read

Aya 199 – 203: Shika Usamehevu

Maana

Shika usamehevu na amrisha mema na achana na wajinga.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimfunza tabia njema Mtume wake Nabii Muhammad (s.a.w.), naye alikuwa akisema katika dua yake: “Ewe Mwenyezi mungu nifanye mzuri wa maumbile na tabia na niepushe na tabia mbaya.” Alimwitikia dua yake na akamtimizia tabia njema kisha akamtuma kutimiza tabia njema kwa watu wote.

Aya hii ni miongoni mwa mafunzo ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake mtukufu (s.a.w.). nayo imekusanya misingi mitatu ya sharia na adabu.

Usamehevu.

Nao ni kuchukulia upole bila uzito wala mashaka. Nako kunakua katika vitendo na hulka. Na katika mali ni ile iliyozidi haja.
Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake kutowatia kwenye uzito na mashaka katika anayowaamrisha na kuwakataza. Na kuchukua Zaka ya mali yao katika kinachozidi haja zao. Huu ni msingi katika misingi ya sharia.

وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ۚ {78}

Wala hakuweka juu yenu uzito katika dini.” (22:78).

Na pia alimwamrisha kutowakalifisha hulka; kama kumwamrisha mmoja wao asamehe deni lake au asichukue kisasi.
Kuamrisha mema.

Ni kheri inayojulikana na iliyo wazi anayoijua mtu kwa umbile lake.

Na achana na wajinga.

Wale ambao hakutarajiwi kuongoka kwao kwa hoja na dalili wala kwa mawaidha na uongozi. Huenda ikawa kuwapuuza na kuachana nao ni vizuri kuliko kuwaongoza.

Amesema Sheikh Maraghi katika tafsir ya Aya hii: “Imepokewa kutoka kwa Jafar As-Sadiq (r.a.) kwamba yeye amesema: “Hakuna katika Qur’an Aya inayokusanya maadili mema kama hii.”

Na kama uchochezi wa shetani ukikuchochea, basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu; hakika yeye ndiye asikiaye na ajuaye.

Mtume hukasirika, hilo halina shaka, lakini yeye anakasirika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; hata kukasirika kwa nafsi yake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Huenda akakasirikia ujinga wa mjinga katika alioamrishwa kuachana nao na kutaka kumkabili kwa neno litakalomstahiki.

Ndipo Mwenyezi Mungu mtukufu akamwambia kwa kumfundisha: Ikisadifu kukutokea mfano wa hali hii, basi ghadhabu isiondoe upole wako, vumilia na mtake hifadhi Mwenyezi Mungu, kwani yeye anakusikia na kukuitikia na anajua yanayokupata kutoka kwa wajinga.

Hapana budi kuishiria kuwa kauli yake hii Mwenyezi Mungu ni kiasi cha kukadiria tu, kutokana na neno ‘kama’ sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ {65}

”Kama ukishirikisha, hakika amali zako zitapomoka na utakuwa miongoni mwa wenye hasara” (39:65).

Kimsingi ni kwamba kukadiri muhali sio muhali. Katika Juz.3 (3:60) kifungu ‘Mtume na Isma’, tumebainisha kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaweza kuwakataza maasi Mitume wake walio maasum. Kwa sababu kukataza kwake kunatoka juu kuja chini; na wala haijuzu kwa yeyote, asiyekuwa Mwenyezi Mungu, kuwaamrisha au kuwakataza.

Hakika wale wenye takuwa zinapowagusa pepesi za shetani huzinduka.

Hakuna mtu asiyeshindana na misukumo ya kibinafsi, baadhi yake ni ya tamaa ya moyo, mingine ni ya akili na pia ya kidini.

Mara nyingi dini na akili hushindwa na msukumo wa moyo. Kwa sababu unachimbuka katika dhati ya mtu, na unakuwa naye tangu yuko tumboni mwa mama yake.

Na akili inakuja baadae, nayo hukua kwa mafunzo na majaribio. Ama dini imeletwa kuuzoeza msukumo wa moyo na kuufunga hatamu.
Nayo utendaji kazi wake ni dhaifu, isipokuwa tu kwa mtu aliyekinai kwa nafsi yake na dhati yake, kwa namna ambayo haoni wema, isipokuwa wa dini na kufanya amali kulingana na hukumu zake.

Aina hii ya wanadini ndio wale ambao dini yao inashinda mapondokeo yao. Ndio wanokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: Zinapowagusa pepesi za shetani huzinduka” Yaani shetani akiwahadaa kwa maasia ya Mwenyezi Mungu au akiwapa wasiwasi wa nafsi inayoamrisha uovu, basi hukumbuka aliyowaamrisha Mwenyezi Mungu na aliyowakataza. Mara wao hutambua vitimbi vya shetani na wasiwasi wa nafsi, basi hujizuia na maasi na dini yao hushinda hawa zao.

Na ndugu zao wanawavutia katika upotofu kisha wao hawaachi.

Makusudio ya ndugu hapa ni mashetani. Dhamir ya ndugu zao inarudia kwa washirikina ambao wametajwa. Makusudio ya hawaachi, ni kuwa shetani haachi kuwapoteza washirikina na kuwaharibu. Kwa ufupi ni kwamba mashetani ndio ndugu wa washirikina hawaachi kuwapoteza.

Na usipowaletea ishara, husema: Kwa nini hukuibuni?

Washirikina walikuwa wamemtaka Mtume miujiza maalum kwa njia ya inadi. Kama hakuwaletea muujiza huo husema: Kwani huwezi kuufanya mwenyewe, kwani wewe si ni Mtume?

Sema: Hakika nafuata niliyopewa wahyi kutoka kwa Mola wangu tu.

Yaani sema ewe Muhammad kuwaambia hawa wenye inadi: Ndio mimi ni Mtume, lakini Mtume hatengenezi muujiza wala haonyeshi ishara yoyote au kuipendekeza kwa Mwenyezi Mungu; bali anangoja wahyi na kuufik- isha kwa waja wake.

Hii ni busara zitokazo kwa Mola wenu na ni uwongofu na rehema kwa watu wanaoamini.

Hii ni ishara ya Qur’an na busara ni hoja na dalili ambazo mwenye akili anapata busara kwazo.

Baada ya Mtume (s.a.w.) kuwaambia washirikina kuwa nafuata niliyope- wa wahyi kutoka kwa Mola wangu, aliwaambia, na Mwenyezi Mungu amenipa wahyi hii Qur’an ambayo ina dalili wazi za utume wangu. Nayo ni uwongofu na rehema kwa anayetaka kuamini haki kwa njia ya haki.

Mkiwa mwaitafuta haki, kama mnavyodai, basi acheni shirk na msilimu. Vinginevyo basi nyinyi ni watafutaji manufaa na watu wa malengo yenu tu.

وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنْصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ {204}

Na isomwapo Qur’an isikilizeni na mnyamaze ili mpate kurehemiwa.

وَاذْكُرْ رَبَّكَ فِي نَفْسِكَ تَضَرُّعًا وَخِيفَةً وَدُونَ الْجَهْرِ مِنَ الْقَوْلِ بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ وَلَا تَكُنْ مِنَ الْغَافِلِينَ {205}

Na mtaje Mola wako nafsini mwako kwa unyenyekevu na hofu na bila ya kupiga kelele kwa kauli, asubuhi na jioni. Wala usiwe miongoni mwa walioghafilika.

إِنَّ الَّذِينَ عِنْدَ رَبِّكَ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَيُسَبِّحُونَهُ وَلَهُ يَسْجُدُونَ ۩ {206}

Hakika wale walioko kwa Mola wako hawajivuni wakaacha kumwabudu na wanamtakasa na wanaumsujudia.