read

Jihadi Ndani ya Qur’ani Tukufu

a) Aya za mwanzo

Hebu sasa tuende kwenye baadhi ya aya kutoka kwenye Qur’ani Tukufu.

Vita vya kwanza alivyopigana Mtume na wafuasi wake vilikuwa ni vita vya kujihami kiulinzi. Vinajulikana kama vita vya Badr, sehemu ambayo iko karibu na mji wa Madina (ule mji wa Mtume huko Arabuni). Hivi vilikuwa ni vita ambavyo Mtume alitoka na wafuasi wake kukabiliana na majeshi ya adui ambayo yamekuja kutokea Makkah ambako kulikuwa bado kunadhibitiwa na makafiri.

Aya ya kwanza ya Jihadi ndogo, mapambano ya silaha, ambayo ilishuka kwa wakati huo, imo kwenye Sura ya 22 ya Qur’an Tukufu, aya ya 39-40. inaelezea wazi kabisa lengo la hii Jihadi ndogo:

“Imeruhusiwa (kupigana) kwa wale ambao wanapigwa, kwa sababu wamedhulumiwa, na kwa hakika Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kuwasaidia, wale ambao wametolewa majumbani mwao bila sabau ya haki………”

Halafutena ikizungumzia kuhusu wale makafiri wa Makkah ambao walipigana vita baada ya vita dhidi ya Mtume na wafuasi wake huko Madina, Qur’ani Tukufu katika sura ya 2, aya ya 190 inasema:

“Na wapigeni vita katika njia ya Mwenyezi Mungu wale ambao wanakupigeni vita, wala msiruke mipaka, hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wanaoruka mipaka.”

Katika aya hii, mazungumzo ni kuhusu kutoa majibu kwenye vita kwa kujilinda na kujihami wenyewe, hakuna kauli ya kuanzisha uchokozi hata kidogo. Hata katika mtindo wa mapambano ya kujihami, Mwenyezi Mungu Mtukufu bado anawaonya Waislam kwamba wasije “wakavuka” mipaka inayostahiki.

Uislam unawafundisha Waislam wawe wenye nguvu ili kuweza kujilinda wenyewe, lakini hivyo haina maana kwamba wao wawe wachokozi au madhalimu. Katika Sura ya 8, aya ya 60-61 ya
Qur’an Tukufu, Mwenyezi Mungu ametoa mwongozo huu wa jumla kwa uwazi kabisa pale ambapo anazungumza na Waislam kwa namna ifuatayo:

“Na waandalieni nguvu kiasi mnavyoweza, na kwa farasi ambao wamefunzwa (kwa maandalizi hayo) ili muogopeshe maadui wa Mwenyezi Mungu, na maadui zenu, na wengine wasiokuwa wao, msiowajua, bali Mwenyezi Mungu anawajua.”

Baada ya kutoa maelekezo hayo ya Jumla na mwongozo wa kuwa wenye nguvu na waliojiandaa tayari kwa kujilinda wao wenyewe, aya inaendelea kusema:

“Na kama wakiaelekea (hao maadui) kwenye amani, nawe pia ielekee na umtegemee Mwenyezi Mungu……..”

Kwa ufupi, Uislam unawataka Waislam kuwa na nguvu ili kwamba watu wengine wasije wakawaonea; lakini pia wanapaswa kunyoosha mkono wa amani hata kuelekea kwa maadu zao kama kuna kuwepo na mwelekeo wa amani kwa upande wa adui.

b) Tatizo la Maandiko na Muktadha wake

Baadhi ya waandishi na wazungumzaji wanazinukuu aya za Qur’an Tukufu nje ya muktadha wake na kujaribu kuulaumu Uislamu kwa kueneza vurugu na ugaidi. Wanachukua maandishi na wanayatumia nje ya “muktadha” wake.

Ni sawasawa kabisa na mtu anayetafuta ndani ya Biblia na kuchukua maneno au sentensi zifuatazo ili kuthibitisha kwamba Biblia inaendeleza vurugu:

“Chukua viongozi wote wa watu hawa na uwauwe.” (Hesabu 25:7)

“Sasa wauwe watoto wa kiume wote. Na muue kila mwanamke ambaye amelala na mwanaume, lakini muacheni kila msichana ambaye hajalala na mwanaume kamwe.” (Numbers 31:17-18)

“Muue kila mwanaume na kila mwanamke ambaye sio bikira.” (Waamuzi – 21:11)

Hakuna mtu mwenye akili timamu atakayekubali uwasilisho wa “nje ya muktadha” kama huo wa mistari ya Biblia. Hata hivyo, bado tunawaona wainjilisti na wahubiri wengi wa Kikristo wakifanya hivyo hivyo hasa kwenye Qur’an bila hata kusita kokote kule.

Hivyo hebu tuangalie baadhi ya mifano ya kuchukua “maneno” ya Qur’an Tukufu nje ya “muktadha” wake.

Mfano wa kwanza

Sura ya 2 aya ya 191 inanukuliwa kama ifuatavyo:

“Waueni popote mtakapowakuta.”

Ili kuuelewa muktadha kamili wa aya hii, soma kuanzia aya ya 190 hadi 193 kwa pamoja zote:

“Na wapigeni vita katika njia ya Mwenyezi Mungu wale ambao wanakupigeni vita, wala msiruke mipaka, hakika Mwenyezi Mungu hawapendi warukao mipaka. Na wauweni popote muwakutapo, na muwatoe popote pale walipowatoeni, na fitna ni mbaya zaidi kuliko kuua. Wala msipigane nao katika Msikiti Mtukufu mpaka wao wawapigeni ndani yake. Na ikiwa watakupigeni basi nanyi pia wapigeni, kama hiyo ndio malipo kwa makafiri. Lakini watakapokoma, basi (waacheni) hakika Mwenyezi Munguni mwingi wa kusamehe, mwenye kurehemu. Na wapigeni mpaka pasiwepo na mateso, na dini iwe ni ya Mwenyezi Mungu peke yake, watakapokoma basi pasiwepo na uadui ila dhidi ya madhalimu.”

Muktadha huu unafafanua kwamba ile aya ya 191 inawaruhusu Waislamu wa Madina kujihami wenyewe kiulinzi dhidi ya uchokozi na uvamizi wa makafiri wa Makkah. Kwa hakika haisemi kwamba waende wakipita duniani kote ili kumuua kila kafiri watakayemkuta!

Mfano wa pili

Sura ya 4, aya ya 74 ambayo inadhaniwa kwamba inahimiza umwagaji damu:

“Basi wapigane katika njia ya Mwenyezi Mungu wale wanaouza maisha (yao) ya dunia kwa akhera. Na anayepigana katika njia ya Mwenyezi Mungu akauawa au akashinda, basi hivi karibuni tutampa malipo makubwa.”

Wale wanaoinukuu aya hii, kwa manufaa yao, kwa urahisi tu wanaiacha ile aya inayofuatia ya 75 ambayo inaelezea lengo na uhalali wa hii Jihadi ndogo.

“Na mna nini, hampigani katika njia ya Mwenyezi Mungu, na wale wanaoonewa katika wanaume na wanawake na watoto ambao husema: Mola wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na utujaalie mlinzi kutoka kwako, na utujaalie msaidizi kutoka kwako…………”

Aya hii dhahiri kabisa inawahimiza Waislam kusimama kwa ajili wanaume, wanawake na watoto wanaonewa.

Hivi dini za kimungu zisiwatetee wanaume, wanawake na watoto wanaoonewa?

Mfano wa tatu

Sura ya 9, aya ya 12: “Basi wauweni viongozi wa ukafiri.”

Hii ni sehemu tu ya fungu zima la maneno ambamo Mwenyezi Mungu anazungumzia kuhusu Waislam huko Madina na mkataba wao wa makubaliano ya kusimamisha mapigano na makafiri wa Makkah. Tazama aya ya 12 -14:

“Na kama wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao na wakatukana dini yenu, basi wauweni viongozi wa ukafiri kwani viapo vyao havina maana ili wapate kujizuia. Je, hamtapigana na watu waliovunja viapo vyao na wakafunga nia ya kumfukuza Mtume, nao ndio waliokuanzeni mara ya kwanza? Je mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumuogope, ikiwa nyinyi mmeamini. Peganeni nao, Mwenyezi Mungu atawaadhibu kwa mikono yenu, na awahuzunishe na akunusuruni juu yao na avipoze vifua vya waumini aondoe ghadhabu ya nyoyo zao, na Mwenyezi Mungu humkubalia toba ampendaye, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.”

Muktadha huu kwa uwazi kabisa unatoa haki ya kujihami kwa Waislam, bali kwa hali yoyote ile, hautangazi uchokozi.

Mfano wa Nne

Sura ya 9, aya ya 36: “Na nyote piganeni na washirikina.” Kwa kweli, msitari huu ni sehemu ya aya nzima ambamo Mwenyezi Mungu anazungumzia kuhusu utakatifu wa miezi minne kati ya miezi yote kumi na mbili, ambamo kupigana kumekatazwa. Kisha inasema:

“Na piganeni na washirikina kwa pamoja kama wao wote wanavyopigana nanyi, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanao muogopa.”

Wale wanaopenda kuzichukua aya za Qur’an Tukufu nje ya muktadha wake kwa faida yao wanaiacha ile sehemu “kama wao wote wanavyopigana nanyi.” Kama unavyoona, aya hii pia inatoa majibu kwa ule uchokozi ulioanzishwa na washirikina dhidi ya Waslamu; haizungumzii juu ya kuanza vita.

c) Hitimisho

Kutokana na mifano hii, ni dhahiri kabisa kwamba Uislam hauzungumzii juu ya Jihadi ndogo kwa ajili ya uchokozi; bali inawaruhusu Waislam kujilinda kivitendo maisha yao, mali zao na ardhi zao dhidi ya uchokozi wowote ule, na pia kupigana kwa ajili ya kukomesha udhalimu dhidi ya wanaume, wanawake na watoto wanaoonewa.

Zile aya kuhusu waabudu masanamu wa Makkah zenyewe ni makhsusi sana na zilizohusika kwa kipindi kile tu. Hebu tuangalie tena ile sura ya 22, aya ya 39 hadi 40:

“Imeruhusiwa kupigana kwa wale wanaopigwa kwa sababu wamedhulumiwa, na kwa hakika Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kuwasaidia. Ambao wametolewa majumbani mwamo pasipo haki ila kwa sababu wanasema Mola wetu ni Mwenyezi Mungu. Na kama Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangelivunjwa mahekalu na makanisa, masinagogi na misikiti ambamo jina la Mwenyezi Mungu hutajwa kwa wingi. Na bila shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayemsaidia Yeye. Hakika MwenyeziMungu ni Mwenye nguvu Mtukufu.”

Uislamu unashughulika na jamii ya mwanadamu yenye uhalisia na sio ya kidhanifu. Katika maneno ya Dr. Sayyed Hussain Nasr, “Waislam wanayaona maadili ya Kikristo ni adhimu sana kwa wanadamu wa kawaida kuweza kuyafuata; inaelekea kwamba ile amri ya sheria ya kugeuza shavu la pili ilikuwa ikilengwa kwa watakatifu tu. Wakristo kwa karne nyingi hawakuonyesha kujizuia katika vita kuliko watu wasiokuwa Wakristo. Wazo lililohubiriwa na utaratibu uliofuatwa vimekuwa wakati mwingi havihusiani.” 2

Tumalizie na Sura ya 109 ya Qur’an Tukufu:

“Sema: Enyi makafiri! mimi siabudu mnachokiabudu, wala ninyi hamuabudu ninayemuabudu. Wala sitaabudu mnachoabudu. Wala ninyi hamtaabudu ninayemuabudu. Ninyi mna dini yenu nami nina dini yangu.”