read

Aya 130-133: Tuliwaadhibu Watu Wa Firauni.

Maana.

Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa ukame na kwa kupungukiwa na mazao, ili wapate kukumbuka.

Misri ilikuwa ikibubujika rutuba na mazao. Firauni akajifaharusha kwa rutuba hii na kusema:

وَهَٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِنْ تَحْتِي ۖ {51}

"Na pia mito hii ipitayo chini yangu." (43:51)

Mwenyezi Mungu alitia balaa ya kahati na dhiki ya maisha wakati wa Firauni wa Musa ili ajutie upotevu wake na aitikie mwito wa haki. Kuna Hadith isemayo: "Wakiwa waovu watawala hufungwa mvua."

Ni sawa iwe kulikuwako na uhusiano baina ya dhuluma ya mtawala na kahati kwa njia ya ujumla au isiweko, lakini Mwenyezi Mungu aliwaadhibu watu wa Firauni kwa dhulma yao ili wao wakumbuke kabla ya kuwaingiza ndani kwenye uchungu.

Ulipowafikia wema, walisema: Huu ni kwa ajili yetu na ulipowafikia ubaya walimnasibishia mkosi Musa na walio pamoja naye.

Wanafasiri matukio kwa mantiki haya. Kila heri inayowapata basi wanaistahiki wao. Kwa sababu wao wanatawala watu, na kila ubaya unaowapa- ta, basi sababu yake ni yule anayewalingania kwenye haki. Ama rutuba na ukame wanautenga na Mwenyezi Mungu na maumbile aliyo yaumba.

Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu kwa kusema: Sikilizeni! Hakika mkosi wao unatoka kwa Mwenyezi Mungu lakini wengi wao hawajui. Mkosi wao ni fumbo la ukame uliowapata na huo ni kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu ambayo sababu zote huishia kwake, na kumnasibishia Musa na ujinga na upumbavu tu.

Utauliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu ametumia neno wema kwa ibara yenye al (Al-Hasana) ambayo katika sarufi ya Kiarabu inaitwa ma'rifa, na neno ubaya aktumia bila ya al ambyo ni nakira?

Jibu: Sio mbali kuwa ni ishara ya kwamba maumbile ya heri, kama vile rutuba n.k, ni mengi, na kwamba ubaya, kama vile matetemeko na tufani na ukame ni machache.

Na wakasema: Hata ukituletea ishara yoyote kuturoga hatutakuamini

Huku ni kukiri wazi, kwamba wao wanaikataa haki, wakati huo huo wanakiri kushindwa kwao kwa hoja na dalili. Yakawa malipo ya inadi yao hii ni kuwapata balaa ya aina tano za adhabu:

1. Tukawapelekea tufani ya mvua ikaharibu mimea na mifugo.

2. Na nzige waliokuja baada ya tufani,kama kawaida, wakala mimea yao iliyobakia.

3. Na chawa.

4. Na vyura waliowaghasi maisha yao.

5. Na damu. Inasemekana maji yao yaligeuka kuwa damu na wasi weze kupata maji matamu. Na inasemekana walipatwa na maradhi ya kutokwa na damu za pua.

وَلَمَّا وَقَعَ عَلَيْهِمُ الرِّجْزُ قَالُوا يَا مُوسَى ادْعُ لَنَا رَبَّكَ بِمَا عَهِدَ عِنْدَكَ ۖ لَئِنْ كَشَفْتَ عَنَّا الرِّجْزَ لَنُؤْمِنَنَّ لَكَ وَلَنُرْسِلَنَّ مَعَكَ بَنِي إِسْرَائِيلَ {134}

Na ilipowaangukia adhabu wakasema: Ewe Musa Tuombee kwa Mola wako kwa yale aliyokuahidi. Kama ukituondolea adhabu bilashaka tutakuamini na hakika tutawaacha wana wa Israil waende nawe.

فَلَمَّا كَشَفْنَا عَنْهُمُ الرِّجْزَ إِلَىٰ أَجَلٍ هُمْ بَالِغُوهُ إِذَا هُمْ يَنْكُثُونَ {135}

Lakini tulipowaondolea adhabu kwa muda watakaoufikia, mara wakavunja ahadi.

فَانْتَقَمْنَا مِنْهُمْ فَأَغْرَقْنَاهُمْ فِي الْيَمِّ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا عَنْهَا غَافِلِينَ {136}

Basi tuliwapatiliza na tukawazamisha baharini kwa sababu walizikadhibisha ishara zetu na wakaghafilika nazo

وَأَوْرَثْنَا الْقَوْمَ الَّذِينَ كَانُوا يُسْتَضْعَفُونَ مَشَارِقَ الْأَرْضِ وَمَغَارِبَهَا الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا ۖ وَتَمَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ الْحُسْنَىٰ عَلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ بِمَا صَبَرُوا ۖ وَدَمَّرْنَا مَا كَانَ يَصْنَعُ فِرْعَوْنُ وَقَوْمُهُ وَمَا كَانُوا يَعْرِشُونَ {137}

Tukawarithisha watu walionekana wadhaifu mashariki na magharibi ya ardhi tuliyoibariki. Na likatimia neno jema la Mola wako kwa wana wa Israil, kwa sababu walikuwa na subira; na tukayaangamiza yale aliyokuwa akiyafanya Firauni na kaumu yake na yale waliyokuwa wakiyajenga.