read

Aya 36 – 40: Waliokufuru Hutoa Mali Zao

Maana

Hakika wale waliokufuru hutoa mali zao ili kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watazitoa, kisha zitakuwa majuto juu yao, kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahanamu.

Washirikina walikuwa wakitoa mali zao katika kupigana na waislamu na kuzuilia watu Uslamu.

Ndipo Mwenyezi Mungu akabainisha, katika Aya hii, kwamba mali hizo zitawarudishia majuto, udhalili duniani na adhabu kali huko akhera. Kwa sababu mwisho ushindi utakuwa wa dini ya Mwenyezi Mungu na watu wake.

Ili Mwenyezi Mungu apate kuwapambanua walio wabaya na walio wazuri.

Hii ni sababu na kubainisha sababu yenye kuwajibisha majuto ya Washirikina na udhalili wao. Nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwadilifu na mwenye hekima.

Miongoni mwa uadilifu wake ni kutokuwa sawa mbele yake mwema na mwovu na Mu’min na kafiri, bali atampambanua kila mmoja na kumfanyia anayostahiki.

Kwa ajili hii, atampa thawabu mwema na kumwinua huko akhera. Na pengine humchanganyia malipo ya dunia na akhera. Na atamdhalilisha mwovu na kumwadhibu huko akhera kwenye nyumba ya hisabu na malipo. Pengine humpa aina fulani ya adhabu katika dunia kwa kadiri hekima yake inavyotaka.

Na kuwaweka wabaya juu ya wabaya wengine na kuwarundika wote pamoja na kuwatupa katika Jahanamu.

Makusudio ni jinsi ya wabaya; yaani wanaofungamana na jina hilo. Kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu.

Hao ndio waliohasirika.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu kesho atawakusanya wabaya wakiwa mrundo kisha awatupe katika Jahanamu, kama anavyofanya mtafuta kuni akizikusanya pamoja na kuzitia motoni. Mwenyezi Mungu anasema:

وَأَمَّا الْقَاسِطُونَ فَكَانُوا لِجَهَنَّمَ حَطَبًا {15}

“Na ama wanaokengeuka (kuiacha haki) watakuwa kuni za Jahanamu.” (72: 15).

Hao ndio waliohasirika.

Kuna hasara gani kubwa zaidi ya kuwa mtu na nyama zake na damu yake ni kuni za moto alioukoka Mwenyezi Mungu kwa ghadhabu yake juu ya aliyemfanyia hiyana Mola wake na dhamir yake!

“Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika sisi tunaihofia adhabu yako. Na tunakimbilia kwako. Wewe ni mkarimu humfukuzi mwenye kutaka hifadhi ya ukarimu wako na kukimbilia rehema yako.”

Waambie wale waliokufuru, kama watakoma, watasamehewa yaliyopita.

Maneno haya anaambiwa Mtume (s.a.w.). Mwenyezi Mungu anamwamrisha kuwapa mawaidha makafiri na kuwaambia mlango wa toba uko wazi mbele yao, na kwamba wamepewa fursa ya kuacha ukafiri na uadui kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, wakitubia basi Mwenyezi Mungu atawakubalia toba.

Kwa sababu Uislamu unakata yaliyokuwa kabla yake; kama ilivyoelezwa katika Hadith.

Na wakirudia basi imekwishapita desturi ya watu wa zamani.

Mfano wale waliokadhibisha Mitume na kuwapiga vita. Makusudio ya desturi ya Mwenyezi Mungu kwa waliopita – ni kuangamizwa makafiri, na Mitume kuwa washindi.

Mwenyezi Mungu amekwishandika: Hakika nitashinda mimi na Mitume wangu.

إِنَّ اللَّهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ {21}

“Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye kushinda.” (58:21).

Na piganeni nao mpaka kusiwe na fitna na dini yote iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Wakikoma, basi hakika Mwenyezi Mungu anayaona wanayotenda.

Makusudio ya Fitna hapa ni ukafiri. Aya imetangulia na tafsiri yake katika Juz.2 (2:193).

Na wakigeuka, basi jueni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mola wenu, ni Mola mwema na msaidizi mwema.

Yaani kama washirikina wakipingana na ubainifu wa Mtume na amani yake, basi mjiizatiti enyi Waislamu wala msiwaogope. Kwani Mwenyezi Mungu atawasaidia na atawalinda; naye ni mbora wa walinzi na wasaidizi.