Ikiwa umekuja na ishara, basi ilete ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.

فَأَلْقَىٰ عَصَاهُ فَإِذَا هِيَ ثُعْبَانٌ مُبِينٌ {107}

Akaitupa fimbo mara ikawa nyoka dhahiri.

وَنَزَعَ يَدَهُ فَإِذَا هِيَ بَيْضَاءُ لِلنَّاظِرِينَ {108}

Na akautoa mkono wake. Mara ukawa mweupe kwa watazamao.

قَالَ الْمَلَأُ مِنْ قَوْمِ فِرْعَوْنَ إِنَّ هَٰذَا لَسَاحِرٌ عَلِيمٌ {109}

Wakasema wakuu wa watu wa Firauni: Hakika huyu ni mchawi mjuzi.

يُرِيدُ أَنْ يُخْرِجَكُمْ مِنْ أَرْضِكُمْ ۖ فَمَاذَا تَأْمُرُونَ {110}

Anataka kuwatoa katika ardhi yenu. Basi mnatoa shauri gani?

قَالُوا أَرْجِهْ وَأَخَاهُ وَأَرْسِلْ فِي الْمَدَائِنِ حَاشِرِينَ {111}

Wakasema: Mwache kidogo yeye na ndugu yake, na uwatume wakusanyao watu mijini.

يَأْتُوكَ بِكُلِّ سَاحِرٍ عَلِيمٍ {112}

Wakuletee kila mchawi, mjuzi.