read

Aya 163 – 166: Waulize Habari Za Mji

Maana

Na waulize habari za mji uliokuwa kando ya bahari.

Maneno anaambiwa Nabii Muhammad (s.a.w.), na mji maana yake ni watu wa mji. Dhamir ya waulize ni ya mayahudi wa Madina ambao waliishi na Mtume Nabii Muhammad (s.a.w.). Kwa sababu Aya hii ilishuka Madina kutokana na inavyowakabili mayahudi wa huko, imeingizwa katika Sura ya Makka kwa kukamilisha mazungumzo kuhusu mayahudi. Mwenyezi Mungu hakutaja jina la mji. Inasemekana ulikuwa kando kando ya bahari ya Sham.

Kwa vyovote iwavyo mji wenyewe unajulikana kwa Mayahudi walioulizwa na Mtume Nabii Muhammad (s.a.w.).

Kuna mambo mawili yaliyoyopelekea swali hili: Kwanza, ni kuwasuta mayahudi wa Madina kwamba wao wamepinga utume wake wakiwa na yakini katika nafsi zao.

Kwa vile yeye amewapa masimulizi mengi katika historia ya wakale wao, ikiwa ni pamoja na kisa hiki cha watu wa mji uiliokuwa kando ya bahari, ingawaje yeye hakusoma katika Kitab wala kusikia kwa yoyote. Ila ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Jambo la pili, ni kuwazindua kuwa wao wana kiburi na ni wapinzani wa haki na kwamba inadi yao hii si jambo la kushangaza, kwani ndio mazoweya yao tangu zamani.

Dalili ni kisa cha watu wa mji huo ambacho kimedokezwa na kauli yake Mwenyezi Mungu.

Walipokuwa wakivunja Sabato, samaki wao walipowajia juu juu siku ya Sabato yao na siku wasiyofanya Sabato hawakuwajia. Namna hiyo tuliwajaribu kwa sababu walikuwa wakifanya ufuska.

Ufupi wa kisa hiki ni kwamba Mwenyezi Mungu aliwaharamishia Mayahudi kufanya kazi siku ya Sabato (Jumamosi) ikiwa ni pamoja na kuvua samaki, kwa ajili ya kuwajaribu hali yao na kuwadhihirishia watu hakika yao.

Mwenyezi Mungu alikuwa akiwapelekea samaki kwa wingi wakionekana juu juu ya maji siku ya Jumamosi na kuwazuia siku nyingine, wakafanya hila ya kuhalalisha aliyowaharamishia Mwenyezi Mungu, wakachimba mfuo unaoungana na maji na kuwavuta samaki mpaka kwenye mfuo kisha hawawezi kutoka. Wakawa wanawachukua siku ya Jumapili huku wakisema: “Tunavua siku ya Jumapili.“

Wenzao wakawakataza na kuwakemea kutokana na hila hii na kuchezea dini, na wakawahadharisha na adhabu ya Mwenyezi Mungu, lakini hawakusikia.

Na kikundi katika wao waliposema: Kwa nini mnawaonya watu ambao Mwenyezi Mungu atawaangamiza au atawaadhibu kwa adhabu kali?

Yaani, kikundi katika waisrael kiliwaambia wenzao waliowakataza mambo mabaya: Kuna faida gani kuwakataza waasi na kuwahadharisha maadam hawataacha wala kuwa na hadhari? Waacheni, kwani Mwenyezi Mungu atawango’a hadi wa mwisho wao kutoka katika ardhi hii, au awabakishe na kuwaadhibu adhabu kali.

Wakasema wale wa kundi la kuamrisha mema:

Ili uwe ni udhuru mbele ya Mola wenu na huenda wakawa na takuwa.

Yaani tumewakataza maovu ili Mwenyezi Mungu ajue kuwa hatuko pamoja nao na kwamba tunachukia matendo yao; wakati huohuo tukitaraji kuwa huenda wakunufaika na makatazo na mawaidha yetu.

Basi walipoyasahau waliyokumbushwa tuliwaokoa waliokuwa wakikataza maovu na tukawapatiliza waliodhulumu kwa adhabu kali kwa vile walivokuwa wakifanya ufuska.

Mwenyezi Mungu amewasifu na ufuska, kwa vile waliasi amri yake, na waliodhulumu, kwa sababu kila anayeasi amri ya Mola wake basi huyo ameidhulumu nafsi yake. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwaadhibu wakosaji kwa sababu ya madhambi yao na aliwaokoa watiifu kwa sababu ya utiifu yao.

Walipoasi waliyokatazwa, tuliwaambia: Kuweni manyani wadhalilifu

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwaadhibu waasi hao kwa kuwageuza manyani. Kuna Hadith inayosema kuwa wao walibakia siku tatu, kisha wakaangamia kwa sababu mwenye kugeuzwa haishi zaidi ya muda huu wala hazai chochote jinsi yake.

Utauliza: Desturi ya Mwenyezi Mungu imepita kutomwadhibu mwenye dhambi kwa dhambi zake katika dunia, kwa ushahidi ulivyoonekana, kuongezea kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّهُ النَّاسَ بِمَا كَسَبُوا مَا تَرَكَ عَلَىٰ ظَهْرِهَا مِنْ دَابَّةٍ وَلَٰكِنْ يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُسَمًّى ۖ {45}

“Lau Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa waliyoyachuma, asingeliacha juu ya ardhi hata mnyama mmoja” (35:45).

Kwa nini aliwaadhibu hao waliotoka kwenye twaa yake katika kuvua samaki, na kuwaacha wale waliomwaga damu za watu wasiokuwa na hatia katika Palestina na Vietnam, na kabla yake Congo, Japan na wengineo wengi wasiokuwa na idadi?

Jibu, ndio imepita desturi yake Mwenyezi Mungu mtukufu kutomuadhibu mwenye dhambi kwa dhambi zake katika maisha haya kadiri itakavyokuwa kubwa.

Na kama angefanya hivyo basi asingelipambanuka mwovu na mwema, na mwenye kuacha uovu asingelikuwa na fadhila yoyote.

Kwa sababu kuacha kutakuwa ni kwa msukumo wa hofu. Sio kupenda kheri na kuchukia shari, lakini hekima yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) imepitisha kuivua desturi hii kwa miujiza ya Mitume na kuitikia dua zao kwa waasi na wafisadi kwa vyeo vyao mbele ya Mwenyezi Mungu na kuthibitisha utume wao. Wafasiri wanasema katika kufasiri:

لُعِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ لِسَانِ دَاوُودَ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ۚ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوْا وَكَانُوا يَعْتَدُونَ {78}

Walilaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa wana wa Israil kwa ulimi wa Daud na wa Isa mwana wa Maryam. Hayo ni kwa sababu waliasi, nao walikuwa wakiruka mipaka.” (5:78)

Kwamba Daud (a.s.) aliwalaani watu wa Ayla katika waisrael walipoasi kwa kuvua siku ya Sabato na kusema: “Ewe Mwenyezi Mungu wavishe laana mfano wa nguo.” Mwenyezi Mungu akawageuza manyani.

Kwa hiyo sababu ya kugeuzwa wavuvi kuwa manyani ni dua ya Mtume Daud wala hakuna Mtume wakati huu atakayewaombea wamwagaji damu na waporaji wa mali za wananchi.

Vyovyote iwavyo, sisi tunaamini uadilifu wa Mwenyezi Mungu na kuwa haki haiendi bure, na mtu atalipwa kwa matendo yake.

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكَ لَيَبْعَثَنَّ عَلَيْهِمْ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَنْ يَسُومُهُمْ سُوءَ الْعَذَابِ ۗ إِنَّ رَبَّكَ لَسَرِيعُ الْعِقَابِ ۖ وَإِنَّهُ لَغَفُورٌ رَحِيمٌ {167}

Na alipotangaza Mola wako (kwamba) hakika atawaleta watu ambao watawaadhibu kwa adhabu mbaya mpaka siku ya Kiyama. Hakika Mola wako ni mwepesi wa kuadhibu na hakika yeye ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.