read

Aya 189 – 190: Aliyewaumba Katika Nafsi Moja

Maana

Aya mbili hizi sio masimulizi ya tukio lililotokea baina ya mtu na mkewe, kama inavyoonyesha dhahiri ya matamshi, isipokuwa ni kuzungumzia hali ya mtu alivyo, bila ya kuangalia mtu maalum.

Kwa ufupi masimulizi ya hali hiyo au tamthilia hiyo ni kuwa mtu akipatwa na machukivu au akitaka kupata ayatakayo hukimbilia kwa Mwenyezi Mungu akimwomba na kunyenyekea huku akiweka ahadi kwamba Mwenyezi Mungu akimpatia anayoyataka basi atamshukuru na kumtii, lakini akimpatia yale anayoyataka, hana habari tena na ahadi zake.

Baada ya utangulizi huu, inatakikana kufahamiwa misingi ya Aya hizi tunayoifafanua kama ifuatavyo.

Yeye ndiye aliyewaumba katika nafsi moja, na katika hiyo akamjaalia mkewe ili apate utulivu kwake.

Maneno katika ‘Aliyewaumba’ yanaelekezwa kwa watu wote. Maana ni kuwa. Enyi watu wote nyinyi ni kitu kimoja, kwa kwa jinsia, maumbile na rangi. Hakuna tofauti kabisa baina ya wa mashariki na wa magharibi, mwarabu na mwajemi, mweusi na mweupe wala baina ya mwanamume na mwanamke.

Suala la jinsia linahusu vitu vyote. Mwenyezi Mungu anasema:

وَمِنْ كُلِّ شَيْءٍ خَلَقْنَا زَوْجَيْنِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ {49}

“Na katika kila kitu tumeumba dume na jike ili mpate kujua.” (51:49)

Lengo katika hilo linajulikana, nalo ni kuchunga aina. Kuongezea lengo hilo ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amemuumba mtu mke katika jinsi yake ili kila mmoja kati ya wawili hao apate utulivu kwa mwenzake na kuweko mapenzi na kuhurumiana baina ya wawili hao.

Alipomkurubia alishika mimba nyepesi na kutembea nayo. Hata alipokuwa mzito, wote wawili walimwomba Mola wao, kama ukitupa mwema tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.

Kumkurubia, ni kumwingilia, kutembea nayo, ni kuendelea mimba bila ya kutoka, na kuwa mzito, ni kukaribia wakati wa kuzaa. Wakati huu ndipo baba na mama huelekea kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na kumnyenyekea awaruzuku mtoto mwema; yaani aliye sawa kimaumbile na kihulka. Na kama Mwenyezi Mungu akiwatakabalia basi watashukuru neema hii kwa ukamilifu.

Basi alipowapa mwema walimfanyia washirika katika kile alichowapa.

Dhamir ya walifanya, ni ya mume na mke. Makusudio ya alichowapa ni mtoto waliyemtaka. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu alipowapa mtoto, walisema, kuwa fadhila na baraka ni za masanamu na wakamsahau Mwenyezi Mungu na yale waliyomwahidi.

Basi ametukuka Mwenyezi Mungu na hao wanaowashirikisha.

Yaani wanashirikisha makafiri wakiwemo hawa wawili mke na mume. Kwa mara nyingine tena tunasema kuwa lengo la masimulizi ni hali ya mtu alivyo, sio tukio maalum.

أَيُشْرِكُونَ مَا لَا يَخْلُقُ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ {191}

Je, wanawashirikisha wale ambao hawaumbi kitu, hali wao wameumbwa?

وَلَا يَسْتَطِيعُونَ لَهُمْ نَصْرًا وَلَا أَنْفُسَهُمْ يَنْصُرُونَ {192}

Wala hawawezi kuwasaidia wala kujisaidia wenyewe.

وَإِنْ تَدْعُوهُمْ إِلَى الْهُدَىٰ لَا يَتَّبِعُوكُمْ ۚ سَوَاءٌ عَلَيْكُمْ أَدَعَوْتُمُوهُمْ أَمْ أَنْتُمْ صَامِتُونَ {193}

Na kama mkiwaita kwenye uwongofu hawatawafuata. Ni sawa ikiwa mtawaita au mtanyamaza.

إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ عِبَادٌ أَمْثَالُكُمْ ۖ فَادْعُوهُمْ فَلْيَسْتَجِيبُوا لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {194}

Hakika hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni waja mfano wenu. Hebu waombeni nao wawaitikie ikiwa nyinyi mnasema kweli.

أَلَهُمْ أَرْجُلٌ يَمْشُونَ بِهَا ۖ أَمْ لَهُمْ أَيْدٍ يَبْطِشُونَ بِهَا ۖ أَمْ لَهُمْ أَعْيُنٌ يُبْصِرُونَ بِهَا ۖ أَمْ لَهُمْ آذَانٌ يَسْمَعُونَ بِهَا ۗ قُلِ ادْعُوا شُرَكَاءَكُمْ ثُمَّ كِيدُونِ فَلَا تُنْظِرُونِ {195}

Je, wao wanayo miguu ya kuendea? Au wanayo mikono ya kushika? Au wanayo macho ya kuonea? Au wanayo masikio ya kusikiliza? Sema: Waiteni hao mnaowashirikisha kisha nifanyieni vitimbi wala msinipe muda.

إِنَّ وَلِيِّيَ اللَّهُ الَّذِي نَزَّلَ الْكِتَابَ ۖ وَهُوَ يَتَوَلَّى الصَّالِحِينَ {196}

Hakika mlinzi wangu ni Mwenyezi Mungu aliyeteremsha Kitab naye ndiye awalindaye wafanyao mema.

وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِنْ دُونِهِ لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَكُمْ وَلَا أَنْفُسَهُمْ يَنْصُرُونَ {197}

Na wale mnaowaabudu badala yake hawawezi kuwasaidia wala kujisaidia wenyewe.

وَإِنْ تَدْعُوهُمْ إِلَى الْهُدَىٰ لَا يَسْمَعُوا ۖ وَتَرَاهُمْ يَنْظُرُونَ إِلَيْكَ وَهُمْ لَا يُبْصِرُونَ {198}

Na kama mkiwaita kwenye uongofu hawatasikia. Na unawaona wanakutizama, nao hawaoni.