read

Aya 24: Dini Na Maisha

Mwenye kuujua vilivyo Uislamu atakuta kila asili ya itikadi yake na kila tawi la sharia yake inasimamia kwa uwazi au kuwa na madhumuni ya kufanya kazi kwa ajili ya uhai (maisha).

Kumwamini Mungu ni imani iliyo na mwito wa kujikomboa na utumwa, isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu mmoja peke yake, na kwamba hakuna utawala kwa sababu ya mali wala jaha au jinsi au kitu chochote kile isipokuwa kwa haki na uadilifu.

Kimsingi ni kwamba maisha mema yenye nguvu hayapatikani na ni muhali kupatikana ila kwa kushikamana na msingi huu na kuufuatilia.

Ama kuamini Utume wa Muhammad (s.a.w.) kwenyewe ni kuamini sharia ya udugu na usawa, uhuru wa mtu na himaya yake na kila msingi ambao unampa binadamu kheri njema. Hilo ni kwa vile utume wa Muhammad unalenga kwenye uongofu wa mtu na wema wake na kueneza uadilifu baina ya watu.
Kuamini siku ya mwisho ni kuamini kuwa mtu hataachwa bure na kwamba yeye ataulizwa kila dogo na kubwa katika amali zake. Atahisabiwa na kulipwa; ikiwa ni kheri basi atalipwa kheri, na ikiwa ni shari basi atalipwa shari. Imani hii, kama unavyoona, inafanana na serikali kuu, au mhimizaji wa matendo yanayowajibisha kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume.

Hayo ni katika yale yanayohusiana na misingi ya itikadi. Ama matawi ya dini, yaani yale yanayofaa kufanywa na yasiyofaa katika sharia ya kiislamu, huwa yanasimamia misingi ya binadamu, iliyoashiriwa na kauli yake Imam Jafar As-Sadiq (a.s.): “Kila lililo na masilahi kwa watu kwa upande fulani basi linajuzu na kila lililo na ufisadi kwa upande fulani basi halijuzu.

Huu ndio mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume ulioelezwa na Qur’an waziwazi:

Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita kwenye lile litakalowapa uhai.

Tukiinganisha Aya hii na ile isemayo: “Sema mtiini Mwenyezi Mungu, kama wakikata, basi hakika Mwenyezi Mungu hawapendi Makafiri” Juz.3 (3:32), tutapata picha hii ya makisio ya kimantiki kuwa: Mungu na Mtume wametoa mwito kwa ajili ya maisha na akahukumu ukafiri wa kila anayepinga mwito huu. Kwa hiyo natija ni kuwa asiyetenda kwa ajili ya maisha basi ni kafiri1.

Kwa hali hiyo basi inatubainikia kuwa Uislamu unakwenda sambamba na maisha, na kwamba kila ambalo liko mbali na maisha basi si Uislamu chochote.

Kila mtu, vyovyote awavyo, akilingania kwenye maisha yasiyokuwa na unyanyasaji, dhulma au matatizo, basi mwito wake huo unakutana na mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume, apende asipende.

Na yule anayeikingamia njia ya maisha na maendeleo yake, basi huyo ni adui wa Mwenyezi Mungu na Mtume, hata akiswali usiku na kufunga mchana.

Ama vikundi vilivyojitokeza siku hizi ambavyo vimeiuza dini yake kwa uzayuni na ukoloni, huku vikijificha kwa jina la dini, tumevielezea kaatika Juz. 4 (3:142).

Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake na kwamba mtakusanywa kwake.

Moyo ndio mahali pa imani, ukafiri, ikhlas na unafiki. Pia ni mahali pa pendo na chuki. Kwenye moyo hutokea matendo mema na mbaya. Lau si moyo mtu asingekuwa mtu.

Inatosha kuwa moyo ni kitu kikubwa, kauli yake Mwenyezi Mungu katika Hadith Qudsi: “Haikunipanua ardhi yangu wala mbingu yangu, lakini umenipanua moyo wa mja wangu muu’min.” Hakuna mwenye shaka kwamba kinachompanua aliyeshindwa kupanuliwa na mbingu na ardhi, kuwa ni kikubwa zaidi ya ardhi na mbingu.

Utauliza vipi kiungo hiki kidogo kiweze kupanua aliyeshindikana na ardhi na mbingu? Tena, kwa nini Mwenyezi Mungu mtukufu amehusisha moyo wa Mumini na wala sio wa kafiri?

Jibu: Makusudio ya upana katika Hadith Qudsi hii, sio upana wa mahali. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hana mahali isipokuwa makusudio ni kumfahamu Mwenyezi Mungu, na kwamba moyo wa mumini unamfahamu Mwenyezi Mungu mtukufu kwa namna isiyoweza mbingu na ardhi kufahamu.

Vilevile moyo wa kafiri, haufahamu chochote kuhusu Mwenyezi Mungu, kwa vile uko katika kifuniko cha upotevu na ufisadi. Mwenyezi Mungu mtukufu, anasema:

وَقَالُوا قُلُوبُنَا فِي أَكِنَّةٍ مِمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ وَفِي آذَانِنَا وَقْرٌ وَمِنْ بَيْنِنَا وَبَيْنِكَ حِجَابٌ {5}

“Na wakasema: Nyoyo zetu ziko katika vifuniko kwa yale unayotulingania, na katika masikio yetu mna uzito, na baina yetu na baina yako kuna pazia” (41:5).

Kwa hivyo basi inatubainikia kuwa makusudio ya mtu ambaye Mwenyezi Mungu huingia kati yake na moyo wake, ni yule ambaye amepofushwa na hawaa zake na upotevu. Hivyo Aya hii inakuwa na maana ya Aya isemayo: “Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na juu ya macho yao pana kifuniko,”

Yaani hawanufaiki kwa nyoyo zao kwa sababu ya kutu za upotevu zilizo juu yake, mpaka ikawa kama kwamba Mwenyezi Mungu amepiga sili au amekaa kati yake na mwenye moyo huo.

Hivyo anakuwa kunasibisha muhuri na kuzuia kwake Mwenyezi Mungu mtukufu ni kimajazi sio kihakika.

Kundi la wafasirii wamesema kuwa maana ya kuingia kati ya mtu na moyo wake ni kwamba moyo unashikwa na Mwenyezi Mungu akiugeuza vile anavyotaka, hubadilisha ukumbusho ukawa usahaulivu na usahaulivu ukawa ukumbusho, hofu kuwa amani na amani kuwa hofu. Lakini tafsiri zote hizo ni za kudhania tu.

وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْكُمْ خَاصَّةً ۖ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ {25}

Na jikingeni na fitna ambayo haitawasibu wale waliodhulumu miongoni mwenu peke yao, na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

وَاذْكُرُوا إِذْ أَنْتُمْ قَلِيلٌ مُسْتَضْعَفُونَ فِي الْأَرْضِ تَخَافُونَ أَنْ يَتَخَطَّفَكُمُ النَّاسُ فَآوَاكُمْ وَأَيَّدَكُمْ بِنَصْرِهِ وَرَزَقَكُمْ مِنَ الطَّيِّبَاتِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ {26}

Nakumbukeni mlipokuwa wachache, mkionekana wadhaifu katika nchi; mkawa mnaogopa watu wasiwanyakue; akawapa makao na akawatia nguvu kwa nusura yake na akawapa riziki njema ili mpate kushukuru.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَخُونُوا اللَّهَ وَالرَّسُولَ وَتَخُونُوا أَمَانَاتِكُمْ وَأَنْتُمْ تَعْلَمُونَ {27}

Enyi mlioamini! Msimfanyie hiyana Mwenyezi Mungu na Mtume na mkahini amana zenu na hali mnajua.

وَاعْلَمُوا أَنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ وَأَنَّ اللَّهَ عِنْدَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ {28}

Na jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni fitna. Na hakika kwa Mwenyezi Mungu yako malipo makubwa.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنْ تَتَّقُوا اللَّهَ يَجْعَلْ لَكُمْ فُرْقَانًا وَيُكَفِّرْ عَنْكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۗ وَاللَّهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ {29}

Enyi mlioamini! Mkimcha Mwenyezi Mungu atawajaalia upaambanuzi, na atawafutia makosa yenu na atawasamehe; na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kuu.
  • 1. Tulipofasiri Juz.6 (5:47) tulisema kuwa ukafiri ukitegemezwa kwenye kitendo, makusudio yake yanakuwa ufasiki, na ufasiki ukitegemezewa kwenye itikadi, basi makusudio yake ni ukafiri. Kwa hivyo makusudio ya ukafiri wa kuacha kutenda kwa ajili ya maisha ni ukafiri wa kimatendo, sio wa kiitikadi.