read

Aya 178 – 181: Atakaowaongoza Mungu Ndio Watakaoongoka

Maana

Atakayeongozwa na Mwenyezi Mungu ndiye aongokaye, na atakayepotezwa, basi hao ndio watakaopata hasara.

Makusudio sio kuwa yule aliyeumbiwa kuongoka ndiye atakayeongoka na kwamba aliyeumbiwa kupotea ndiye mpotevu. Hapana si hivyo! Maana haya yanakataliwa na maumbile na hali ilivyo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.

Vilevile inakataliwa na nukuu ya Qur’an:

فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا ۖ {108}

“…Basi anayeongoka anaongoka yeye mwenyewe na anayepotea hupotea yeye mwenyewe…” (10:108).

Vipi Mwenyezi Mungu awe na sifa ya uadilifu na wakati huo huo awe ni mpotezaji. Mpotezaji ni shetani:

قَالَ هَٰذَا مِنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ ۖ إِنَّهُ عَدُوٌّ مُضِلٌّ مُبِينٌ {15}

“Akasema hii ni kazi ya shetani, hakika yeye ni adui mpotezaji aliye wazi” (28:15).

Tuanavyo sisi ni kuwa makusudio ya Aya ni kuwa mwenye kuongoka hasa ni yule aliyeongoka mbele ya Mwenyezi Mungu, hata kama mbele ya watu ni mpotevu.

Hakuna mwenye shaka kwamba mtu hawezi kuwa ni muongofu katika mizani ya Mungu ila akiamini na kutenda mema:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ يَهْدِيهِمْ رَبُّهُمْ بِإِيمَانِهِمْ ۖ {9}

“Hakika wale walioamini na wakatenda mema, Mola wao atawaongoa kwa sababu ya imani yao” (10:9).

وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا ۚ {69}

“Na wanaofanya juhudi kwa ajili yetu, tutawaongoa kwenye njia yetu” (29:69)

Vilevile mpotevu ni yule aliyepotea kwa Mwenyezi Mungu sio kwa watu. Kwa maneno mengine ni kwamba Aya inapinga maana ya kuwa basi amefanywa hivyo na Mwenyezi Mungu; kama alivyosema Imam Ali (a.s.): “Utajiri na ufukara ni baada ya kuonekana kwa Mwenyezi Mungu.”

Na hakika tumewauumbia Jahannam majini wengi na watu.

Mwenyezi Mungu hakuumba wala hataumba yeyote kwa ajili ya kumwadhibu. Vipi iwe hivyo? Kwani Mwenyezi Mungu anaona raha kuwaadhibu wanyonge ambao hawana hila yoyote na wala hawanyookewi.

Katika baadhi ya mambo niliyoyasoma, ni kwamba wamarekani walikuwa wanapotaka kujistarehesha, humleta mmoja asiyekuwa mweupe, wanamzunguka na kumiminia mvua ya risasi za bastola zao. Anapoanguka chini akiwa amelowa damu, wao hucheka sana.

Na kwamba Mwenyezi Mungu hatamwunguza mtu katika moto wake akiwa ana jinsia ya kimarekani au Kizayuni. Ametakata Mwenyezi Mungu na wanavyomsifu.

Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemuumba mwanadamu kwa ajili ya kupata elimu yenye manufaa amali njema, na akampa maandalizi yote ya hayo.

Akampa akili yenye kupambanua baina ya uongofu na upotevu, akampelekea Mitume wa kumzindua na kumwongoza, na akamwachia hiyari ya kufuata njia anayoitaka. Kwa sababu uhuru ndio msimamo wa hakika ya mtu. Lau asingempa uhuru angelikuwa sawa na mawe.

Kwa hiyo basi, akichagua njia ya uongofu itampeleka kwenye radhi ya Mwenyezi Mungu na thawabu zake; na akifuata njia ya upotevu basi mwisho wake ni Jahannam, ni marejeo mabaya. Kwa hali hiyo herufi Laam ni ya umwisho; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

فَالْتَقَطَهُ آلُ فِرْعَوْنَ لِيَكُونَ لَهُمْ عَدُوًّا وَحَزَنًا ۗ{8}

“Basi wakamwokota watu na Firauni ili awe adui kwao na huzuni.” (28:8).

Yaani mwisho wake alikuwa adui yao. Utauliza: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنْسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ {56}

“Sikuumba majini na watu ila waniabudu.” (51:56)

Na wewe unasema kuwa mtu ameumbwa kwa ajili ya elimu yenye manu- faa na amali njema, sasa ni vipi?

Jibu: Elimu yenye manufaa na amali njema ni katika twa’a bora zaidi. Imekuja riwaya isemayo: “Mwanachuoni mmoja ni bora kuliko wenye kuabudu elfu na wenye zuhudi elfu.” Riwaya nyingine inasema: “Mwanachuoni anayepatiwa manufaa kwa elimu yake ni bora kuliko wenye kuabudu elfu sabini.”

Wana nyonyo, lakini hawafahamu kwazo, na wana macho, lakini hawaoni kwayo, na wanayo masikio, lakini hawasikii kwayo.

Kitu chochote ambacho hakitekelezi lengo linalotakiwa basi kuweko kwake na kutokuwepo ni sawa. Na katika malengo yaliyokusudiwa moyo ni kufungukia dalili za haki, macho yaone dalili hizi na masikio yasikie. Kama vifaa hivi vitatu ukiviepusha na hayo na wala visinufaike kwa chochote katika dalili ya haki, basi kuweko kwake ni sawa na kutokuwepo. Mwenyezi Mungu anasema:

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ {37}

“Kwa hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au ategaye sikio naye yupo.” (50:37).

Moyo upo na masikio yapo, lakini inafaa kusema haupo ikiwa umeghafilika na haki na dalili zake.

Hao ni kama wanyama

Wana nyoyo, macho na masikio, lakini nyoyo zao hazifungukii haki, macho yao hayaoni dalili za haki na masikio yao hayasikii, basi wakawa kama wanyama.

Bali wao ni wapotevu zaidi.

Kwa sababu wanyama wanatekeleza lengo wanalotakiwa kwa njia ya ukamilifu kwa vile wanashindwa kufikia ukamilifu, na wala hawahisabiwi au kuadhibiwa; na tena mnyama hulijua umbile lake la asili. Makafiri hawatekelezi wanayotakiwa kuyafanya, wanaweza kufikia ukamilifu laki- ni hawafanyi, nao watahisabiwa na kuadhibiwa.

Hao ndio walioghafilika na dalili za Mwenyezi Mungu zilimo katika nafsi zao na pambizoni mwao. Pia wameghafilika na mwisho wao na yale yatakayowapata huko akhera katika hizaya na adhabu.

Je, Majina Ya Mwenyezi Mungu Ni Hayohayo Au Yana Kiasi

Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri.

Majina yote ya Mwenyezi Mungu ni mazuri, kwa sababu yana maana mazuri na makamilifu, na yote yako sawa katika uzuri. Kwani Mwenyezi Mungu hana hali mbalimbali wala sifa zenye kugeuka; hata kwa wale wasemao kuwa sifa yake sio dhati yake, wala pia hana vitendo vinavyotofautiana. Kuumba bawa la mbu na kuumba ulimwengu wote ni sawa kwake. Vyote hupatikana kwa neno “Kuwa na Ikawa.”

Basi mwombeni kwayo.

Yaani mtajeni Mwenyezi Mungu na mwombeni kwa jina lolote mnalolita- ka katika majina yake. Yote hayo ni matamko yanaelezea utakatifu wake na ukuu wake kwa kipimo kimoja; wala Mwenyezi Mungu hana jina kubwa na jina lisilokuwa kubwa.

Kwa ajili hiyo, sisi hatusemi kama wale wanaosema kuwa Mwenyezi Mungu ana jina mahsus ambalo ni katika majina matukufu (Ism A’dham), na kwamba mwenye kulijua atamiminikiwa na kheri nyingi na kuwa na miujiza.
Pia imesemekana kuwa Mwenyezi Mungu ana majina tisini na tisa, na kwamba mwenye kuyajua ataingia peponi; kama kwamba pepo imeumbi- wa watungaji kamusi za lugha na sio wacha Mungu.

Na waacheni wale wanaoharibu utakatifu wa majina yake, watalipwa waliyokuwa wakiyatenda.
Kuharibu ni kuacha lengo lililokusudiwa. Maana ya ujumla ni kukataza kabisa tamko lolote linalotambulisha Uungu kwa mwingne; awe Mtume, nyota, sanamu au kitu chochote kingine. Vilevile haijuzu kabisa kutumia tamko litakalofahamisha usiokuwa Ungu, kama vile baba na mwana.

Wametofautiana maulamaa wa Tawhid kuhusu majina ya Mwenyezi Mungu mtukufu, kuwa je, ni hayo hayo au yana kiasi. Maana ya kuwa ni hayo hayo ni kusimama katika majina yake yaliyotajwa kwenye Qur’an na Hadith; kiasi ambacho haijuzu kabisa jina lolote isipokuwa liwe limetokana na nukuu ya Aya au Hadith.

Maana ya kuwa yana kiasi ni kuwa jina loloate ambalo maana yake yanathibiti katika haki yake Mwenyezi Mungu, basi inajuzu kulitumia, ni sawa liwe limenukuliwa au la.

Maulama wengi wamesema kuwa majina ya Mwenyezi Mungu ni hayo hayo tu. Ama sisi tunaona kuwa inafaa kumwita au kumwomba MwenyeziMungu kwa jina lolote linalofahamisha utukatifu na utukufu wake; ni sawa liwe limenukuliwa kwenye Qur’an na Hadith au la.

Hatujizui ila lile lilozuiwa na Mwenyezi. Tunasema hivyo kwa kutegemea msingi wa: “Kila kitu ni halali mpaka kielezwe kukatazwa kwake.”

Haya ndiyo yanayopitishwa na elimu ya misingi ya kidini; kuongezea kongamano (Ijma’i) la umma, zamani na sasa, kuwa wasiokuwa waarabu wanaweza kuitaja dhati ya Mwenyezi Mungu, sifa zake na vitendo vyake kwa lugha zao.

Na miongoni mwa tuliowaumba wako watu wanaoongoza kwa haki na wafanyao uadilifu.

Katika watu kuna Mu’min na kafiri na mwema na mwovu, wote wanajua hakika hii, sasa kuna makusudio gani kubainisha?

Jibu: Katika Aya iliyotangulia, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amesema kuwa wengi katika majini na watu mwisho wao ni Jahannam, kwa hiyo ikanasi- bu hapa kusema kuwa miongoni mwao mwisho wake ni pepo, hata ingawaje ni wachache kuliko wale; kama lilivyofahamisha neno miongoni. Amewaita watu wa peponi kwa ibara ya wanaoongoza kwa haki na kufanya uadilifu kuishiria kuwa sababu inayowajibisha kuingia kwao peponi ni uongofu na uadilifu.

وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا سَنَسْتَدْرِجُهُمْ مِنْ حَيْثُ لَا يَعْلَمُونَ {182}

Na wale waliokadhibisha ishara zetu, tutawavuta kidogo kidogo kidogo kwa namna wasiyoijua.

وَأُمْلِي لَهُمْ ۚ إِنَّ كَيْدِي مَتِينٌ {183}

Nami nitawapa muda, hakika hila yangu ni madhubuti.

أَوَلَمْ يَتَفَكَّرُوا ۗ مَا بِصَاحِبِهِمْ مِنْ جِنَّةٍ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا نَذِيرٌ مُبِينٌ {184}

Je, hawafikiri kuwa mwenzao hana wazimu? Hakuwa yeye ila ni mwonyaji aliye dhahiri.

أَوَلَمْ يَنْظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّهُ مِنْ شَيْءٍ وَأَنْ عَسَىٰ أَنْ يَكُونَ قَدِ اقْتَرَبَ أَجَلُهُمْ ۖ فَبِأَيِّ حَدِيثٍ بَعْدَهُ يُؤْمِنُونَ {185}

Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na alivyoviumba Mwenyezi Mungu. Na kuwa pengine ajali yao imekwisha karibia. Basi ni mazungumzo gani baada yake watakayoyaamini?

مَنْ يُضْلِلِ اللَّهُ فَلَا هَادِيَ لَهُ ۚ وَيَذَرُهُمْ فِي طُغْيَانِهِمْ يَعْمَهُونَ {186}

Ambaye Mwenyezi Mungu humpoteza hana wa kumwongoza. Na anawaacha katika upotofu wao waki-mangamanga.