read

Aya 25 – 29: Ogopeni Adhabu

Lugha

Neno Fitna lina maana nyingi, miongoni mwa maana hizo ni adhabu ambayo ndiyo makusudio yake katika Aya hii ya 25. Ama katika Aya 28, makusudio yake ni mapenzi na hawaa zinazozuia haki. Makusudio ya upambanuzi ni mwongozo.

Maana

Na jikingeni na fitna ambayo haitawasibu wale waliodhulumu mion- goni mwenu peke yao, na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

Ni tahadhari inayotoka kwake Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kila mfitini anayeharibu nchi; hasa wale wanaoeneza farakano na kuvuruga amani na kuwachokoza wanyonge. Hadhari ni kwamba ubaya wa adhabu hautaishia kwa madhalimu tu, bali utaenea katika jamii yote na kumwenea mwema na mwovu.

Imeelezwa katika Tafsir Tabari akimnukuu Sadiy, ambaye ni mfasiri mkubwa, kwamba Aya hii inafungamana na watu wa (Vita vya Jamal) ngamia ambao walimpiga vita Ali bin Abu Talib.

Ametaja Razi katika kufasiri Aya hii: “Zubeir siku moja alikuwa akibarizi na Mtume (s.a.w.) mara akatokea Ali (r.a.), Zubeir akamcheka. Mtume wa Mwenyezi Mungu akamwambia: “Vipi unavyompenda Ali?” Akajibu “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ninapenda kama ninavyompenda mwanangu au zaidi.” Mtume akamwambia: ‘’Utakuwaje ukienda kupigana naye?”

Vilevile imeelezwa katika Tafsiru Tabari: “Zubeir bin Al-a’wam alisema: “Tumesoma Aya hii zama zilizopita, lakini hatukuwaona wanaohusika nayo, mara sisi ndio tunahusika nayo”.

Na kumbukeni mlipokuwa wachache, mkionekana wadhaifu katika nchi; mkawa mnaogopa watu wasiwanyakue; akawapa makao na akawatia nguvu kwa nusura yake na akawapa riziki njema ili mpate kushukuru.

Maneno wanaambiwa Maswahaba wa Mtume (s.a.w.). Mwenyezi Mungu mtukufu anawakumbusha udhaifu na hofu waliyokuwa nayo kabla ya Uislamu. Vilevile udhalili na ufukara, na jinsi alivyowapa amani utajiri na utukufu baada ya Uislamu, kwa vile wao wameitikia mwito wa maisha waliyopewa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Lengo la ukumbusho huu ni kuwa waendelee na utiifu na kuitikia mwito wa uhai, ili waishi wakiwa wenye nguvu na heshima. Na kwamba wao pindi tu wakikengeuka na kuasi watarudia unyonge na udhalili waliokuwa nao wenzao, kama ilivyo hali ya waislamu leo, hasa waarabu.

Enyi mlioamini! Msimfanyie hiyana Mwenyezi Mungu na Mtume.

Kumfanyia hiyana Mwenyezi Mungu sio kuacha kufunga na kuswali tu; isipokuwa hiyana kubwa ni kuufanyia hiyana umma na nchi, kwa kuwatawalisha mataghuti kwenye sehemu za uongozi wakatawala nchi na huku tunawavumilia na kuwanyamazia bila ya kuwapiga vita.

Na mkahini amana zenu.

Yaani wala msihini amana zenu. Wafasiri wengi wamesema kuwa ukatazo huu ni wa hiyana ya amana ya mangiliano ya kimali baina ya watu. Hakuna mwenye shaka kwamba kurudisha amana ni wajibu na kuifanyia hiyana ni haramu, lakini hiyana kubwa ni kuacha kusaidiana na wanyonge kurudishahakizaokutokakwawenyenguvuwaliomadhalimu.

Na hali mnajua.

Hakuna mjeuri zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko yule anayemuasi Mwenyezi Mungu kwa makusudi hali anajua.

Jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni fitna.

Imekuja Aya hii baada ya makatazo ya hiyana ili kumzindua Mumini kwamba haitakikani mali na watoto wamzuie kutekeleza wajibu wake kwa umma na nchi mbele ya Mungu. Makusudio ya fitna hapa ni mapenzi yanayozuia haki na kheri.
Imepokewa Hadith kutoka kwa Mtume (s.a.w.) amesema: “Mtoto ni tunda la moyo. Na yeye ni mahali pa woga, ubahili na huzuni”. Sawa na mali ambayo ni matunda ya jasho na mkono.

Ni woga kwa sababu, mwenye nayo huhofia kusema haki na kufanya kwa kuihofia; kama ambavyo anahofia juu ya mtoto wake.

Ni ubahili, kwa sababu mwenye kuimiliki anakuwa na pupa nayo na uchoyo; kama anavyokuwa na pupa na mtoto wake.

Nayo ni huzuni kwa sababu mwenye kuikusanya huhuzunika ikipatwa na jambo; kama anavyohuzunika likipatwa na jambo tunda la moyo wake.

Maneno mazuri niliyosoma kuhusu maudhui haya ni shairi la bedui mmoja akisema:

• Alikuwa fukara

• Akatajirika akapenda mali uchu ukamshika

• Akitaka kutumia huhuzunika

Na hakika kwa Mwenyezi Mungu yako malipo makubwa.

Mwenye akili hupendelea malipo haya na kuyahangaikia kwa juhudi na amali njema; wala haathiriki na mali inayokwisha na mtoto asiyebakia.

Enyi mlioamini! Mkimcha Mwenyezi Mungu atawajalia upaambanuzi.

Mara nyingi sana mtu anakuwa mateka wa matamanio. Humgeuzia zuri likawa baya na baya likawa zuri. Mara nyingi hilo huwa katika mambo yanayohusiana na mali na watoto ambapo matamanio hufikia kilele chake.

Kwa ajili hii ameamrisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) takuwa baada ya kuhadharisha fitna ya mali na watoto. Ama upambanzi, yaani mwongozo, anaowapa Mwenyezi Mungu wenye kumcha ili wapambanue haki na batili, ni natija ya kujikomboa na hawa na matamanio.

Kwa sababu, matamanio hupofusha na hutia uziwi.

Kunasibisha mwongozo kwa Mwenyezi Mungu ni kuwa yeye ndiye aliyeuwekea dalili. Mwenye kuzichunguza vizuri, akiwa hana malengo mengine yoyote isipokuwa kutafuta mwongozo wa haki, basi ataifikia tu.

Na atawafutia makosa yenu na atawasamehe; na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kuu.

Wafasiri wanasema kuwa makusudio ya kufutiwa makosa ni kusitiriwa duniani; na kusamehewa ni kusamehewa akhera. Wamesema hivi kukimbia kukaririka.

Ama sisi hatukimbii kukarika Qur’an na tumebainisha njia yake katika Juz.1 Maana ya Aya yote ni kuwa mwenye kumcha Mwenyezi Mungu atampa mwongozo, msamaha na thawabu.

Hilo kwa Mwenyezi Mungu si kubwa. Kwa sababu ni mkuu wa fadhila na kutoa kwake ni sahali kunamfikia kila mwenye kutafuta na kutaka radhi zake.

وَإِذْ يَمْكُرُ بِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِيُثْبِتُوكَ أَوْ يَقْتُلُوكَ أَوْ يُخْرِجُوكَ ۚ وَيَمْكُرُونَ وَيَمْكُرُ اللَّهُ ۖ وَاللَّهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ {30}

Na walipokupangia njama wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe. Na wakapanga njama na Mwenyezi Mungu akapanga njama. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kupanga njama.

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا قَالُوا قَدْ سَمِعْنَا لَوْ نَشَاءُ لَقُلْنَا مِثْلَ هَٰذَا ۙ إِنْ هَٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ {31}

Na wanaposomewa Aya zetu, husema: Tumekwishasikia, na lau tungependa tungelisema kama haya. Haya si chochote ila ni ngano tu za watu wa kale.

وَإِذْ قَالُوا اللَّهُمَّ إِنْ كَانَ هَٰذَا هُوَ الْحَقَّ مِنْ عِنْدِكَ فَأَمْطِرْ عَلَيْنَا حِجَارَةً مِنَ السَّمَاءِ أَوِ ائْتِنَا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ {32}

Na waliposema: Ewe Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya ni haki itokayo kwako, basi tupige mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu iumizayo.

وَمَا كَانَ اللَّهُ لِيُعَذِّبَهُمْ وَأَنْتَ فِيهِمْ ۚ وَمَا كَانَ اللَّهُ مُعَذِّبَهُمْ وَهُمْ يَسْتَغْفِرُونَ {33}

Na Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwaadhibu maadamu wewe umo pamoja nao. Wala hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaadhibu hali wanaomba msamaha.

وَمَا لَهُمْ أَلَّا يُعَذِّبَهُمُ اللَّهُ وَهُمْ يَصُدُّونَ عَنِ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَمَا كَانُوا أَوْلِيَاءَهُ ۚ إِنْ أَوْلِيَاؤُهُ إِلَّا الْمُتَّقُونَ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ {34}

Na wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu; hali wao wanazuilia (watu) msikiti mtakatifu? Wala wao hawakuwa ndio walinzi wake. Hawakuwa walinzi wake isipokuwa wenye takuwa tu, lakini wengi wao hawajui.

وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِنْدَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً ۚ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنْتُمْ تَكْفُرُونَ {35}

Na haikuwa Swala yao kwenye hiyo nyumba ila miluzi (kupiga mbinja) na makofi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkikufuru.