read

Aya 127 – 129: Utamwacha Musa?

Maana

Na wakasema wakuu wa kaumu ya Fir’aun: Je, utamwacha Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi.”

Baada ya kwisha tukio hilo la kutisha ambalo Nabii Musa alipata ushindi na kufedheheka Firauni. Nabii Musa aliendelea kuwalingania kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake, na dalili yake ni yaliyotukia jana tu kati yake na wachawi. Watu wengi wakamkusanyikia.

Wakuu wa Firauni wakahofia hali isibadilike na mambo yakawageukia wao na bwana wao, hapo wakamchochea Firauni na kumwambia: “Mpaka lini utamnyamazia Musa na kumwacha akiharibu nchi?” Kuharibu nchi, wanamaanisha watu kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake.

Na wakuache wewe na waungu wako.

Kauli hii ya wakuu wa Firauni inafahamisha kuwa alikuwa nao waungu anaowaabudu; nayo inapingana, kwa dhahiri yake, na kauli ya Firauni kuwa Mimi ndiye mola wenu mkubwa na simjui kwa ajili yenu Mungu asiyekuwa mimi.

Wafasiri wamelijibu hilo kwa majibu kadhaa. Lenye nguvu zaidi ni kuwa Firauni alikuwa na miungu akidai kuwa yeye ni mwana kipenzi wa hiyo miungu na kwamba yeye anaitegemeza hukumu yake na utawala wake kwenye hiyo miungu. Kwa hiyo kauli yake simjui kwa ajili yenu Mungu na Mola isipokuwa yeye peke yake inamaanisha kuwa hakuna yeyote mwenye kuhukumu kwa jina la mungu isipokuwa yeye. Maana haya yanatiliwa nguvu na kauli yake:

أَلَيْسَ لِي مُلْكُ مِصْرَ وَهَٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِنْ تَحْتِي ۖ {51}

“Kwani ufalme wa Misri si wangu na hii mito inapita chini yangu?” (43:51).

Akasema: Tutawaua watoto wao wakiume na tutawaacha hai wanawake wao.

Kabla ya kuzaliwa Nabii Musa, Fir’aun alikua akwaiua watoto wa kiume wa Bani Israel waliposisitizia wakuu katika watu wake apambane na Nabii Musa, aliwajibu atarudisha mpango huo wa mwanzo.

Na hakika sisi ni wenye nguvu juu yao.

Yaani tuna nguvu juu yao kama ilivyokuwa kabla ya Musa.

Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi Mungu na subirini. Ardhi ni ya Mwenyezi Mungu atamrithisha amtakaye katika waja wake na mwisho ni wa wenye takuwa.”

Waisrael waliposikia vitisho vya Firauni na kiaga chake waliogopa. Nabii Musa (a.s.) akawatuliza na kuwaamrisha kuwa na subira (uvumilivu) na kumtegemea Mwenyezi Mungu; na akawapa tumaini la ushindi ikiwa wao watasubiri na kumwogopa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu ardhi ni ya Mwenyezi Mungu si ya Firauni, na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye kumcha.

Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia na baada ya kutujia!

Firauni alikuwa akiwakandamiza waisrael kabla ya kuja Nabii Musa na akawashtua kuwakandamiza zaidi baada ya kuja kwake. Walipomwambia Nabii Musa hivyo akasema:

Huenda Mola wenu akamwangamiza adui yenu na kuwafanya makhalifa katika nchi aone jinsi mtakavyokujafanya.

Nabii Musa (a.s.) alikuwa anajua wazi kuwa Firauni ataangamia na kwamba Mungu atawaokoa wana wa Israil na kuwamakinisha katika ardhi, lakini alitoa ibara ya huenda ili wasibweteke na ahadi yake.

Kisha akaishiria Nabii Musa kwamba, si muhimu kuwa adui ataangamia na wao kuwa makhalifa katika ardhi, lakini muhimu zaidi ni kumcha Mungu na kuutumia vizuri huo ukhalifa katika ardhi yake; na kwamba Mungu atawaangalia je, watatengeza au wataharibu?

Na wamefanya mengi sana katika ardhi; hapo mwanzo waliwaua mitume na viongozi wema, baadae wakaunda dola isiyokuwa na sharia isipokuwa matamanio ya kuua na kufukuza watu makwao.

Mwaka huu wa 1968, kimetoka kitabu huko Israil kinaitwa Siyakh lokhamim yaani simulizi za wanajeshi. Gazeti la Al-ahram la Misr toleo la tarehe 23-8-1968, limefasiri baadhi ya yaliyomo katika kitabu hicho:

“Ambaye hawezi kuvunja nyumba na kuwafurusha waliomo katika nyumba hiyo, basi bora akae nyumbani kwake tu. Sisi tulipokuja kwenye nchi ya Palestina kulikuwa na watu wengine wanaoishi humo; hatukuwa na matumaini kuwa wataweza kukubali kutuachia mashamba yao na majumba yao. Kwa hiyo ikawa hakuna budi tuwaue au kuwatishia kuwaua ili wakimbie watuachie majumba na mashamba”

Hii ndiyo sharia na lengo la Israil: kuua na kufukuza. Hii sio dola kama dola nyinginezo; isipokuwa ni kikosi cha kizayuni cha mauaji chenye lengo la kuwafukuza wenyeji na kukalia nchi zao kuanzia mto Nail hadi Furat.

Je Waarabu wamejiandaa na nini? Hakuna njia wala mbinu yoyote isipokuwa misimamo ya kivietnam inayosema: ‘Kufa na kupona’ ama kusiweko na Israil au kusiweko na Mwarabu.

وَلَقَدْ أَخَذْنَا آلَ فِرْعَوْنَ بِالسِّنِينَ وَنَقْصٍ مِنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ {130}

Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa ukame na kwa kupungukiwa na mazao, ili wapate kukumbuka.

فَإِذَا جَاءَتْهُمُ الْحَسَنَةُ قَالُوا لَنَا هَٰذِهِ ۖ وَإِنْ تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ يَطَّيَّرُوا بِمُوسَىٰ وَمَنْ مَعَهُ ۗ أَلَا إِنَّمَا طَائِرُهُمْ عِنْدَ اللَّهِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ {131}

Ulipowafikia wema, walisema: Huu ni kwa ajili yetu na ulipowafikia ubaya walimnasibishia mkosi Musa na walio pamoja naye. Sikilizeni! Hakika mkosi wao unatoka kwa Mwenyezi Mungu lakini wengi wao hawajui.

وَقَالُوا مَهْمَا تَأْتِنَا بِهِ مِنْ آيَةٍ لِتَسْحَرَنَا بِهَا فَمَا نَحْنُ لَكَ بِمُؤْمِنِينَ {132}

Na wakasema: Hata ukituletea ishara yoyote kutur- oga hatutakuamini.

فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الطُّوفَانَ وَالْجَرَادَ وَالْقُمَّلَ وَالضَّفَادِعَ وَالدَّمَ آيَاتٍ مُفَصَّلَاتٍ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا مُجْرِمِينَ {133}

Basi tukawapelekea tufani na nzige na chawa na vyura na damu kuwa ishara mbalimbali, lakini wakatakabari na wakawa watu wakosefu.