read

Aya 187 – 188: Wanakuuliza Saa (Kiyama)

Maana

Wanauliza hiyo saa (Kiyama) kutokea kwake kutakuwa lini? Sema: Ujuzi wake uko kwa Mola wangu. Hakuna wa kuidhihirisha kwa wakati wake ila yeye tu.

Makusudio ya saa ni utakapokwisha ulimwengu na kufa viumbe.

Dhahiri ya Aya inafahamisha kwamba, jamaa walimwuliza Mtume Muhammad (s.a.w.): “Kiyama kitakuwa lini.” Mwenyezi Mungu akamwamrisha awaambie kwamba hiyo ni katika mambo ambayo hayako chini ya uwezo wa mtu katika kuyajua, na kwamba ujuzi wake unahusika na Mwenyezi Mungu tu peke yake, yeye ndiye atakayeidhihirisha wakati wake uliopangwa.

Ni nzito katika mbingu na ardhi.
Yaani ni nzito kutokea kwake kwa watu wa mbingu na ardhi kwa ukuu wake na ukali wake.

Haitawafikia ila kwa ghafla tu, bila ya kutangaza mapema.

Wanakuuliza kama kwamba unaidadisi.
Yaani kama kwamba wewe unapupa sana kujua saa itakuwa lini. Mtume (s.a.w.)hakuwaakijishighulishanakujuaKiyamakitakuwalini;isipokuwa alikuwa akijishughulisha na kuifanyia amali saa hiyo ya kiyama, kuonya watu na kuunganisha kati ya kuokoka na vituko vyake na kufanya amali njema. Kwa ajili hii ndio hakumuliza Mola wake kuhusu saa hiyo.

Imesemekana kuwa bedui mmoja alimwuliza Mtume (s.a.w.): “Ni lini itakuwa hiyo saa? Akamjibu: “Umeiandalia nini?” Kwa jibu hili anakusudia kumfahamisha kuwa ubora kwako ni kuuliza kitakachokuokoa wakati huo itakapofika na si kujua wakati wake na picha yake. Mwenye akili akipatwa na ugonjwa haulizi namna ya kufa na ugonjwa huo, isipokuwa anauliza ni lipi litakalomponesha na ugonjwa huo.

Tena amerudia Mwenyezi Mungu kusema: Sema, Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu tu, kwa kutilia mkazo kuwa ujuzi wa hiyo saa uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake, na pia ni utangulizi wa kauli yake, Lakini watu wengi hawajui kwamba ujuzi wa saa uko kwa aliyeiumba wala hajui mwengine yoyote.

Mtume Na Elimu Ya Ghaib.

Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara ila apendavyo Mwenyezi Mungu.

Hii ndiyo itikadi ya Waislamu kwa Mtume wao Muhammad (s.a.w.) mtukufu wa viumbe vyote vya Mwenyezi Mungu. Yeye mwenyewe hajimilikii nafsi yake sikwambii kummilikia mwingine. Na itikadi hii kwa Nabii Muhammad ni natija ya itikadi ya Tawhid.

Na lau kama ningelijua ghaibu ningelijizidishia kheri nyingi, wala isingelinigusa dhara.

Neno ghaibu halifahamishi maana yake tu, bali vilevile linafahamisha kuwa ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu peke yake.

Zaidi ya dalili hii ni kwamba aliye karibu zaidi na Mola wake kuliko yey ote, anawatangazia watu kuwa yeye mbele ya ghaibu ni mtu wa kawaida tu, hana tofauti na watu wengine. Kisha hatosheki na tangazo hili, bali analitoleadalilihilokwahisianadhamiri,kuwalaukamayeyeangelijua ghaibu basi angelijua mwisho wa mambo, hapo angefanya lile ambalo mwisho wake ni wema na kuliacha lile ambalo mwisho wake ni shari na yasingempata yale anayoyachukia kumpata katika maisha haya.

Na ili mtu asije akasema: Itakuwaje Nabii Muhammad (s.a.w.) hajui ghaibu naye ni Mtume mwenye kukurubishwa kwa Mwenyezi Mungu, ndio Nabii Muhammad akasema:

Mimi si chochote ila ni mwonyaji na mtoaji bishara kwa watu wanaoamini.

Yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, hilo halina shaka, lakini umuhimu wa Mtume unathibitika kwa kufikishia watu ujumbe wa Mola wao na kumwonya kwa adhabu yule mwenye kutii. Ama elimu ya ghaibu, kunufaisha na kudhuru, hayo yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu peke yake.

Amewahusisha waumini kwa bishara na maonyo, pamoja na kuwa yanawahusu watu wote, kuishiria kwamba anayenufaika na hayo ni yule tu anayeitaka haki na imani, ama mwenye kiburi halimfai yeye jambo lolote. Utauliza: Yamekuja maelezo katika sera ya Mtume na vitabu vya Hadith kwamba Nabii Muhammad (s.a.w.) ametolea habari mambo mengi ya ghaibu, kama vile kuwa waislamu baadaye watawashinda warumi na wafursi, na kwamba Salman Farsy atavishwa taji la Kisra kichwani kwake, na ikawa.
Vilevile alitoa habari ya mauti ya Najash, na kufa shahid Zaid bin Harith, Jafar bin Abu Talib na Abdallah bin Rawaha, na pia kuhusu mbweko wa mbwa wa Hawab kwa Aisha kupigana na Ali bin Abu Twalib na wavunja ahadi waliokengeuka, na Khawarij, kufa shahid kwa mjukuu wake, Husein bin Ali na mengine mengi. Sasa itakuwaje hayo na kauli yake. Lau ningelijua ghaibu.

Jibu: Ghaib za Mwenyezi Mungu hazina mpaka wala idadi. Na ghaibu ziko aina nyingi.
Kuna aina anayoificha Mwenyezi Mungu na wala hamfichulii yeyote katika waja wake vyovyote walivyo, kama vile kuja saa ya Kiyama.

Aina nyingine humfichulia anayemridhia katika waja wake. Hayo ameyashiria katika Aya isemayo:

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا {26}إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِنْ رَسُولٍ فَإِنَّهُ{27}

Yeye ndiye mjuzi wa ghaibu wala hamdhihirishii ghaibu yake yoyote, isipokuwa Mtume wake aliyemridhia.” (72: 26 27).

Na pia Aya isemayo:

وَمَا كَانَ اللَّهُ لِيُطْلِعَكُمْ عَلَى الْغَيْبِ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ يَجْتَبِي مِنْ رُسُلِهِ مَنْ يَشَاءُ ۖ فَآمِنُوا بِاللَّهِ وَرُسُلِهِ ۚ وَإِنْ تُؤْمِنُوا وَتَتَّقُوا فَلَكُمْ أَجْرٌ عَظِيمٌ {179}

“Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwafunulia mambo ya ghaibu, lakini Mwenyezi Mungu humchagua amtakaye katika Mitume yake. Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mitume Yake.” Juz.4 (3:179).

Na kuna aina nyingine anawafichulia watu wote, kama vile ufufuo, pepo na moto.

Makusudio ya kuwa ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu na iko kwa Mwenyezi Mungu, ni kuwa hakuna njia ya kuijua kwa majaribio, akili wala kwa kitu chochote isipokuwa kwa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu mtukufu. Naye humpa wahyi kwa sehemu ndogo ya ghaibu yake kulingana na heki- ma inavyotaka na haja ya watu. Na Mtume naye kwa nafasi yake hii huwapa watu habari ya ghaibu hiyo; kama alivyoipokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa hiyo basi hakuwi kutolea habari kwa Mtume kuwa ni kujua ghaibu, bali ni kunakili kutoka kwa mwenye ujuzi wa ghaibu. Na tofauti ni kubwa baina ya chimbuko la ujuzi na yule anayenukuu kutoka kwenye chimbuko hilo. Kwa sababu, wa kwanza ni shina na wapili ni tawi. Vilevile kuna tofauti baina ya anayenukuu kutoka kwenye shina moja kwa moja na yule anaye nukuu kwa mnukuu huyu.

قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنْتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ {32}

Wakasema: Utakatifu ni wako hatuna elimu isipokuwa ile uliyotufundisha; hakika wewe ndiwe mjuzi, mwenye hekima.” Juz.1 (2:32).

Aya hizi ni dalili mkataa juu ya kubatilika wanayoyasema masufi kwamba nafsi ya mtu kwa upande wa mazoezi ya kiroho inageukea kwenye mambo ya ghaibu na mgeuko huu wameuita elimu ya kimungu. Sijui masufi wanachanganya vipi itikadi hii ya elimu ya kimungu na kumwamini Mwenyezi Mungu na Utume wa Nabii Muhammad (s.a.w.)?

Ya kushangaza zaidi ni yale aliyoyasema Ibn Al-Araby, katika Kitab Futuhatil – Makkiyya Juz.3 mlango wa 311, kwamba mwenye kumpenda Mwenyezi Mungu kwa mapenzi halisi anaweza kuigeuza nafsi yake kwenye kitu chochote anachotaka, iwe mnyama, mti, jiwe au maji.

Na kuwa hayo yametokea. Kwamba mmoja wa wapenzi wa Twariqa hii, yaani ya kisufi aliingia kwa Sheikh akajigeuza mbele yake kuwa ukufi wa maji. Sheikh alipoulizwa, fulani ameingia kwako na hakutoka, yuko wapi? Akawaambia: “Haya maji ndiye yeye!”

هُوَ الَّذِي خَلَقَكُمْ مِنْ نَفْسٍ وَاحِدَةٍ وَجَعَلَ مِنْهَا زَوْجَهَا لِيَسْكُنَ إِلَيْهَا ۖ فَلَمَّا تَغَشَّاهَا حَمَلَتْ حَمْلًا خَفِيفًا فَمَرَّتْ بِهِ ۖ فَلَمَّا أَثْقَلَتْ دَعَوَا اللَّهَ رَبَّهُمَا لَئِنْ آتَيْتَنَا صَالِحًا لَنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ {189}

Yeye ndiye aliyewaumba katika nafsi moja, na katika hiyo akamjaalia mkewe ili apate utulivu kwake Alipomkurubia alishika mimba nyepesi na kutembea nayo. Hata alipokuwa mzito, wote wawili walimwomba Mola wao, kama ukitupa mwema tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.

فَلَمَّا آتَاهُمَا صَالِحًا جَعَلَا لَهُ شُرَكَاءَ فِيمَا آتَاهُمَا ۚ فَتَعَالَى اللَّهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ {190}

Basi alipowapa mwema walimfanyia washirika katika kile alichowapa. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu na hao wanaowashirikisha.