read

Aya 9 – 14: Mlipokuwa Mkimwomba Msaada Mola Wenu

Maana

Mlipokuwa mkimwomba msaada Mola wenu. Naye akawajibu kuwa: Hakika mimi nitawasaidia kwa Malaika elfu moja wanaofuatana mfululizo.

Waislamu walipohakikisha kwamba kupigana na adui mwenye nguvu na idadi kubwa ya wapiganaji, kutakuwa tu, basi walikimbilia kwa Mwenyezi Mungu wakitaka kuokoka na ugumu huu. Naye Mwenyezi Mungu alipoona ukweli wa nia na azma yao, aliwapa habari kupitia kwa Mtume wake (s.a.w.), kwamba yeye amewatikia dua yao kwa Malaika elfu moja wanaofuatana.

Utauliza hapa Mwenyezi Mungu amesema: Nitawasaidia kwa Malaika elfu moja wanaofuatana, mahali pengine akasema: “Je, haiwatoshi kuwasaidia Mola wenu kwa Malaika elfu tatu wenye kuteremshwa?”

Tena akasema: “Atawasaidia Mola wenu kwa Malaika elfu tano wenye alama” Juz.4 (3:124-125).

Jibu la swali hili tumelijibu huko Juz.4 (3:124-125).

Na Mwenyezi Mungu hakuyafanya haya ila ni bishara na ili nyoyo zenu zitue kwayo.
Na hakuna msaada ila utokao kwa Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hakima.

Mwenyezi Mungu anasema lengo la msaada huu ni kutua nyoyo zenu na mvumilie katika kupigana na adui sio, kutegemea Malaika. Bali ni juu yenu kumaliza juhudi zenu zote. Ama ushindi hauwi wala hautakuwa ila kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, si kwa juhudi zenu na wala kwa msaada wa Malaika. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz.4. (3:126).

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akataja njia sita za neema yake kwa Waislamu:

1. Alipowafunika usingizi uliokuwa amani itokayo kwake.

Waislamu waliwahofia Washirikina kwa wingi wao, Mwenyezi Mungu akaipoza hofu yao kwa usingizi; Hawakuamka ila nafsi zao zimejawa na uutulivu.

Sote tunajua, kwa majaribio, kwamba usingizi unapunguza sehemu ya huzuni na hofu. Imam Ali (a.s) anasema: “Ni kuvunja kulikoje kwa usingizi, kwa tatizo la siku.” Yaani mtu anaweza kufikiria tatizo fulani akilala, mpaka atakapoamka hulikuta limetatuka.

2. Na akawateremshia maji kutoka mawinguni ili awatwaharishe kwayo.

Baada ya waislamu kupumzika kwa usingizi walijikuta wana haja ya maji. Kwa sababu walikuwa hawajafika Badr wakati huo. Ndipo Mwenyezi Mungu akawateremshia mvua, wakanywa na wakajisafisha. Hii ni neema ya pili baada ya usingizi.

3. Na kuwaondolea uchafu wa shetani.

Shetani alikuwa akiwatia wasiwasi waislamu na kuwahofisha na washirikina. Mwenyezi Mungu akawaondolea hofu hii, ambayo ameiita uchafu wa shetani, kwa usingizi na kusaidiwa na Malaika.

4. Na kuzikazanisha nyoyo zenu kwa kuondoa hofu na fazaa.

5. Na kuimarisha nyayo zenu kwayo.

Wafasiri wengi wanasema kuwa dhamir ya kwayo inarudi kwenye maji, na nyayo ni miguu. Kwamba waislamu walikuwa katika tifu tifu, miguu yao haina uimara, mvua iliponyesha mchanga ukashikana na miguu ya waislamu ikawa imara.

Hayo ndiyo yalioelezwa katika tafsir nyingi. Ama sisi tunaona kuwa dhamir ya kwayo inarudia kwenye kukazana nyoyo. Kwamba makusudio ya kuimarika nyayo ni uimara katika uwanja wa vita, na kuacha kukimbia. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amewapa uimara katika uwanja wa vita kama alivyowapa utulivu na uimara wa moyo.

6. Mola wako alipowapa wahyi Malaika: Hakika mimi niko pamoja nanyi, basi watieni nguvu wale walioamini; nitatia woga katika nyoyo za makafiri.

Msemo katika ‘Mola wako’ unaelekezwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.) na katika ‘pamoja nanyi’ na ‘watieni nguvu’ ni kwa Malaika. Hiyo ni kwa kuangalia dhahir ya mfumo wa maneno.

Utauliza: Malaika walishiriki kinamna gani katika kuwasaidia waislamu siku ya Badr? Je, ilikuwa ni kwa kupiga na kuua au ni kwa kushajiisha; kwamba wao walikuwa wanakwenda mbele ya safu kwa sura za watu wanaopigana na wala hawapigani, isipokuwa kuwaambia waislamu: Furahini, hakika Mwenyezi Mungu atawanusuru; kama walivyosema baadhi ya wafasiri?

Jibu : Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliwaamrisha Malaika kuwapa uimara waumini. Hakuna mwenye shaka kwamba wao walifanya, kwa sababu wao wanafanya yale wanayoamrishwa. Vilevile hakuna mwenye shaka kwamba washirikina waliwaogopa waislamu.
Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwaahidi na ahadi yake ni kweli na kwamba waumini wali- washinda washirikina.

Haya ndiyo yanayofahamishwa na dhahiri ya Aya. Ama ufafanuzi na vipi walivyofanya, hayo ni katika mambo ya ghaibu yaliyonyamaziwa na wahyi. Na sisi ni bora kuyanyamazia.

Kunyamaza kwa wahyi ni dalili mkataa kwamba kuamini ufafanuzi si chochote katika itikadi, vinginevyo ingelikuwa wajibu kubainisha.

Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.

Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa msemo ‘Pigeni’ unaelekezwa kwa Malaika. Wengine wakasema wanaambiwa waislamu. Kisha wakatofautiana katika makusudio ya juu ya shingo.

Kuna waliosema makusudio ni shingo zenyewe na kwamba maana ya juu ni kwenye; na wengine wakasema ni vichwa. La kushangaza ni kauli ya baadhi ya masufi kwamba makusudio ni nafsi chafu.

Tuonavyoona sisi ni kwamba maneno hayo wanaambiwa waislamu, kwa sababu ndio waliokusudiwa kupigana. Na kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Juu ya shingo na kila ncha ya vidole’ ni fumbo la kuwahimiza waislamu kukazana kuwaua; wasiwape nafasi ila wawapige kiungo chochote katika viungo vyao.

Aya hii inafanana na Aya isemayo:

وَلَا تَأْخُذْكُمْ بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّهِ إِنْ كُنْتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۖ {2}

Wala isiwashike huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho” (24:2).

Hayo ni kwa kuwa wamemwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

Hayo ni ishara ya ulazima wa kuwatumilia ukali washirikina, kwa vile wao wamekuwa katika msimamo wa upinzani na uhalifu.

Ndiyo hivyo! Basi onjeni! Na hakika makafiri wana adhabu ya moto mbali na yale yaliyowapata duniani. miongoni mwa kuuawa, kutekwa na kushindwa, na hayo si chochote kulinganisha na moto mkubwa.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا زَحْفًا فَلَا تُوَلُّوهُمُ الْأَدْبَارَ {15}

Enyi mlioamini! Mnapokutana vitani na wale waliokufuru, basi msiwageuzie migongo.

وَمَنْ يُوَلِّهِمْ يَوْمَئِذٍ دُبُرَهُ إِلَّا مُتَحَرِّفًا لِقِتَالٍ أَوْ مُتَحَيِّزًا إِلَىٰ فِئَةٍ فَقَدْ بَاءَ بِغَضَبٍ مِنَ اللَّهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ {16}

Na atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo – isipokuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi - hakika amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu; na makazi yake ni Jahannam, napo ni mwishilio muovu.

فَلَمْ تَقْتُلُوهُمْ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ قَتَلَهُمْ ۚ وَمَا رَمَيْتَ إِذْ رَمَيْتَ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ رَمَىٰ ۚ وَلِيُبْلِيَ الْمُؤْمِنِينَ مِنْهُ بَلَاءً حَسَنًا ۚ إِنَّ اللَّهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ {17}

Hamkuwaua nyinyi, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaua. Na hukutupa wewe ulipotupa, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa. Ili awajaribu waumini majaribu mazuri. Hakika Mweyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.

ذَٰلِكُمْ وَأَنَّ اللَّهَ مُوهِنُ كَيْدِ الْكَافِرِينَ {18}

Ndiyo hivyo! Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye adhoofishaye vitimbi vyamakafiri.

إِنْ تَسْتَفْتِحُوا فَقَدْ جَاءَكُمُ الْفَتْحُ ۖ وَإِنْ تَنْتَهُوا فَهُوَ خَيْرٌ لَكُمْ ۖ وَإِنْ تَعُودُوا نَعُدْ وَلَنْ تُغْنِيَ عَنْكُمْ فِئَتُكُمْ شَيْئًا وَلَوْ كَثُرَتْ وَأَنَّ اللَّهَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ {19}

Kama mnataka ushindi, basi ushindi umekwishawajia, na kama mkiacha, basi itakuwa kheri kwenu; na kama mtarudia sisi pia tutarudia; na jeshi lenu halitawafaa chochote hata likiwa kubwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wau- mini.