read

Aya 15 – 19: Kukimbia Vita

Maana

Enyi mlioamini! Mnapokutana vitani na wale waliokufuru, basi msi- wageuzie migongo.

Yametangulia maelezo kuwa washirikina walitoka Makka kuja kupambana na waislamu. Aya hii ni katika mafunzo ya vita. Inamaanisha waislamu wawe imara kumkabili adui wala wasikimbie wanapokutana vitani. Kwa sababu kukimbia ni unyonge katika dini na udhalili kwa waislamu.

Na atayewageuzia mgongo wake siku hiyo - isipokuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi - hakika amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu; na kimbilio lake ni Jahannam, napo ni mwisho muovu.

Mbinu za vita, ni kama kuacha mahali pake na kwenda mahali pazuri zaidi. Na kuungana na kikosi, ni kuungana na kikosi kingine kinachomhitajia au anachokihitajia.

Maana ni kuwa: Enyi waislamu! Mjizatiti na adui yenu katika vita wala msimkimbie ila ikiwa ni kuchagua sehemu nzuri au kupanga mpango mzuri kwa kuungana; na kwamba mwenye kukimbia adui bila ya sababu za msingi basi amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na marejeo yake ni Jahannam.

Mafakihi wametoa fatwa kuwa ni haramu kukimbia vita ila ikiwa idadi ya jeshi la adui ni kubwa kuliko jeshi la waislamu.

Tuanavyo sisi ni kuwa mafakihi hawawezi kuwa na fatwa hapa ya wajibu wa kubaki au kujuzu kukimbia; isipokuwa amri katika hilo ni lazima aachiwe kamanda mwaminifu mwenye majukumu ya vita na wala sio mafakihi. Kwa hiyo ni wajibu yeye aachiwe kupanga wajibu wa kubaki au kukimbia.

Anaweza akaonelea kuwa wabakie licha ya kuzidi idadi ya adui mara tatu zaidi, na anaweza akaona lazima wakimbie na kujiondoa vitani hata kama idadi ya waislamu ni maradufu ya maradufu. Kwa sababu kubaki ni tendo la kujiua. Na, katika hali zote ni wajibu kuchukua kauli yake sio kauli ya mafakihi wanayofutu wenyewe wakiwa wamelalia mito.

Zaidi ya hayo ni kwamba kauli ya mafakihi imepitwa na wakati, ambapo nguvu zilikuwa zikipimwa na idadi sio kwa aina, na kwa idadi ya jeshi sio kwa maandalizi yake ya silaha za kisasa.

Hamkuwaua nyinyi, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaua.

Waislamu waliwashinda washirikina Badr; wakawauwa na kuwateka. Sababu ya ushindi huu ni uimara wa waislamu na uvumilivu. Ama sababu ya uimara huu na uvumilivu ni ile iliyoashiriwa na Aya iliyotangulia kuwa Mwenyezi Mungu alizikazanisha nyoyo za waislamu, akaimarisha nyayo zao, akawasaidia kwa Malaika na akaondoa hofu katika nyoyo zao na kuitia katika nyoyo za washirikina.

Kwa hali hiyo inafaa kunasibisha kwa waislamu kuuwa washirikina, kwa sababu ilikuwa ni kwa mikono yao na ni kwa sababu ya uimara na subira yao. Vilevile itafaa kunasibisha kwa Mwenyezi Mungu mtukufu kwa sababu yeye ndiye aliyewaandalia uimara na subira hiyo. Zaidi ya hayo yeye ndiye sababu ya sababu zote.

Imesimuliwa kwamba baadhi ya waislamu walisema siku ya Badr: “Mimi nimemuuwa fulani”, mwengine naye akasema. Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha kauli yake hiyo.

Na hukutupa wewe ulipotupa, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa.

Ndio Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa, lakini yeye alichagua kiganja cha kutupa cha Nabii Muhammad (s.a.w.) ambaye amemfadhilisha juu ya viumbe vyote; akamhusisha na ujumbe wake ambao rehma yake imewaenea walimwengu wote.

Imepokewa kuwa Mtume alichukua gao la changarawe au mchanga, akawatupia washirikina, akasema: “Na zihizike nyuso”, hilo likafuatiwa na kushindwa kwao. Sio mbali kuwa riwaya hii ni sahih. Vilevile sio mbali kuwa makusudio ya kutupa ni kupanga mambo.

Vyovyote itakavyokuwa ni kwamba matakwa ya Mwenyezi Mungu ndiyo sababu ya sababu. Kwani sababu yoyote ya tukio lolote iwe ya moja kwa moja au si ya moja kwa moja, basi itaishia kwenye nguvu kuu iliyopatikana bila ya mpatishaji. Vinginevyo basi neno kupatikana lisingekuwa na maana.

Ili awajaribu waumini majaribu mazuri.

Majaribu (mtihani) yanaweza kuwa ya neema ili kudhihirisha shukrani na yanaweza kuwa ni misukosuko ili kudhihirisha uvumilivu. Pia maana yake yanakuwa ni kupewa. Hayo ndio maana yaliyokusudiwa katika Aya hii.

Ama makusudio ya mazur ni ushindi na ngawira; yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewaamrisha waislamu kuwa imara, wavumilivu na kuacha kukimbia vita; na akawaandalia wao njia ya hilo, ili awatimizie neema yake ya ushindi na ngawira.

Hakika Mweyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.

Amesikia maombi ya msaada na akawaitikia, kwa vile alijua usafi wao wa nia na usahihi wa azma.

Ndiyo hivyo! Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye adhoofishaye hila za Makafiri.

Hakuna neema kubwa na adhimu kuliko kudhoofishwa adui na kubatilishwa hila zake.

Kama mnataka ushindi, basi ushindi umekwishawajia, na kama mkiacha, basi itakuwa kheri kwenu; na kama mtarudia sisi pia tutarudia; na jeshi lenu halitawafa chochote hata likiwa kubwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na waumini.

Maneno yote wanaambiwa washirikina kwa kuangalia mfumo wa maneno na kutimia maana.

Imepokewa kuwa Washirikina walipotoka Makka kuelekea Badr waliishika nguo inayofunika Al-Kaaba, wakamtaka nusura ya ushindi Mwenyezi Mungu, wakasema: “Ewe Mwenyezi Mungu lipe ushindi jeshi lililo juu na lililo tukufu kati ya majeshi mawili.”

Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu: Kama mnataka ushindi; yaani mkitaka ushindi kwa jeshi lililo juu na lililo na uongofu basi amekwisha lipa ushindi. Na kama mkiacha kupigana na waislamu na kumpinga Mwenyezi Mungu na Mtume, basi itakuwa ni bora kwenu baada ya kuonja kipigo cha kuuawa na kutekwa. Na kama mkirudia vita yatawafika tena yale yaliyowafika mwanzo.

Ama wingi ambao mnajitukuza nao, mmeuona haufai kitu, hauwazuilii kuuliwa, kutekwa na kushindwa. Kwani Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kutoa ushindi, naye yuko pamoja na waumini.
Ikiwa mnataka ushindi wa kweli basi acheni shirk na mumuami Mwenyezi MungunaMtumewake.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَوَلَّوْا عَنْهُ وَأَنْتُمْ تَسْمَعُونَ {20}

Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msijiepushe naye hali mnasikia.

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ قَالُوا سَمِعْنَا وَهُمْ لَا يَسْمَعُونَ {21}

Wala msiwe kama wale wanaosema: Tumesikia; na kumbe hawasikii.

إِنَّ شَرَّ الدَّوَابِّ عِنْدَ اللَّهِ الصُّمُّ الْبُكْمُ الَّذِينَ لَا يَعْقِلُونَ {22}

Hakika wanyama waovu mbele ya Mwenyezi Mungu ni viziwi, mabubu ambao hawatumii akili.

وَلَوْ عَلِمَ اللَّهُ فِيهِمْ خَيْرًا لَأَسْمَعَهُمْ ۖ وَلَوْ أَسْمَعَهُمْ لَتَوَلَّوْا وَهُمْ مُعْرِضُونَ {23}

Na kama Mwenyezi Mungu angelijua wema wowote kwao angeliwasikilizisha;na kama angeliwasikilizisha, wangeligeuka wakipuuza.