read

Aya 5 – 8: Kama Alivyokutoa Mola Wako

Kwenda Badr

Mtume (s.a.w.) alitumwa kufikisha ujumbe akiwa na umri wa miaka arubaini na akakaa Makka, miaka kumi na tatu. Kisha akahamia Madina ambako aliingia siku ya Jumatatu tarehe 12 Rabiul-Awwal (Mfungo sita).

Akaishi hapo kwa muda wa mika kumi, na kufariki Jumatatu, tarehe 12 Rabiul-Awwal akiwa na umri wa miaka Sitini na tatu.1

Alipotulia Madina akawa anatuma vikosi kwenye misafara ya washirikina kuchunguza habari zao na kuwashtua. Al-Mas’udi anasema: Vita alivyoviongoza Mtume mwenyewe ni 26, katika hivyo alipigana tisa.

Hapa tunaeleza kutoka kwake kwenda Baadr kwa sababu ni maudhiu ya Aya tulizo nazo sasa, vita hii ilidhihirisha mwanzo wa nguvu za waislamu dhidi ya washirikina ambao walikuwa wakiwanyanyasa na kuwaudhi waislamu zaidi ya miaka kumi na tatu, huku waislamu wakipata mateso hayo na maudhi kwa kuvumilia kwa kustahmili. Kwa sababu kushindana nao na udhaifu waliokuwa nao ni sawa na kujichinja.

Kwa ufupi kisa cha Badr ni kwamba Mtume (s.a.w.) alisikia kuwa Abu Sufyan anarudi kutoka Sham na msafara ulio na mali nyingi. Katika jumla ya mali hizo ni zile walizozitaifisha kutoka kwa Muhajirin (Wahamiaji) walizoziacha Makka.

Basi Mtume akawakusanya maswahaba akawahimiza kutoka kuchukua mali za msafara. Baadhi wakaingia uvivu na kuchukia kutoka kwa kuhofia Maquraish. Kisha wakaenda pamoja na Mtume.

Hapo ilikuwa ni tarehe 17 Ramadhan mwaka wa pili wa Hijra. maswahaba walikuwa hawajui kuwa sasa wanakwenda kwenye mojawapo ya vita kuu ya waislamu na yenye athari kubwa katika maisha ya Kiislamu na waislamu.

Mayahudi wakamtuma mtu wa kumwonya Abu Sufyan akiwa njiani. Naye akatuma ujumbe kwa maquraish akiwataka waende wakawaokoe. Kukatokwa huko Makka, hakubaki hata mtu mmoja awezaye kushika silaha. Waislamu wakati huo bado wako njiani kuelekea Badr. Lakini Abu Sufyan akabadisha njia akapitia mwambao wa Bahari nyekundu.

Mtume alipopata habari hiyo akawashauri Maswahaba kuwa je, waaendelee na vita au watarudi Madina? Wakati huo huo akawaambia kuwa Mungu amewaahidi mojawapo ya makundi mawili kama wakienda kupigana.

Makundi mawili hayo, ni masfara uliobeba mali, na jeshi la maquraish waliotoka kuja kuhami mali. Wengi wakashauri kuendelea na vita, na baadhi wakachukia, kama walivyochukia tangu mwanzo.

Hatimaye wakaungana kuwakabili maquraish. Hapo Mtume (s.a.w.) akawaambia: “Nendeni kwa baraka ya Mwenyezi Mungu. Wallah kana kwamba mimi ninaona vifo vya watu, basi jiandaeni na vita.”

Idadi ya maquraish walikuwa wapiganaji elfu moja wakiwemo wapanda farasi mia moja. Waislamu walikuwa mia tatu wakiwa na mpanda farasi mmoja tu, wengine wanasema walikuwa wawili. Wakawaua washirikina sabini na kuteka sabini waliobaki wakakimbia. Kwa upande wa Waislamu walikufa mashahidi watu 14 na hakuna aliyetekwa.

Vita hii ilikuwa ushindi wa kwanza wa waislamu uliobadilisha hali zao, na kupata watu wengi, wakawa wanakabili nguvu kwa nguvu na ukali kwa ukali sio tena kunyamaza au kukimbia nchi.

Baadayautangullizihuuu,sasatunaingiliakufasiriAya:

Maana

Kama alivyokutoa Mola wako nyumbani kwako kwa haki, na hakika kundi moja la Waumini linachukia.

Makusudio ya nyumba ni Madina. Wakati Mtume alipotaka kutoka Madina kwenda kuukamata msafara, baadhi ya jamaa walikuwa wazito na wakasema: “Hatuwawezi Maquraish.” Wakatoka kwa kuchukia pamoja na waliotoka kwa kupenda.

Huko njiani Mtume akawapa habari ya maquraish kuwa wanakuja kutoka Makka. Akawataka ushauri kuwa wataendelea na vita au watarudi Madina? Baadhi wakachukia na kusema kuwa sisi tumetoka kwa ajili ya msafara tu. Lakini wengi wakasema: “Tutakwenda nawe kupigana.” Kisha wakaenda wote kwa baraka ya Mwenyezi Mungu.

Aya hii inaashiria misismamo miwili ya baadhi ya Swahaba: Kuchukia kutoka Madina kwenda kwenye msafara na wapili ni kuchukia kuendelea na vita, baada ya kutoka kwa ajili ya msafara tu.

Hayo ndiyo maana ya Aya hiyo, yako wazi na hayana ugumu wowote. Lakini baadhi ya wafasiri wamedangana katika kuifasiri kwake. Mwenye Al-bahrul Muhit ametaja kauli kumi na tano.

Ajabu ni yale aliyoyasema mfasiri huyu katika Kitab kingine kwamba yeye ametaja kauli 15 katika Bahrul-muhit. Lakini hakukinaika na kitu chochote katika kauli hizo, mpaka akaota usingizini kwamba yeye anatembea kwenye njia iliyotandikwa mawe mapana akiwa na mtu mwingine akifanya naye utafiti kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu: “Kama alivyokutoa Mola wako nyumbani kwako.”

Akamwambia: “Haujanipitia mushkeli katika Qur’an mfano wa huu.” Pengine kuna maneno yaliyokadiriwa yanayotengeneza maana ambayo hakuyaeleza mfasiri yeyote. Kisha nikamwambia yule mtu: “Nimejua sasa, kuwa yale maneno yaliyokadiriwa ni ‘Nusura yako.’

Ninachotaka kusema, sio kumdharau mfasiri huyu mkubwa; isipokuwa ninataka kutoa dalili kuwa hata ulamaa, mwenye akili, mara nyingine akili yake inafungika; mpaka akawa anafasiri Qur’an kwa ndoto, na yeye katika hali halisi yuko kwenye makosa naye hajijui. Ni ajabu, lakini ndivyo ilivyo. Dalili ya kuwa yeye yuko kwenye makosa ni kwamba lau ataona jengine, basi lile angelilipinga.

Wanajadiliana nawe katika haki baada ya kubainika.
Kundi moja la waumini walibishana katika kupigana na kikosi cha waliotoka Makka ingawaje kupigana huku ni haki na kheri. Wakaathirika na msafara wa ngamia, kwa vile ulikuwa na mali nyingi na watu wachache.

Kauli yake Mwenyezi Mungu: “Baada ya kubainika” inaashiria kwamba wao walibishana baada ya Mtume (s.a.w.) kuwapa habari ya ushindi.

Kama kwamba wanasukumwa katika mauti na huku wanaona wazi sababu za mauti.

Hii ni Sura inayochorwa na Qur’an ya kuwogopa kwao Maquraish sana. Kwa sababu wamejiandaa kwa nguvu na wako wengi.

Utauliza: Waislamu wanawatukuza sana watu wa Badr na kuwaweka kwenye cheo cha juu; na hapa Qur’an inawadunisha waziwazi. Na kwamba wao walibishana na Mtume pamoja na kubainishiwa haki na kuwekewa wazi, kwa sababu wahyi umemshukia.

Jibu: Hili haliwagusi na wala haligusi imani yao kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wao ni wanadamu, nafsi zao hutetema zionapo mauti japo wana imani na utulivu. Zaidi ya hivyo, hayo yalikuwa ni mawingu ya Kaskazi tu, yalifunga kisha yakaondoka. Wakaenda pamoja na Mtume wakayakabili mauti kwa azma na uthabiti.

Na alipowaahidi moja ya makundi mawili kuwa ni lenu:

Ama ushindi katika vita bila ya mali ya msafara; au mali ya msafara bila ushindi.

Nanyi mkapenda lile lisilo na nguvu ndio liwe lenu.

Lisilo na nguvu ni msafara wa mali zao, ambalo ndilo waliloathirika nalo kuliko jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Lakini Mwenyezi Mungu aliwatakia kheri wao na Uislamu kwa kuvunja ushirikina na utaghuti.

Na Mwenyezi Mungu anataka kuihakikisha haki kwa maneno yake na kuikata mizizi ya makafiri.

Makusudio ya haki hapa ni ushindi wa waislamu dhidi ya washirikina. Na makusudio ya maneno yake, kuwa ni ahadi yake kuwa mojawapo ya makundi mawili ni ya waislamu.

Maana ni kuwa: “Enyi waislamu! Nyinyi mmetaka mali inayokwisha, na Mwenyezi Mungu ametaka kuwanusuru juu ya mamwinyi wa Kiquraish, maadui wa Mweneyzi Mungu na maadui zenu; awaangamize kwa mikono yenu, aing’oe mizizi ya makafiri na ahakikishe ahadi yake kwa kuwanusuru. Basi ni nini bora katika haya? Utukufu huu, au ngamia na shehena zao?

Ili kuihakikisha haki na kuivunja batili; ijapokuwa watachukia wafanyao makosa.

Makusudio ya haki katika Aya iliyotangulia, ni ushindi wa waislamu dhidi ya washirikina. Na makusudio ya haki hapa ni Uislamu, na wenye makosa ni maadui wa Uislamu. Makusudio ya batili ni shirki.

Kuihakikisha haki na kuitangaza na kuidhihirisha kwa watu au kwa kuwanusuru watu wake, au yote mawili. Na kuivunja batili ni kwa kui- tangaza au kuwadhalilisha wabatilifu, au yote pamoja. Ufafanuzi zaidi wa tafsir ya Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ {33}

Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokuwa watachukia washirikina.” (9:33).

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُمْ بِأَلْفٍ مِنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ {9}

Mlipokuwa mkimwomba msaada Mola wenu. Naye akawajibu kuwa: “Hakika mimi nitawasaidia kwa Malaika elfu moja wanaofuatana mfululizo.”

وَمَا جَعَلَهُ اللَّهُ إِلَّا بُشْرَىٰ وَلِتَطْمَئِنَّ بِهِ قُلُوبُكُمْ ۚ وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِنْدِ اللَّهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ {10}

Na Mwenyezi Mungu hakuyafanya haya ila ni bishara na ili nyoyo zenu zitue kwayo. Na hakuna msaada ila utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye hekima.

إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِنْهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُمْ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً لِيُطَهِّرَكُمْ بِهِ وَيُذْهِبَ عَنْكُمْ رِجْزَ الشَّيْطَانِ وَلِيَرْبِطَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمْ وَيُثَبِّتَ بِهِ الْأَقْدَامَ {11}

Alipowafunika kwa usingizi uliokuwa amani itokayo kwake, na akawateremshia maji kutoka mawinguni ili awatwaharishe kwayo, na kuwaondolea uchafu wa shetani na kuzikazanisha nyoyo zenu na kuimarisha nyayo zenu kwayo.

إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلَائِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُوا الَّذِينَ آمَنُوا ۚ سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ فَاضْرِبُوا فَوْقَ الْأَعْنَاقِ وَاضْرِبُوا مِنْهُمْ كُلَّ بَنَانٍ {12}

Mola wako alipowapa wahyi Malaika: Hakika mimi niko pamoja nanyi, basi watieni nguvu wale walioamini; nitatia woga katika nyoyo za makafiri, basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ شَاقُّوا اللَّهَ وَرَسُولَهُ ۚ وَمَنْ يُشَاقِقِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ اللَّهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ {13}

Hayo ni kwa kuwa wamemwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

ذَٰلِكُمْ فَذُوقُوهُ وَأَنَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابَ النَّارِ {14}

Ndiyo hivyo! Basi onjeni! Na hakika makafiri wana adhabu ya moto.
  • 1. Hata hivyo kauli yenye nguvu kwa upande wa shia ni kuwa alifariki 28 Safar (mfunguo tano)