read

Neno La Mchapishaji

Kijitabu kilichoko mikononi mwako ni tarjuma ya Kiswahihi kutoka Kiingereza.

Ni tafsiri pana ya khutba iliyotolewa na mmoja wa wanachuoni wetu mashuhuri wa Kiislamu Sayyid Muhammad Rizvi, katika Bunge la Canada, Ottowa tarehe 20 Septemba, 2006 katika lugha
ya Kiingereza.

Tarjuma yake inatolewa hapa kwa faida ya ndugu zetu wazungamzaji wa Kiswhili wa Afrika ya Mashariki na pengine popote.

.Amani na Jihadi. ni mada ambayo imetumiwa nje ya muktadha wa Kiislamu dhidi ya Uislamu na vyombo vya habari visivyo amini (Uislamu) vya mlengo wa kulia, wanasiasa na pia wanahistoria.

Sayyid Muhammad Rizvi kwa ufupi anaelezea hapa kuhusu amani na Jihadi kama ilivyo katika Uislamu.

Kwa hakika wasomaji wasio na upendeleo watafaidika kutokana na toleo hili.

Tunawashukuru wale wote ambao kwa njia moja au nyingine wamechangia katika utoaji wa tarjuma hii ya Kiswahili ambayo inawasilishwa hapa.

Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es- Salaam , Tanzania .

Utangulizi

Mnamo tarehe 11, Septemba, 2001, watu wachache waliteka nyara ndege ne za kiraia na kuzitumia kama silaa kuzua hofu ndani ya Marekani, hususan kwenye yale majengo mawili ya kituo cha Biashara cha Ulimwengu. Wafanyakazi wote na abiria katika ndege hizo, na vile vile takriban raia wapatao elfu tatu walipoteza maisha yao katika mashambulizi yake.

Sera za mambo ya nje za Marekani kuhusiana na nchi za Kiislam hazithibitishi uhalali wa kwamba raia wa Marekani waliokuwa ndani ya ndege zile na yale majengo ya Kituo cha Biashara cha Dunia wauawe. Hivi sivyo Uislam unavyofundisha. Hebu yaangalie yale maelekezo ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) katika wakati wa vita: Yeye kwa uwazi kabisa alikataza mauaji ya wazee, watoto na wanawake.1 Wale ambao walipoteza maisha yao katika yale majumba marefu ya kituo cha Biashara cha Dunia na ndani y a ndege zile wote walikuwa ni raia, na wachache wao walikuwa ni Waislam.

Viongozi wote wa Kiislam ndani ya Marekani, Canada, na Duniani kote kwa uwazi kabisa walishutumu utekaji nyara ule ambao ulitendwa huko Marekani kama ni kitendo cha kigaidi ambacho hakikubaliki katika Uislam.

Shutuma hizo ziliegemea kwenye thamani ya kidunia ya utukufu wa maisha ya mwanadamu. Qur’an Tukufu inasimulia kisa cha mauaji ya kwanza katika historia, kile cha watoto wawili wa Adam (a.s.) ambamo Qabil (Cain) alimuua ndugu yake, Habil (Abel). Hili liko katika Sura ya 5 ya Qur’an Tukufu, aya ya 27 hadi 31.

Mwishoni mwa kisa hiki, Mwenyezi Mungu anasema:

“………………yeyote atakayemuua mtu ambaye hakuua, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote, na mwenye kumwacha mtu hai ni kama amewaacha watu wote hai……….” (5:32)

Ni dhahiri kutokana na aya hii kwamba (1) isipokuwa kama mtu ameshitakiwa na kuthibitika kuwa amemuua mtu, yeye hawezi kuuawa – na (2) kwamba kumuua mtu asiye na hatia ni sawa na kuua watu wote.