read

Aya 96 – 100: Na Lau Kama Watu Wa Mji

Maana

Na lau kama watu wa mji wangeliamini na kuogopa, kwa hakika tungewafungulia baraka za mbingu na ardhi.

Baraka ya mbingu iliyodhahiri zaidi ni mvua na baraka ya ardhi, iliyo dhahiri zaidi, ni mimea mifugo na aina kadhaa za madini.

Tumebainisha katika kufasiri Juz. 7, (5:100) kifungu ‘Je riziki ni sadfa au majaaliwa, kwamba kumwamini Mwenyezi Mungu peke yake hakuwezi kuotesha ngano.

Vilevile tumebainisha katika kufasiri Juz.6 (5:66) kifungu ‘Riziki na ufisadi’ kwamba makusudio ya imani yenye kuwajibisha riziki ni kumwamini Mwenyezi Mungu pamoja na kufanya amali kwa hukumu zote za Mwenyezi Mungu na misingi yake. Vilevile kufanya uadilifu katika kila kitu, na kwamba utakapoenea uadilifu na kutawala, basi hali itakuwa nzuri, na kutoweka ubaya na uovu.

Lakini walikadhibisha, kwa hiyo tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

Yaani hawakujua hukumu za Mwenyezi Mungu, bali walihangaika katika ardhi kueneza ufisadi, dhulma, unyang’anyi na kulimbikizaa mali ya jasho la wanyonge. Mwenyezi Mungu amewapatiliza kwa maangamizi. Kwa sababu wao wamekufuru na kujilimbikiza vyote.

Je, watu wa miji wameaminisha ya kuwa adhabu yetu haitawafikia usiku, hali wamelala?

Huu ni uhofisho na tahadhari kutoka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waasi na wenye kujilimbikizia mali kuwa Mwenyezi Mungu atawashtukizia na adhabu yake wakiwa wameghafilika; kama alivyofanya kwa waliokuwa kabla yao.

Je, mtu ataweza kuizuia hukumu ya Mwenyezi Mungu? Vipi ataweza naye atakuwa kama aliyekufa?

Au watu wa miji wameaminisha kuwa adhabu yetu haitawafikia mchana, hali wanacheza?

Wanacheza, hapa ni fumbo la kughafilika kwao na mshtukizo na kujisahau. Utauliza: hakuna tofauti kabisa baina ya kuwa macho mtu na kughafilika kwake mbele ya adhabu ya Mwenyezi Mungu. Sasa je, kuna makusudio gani ya kutaja usingizi na mchezo?

Jibu: Ni kuwa binadamu atambue udhaifu wake, ili awaidhike au aogope.

Je, wamejiaminisha na hila ya Mwenyezi Mungu? Hawaaminishi hila ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara.
Makusudio ya hila ya Mwenyezi Mungu hapa ni adhabu ambayo inawajia ghafla bila ya kutangulia hadhari yoyote.

Yametangulia maelezo kuhusu hila ya Mwenyezi Mungu katika kufasiri Juz.3 (3:54); kwamba yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anajisifu kuwa ni mwenye hila, kwa vile yeye anapangua hila za wenye hila; na anajisifu kuwa ni mwingi wa shukrani kwa vile anawapa thawabu wenye kushukuru.

Ama kuwa wao ni wenye hasara ni kwamba wao wamejingiza katika hasara kwa sababu ya inadi yao na kutojali kwao.

Je, hawaongoki ambao wamerithi ardhi baada ya wenyeji wake kwamba tukitaka tutawasibu kwa dhambi zao?

Yaani hawa washirikina waliorithi ardhi ya wale tuliyowaangamiza kwa dhambi zao, nao walikuwa na nguvu kuliko wao hawabainishi kwamba hali yetu kwao ni sawa na hali yetu kwa waliokuwa kabla yao? Lau tunataka itawapata adhabu yetu, kama ilivyowapata wengineo kabla yao? Hakika desturi ya Mwenyezi Mungu ni moja kwa viumbe vyake vyote.

Lengo la kuendelea sana huku katika nasaha na tahadhari ni kuwa mtu ajichunge wala asighafilike, na awaidhike na mwengine wala asidan- ganyike na mambo ya dhahiri yasiyo na chochote. “Watu wasioamini, haziwafai kitu ishara na maonyo” (10:101).

Na tutapiga muhuri juu ya nyoyo zao, kwa hiyo hawasikii.

Yametangulia maelezo yake katika Juz.1 (2:53).

تِلْكَ الْقُرَىٰ نَقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ أَنْبَائِهَا ۚ وَلَقَدْ جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُمْ بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانُوا لِيُؤْمِنُوا بِمَا كَذَّبُوا مِنْ قَبْلُ ۚ كَذَٰلِكَ يَطْبَعُ اللَّهُ عَلَىٰ قُلُوبِ الْكَافِرِينَ {101}

Miji Hiyo tunakusimulia baadhi ya habari zake. Hakika waliwajia Mitume wao kwa ishara zilizo wazi-wazi, lakini hawakuwa wenye kuamini waliyoyakadhibisha zamani. Namna hii Mwenyezi Mungu anazipiga muhuri nyoyo za makafiri.

وَمَا وَجَدْنَا لِأَكْثَرِهِمْ مِنْ عَهْدٍ ۖ وَإِنْ وَجَدْنَا أَكْثَرَهُمْ لَفَاسِقِينَ {102}

Na hatukuona kwa wengi wao ahadi yoyote. Na hakika tuliwakuta wengi wao ni mafasiki.