read

Aya 175 – 177: Tumempa Aya Zetu Akajivua

Maana

Na wasomee habari za yule tuliyempa ishara zetu, kisha akajivua nazo na shetani akamwandama akawa miongoni mwa waliopotea.

Maneno hapa anaambiwa Mtume Muhammad (s.a.w.). Wanaosomewa ni Mayahudi.AmayuleambayeMwenyeziMunguamempaisharaakajivua nazo, hatumjui ni nani, nasi hatujiingizi katika kitu kisichokuwa katika Qur’an wala Hadith Mutawatir, lakini wasimulizi wa visa na wafasiri wengi wanasema kuwa mtu huyo alikuwa akiitwa Balam Bin Baur, na kwamba yeye alikuwa kwenye dini ya Nabii Musa na mjuzi wa hukumu zake, kisha akartadi.

Sisi tunaangalia nukuu hii na nyingine kwa hadhari, wala hautulii moyo ila kwa nukuu ya Qur’an. Na nukuu hii inafahamisha tu, kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwamrisha Mtume awape habari Mayahudi juu ya Kisa cha mtu ambaye alikuwa akijua dini ya Mwenyezi Mungu na ishara zake, kisha akahadaliwa na shetani akaacha ilimu yake na dini, akashikamana na upotevu, akawa miongoni mwa wapotevu walioangamia. Kama kawaida maulama wa kiyahudi walikuwa wakimjua mtu huyu.

Na kama tungelitaka tungelimuinua kwazo.

Yaani kwa aliyompa Mwenyezi Mungu kujua ishara zake. Lakini Mwenyezi Mungu hakutaka kumlazimisha kuzitumia ishara zake. Kwa sababu Mwenyezi Mungu mtukufu hawapeleki watu kwa matakwa ya kuumba ambayo ni kukiambia kitu kuwa kikawa. Isipokuwa huwapeleka kwa matakwa ya nasaha na mwongozo yanayoitwa amri zake na makatazo yake. Kwa hiyo akamwachia yule aliyejivua na ishara zake, uhuru na hiyari, akachagua dunia kuliko akhera.

Lakini yeye akashikilia ardhi na akafuata hawaa yake.

Makusudio ya ardhi hapa ni starehe za maisha ya dunia, kwa sababu ardhi ndio chimbuko lake. Maisha yenyewe ni pamoja na starehe na anasa. Maaana ni kuwa huyu aliyejivua amemwasi Mola wake akatii hawaa yake akiwa ameishikilia haiachi.

Razi anasema kuwa Aya hii ni kali zaidi kwa mwenye elimu. Mtume wa Mwenyezi Mungu anasema: “Mwenye kuzidi elimu, lakini asizidi uongofu hatazidi kwa Mwenyezi Mungu ila kuwa umbali.”

Basi mfano wake ni kama wa mbwa, ukimhujumu hutweta na ukimwacha pia hutweta.

Mbwa anayepumua kwa nguvu na kutoa ulimi kwa kiu au kuchoka (kuhaha) anaendelea tu, ukimkemea au ukimwacha yeye ataendelea hivyo hivyo.

Vilevile mwenye kushikilia hawaa yake huendelea katika upotevu wake umwonye au umwache yeye hupotea tu.

Huo ni mfano wa watu waliozikadhibisha ishara zetu.

Yaani hiyo ndiyo hali ya kila mwenye kuendelea na maasi, daima hanufaiki na ishara wala hazingatii mawaidha. Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mwenye kupumua na kutoa ulimi na mwasi mwenye kuendelea kwa kuishiria uduni wake.

Basi simulia visa, huenda wakatafakari.

Yaani “Ewe Nabii Muhammad (s.a.w.) wasimulie mayahudi kuhusu wakale wao na yaliyowafikia, kama watu wa kijiji kilichokuwa ufukweni mwa bahari na huyu aliyejivua ili yawe ni mazingatio kwao na kuwakanya kukadhibisha utume wako.”

Huu ni mfano muovu kabisa wa watu wanaokadhibisha ishara zetu na wakajidhulumu nafsi zao.
Kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo na kuzikadhibisha ishara zake, yote hayo ni uzushi. Hali ya kwanza inathibitisha katika dini yasiyokuwamo.
Ya pili inakanusha yaliyomo, na huo ndio uzushi (bid’a) hasa, na kila uzushi ni upotevu, na kila upotevu ni katika moto. Kwa hiyo mwenye kuzua ameidhulumu nafsi yake kuiingiza kwenye adhabu na maangamizi. Utauliza mwenye kuipindua haki kwa kuhofia nafsi yake na dhalimu, je, anahisabiwa kuwa mzushi?

Jibu: Ndio, ni mzushi anayestahiki adhabu, hilo halina shaka. Kwa sababu ni juu yake kuhofia ghadhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kuipindua haki sio ghadhabu ya dhalimu kwa kuithibitisha haki.

Inawezekana mtu kuacha kufanya haki kwa kujikinga na madhara, lakini kuipindua dini kwa kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo, hakuna sababu yoyote, vyovyote itakavyokuwa.

مَنْ يَهْدِ اللَّهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِي ۖ وَمَنْ يُضْلِلْ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ {178}

Atakayeongozwa na Mwenyezi Mungu ndiye aongokaye, na atakayepotezwa, basi hao ndio watakaopata hasara.

وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنْسِ ۖ لَهُمْ قُلُوبٌ لَا يَفْقَهُونَ بِهَا وَلَهُمْ أَعْيُنٌ لَا يُبْصِرُونَ بِهَا وَلَهُمْ آذَانٌ لَا يَسْمَعُونَ بِهَا ۚ أُولَٰئِكَ كَالْأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ ۚ أُولَٰئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ {179}

Na hakika tumewaumbia Jahannam majini wengi na watu. Wana nyonyo, lakini hawafahamu kwazo, na wana macho, lakini hawaoni kwayo, na wanayo masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotevu zaidi. Hao ndio walioghafilika.

وَلِلَّهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ {180}

Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri. Basi mwombeni kwayo. Na waacheni wale wanaoharibu utakatifu wa majina yake, watalipwa waliyokuwa wakiyatenda.

وَمِمَّنْ خَلَقْنَا أُمَّةٌ يَهْدُونَ بِالْحَقِّ وَبِهِ يَعْدِلُونَ {181}

Na miongoni mwa tuliowaumba wako watu wanaoongoza kwa haki na kwayo wafanya uadilifu.