read

Aya 182 – 186: Waliokadhibisha Aya Zetu

Maana

Na wale waliokadhibisha ishara zetu, tutawavuta kidogo kidogo kwa namna wasiyojua.

Huwa zikafululiza neema kwa mtu, naye akaendelea kupetuka mipaka kwa kuhadalika na wingi wake na utajiri huku akisahau yaliyofichikana na yajayo ghafla, mpaka watu wakisema kheri zote ni zake, basi humjia ghafla kuharibikiwa.

Abu Sufyan alihadaika siku ya Uhud akasema: “Leo tumewalipizia siku ya Badr”, lakini ulipokuja msaada wa Mwenyezi Mungu na ushindi, alisilimu akiwa mnyonge. Imam Ali (AS) anasema: “Ni wangapi wanachukuliwa kidogo kidogo kufanyiwa hisani, na wanaohadaliwa kwa kusitiriwa, na wanaofitiniwa kwa kuambiwa maneno mazuri. Na hakujaribiwa yeyote na Mwenyezi Mungu mfano wa kupewa muda.”

Nami nitawapa muda, hakika hila yangu ni madhubuti.

Makusudio ya hila ya Mwenyezi Mungu ni kwamba yeye atawaacha wahadaike na hisani yake ya dhahir, mpaka wakielemea, basi huwachukua bila ya kujua.

أَيَحْسَبُونَ أَنَّمَا نُمِدُّهُمْ بِهِ مِنْ مَالٍ وَبَنِينَ {55}

نُسَارِعُ لَهُمْ فِي الْخَيْرَاتِ ۚ بَ{56}

“Je, wanadhani ya kuwa kwa vile tunavyowapa mali na watoto ndio tunawahimizia kheri? Bali hawatambui.” (23: 55 56).

Je, hawafikiri kuwa mwenzao hana wazimu? Hakuwa yeye ila ni mwonyaji aliye dhahiri.

Hivi ndivyo wezi, wauaji wanavyoeneza propaganda zao dhidi ya kila mwenye ikhlas, kila wakati na kila mahali. Nabii Muhammad (s.a.w.) ni mwenda wazimu, mchawi na mwongo. Kwa nini? Kwa vile tu yeye anakataa uongo na upotevu na kuupiga vita wizi na unyang’anyi.

Makureish walimzulia Nabii Muhammad (s.a.w.) wakiwa wanamjua tangu utoto wake mpaka kufikia miaka arubaini katika umri wake mtukufu. Wanamjua akili aliyo nayo, ukweli na uaminifu. Lakini Vilevile wanajua kuwa ujumbe wa Nabii Muhammad (s.a.w.) ndio hatari kubwa juu ya utawala wa Kikuraish. Ni kwa ajili hii pekee ndio wakasema yeye ni mwenda wazimu, ili angalau wahadaike wale wanaowatawala na kuwanyonya.

Ndipo Qur’an ikawalingania kwenye kufikiri na kuzingatia jambo la Nabii Muhammad (s.a.w.), naye ni mwenzao na jamaa yao waliyempima, wafikiri, je, wamempata na lawama yoyote au wamepata katika akili yake na hulka yake tuhuma yeyote?

Hakuwa yeye ila ni muonyaji aliye dhahiri anayebainisha haki na kumwonya anayemhalifu. Hili ndilo kosa pekee kwao.

Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na alivyoviumba Mwenyezi Mungu.

Yaani mbingu na ardhi na vyote vilivyomo vinanyenyekea ufalme wake na kufahamisha umoja wake, na kwamba hakuna yeyote mwenye akili atakayeangalia vitu hivi vilivyopo, bila ya kuwa na lengo jingine lolote, ila atamwamini Mwenyezi Mungu, vitabu vyake na Mitume yake.
Ama ambaye hafikirii isipokuwa maslahi yake tu, haongoki wala hataongoka kwa Mwenyezi Mungu wala kwa kitu chochote cha kheri.

Na kuwa pengine ajali yao imekwisha karibia.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuwataka wafikiri kuzingatia maumbile ya ulimwengu na vitu vyake sasa, anawazindua kwenye mauti, mvunja starehe na mtawanyaji makundi, na kwamba hayo mauti huenda yakawajia ghafla hivi karibuni na wao wakiwa wanaendelea katika upotevu wao. Amezindua hivi, huenda wao wakatubu na kuelekea kwenye uongofu.

Basi ni mazungumzo gani baada yake watakayoyaamini?

Dhamir ya yake inarudia Qur’an. Hakuna ubainifu wa kutosheleza baada ya Qur’an wala dalili yenye nguvu zaidi yake. Ambaye hakinaishwi na dalili za Mwenyezi Mungu basi hakinaishwi na chochote.

Ambaye Mwenyezi Mungu humpoteza hana wa kumwongoza.

Tumetaja maana yake punde tu katika kufasiri Aya 178 ya Sura hii.

Na anawaacha katika upotofu wao wakimangamanga.

Yaani Mwenyezi Mungu atawaacha wakitangatanga ovyo katika upotevu na kuwapa muda kisha awalipe yale waliyoyafanya nyuma. Wala kuwapuuza huko sio dhulma. Kwa sababu kumekuja baada ya ubainifu na hadhari, na baada ya kukata tamaa ya kuwakemea na kuwaongoza.

يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِنْدَ رَبِّي ۖ لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ ۚ ثَقُلَتْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا تَأْتِيكُمْ إِلَّا بَغْتَةً ۗ يَسْأَلُونَكَ كَأَنَّكَ حَفِيٌّ عَنْهَا ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِنْدَ اللَّهِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ {187}

Wanauliza hiyo saa (Kiyama) kutokea kwake kutakuwa lini? Sema: Ujuzi wake uko kwa Mola wangu. Hakuna wa kuidhihirisha kwa wakati wake ila yeye tu. Ni nzito katika mbingu na ardhi. Haitawafikia ila kwa ghafla tu. Wanakuuliza kama kwamba unaidadisi. Sema, Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu tu, Lakini watu wengi hawajui.

قُلْ لَا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّهُ ۚ وَلَوْ كُنْتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ ۚ إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ {188}

Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Na lau kama ningelijua ghaibu ningelijizidishia kheri nyingi, wala isingelinigusa dhara. Mimi si chochote ila ni mwonyaji na mtoaji bishara kwa watu wanaoamini.