read

Aya 30 – 35: Walipokufanyia Vitimbi

Lugha

Njama vikinasibishwa kwa mtu maana yake ni hila na hadaa. Na ikinasibishwa kwa Mwenyezi Mungu maana yake ni kuvunja njama.

Maana

Na walipokupangia njama wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe.

Katika Aya iliyotangulia (26) Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewakumbusha Waislamu neema yake juu yao. Katika Aya hii anamkumbush Mtume (s.a.w.) neema yake juu yake ambapo Washirikina wa Kiquraish walikubaliana kummaliza Nabii Muhammad (s.a.w.). Wakatofautiana katika njia ya kummaliza. Mmoja akasema tumfunge, mwingine akasema tumtoe Makka.

Kisha wakaafikiana wachague mtu katika kila ukoo na waivamie nyumba yake akiwa amelala kitandani wampige kwa panga zao pigo moja. Hapo damu yake itakuwa kwa koo zote, na Bani Hashim watashindwa kupigana na waarabu wote.

Wafasiri wanasema, akiwemo Tabari, Razi, na Abul Hayaan Al-Andalusi, kwamba Mwenyezi Mungu alimpa wahyi Mtume wake kumjulisha hilo. Akamwamrisha atoke kuelekea Madina na akamwamrisha Ali bin Abu Talib alale kitandani kwake. Ali akalala kitandani kwake na kujifinika shuka yake. Walipovamia kitanda chake walimwona Ali, wakapigwa na mshangao. Pia Mtume alimwusia Ali kurudisha amana za watu walizoziweka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Na wakapanga njama na Mwenyezi Mungu akapanga njama na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kupanga njama.

NjamayaMaquraishniilemipangoyaoyakumuuaNabiiMuhammadkwa namna ambayo ukoo wa Hashim utashindwa kulipizia kisasi. Ama njama ya Mwenyezi Mungu ni kupangua njama yao kwa kupanga Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Mtume atoke, na Ali alale kitandani kwake. Yametangulia maelezo kuhusu hayo katika kufasiri Juz.3 (3:54).

Na wanaposomewa Aya zetu, husema: Tumekwishasikia. Na lau tungependa tungelisema kama haya. Haya si chochote ila ni ngano tu za watu wa kale.

Maquraish walisema kuwa Qur’an ni ngano za watu wa kale, na kwamba wao wakitaka wanaweza kusema mfano wake. Walisema hivi wakiwa wanajua fika kwamba hiyo inatoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu wao na watu wote walishindwa kuleta mfano wa hata Sura moja tu.

Maquraish wameshindwa ndio maana wanakimbilia uzushi, kuficha kushindwa kwao na upotevu wao; sawa na kila anayeshindwa kuikabili haki kwa hoja na mantiki.

Na waliposema: Ewe Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya ni haki itokayo kwako, basi tupige mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu iumizayo.

Baadhi ya watu wanaweza kung’angania dhambi kwa kiburi chao; sawa na wanavong’ang’ania dini au zaidi; mpaka wanafikia kuwa tayari kufa kuliko kukubali kushindwa, hata kama upande wa pili ni haki.

Wako tayari kuangamia na kuadhibiwa kuliko kuacha mafunzo yao na mila zao. Historia imetaja mifano mingi ya watu wa aina hiyo. Qur’an imetaja Firauni, watu wa Nuh, n.k.

Maquraish walipoitwa na Mtume kwenye Uislamu walisema: “Kama Muhammad ni mkweli basi itupige mvua ya mawe.” Yaani wanaona afadhali kuangamia kwa kupigwa mawe kuliko kumfuata Muhammad, hata kama ni Nabii.

Basi Mwenyezi Mungu akawajibu kwamba adhabu bado iko mbele yao na kwamba mlango bado uko wazi; na aliwapa muda kwa sababu moja aliy oiashiria kwa kauli yake:

Na Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwaadhibu maadamu wewe umo ndani yao.

Yaani Mwenyezi Mungu mtukufu hawaadhibu watu wa Makka maadamu Nabii Muhammad yuko. Hii ikiwa ni kumtukuza na kumwadhimisha.

Wala hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaadhibu hali wanaomba msamaha.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kusema kuwa hatawaadhibu Maquraish maadam Nabii Muhammad yuko kwao, anasema kuwa, vilevile, hatawaadhibu wakiamini, ni sawa Nabii Muhammad awe nao au asiwe nao. Kauli yake hii Mwenyezi Mungu ni sawa na kauli yake nyingine:

مَا يَفْعَلُ اللَّهُ بِعَذَابِكُمْ إِنْ شَكَرْتُمْ وَآمَنْتُمْ ۚ {147}

“Mwenyezi Mungu ana haja gani ya kuwaadhibu kama mtashukuru na mtaamini” Juz.5 (4:147).

Makusudio ya maana haya yanafahamika kutokana na kusema kwake moja kwa moja.

Na wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu?

Na pia kauli yake akiwaambia Maquraish:

Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkikufuru.

Kwa ufasaha zaidi ni kuwa maana ya Aya ni kwamba, Yeye Mwenyezi Mungu hatawadhibu ikiwa Nabii Muhammad yuko kwao. Vilevile hatawaadhibu wakisilimu.
Ametumia neno msamaha kwa maana ya kusilimu, kwa sababu msamaha ni katika mambo yanayolazimiana na Uislamu. Kwa ufafanuzi huu, inatubainikia kuwa hakuna haja ya taawili walizozitaja wafasiri, tena zinamwacha msomaji gizani.

Na wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu; hali wao wanazuilia (watu) msikiti mtakatifu?

Hilo ni swali lenye maana ya kukanusha; yaani hakuna chochote katika dini au tabia kitakachowazuia kuadhibiwa kwao. Kwani wao kwa upande wa ushirikina wao wanazuia waislamu kumwabudu Mwenyezi Mungu katika nyumba yake takatifu.

Mwislamu yeyote, hata Mtume (s.a.w.) alipokuwa Makka, hakuwa akiweza kuswali ndani ya Masjudil-Haram bila ya kupata udhia na mateso. Waliafikiana wamzuie Mtume kwa nguvu asifanye umra mwaka wa Hudaybiya.

Wala wao hawakuwa ndio walinzi wake.

Yaani washirikina si walinzi wa Masjidul Haram wala si watu wa nyumba hiyo, bali ni maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui wa nyumba yake. Kwa hiyo ni wajibu kuwafukuza na kuwazuia, kwa vile wanauchafua kwa najisi zao na uchafu wao. Kwa ajili hii, Uislamu ulipopata nguvu, walizuiliwa kuukurubia:

إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ فَلَا يَقْرَبُوا الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ بَعْدَ عَامِهِمْ هَٰذَا ۚ {28}

“Hakika washirikina ni najisi, kwa hiyo wasiukaribie Msikiti mtakatifu baada ya mwaka wao huu” (9:28).

Hawakuwa walinzi wake isipokuwa wenye takuwa tu.

Yaani hatastahiki yeyote, vyovyote alivyo; kuusimamia Msikiti mtakatifu (Masjidul Haram) ila akiwa ni mwema mwenye kumcha Mungu akiwa Mwislamu aliyepiga shahada, Je, itakuwaje mshirikina na mwenye kupinga?

Ingawaje maudhui ya Aya yanahusika na msikiti mtakatifu, lakini takuwa ni sharti ya kila anayesimamia misikiti au sehemu za kidini. Kwa vile sababu ya hilo ni utwahara wa mahali na utakatifu wake. La kushangaza ni kwamba wengi wanaosimamia mambo haya ni wale viumbe waovu ambao ni mabingwa wa fani ya hila na wizi.

Lakini wengi wao hawajui kwamba mwenye kusimamia msikiti na sehemu takatifu ni lazima awe mwema, mcha Mungu; na kwamba hakuna usimamizi kwa fasiki.

Utauliza kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu” inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu aliwaadhibu Maquraish, ambapo inajulikana kuwa hayakuwapitia kama yaliyowapitia watu wa Mitume waliotangulia, kama vile Ad, Thamud, watu wa Nuh, wa Lut n.k.?

Jibu: Wale waliomuudhi Mtume na waislamu, Mwenyezi Mungu aliwaua siku ya Badr kwa mikono ya waislamu wenyewe. Miongoni mwa waliouwawa ni Abu Jahl, Uqba bin Abu Mui’t, Nadhr bin Al-Harith, Umayya bin Khalaf na wengineo katika vigogo vya Maquraish ambao walikuwa wamezidi mno kuwaudhi waislamu.

Kwa mfano Umayya bin Khalaf alikuwa akimmiliki Bilal mwadhini wa Mtume (s.a.w.). Alikuwa akimwadhibu kwenye mchanga ulio moto sana na kumpa adhabu za kila aina. Siku ya Badr Umayya alitoka pamoja na washirikina, na Bilal naye akatoka pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Mara tu, Bilal alipomwona Umayya alipiga ukelele: “Huyu kiongozi wa ukafiri, ama zake ama zangu.” Wakakusanyika baadhi ya wanyonge waliokuwa wakiteswa na huyu Umayya wakamshika; Bilal naye akampiga Umayya kwa upanga mpaka akamuua.
Akakichukua kichwa chake akakitungika kwenye upanga wake na huku akicheza kwa furaha.

Na haikuwa swala yao kwenye hiyo nyumba ila miluzi (kupiga mbinja) na makofi.

Kama kwamba mwulizaji anauliza: Maquraish walikuwa wakiswali katika msikiti mtukufu, sasa vipi wamestahiki adhabu? Akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwa swala yao ilikuwa ni vurugu tu, haina unyenyekevu.

Kwa sababu ilikuwa ni miluzi (mbinja) ya mdomoni na makofi ya mikononi.

Basi onjeni adhabu iliyowafikia siku ya Badr.

Na adhabu ya akhera ni kali zaidi.

Kwa sababu ya yale mliyokuwa mkikufuru.

Lau mngesilimu mngelisalimika na adhabu ya duniani na akhera.

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا يُنْفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ لِيَصُدُّوا عَنْ سَبِيلِ اللَّهِ ۚ فَسَيُنْفِقُونَهَا ثُمَّ تَكُونُ عَلَيْهِمْ حَسْرَةً ثُمَّ يُغْلَبُونَ ۗ وَالَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ يُحْشَرُونَ {36}

Hakika wale waliokufuru hutoa mali zao ili kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watazitoa, kisha zitakuwa majuto juu yao, kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahanamu.

لِيَمِيزَ اللَّهُ الْخَبِيثَ مِنَ الطَّيِّبِ وَيَجْعَلَ الْخَبِيثَ بَعْضَهُ عَلَىٰ بَعْضٍ فَيَرْكُمَهُ جَمِيعًا فَيَجْعَلَهُ فِي جَهَنَّمَ ۚ أُولَٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ {37}

Ili Mwenyezi Mungu apate kuwapambanua walio wabaya na walio wazuri na kuwaweka wabaya juu ya wabaya wengine na kuwarundika wote pamoja na kuwatupa katika Jahanamu. Hao ndio waliohasirika.

قُلْ لِلَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ يَنْتَهُوا يُغْفَرْ لَهُمْ مَا قَدْ سَلَفَ وَإِنْ يَعُودُوا فَقَدْ مَضَتْ سُنَّتُ الْأَوَّلِينَ {38}

Waambie wale waliokufuru, kama watakoma, watasamehewa yaliyopita. Na wakirudia basi imekwishapita desturi ya watu wa zamani.

وَقَاتِلُوهُمْ حَتَّىٰ لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ وَيَكُونَ الدِّينُ كُلُّهُ لِلَّهِ ۚ فَإِنِ انْتَهَوْا فَإِنَّ اللَّهَ بِمَا يَعْمَلُونَ بَصِيرٌ {39}

Na piganeni nao mpaka kusiwe na fitna na dini yote iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Wakikoma, basi hakika Mwenyezi Mungu anayaona wanayotenda.

وَإِنْ تَوَلَّوْا فَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّهَ مَوْلَاكُمْ ۚ نِعْمَ الْمَوْلَىٰ وَنِعْمَ النَّصِيرُ {40}

Na wakigeuka, basi jueni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mola wenu, ni Mola mwema na msaidizi mwema.