read

Aya 88 – 89: Tutakutoa Ewe Shuaib

Maana

Wakuu waliotakabari katika kaumu yake wakasema: Ewe Shuaib! Tutakutoa wewe na wale walioamini pamoja nawe katika mji wetu au mrejee katika mila yetu.

Tumetangulia kueleza katika Juz.8, kwamba Shuaib aliwataka makafiri kuishi kwa amani na wale walioamini na kumwachia hiyari anayetaka kuingia dini anayotaka. Lakini makafiri wakakataa mwito wake na wakamuhiyarisha mambo mawili tu: Ama atoke yeye na wale walioamini mjini mwao, au wale walioamini warudie ukafiri, na yeye arudie msimamo wake wa kwanza, kabla ya utume, asiwe wa kuunga mkono dini yao wala kuipinga. Kwa maneno mengine ni kuwa hali irudie kama ilivyokuwa kabla ya Utume.

Akasema: Je, ingawa tunaichukia?

Hiyo ndiyo mantiki ya mwenye kuchunga haki mwenye ikhlasi, hamchukii yeyote kwa analolichukia, wala hataki yeyote amchukue kwenye lile asilolitaka. Kisha je, inawezekana imani kwa kulazimishwa? Je, Mu’min wa kweli dini yake na itikadi yake inaathirika kwa kukaa katika mji?

Hakika tutakuwa tumemzulia Mwenyezi Mungu uwongo ikiwa tutarudi katika mila yenu baada ya kwisha kutuokoa nayo Mwenyezi Mungu.

Washirikina walimtaka Shuaib (a.s.) artadi awe kwenye shirk. Akawaambia, kurtadi ni kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo; na mwisho wa kumzulia Mwenyezi Mungu ni balaa na adhabu; na Mwenyezi Mungu amekwisha tuokoa nayo, sasa vipi tumzulie? Ama kuwa murtadi ni kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo ni wazi, kwa sababu maana yake ni kuwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu ni bora kwake kuliko kumwamini.

Wala haiwi kwetu kuirudia mpaka akipenda Mwenyezi Mola wetu.

Dhamir ya ‘kuirudia’ ni ya mila ya ukafiri na shirk. Sharti la kupenda kwa Mwenyezi Mungu hapa ni sharti la muhali (lisilowezekana). Kwa sababu Mwenyezi Mungu hapendi shirki na ukafiri, ni sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya ya 40 ya Sura hii. “Wala hawataingia peponi mpaka ngamia apite kwenye tundu ya sindano.”

Ujuzi wa Mola wetu umeenea katika kila kitu.

Umetangulia mfano Aya hii katika Juz. 7 (6:80).

Kwa Mwenyezi Mungu tunategemea.

Na mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu haogopi vitisho wala makamiano. Kwa sababu anajua kwa yakini kwamba kiumbe hadhuru wala kunufaisha.

Mola wetu! Hukumu baina yetu na baina ya kaumu yetu kwa haki, nawe ndiye bora wa wenye kuhukumu.

Baada ya Shuaib kukata tamaa nao na kuona kung’ang’ania kwao ukafiri, alikimbia kwa Mwenyezi Mungu na akanyenyekea kwake ahukumu baina yake na waliokufuru katika watu wake. Kwa sababu Yeye Mwenyezi Mungu ndio rejea ya nguvu na uadilifu.

وَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ قَوْمِهِ لَئِنِ اتَّبَعْتُمْ شُعَيْبًا إِنَّكُمْ إِذًا لَخَاسِرُونَ {90}

Na wakuu waliokufuru katika kaumu yake wakasema: Kama nyinyi mkimfuata Shuaib, hapo hakika mtakuwa wenye hasara.

فَأَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ {91}

Ukawanyakua mtetemeko wakaamkia majumbani mwao wamejifudikiza.

الَّذِينَ كَذَّبُوا شُعَيْبًا كَأَنْ لَمْ يَغْنَوْا فِيهَا ۚ الَّذِينَ كَذَّبُوا شُعَيْبًا كَانُوا هُمُ الْخَاسِرِينَ {92}

Wale waliomkadhibisha Shuaib wakawa kama kwamba hawakuwako. Wale waliomkadhibisha Shuaib ndiyo wenye hasara.

فَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا قَوْمِ لَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَنَصَحْتُ لَكُمْ ۖ فَكَيْفَ آسَىٰ عَلَىٰ قَوْمٍ كَافِرِينَ {93}

Basi (Shuaib) akaachana nao na akasema: Enyi watu wangu! Kwa hakika nimewafikishia ujumbe wa Mola wangu na nikawanasihi, basi vipi nihuzunike juu ya watu makafiri.