read

Mwanzo mwanzo wa mwezi huu (Muharram 1424), hapa Mombasa, pametolewa karatasi zenye kichwa cha habari "Barua ya wazi kwa wahubiri na ma-imamu wa sunna". Lengo la karatasi hizo ni kuwaonyesha hao wahubiri na maimamu wa kisunni makosa wanayoyafanya ya kuweka "vikao vya mawaidha, khususan katika siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Muharram".

Barua Ya Wazi Kwa Mawahhabi

1) 8 Muharram, 1424, 12 Machi, 2003

Mwanzo mwanzo wa mwezi huu (Muharram 1424), hapa Mombasa, pametolewa karatasi zenye kichwa cha habari "Barua ya wazi kwa wahubiri na ma-imamu wa sunna". Lengo la karatasi hizo ni kuwaonyesha hao wahubiri na maimamu wa kisunni makosa wanayoyafanya ya kuweka "vikao vya mawaidha, khususan katika siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Muharram". Kwa maoni ya waandishi wa karatasi hizo, "hakuna hadith (dalili) ambayo inatuambia tufanye hivyo" isipokuwa huo ni "uzushi" ambao, kwa kuufanya, "mwawapoteza wafuasi wa Sunna kwa kuwaiga hao hao Ma-Shia".

Waliozitoa karatasi hizo wamejiita "Ahlul-Tawheed" ambao, kama wasomi wote wanavyojua, ni mawahabi. Wao hutumia jina hilo kwa sababu mbili. Sababu ya kwanza ni kuficha uwahabi wao wanaojua kwamba unapingwa na Waislamu wote. Kwa hivyo wanaogopa kukosa kuungwa mkono. Sababu ya pili ni kutokana na ile imani yao kwamba wao peke yao ndio wanaompwekesha Mwenyezi Mungu; Waislamu wengine wote wasiokubaliana nao, kivyao, ni mushrikina. Lakini kwa kuwa Waislamu wote wanaamini kwamba ni ahlut tawhiid, kwa vile wote wanaikiri Laa ilaaha illallaah, waandishi wa karatasi hizo, kwa kutumia jina hilo, wanataka kuwavungavunga Waislamu wawafikirie kuwa ni wenzao.

Katika karatasi zangu hizi si nia yangu kuwajibia ndugu zangu, wahubiri na maimamu wa kisunni, kwa sababu ninaamini kwamba wao wenyewe wanao uwezo wa kufanya hivyo - lau wataona ni dharura. Nia yangu khaswa ni kujibu yale waliyoyaandika kuhusu mashia na ushia.

Katika karatasi zao wamesema: "Waandishi wa ki-Sabai wa Iraq walizua hadithi za urongo, za kikatili na za kutisha, kama vile kunyimwa maji ya kunywa (Hussein na watu wake) na kulazimishwa kupigana, kukatwa vichwa. Ambazo haziaminiki wala haziwezi kutegemewa na pia ziko mbali na ukweli."

Majibu yetu: Penye vitabu vya Kiswahili, viwezavyo kupatikana madukani humu humu mwetu, hapana haja ya kutaja vitabu vya lugha nyengine ambavyo wengi wa watu hawana au hawawezi kuvipata au hawaijui lugha iliyoandikiwa vitabu hivyo. Kwa hivyo tuangalie kitabu kiitwacho Maisha ya Sayyidna Huseyn (chapa ya 1999) kilichoandikwa na Sheikh Abdalla Saleh Farsy na kuchapishwa na Adam Traders wa Mombasa.

Katika uk. 37 wa kitabu hicho, Sheikh Abdalla ameandika hivi: "Alipowajibu kwa yakini (yaani Imam Husein) kuwa hakubali kwenda kuuawa na Ubeydillah na kudhalilishwa, wala kuuawa watu wake na kudhalilishwa, wanaume na wanawake na watoto, waliwazunguka darmadar wasiwe na njia ya kupenya na kukimbia. Wakakosa maji na chakula tangu hapo mwezi nane Mfunguo Nne 61 mpaka mwezi kumi 61; hapo wakaingia kuwapiga baada ya kuwa hawajifai kwa njaa na kiu". Baada ya hayo, akataja orodha ya watu kumi na moja ambao ndio "wa mwanzo kuuawa"; wote wakiwa ni jamaa zake Mtume (s.a.w.w.)!

Na katika uk. 39 wa kitabu hicho hicho, akasema kwamba baada ya kuuliwa hivyo, walipelekwa "kwa shangwe kubwa na ngoma mpaka Al Kufa kwa Liwali. Kila mtu akajitapa mbele ya huyo Liwali 'Mimi nimemuua fulani …. Mimi nimemuua fulani…' na huku wanapewa tuzwa (tunza)". Wakifika huko, Sheikh Abdalla anasema, ikawa "vichwa vimetawanywa chini".

Jee, vichwa hivyo vilitoka vyenyewe miilini mwao au vilikatwa?

Wakasema tena katika hiyo karatasi yao: "Na madai ya Mashia kwamba Hussein alikatwa kichwa chake ni urongo mtupu."

Majibu yetu: ni tumsome tena Sheikh Abdalla Saleh Farsy. Katika uk. 38 wa hicho kitabu chake, shekhe wetu huyo anaeleza kwamba, baada ya kumzingira "kila upande kwa kumpiga kwa mishare, mikuki na panga mpaka akaanguka chini wakamkata kichwa. Na qawli mashuhuri (ni) kuwa aliyemkata kichwa ni Shimr bin Dhiljawshan…" Kisha akaongeza: "Pesa na kutaka ukubwa kunafanya kazi."

Wala madhalimu hao hawakutosheka tu na kukikata kichwa cha Imam Hussein (a.s). Anavyoeleza Sheikh Abdalla Saleh Farsy (uk. 39) ni kwamba, kilipofika kwa Liwali Ubeydillah, ikawa "anakigonga kichwa cha Al Huseyn kwa kifimbo mkononi kama kwamba anapiga upatu au chapuo." Na kilipofika kwa Mfalme mwenyewe (Yazid bin Muawiya), Sheikh Abdalla anaeleza (uk. 40), alifanya "kama yale aliyoyafanya Liwali wake wa Al Kufa. Akakamata kifimbo akawa anayagonga meno ya Huseyn …"

Basi hayo ndiyo aliyoyaandika Sheikh Abdalla Saleh Farsy aliyekuwa Kadhi Mkuu wa Kenya na, kabla ya hapo, Zanzibar. Jee, yeye alikuwa "mwandishi wa ki-Sabai wa Iraq?" Alikuwa Shia? Ni "mrongo"? Hakuwa shekhe mkubwa waliyekuwa wakijifakhiri naye hao "Ahlul Tawheed", na mpaka leo hujifakhiri naye? Sasa wanasemaje?

ABDILAHI NASSIR
S.L.P. 84603
MOMBASA
8 Muharram, 1424
12 Machi, 2003
(Inaendelea)

2) 15 Muharram, 1424 19 Machi, 2003

Katika karatasi yetu ya kwanza, kinyume na walivyodai mawahabi katika karatasi yao, tulionyesha kwamba si "urongo", wala si uzushi wa mashia, kusema kuwa Imam Hussein (a.s) na watu wake waliuliwa kinyama kwa kukatwa vichwa vyao huko Karbalaa, Iraq. Tuliyatia nguvu maneno yetu hayo kwa ushahidi wa yaliyoandikwa na Sheikh Abdalla Saleh Farsy katika kitabu chake kiitwacho Maisha ya Sayyidna Huseyn. Leo inshallah tutalijadili dai lao jengine: la kuwa ati Yazid, ambaye chini ya utawala wake ndipo mauwaji hayo yalipofanywa, alikuwa "Amirul-muuminin"!

Lakini kabla ya kuonyesha kuwa mtu huyo -- kwa vipimo vya Kiislamu -- hakuwa, wala hawezi kuwa hivyo, ni muhimu kwanza tuelewe jinsi alivyoupata utawala wake huo. Na hilo, kama tulivyofanya katika karatasi yetu ya kwanza, tutamwachia Sheikh Abdalla S. Farsy alifanye japokuwa aliyoyaandika yeye, tukilinganisha na yaliyoandikwa na wanazuoni wengine wa kisunni kwa lugha ya Kiarabu, ameyazimua mno.

Kabla ya Yazid kutawala katika mwaka wa 60 BH, Waislamu walitawaliwa na babake aliyekuwa akiitwa Muawiya bin Abii Sufyan. Wote wawili hao -- babake na babu yake -- walisilimu kwa kukosa budi baada ya Makka kutekwa na (kabla ya hapo) baada ya kuongoza upinzani mkali dhidi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.), na kushindwa.

Huyo Muawiya ndiye yule aliyesimama kumpinga na kumpiga vita "Khalifa wa Nne" (Imam Alii bin Abii Twaalib a.s.) alipochaguliwa na Waislamu kuwa Khalifa wao; na baada ya Imam Alii (a.s) kuuliwa, akaingia kumpinga na kumpiga vita Imam Hassan a.s. (ndugu yake Imam Hussein a.s.) ambaye, anavyotwambia Sheikh Abdalla S. Farsy, aliuliwa "kwa sumu" na yeye huyo Yazid tunayeambiwa kuwa ati ni "Amirul-muuminin"! (Tizama uk. 24 wa kitabu chengine cha Sheikh Abdalla S. Farsy kiitwacho Maisha ya Sayyidna Hassan (chapa ya 1999) kilichochapishwa na Adam Traders wa Mombasa vile vile).

Lakini kwa kiasi cha miaka kumi kabla ya kupawa hiyo sumu, Imam Hassan (a.s) na Muawiya, babake Yazid, baada ya vita vikali, walifanyiana suluhu na kuandikiana mkataba. Kati ya waliyokubaliana katika mkataba huo, anavyotueleza tena Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 16 wa kitabu chake hicho, ni kwamba Imam Hassan (a.s) amwachie Muawiya Ukhalifa. Lakini Muawiya akifa, basi Imam Hassan (a.s) ataukamata yeye. Na lau Imam Hassan (a.s) atakufa, basi ushikwe na Imam Hussein (a.s).

Kuona hivyo, Sheikh Abdalla S. Farsy anaendelea kutueleza katika uk. 24 wa kitabu chake hicho hicho cha Maisha ya Sayyidna Hassan, "akili ilimjia (Yazid) akaona kuwa huu ufalme wa baba yangu utanipotea kwani akifa baba yangu atatawala Hasan, wala haikuandikwa kuwa akifa nitatawala mimi. Akaona amuue kwa sumu. Akapeleka watu madhubuti kwa siri kwa mke wa mwisho wa Sayyidnal Hasan, wala hakuzaa naye, akiitwa Jaada bint Ash-ath. Wamtumainishe kuwa akimuua huyu mumewe atamuoa Yazid na tangu sasa atampa dirham laki moja,, na mengineyo makubwa kabisa anayoyataka. Bibi akavutika akampa sumu kali kabisa huyo mumewe. Akasononeka muda wa siku arbaini; kisha akakata roho hali ya kuwa shahidi…"

Na katika uk. 18 wa Maisha ya Sayyidna Huseyn, Sheikh Abdalla S. Farsy anasema: "Kabla ya kufa Sayyidna Hasan … Muawiya aliona ajifungue na ahadi ya kumtawalisha Al Hasan wala hana ahadi ya kumtawalisha mwengine. Basi aliona amfanye mwanawe anayempenda zaidi - naye ni Yazid - awe waliyyul ahdi (heir-apparent). Itangazwe kwa raia wote kuwa akifa yeye hakuna uchaguzi wowote ila kuwa mwanawe - Yazid - ndiye Khalifa tu. Akiridhia Hasan asidhie na mwengine yeyote yule akiridhia asiridhie." Akamalizia kwa: "Maliwali wake wengine -- kwa ajili ya kutaka kujipendekeza ili waendelee na Uliwali wao -- walimtia nguvu katika fikira hii ijapokuwa siyo ya Uislamu…"

Inshallah tutaendelea na yaliyobakia, ya jinsi Yazid alivyotawalishwa, katika karatasi ijayo. Kwa sasa tunalopenda ujiulize, ewe ndugu msomaji, ni: Kweli, mtu anayetawalishwa kama ilivyoelezwa hapo juu, huwa ni "Amirul-muuminin"? Hivyo ndivyo Uislamu usemavyo?

ABDILAHI NASSIR
S.L.P. 84603
MOMBASA
15 Muharram, 1424
19 Machi, 2003
(Inaendelea)

3) 22 Muharram, 1424 26 Machi, 2003

Katika karatasi ya pili, kabla ya kuonyesha kuwa ni muhali Yazid kuwa Amiirul-mu'minin, tulianza kwa kueleza jinsi alivyoupata utawala wake. Kwa yaliyoandikwa na Sheikh Abdalla Saleh Farsy katika vitabu vyake tulivyovinukuu mpaka sasa hivi, inatudhihirikia kuwa aliupata kwa yeye kumuuwa Imam Hussein a.s., kwa babake (Muawiya) kuvunja ahadi aliyopanana na Imam Hassan a.s., na pia kwa kutumia hongo, vitisho na mabavu. Leo tuendelee na yaliyobakia.

Baada ya Imam Hassan a.s. kufa kwa ile sumu, Muawiya alipanga mikakati yake ya kumtawalisha mwanawe (Yazid). Lakini, hata hivyo, haikuwa rahisi. Anavyosema Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 18 wa kitabu chake, Maisha ya Sayyidna Huseyn, ni kwamba "aliona ni uzito kabisa kutaka kulivunja jambo hili, sharti alichukulie mbinu kwa taratibu, akaona awafundishe Maliwali wake watoe fikira hii, isiwe imetokana na yeye. Akawaambia walisemeseme wenyewe tu huko katika nchi wanazoziendesha kama mchezo tu hivi kwanza."

Baada ya hapo, aliwakusanya wote mahali pamoja na, kama alivyowafundisha, ikawa mmoja baada ya mmoja husimama na kupendekeza utawala aachiwe Yazid. Lakini hata hivyo, si wote walimkubalia Muawiya; wengine walipinga: mmoja wao akiwa Al Ahnaf bin Qays. Huyu, Sheikh Abdalla S. Farsy anatwambia (uk. 20 wa hicho kitabu chake), alisema hivi: "La! Sisi watu wa Iraq sote si radhi kwa haya, na watu wa Hijaz wote pia hawawafiki. Hatumridhii kattu Yazid kuwa Khalifa wa Waislamu. Na wewe unamjua zaidi mwanao, kuliko watu wengine, kuwa hafai. Usijitwike mzigo wa kukutia Motoni kwa khiyari yako. Sisi haturidhii ila kizazi cha Ali.”

Mambo yakakorogeka. Sheikh A. S. Farsy anasema (uk. 20): "Akainuka Abu Khunayf akatoa upanga wake akamwonyesha … Muawiya akamwambiya 'Asiyekubali mlishe huu atashika adabu yake'. Akainuka …Muawiya akasema, 'Huyu ndiye khatibu barabara. Khatibu vitendo si maneno tu. Na huyu ndiye bora wa wote waliohudhuria hapa na wengineo'. Baraza ikavunjika."

Bibi Aisha, mke wa Bwana Mtume s.a.w.w., aliposikia habari hiyo, Sheikh A. S. Farsy anaendelea (uk. 21), "alikasirika sana sana kuona vile … Muawiya anazivunja zile ahadi alizompa Sayyidnal Hasan…"

Mambo yakamalizikia hapo, yasende mbele zaidi. Lakini baada ya muda (mwaka wa 50 BH), Muawiya alikwenda Madina, asemavyo Sheikh A. S. Farsy (uk. 21), "kugonga gogo asikie vipi mlio wake". Huko alikutana na "watoto wa kisahaba wenye jina kubwa kabisa"; nao ni mabwana "Abdulla bin Abbas bin Abdul Muttalib (hakuweta ndugu zake), Abdulla bin Jaafar bin Abii Talib bin Abdil Muttalib (hakuweta ndugu zake), na Abdulla bin Zubeir bin Awam (hakuweta ndugu zake) wala hakumwita Sayyidnal Huseyn." Akasema nao kwa ulatifu ili wamkubali Yazid, lakini wote wakapinga; na baada ya siku mbili tatu, akenda zake mtungi mtupu!

"Alipokufa Sayyidnal Hasan", Sheikh A. S. Farsy anazidi kutueleza (uk. 22), "…Muawiya aliwaamrisha watu wa Sham wote wamkubali Yazid kuwa ndiye Khalifa baada yake. Wakakubali wote kwa umoja wao." Akamwamrisha Liwali wa Madina awalazimishe watu wake nao wamkubali Yazid. Yeye, anavyosema Sheikh A. S. Farsy (uk. 23), "yakamuudhi haya akaona kwa nini tumkubali kijana asiyekuwa na mwendo mzuri atutawale sisi watu wazima na Masahaba". Kwa hivyo akamjulisha Muawiya msimamo wake, na Muawiya papo hapo "akamwandikia barua ya kumtoa katika Uliwali".

Alipopata barua hiyo, Liwali huyo (Marwan bin Hakam) alihamaki "sana sana na akachukua wakubwa wa jamaa zake wa kukeni -- Bani Kinana -- mpaka Sham kwa Muawiya kumtishia kuwa atafanya thora (mapinduzi). Muawiya akamwogopa akampa -- na akawapa na hao jamaa zake -- maneno mazuri na fedha nyingi na mshahara wa maisha. Yeye pouni mia tatu kila mwezi, na kila mmoja katika hao jamaa zake pouni khamsini kila mwezi."

Huko Madina, Liwali mpya aliifuata baraabara ile amri ya Muawiya ya kuwalazimisha watu wake wamkubali Yazid. Lakini hawakukubali; walipinga. Liwali akamjulisha Muawiya hilo pamoja na kumtajia waliokuwa mstari wa mbele katika upinzani huo. Naye akampelekea "barua za watu hao, akamwamrisha awapelekee na amletee jawabu ya kila mmoja katika wao. Nao ni mabwana hawa: Abdulla bin Abbas bin Abdil Muttalib, Huseyn bin Ali bin Aby Talib bin Abdil Muttalib, Abdalla bin Jaafar bin Aby Talib bin Abdil Muttalib, na Abdalla bin Zubeir bin Safiyya bint Abdil Muttalib." Aliwaandikia "maneno makali kabisa", Sheikh A. S. Farsy anaeleza katika uk. 24 wa kitabu chake hicho, "na kuwahadidi kuwa atawaua wakikataa kumkubali Yazid awe Khalifa baada yake."

Baada ya hapo ilikuaje? Hilo tutalizungumza katika karatasi ijayo inshallah. Kwa sasa tunauliza tena: Anayetawalishwa hivyo huweza kuitwa Amiirul-mu'minin? Ndivyo Kiislamu hivyo

ABDILAHI NASSIR
S.L.P. 84603
MOMBASA
22 Muharram, 1424
26 Machi, 2003
(Inaendelea)

4)1 Safar,1424 ,4 Aprili, 2003

Katika karatasi yetu ya tatu tulionyesha, kwa ushahidi wa maneno ya Sheikh Abdalla S. Farsy, jinsi Muawiya alivyotumia njama, vitisho na hongo kumtawalisha mwanawe (Yazid). Lakini mbinu zote hizo hazikufaa kitu. Ndipo pale alipowaandikia wale mabwana wane wa Madina, tuliowataja katika karatasi yetu Na. 3, barua kali za kuwaonya.

Walipozipata barua hizo, mabwana hao (anavyosema Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 24) walimjibu "kwa maneno makali kabisa na tahadidi kubwa kabisa. Na aliyemwandikia maneno mengi kabisa ni Sayyidnal Huseyn."

Alipozipata jawabu zao hizo, Muawiya alimwambia tena huyo Liwali wake "azidi kuwalazimisha kwa tashdidi kubwa zaidi kabisa. Akafanya", Sheikh Abdalla S. Farsy anasema (uk. 24), "zisifae kitu." Kwa hivyo akamwandikia Muawiya ende tena huko Madina akaonane nao yeye mwenyewe.

Alipofika Madina, na "baada ya kupumzika", Sheikh Abdalla anasema (uk. 25), Muawiya "aliwaita kila mmoja akamsemeza siri peke yake ili wasimjibu wote kwa jawabu moja." Wa kwanza alikuwa ni Imam Hussein a.s. "Akamwambia, 'Mwanangu! Usiutilie fujo uma wa babu yako. Watu wote wamekwisha kuridhia kuwa Yazid awe Khalifa baada yangu. Hakuna wanaopinga ila nyinyi tu, na wewe ndiye unayewaongoza. Ukikubali wewe na wao wataridhia, kama walivyonambia.' (Imam Hussein a.s.) akamwambia, 'Wete mbele yangu hapa waseme hayo. Mimi sisadiki kuwa wamesema hivyo. Wakikiri mbele yetu hapa na mimi nitakuwa pamoja nao. Lakini nina yakini kuwa hawatakiri.' Akamwambia, "Basi nenda zako. Lakini usimhadithie yo yote lo lote katika tuliyoyasema." Hivyo ndivyo alivyoandika Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 25 wa kitabu chake hicho.

Baada ya Imam Hussein a.s., alimwita Bwana Abdalla bin Zubeir, kisha Bwana Abdulla bin Umar bin Al Khattab. Nao wakamjibu kama alivyojibu Imam Hussein a.s. "neno kwa neno". Hapo tena, Sheikh Abdalla anasema (uk. 25 -- 26), "akapeleka mtu kumwita Bwana Abdur Rahman bin Aby Bakrinis Sidiqq. Akamsemesha maneno makali kabisa na yeye akamjibu makali kabisa. Wakaghadhibishana kweli kweli kwani yeye alikuwa mtu mzima kama yeye."

Baada ya hapo ilimbidi Muawiya abadilishe mbinu. Kwa hivyo "siku ya pili", Sheikh Abdalla anasema (uk. 26), " akapeleka mtu kumwita Sayyidnal Huseyn bin Ali na Bwana Abdalla bin Abbas." Baada ya kuzungumza nao "mambo ya hali zao na hali za majumbani mwao", aliingia "kumsifu mwanawe Yazidi kwa aliyonayo na asiyokuwa nayo. Kisha akawaambia, 'Basi kwa hivi anastahiki kuwa Khalifa wa Waislamu…' " Imam Hussein a.s. akamjibu, Sheikh Abdalla anaendelea (uk. 26), kwa kumtajia "sifa mbovu za Yazid na akamwambia, 'Usizidishe madhambi kuliko uliyoyachuma. Yamekutosha hayo.' Na akamwambia, 'Unaudhulumu Uislamu na Waislamu kwa hayo uliyoazimia kufanya.'"

Baada ya kutofaulu mbinu zake hizo, aliamrisha waitwe mabwana wote watatu: Abdur Rahman bin Aby Bakr, Abdulla bin Umar, na Abdalla bin Zubeir. Sheikh Abdalla anasema (uk. 27), "Akawakaribisha wote pamoja kwa wakati mmoja. Akawaambia, 'Hili jambo la kufanywa Yazid kuwa Khalifa kishalichagua Mwenyezi Mungu na watu wote wameliridhia isipokuwa nyinyi. Basi tahadharini na kuleta balaa. Itakufikeni wenyewe kwa adhabu ya Mwenyezi Mungu na yangu …' Wakampinga wote… Akataka aseme faragha na Bwana Abdur Rahman bin Abi Bakr. Alipomwambia maneno hayo ya kutawalishwa Yazid, alimwambia, 'Hatutaki. Na ukiyapitisha kwa nguvu tutavirejesha upya vita vya mwanzo wa Uislamu; uwe na wenye shauri moja na wewe upande wa ukafiri kama alivyokuwa baba yako.' " Hapo Bwana Abdur Rahman akaondoka.

Baada ya siku tatu ikatoka amri ya kukusanyika watu wote wa Madina. Hapo Muawiya akawaweka wale wapinzani karibu yake, na akawaeleza waliohudhuria kuwa mikoa yote imemkubali Yazid kuwa Khalifa isipokuwa wao watu wa Madina, na kuwa lau yeye (Muawiya) angelikuwa anamjua aliye bora kuliko Yazid, angelimtawalisha; lakini hakuna bora kuliko yeye! Kisha akawaonya asisikie "kupinga kokote kule". Na akatangaza mkutano mwengine jioni.

Kabla ya huo mkutano, Sheikh Abdalla anaeleza (uk. 28 -- 29), aliweta wale wapinzani "wote pamoja ili atoke nao wende mkutanoni. Walipofika akawaambia: 'Nimekwisha weka machakari (wauaji) huko mkutanoni. Na mimi nitawaambia watu wote huko kuwa nyinyi nyote sasa mmekubali kutawalishwa Yazid. Asiyetaka roho yake ainuke hapo anipinge. Papo hapo kitaonekana kichwa chake kinagaragara chini.' " Na huko mkutanoni alikuwa ameshawaambia "mbele hao maaskari kuwa ye yote atakaesema kitu muuweni. Na akafanya ijulikane habari hii kwa watu wote ili wote wawemo katika khofu."

Haya! Huyo ndiye Muawiya! Na hivyo ndivyo alivyopanga kumtawalisha mwanawe (Yazid) ambaye leo mawahabi wetu wasema kuwa mtu kama huyo ni Amiirul-mu'minin! Astaghfirullaah!

Inshallah, katika karatasi yetu ijayo, tutayaeleza yaliyotokea huko mkutanoni na aliyoyafanya Yazid baada ya kutawalishwa. Kisha tujiulize tena: mtu kama huyo kweli aweza akawa Amiirul mu'minin?

ABDILAHI NASSIR
S.L.P. 84603
MOMBASA
1 Safar, 1424
4 Aprili, 2003
(Inaendelea)

5) 8 Swafar, 1424 11 Aprili, 2003

Katika karatasi yetu ya nne tuliona mbinu na hila mbalimbali ambazo Muawiya alizitumia kumpatia mwanawe, Yazid, utawala. Alitumia ulaghai, hadaa, uswalata, hongo mpaka vitisho na mabavu! Mwisho, baada ya mbinu zote kushindwa, aliita mkutano wa hadhara.

Kwenye mkutano huo, kama alivyowaonya kina Imam Hussein a.s., alipanda juu ya mimbari akasema, “Shuhudieni kuwa hawa waliokuwa wakipinga, sasa wameridhia. Na wenyewe hawa wote wako hapa. Na hawa ndio wazalendo wa Madina na wa Kisahaba. Hakuna lililosalia tena.” Hivyo ndivyo anavyoeleza Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 29 wa kitabu chake; na akaendelea kuandika, “Akatoa hapo mafedha kwa mafedha kuwapa kila wakubwa wa kila qabila za Kimuhajiri na Ansari na nyinginezo…” Na hivyo ndivyo Yazid alivyopatiwa utawala katika mwezi wa Rajab, mwaka wa 60 BH, baada ya babake kufa.

Ewe ndugu Mwislamu! Ikiwa mambo yalikwenda hivyo, kama yalivyoelezwa na Sheikh Abdalla Saleh Farsy, kweli Mwislamu yoyote anayeujua Uislamu wake, na anayetaka kubakisha jina jema la Uislamu, anaweza kujifakhiri kuwa mtu kama Yazid alikuwa ni kati ya viongozi wake wa Kiislamu, sambe (seuze) kumkubali kuwa ni Amiirul mu’minin?! Lakini hayo si aliyoyafanya Yazid, yeye mwenyewe; ni aliyofanyiwa na babake, Muawiya. Aliyoyafanya yeye mwenyewe, baada ya kutawala, ni makubwa zaidi! Ni yapi?

Kwa ufupi, anavyotueleza Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 29-41 wa kitabu chake hicho, alifanya yafuatayo:

1. Alimpelekea habari Liwali wake wa Madina wa wakati huo, naye ni Khalid bin Hakam, awaapishe mabwana hawa: Huseyn bin Ali bin Abi Talib, Abdalla bin Umar bin Al Khattab, Abdalla bin Al Abbas na Abdalla bin Zubeir. (Abdur Rahman bin Abi Bakr hakuwamo; alikuwa ashakufa). Alimwamrisha “awaapishe yamini kali kabisa kuwa wamekwisha mkubali Yazidi kuwa ndiye Khalifa wa Waislamu wote. Na kuwa wakenda kinyume naye mali yao yawe halali yake, wake zao waachike. Na watumwa wao wawe mahuru,”

2. Liwali huyo alipoweta Imam Hussein a.s. na Abdalla bin Zubeir, waliomba waachwe mpaka siku ya pili. “Kufika majumbani mwao tu”, Sheikh Abdalla anaeleza (uk.30),“waliwaaga watu wao wakatoka kwa siri kwenda Makka kukaa huko kwani mwenye kuweko huko huwa katika amani…” Yazidi, kupata habari hiyo tu, alihamaki “akamtoa( Liwali huyo) katika Uliwali wake.”

3. Alipotawala Yazid, kimabavu kama tulivyokwisha kuona, watu wa Al Kufa (Iraq) walimpelekea Imam Hussein a.s. “mabarua ya kumhimiza ende huko Iraq azatiti vita huko kumuondoa huyo asiyestahiki kuwa Khalifa wa Waislamu”. Hata hivyo, Imam Hussein a.s. hakwenda papo hapo, bali alimtuma binami yake (Muslim bin Aqyl) ende huko ili amjulishe ukweli wa mambo ulivyo. Alipopata habari hiyo, Sheikh Abdalla anatueleza (uk 34-35), Yazid “alimchagua Liwali qatili,dhalimu, jabbar, shujaa anayemchukia Sayyidna Ali na kizazi chake, aliyekuwa akiitwa Ubeidillah bin Ziyad ambaye baba yake alithibitishwa na…. Muawiya -- kwa siyasa tu -- kuwa ndugu yake. Akatiwa katika kabila yake ya Bani Umayya hali ya kuwa hakhusiani naye hata chembe, wala hakhusu Uqureshi hata kidogo, bali wala Uwarabu. Ni mtu mwanaharamu tu aliyekuwa hodari sana hata akampinga Muawiya kweli kweli. Akaona amthibitishe kuwa ndugu yake na amwachie amri ya Iraqi yote". Hivyo akawa mwana haramu wa kwanza, katika historia ya Uislamu, kufanywa mwana halali!

4. Baada ya kumchagua Liwali huyo, Sheikh Abdalla anaeleza (uk. 35), Yazid alimpa amri hii: "Muuwe huyu Muslim bin Aqyl, na kila waliokuja pamoja naye, na kila waliompokea, na kila walio pamoja naye; na mfunge umuadhibu jamaa na jirani wa kila mmoja katika hawa, usiwe na huruma na yeyote." Na hivyo khaswa ndivyo ilivyokuwa. "Alifanya kama alivyoamrishwa na Yazid, akawamaliza hao wote alioamrishwa awaue, na akawafunga hao alioamrishwa awafunge…"

Katika kitabu chake, Sheikh Abdalla S. Farsy hakueleza jinsi alivyouliwa Muslim bin Aqyl. Lakini vitabu vyengine vya historia vinaeleza kwamba alichukuliwa mpaka juu ya kasri moja, akakatwa kichwa ambacho kilitupwa chini kikifuatishwa na pingiti lake. Baadaye kichwa hicho kikapelekwa kwa Yazid!

5. Kama tulivyokwisha kuona katika karatasi yetu Na.1, baada ya Imam Hussein a.s. na aliokuwa nao kuuwawa kikatili na kukatwa vichwa vyao, Yazid (alipopelekewa vichwa hivyo) alikamata kifimbo, Sheikh Abdalla S. Farsy anatueleza (uk 40), "akawa anayagonga meno ya Huseyn na kuimba kusema, ' Nimemlipa leo Muhammad ! Kama alivyoniuliya wazee wangu siku ya Vita vya Badr, leo nimemuulia wajukuu wake. Na huu ndio mwendo wetu utakaokuwa. Kila anayetupinga tutamwua japokuwa anatukhusu…"

Ewe ndugu Mwislamu! Hebu jiulize: Mtu anayejasiri kusema kuwa anamlipa kisasi Mtume Muhammad s.a.w.w. kwa kuwauwa makafiri (waliokuwa babu zake yeye Yazid) hufaa au huweza kuitwa Amiirul-mu'minin? Acha hilo! Huweza hata kuitwa Mwislamu? Hivi hao mawahabi wetu hawakulijua hilo? Au watatwambia kuwa Sheikh Abdalla Saleh Farsy alikuwa Shia?

Kuna yaliyobaki, na si madogo! Inshallah hayo tutayamaliza katika karatasi ijayo.

ABDILAHI NASSIR
S.L.P. 84603
MOMBASA
8 Safar, 1424
11 Aprili, 2003
(Inaendelea)

6) 15 Swafar, 1424 18 Aprili, 2003

Katika karatasi yetu ya tano tuliona, katika mkutano wake wa hadhara aliouita, jinsi Muawiya alivyombandika Yazid kutawala baada yake. Vile vile tulianza kuyadondoa mambo mabaya aliyoyafanya Yazid mara tu baada ya kukikalia kiti cha ufalme wake. Leo tutaendelea na yaliyobakia, japokuwa kwa ufupi, ili tusiyarefushe mambo.

6. Baada ya kumuuwa Imam Husein a.s. na aliokuwa nao katika mwaka wa 61 BH, Yazid aliiingilia Madina. Sheikh Abdalla Saleh Farsy anatwambia (uk. 41): "Wakauawa Masahaba wengi hapo Madina na wasiokuwa Masahaba. Na wakafanya fisadi kubwa sana hapo Madina muda wa siku tatu mfululizo. Ikawa hakuna kisichoharibiwa; si roho wala mali wala hishima. Aliwaamrisha Yazid wafanye hivyo. Na masahaba wasiokufa
aliwaamrisha wapigwe chapa za mgongo za kuonyesha kuwa wao ni watumwa wa Yazid." Subhaanallah! Huyo ndiye Amiirul-mu'minin wa mawahabi wetu!

Katika dondoo hilo hapo juu, hata hivyo, Sheikh Abdalla "amefinika kombe" ; hakulifunua. Lakini wanazuoni wenziwe wamelifunua. Kati ya hao ni Ibn Kathir ambaye, kwa mawahabi wa ulimwengu, ni kama Sheikh Abdalla Saleh Farsy kwa mawahabi wa Afrika ya Mashariki; wanamuenzi sana. Yeye, katika uk 220 wa Juzuu ya Sabaa ya kitabu chake kiitwacho Al Bidaaya Wan Nihaaya, amesema kuwa idadi ya hao "masahaba wengi" waliouwawa ilikuwa " mia sabaa: vigogo vya muhaajiriin na answaar"; na "wasiokuwa masahaba" walikuwa " elfu kumi". Kuhusu " fisadi kubwa sana", alizosema Sheikh Abdalla S. Farsy, Ibn Kathir anasema ( uk. 222) kuwa "hazisemeki hazielezeki; hakuna anayezijua ila Mwenyezi Mungu" japokuwa, kabla ya hapo katika uk. 220, alikuwa ameshatasua kuwa " wanawake walihashiriwa mpaka ikasemwa kuwa 1000 ( elfu moja ) walishika mimba na kuzaa bila kuwa na waume"!

Baada ya Ibn Kathir kuyaeleza hayo, na kama kwamba anataka kuzindua tumfahamu Yazid ni nani, anatutajia (uk 223) Hadith tatu za Bwana Mtume s.a.w.w. Ya kwanza, iliyopokewa na Bukhari, inasema: "Hakuna yoyote atakayewafanyia vitimbi watu wa Madina ila atayayuka kama inavyoyayuka chumvi katika maji." Ya pili, iliyopokewa na Muslim, inasema: " Haikusudii Madina yoyote kwa uovu ila Mwenyezi Mungu atamyayusha katika moto myayusho wa risasi, au myayusho wa chumvi katika maji." Ya tatu, iliyopokewa na Imam Ahmad bin Hambal, inasema: "Anayewatakia khofu watu wa Madina kwa dhulma, Mwenyezi Mungu naye atamtia khofu na ashukiwe na laana ya Mwenyezi Mungu na malaika na watu wote. Wala Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiyama, hatamkubalia toba wala fidia."

Haya! Kama hayo yaliyofanywa Madina yalifanywa kwa amri ya Yazid, kama asemavyo Ibn Kathir (uk. 220 ) na Sheikh Abdalla S. Farsy (uk. 41), mtu huyo -- kwa Hadith zilizotajwa hapo juu -- bado yu salama? Ni Amiirul-mu'minin gani huyo anayeshukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu, malaika Wake na watu wote?

7. Mwaka mmoja baada ya kuiingilia Madina, aliiingilia Makka (katika mwaka wa 64 BH)! Huko, Sheikh Abdalla S. Farsy anasema (uk.41): "Majeshi ya Yazid yaliuwa watu wengi na kuivunja Al Kaaba."

Hapo pia Sheikh Abdalla "amefinika kombe" ; lakini wenziwe wamelifunua. Kwa mfano, huyo huyo Ibn Kathir ameandika (uk. 225) kuwa majeshi hayo "yaliipiga mawe Al Kaaba kwa teo (manjaniiq) na kuishambulia hata kwa moto mpaka ukuta wake ukaungua"! Na katika uk. 72 wa Juzuu ya Tatu ya Shadharaatudh Dhahab, Ibnul Imaad al Hambalii anasema: "mpaka likaanguka jengo lake"!

Haya! Hiyo ni "Nyumba ya Mwenyezi Mungu" ambayo Qur'ani Tukufu inatwambia (Sura 3:97) kwamba aliyeko nje akakimbilia huko, huwa katika amani; leo Yazid anaiondolea amani hivyo! Na huyo ndiye Amiirul-mu'minin wa mawahabi ambaye wanataka Waislamu wamtambue hivyo! Subhaanallah!

Hayo basi, kwa mukhtasari, ndiyo yaliyofanywa na Yazid. Jee, acha ya Amiirul-mu'minin, Mwislamu wa kawaida tu anaweza kuyafanya kama hayo? Bila shaka hawezi. Ikiwa ni hivyo basi, vipi Yazid aliweza?

Kuijibu suali hiyo, itabidi tujue Yazid alikuwa ni mtu wa aina gani. Hilo inshallah tutalitizama katika karatasi ijayo kwa kunukuu maneno yaliyomo katika vitabu vilivyotungwa na wanazuoni wakubwa wakubwa wa Kisunni (si wa Kishia).

ABDILAHI NASSIR
S.L.P. 84603
MOMBASA
15 Swafar, 1424
18 Aprili, 2003
(Inaendelea)

7) 22 Swafar, 1424 25 Aprili, 2003

Katika karatasi yetu ya sita tulimaliza kuyataja baadhi ya mambo mabaya yaliyofanywa na Yazid baada ya kutawalishwa na babake (Muawiya); mambo ambayo ni muhali mtu kuyafanya na akabakia kuwa Mwislamu, seuze kuwa Amiirul-mu'minin. Leo tutayaangalia yaliyosemwa na wanazuoni mbalimbali wa Kisunni (si wa Kishia) kuhusu mtu huyu.

Tuanze na Sheikh Abdalla Saleh Farsy. Yeye amesema hivi katika uk.40 wa kitabu chake, Maisha ya Sayyidna Huseyn: "Utawala wa Yazid --kama tulivyoona-- ulikuwa wa nguvu tu bila ya ridhaa ya watu". Suali ya kuulliza hapa ni: jee, inawezekana utawala wake ukawa ni "wa nguvu", lakini yeye mwenyewe akawa si wa aina hiyo? Jee, kwa mafunzo ya Kiislamu, Amiirul-mu'minin huruhusiwa kutawala watu kwa "nguvu tu bila ya ridhaa" yao?

Maneno kama hayo takriiban yamesemwa na Sheikh Muhammad Abduh. Chini ya maelezo ya Sura 5:36-37, katika uk 367 wa Juzuu ya Sita ya tafsiri yake ya Qur'ani Tukufu ijulikanayo kwa jina la Tafsiirul Manaar, shekhe huyo amemwita Yazid "kiongozi wa dhulma na ukandamizaji ambaye alitawala mambo ya Waislamu kwa nguvu na makri"! Jee, aliye hivyo huitwa Amiirul-mu'minin ?

Wa tatu ni Allaamah Shawkaani katika kitabu chake cha Hadith za Mtume s.a.w.w. kiitwacho Naylul Awtwaar. Katika uk. 362 wa Juzuu ya Sabaa ya kitabu hicho, amemweleza Yazid kuwa: "mlevi, katembo, mvunjaji utukufu wa sharia takatifu"! Huyo ndiye Amiirul-mu'minin kwa mawahabi wetu?

Wa nne ni Abul Hassan Alii bin Muhammad bin Alii at Twabarii, mwanachuoni mashuhuri wa Kishaafi'i. Alipoulizwa kuhusu Yazid, kati ya ila alizomtia ni: "alikuwa mlevi wa kutopea (kubobea) ambaye mashairi yake ya (kusifu) ulevi yanajulikana". Hayo yamenukuliwa katika uk. 287 wa Juzuu ya Tatu ya Wafayaatul A'yaan ya Ibn Khalikaan.

Wa tano ni Imam Ibn Hazm, katika uk. 98 wa Juzuu ya Kumi na Moja ya kitabu chake kiitwacho Al Muhallaa, amemtia Yazid bin Muawiya katika kundi la wale "waliosimama kwa lengo la kutaka dunia tu", na akasema kuwa msimamo wake huo ulikuwa "ni ukandamizaji mtupu usiokuwa na udhuru (wa kisharia)". Haya! Mtu wa aina hiyo huwa Amiirul-mu'minin?

Wa sita ni Abul Falaah Abdul Hayy Ibnul Imaad, mwanachuoni mkubwa wa Kihambali, katika uk. 69 wa Juzuu ya Tatu ya kitabu chake mashuhuri kiitwacho Shadharaatudh Dhahab. Katika ukurasa huo amemnukuu Imam Dhahabi, mwanachuoni mwengine mkubwa, kuwa amesema kwamba. Yazid "alikuwa naasiby (mtu anayemchukia Imam Alii a.s), fidhuli, jeuri, anakunywa pombe na kufanya munkar. Aliianzisha dola yake kwa kumuuwa Hussein, na akaimaliza kwa tukio la Harra. Watu wakamchukia, wala hakubarikiwa katika umri wake". Tukio la Harra ni lile shambulizi la Madina tulilolitaja katika karatasi yetu Na.6.

Jee, mtu ambaye ameianza dola yake kwa kumuuwa mjukuu wa Bwana Mtume s.a.w.w., na kuimaliza kwa kuushambulia "mji wa Mtume s.a.w.w." (Madina) na kuwaachia mimba za haramu wanawake wasiopungua elfu moja, hufaa kuitwa Amiirul-mu'uminin? Tunawauliza mawahabi wetu: Kwa hujja gani ya Kiislamu?

Wa sabaa ni Ibn Kathir ambaye, kwa kawaida, mawahabi humtegemea mno. Yeye, katika uk. 235 - 236 wa Juzuu ya Nane ya kitabu chake kiitwacho Al Bidaaya Wan Nihaaya, ameyataja "yaliyopokewa" kuhusu Yazid. Kati ya hayo ni "kwamba Yazid alikuwa mashuhuri kwa kupenda muziki na kunywa pombe … kufanya urafiki na watoto wa kiume na wanawake waimbaji … Na hakuna siku ambayo aliamka hakulewa …"!

Na kabla ya hapo, katika uk. 216 wa kitabu hicho hicho na juzuu hiyo tuliyoitaja hapo juu, Ibn Kathir anaeleza ya ujumbe wa "watukufu wa watu wa Madina" uliokwenda kwa Yazid. Anasema: "Waliporejea Madina, walitangaza shutuma zao dhidi ya Yazid na aibu zake. Wakasema, 'Tunatoka kwa mtu asiyekuwa na dini, anayekunywa pombe, ambaye wanawake waimbaji humuimbia na kumpigia muziki…'" Pia ametaja yaliyosemwa na kiongozi wa ujumbe huo, Mundhir bin Zubeir, aliporejea Madina baada ya kupitia Basra kwa swahibu yake, Liwali wa huko (Ubaidillaah bin Ziyaad), kuwa Yazid "anakunywa pombe na kulewa mpaka akaacha swala"!

Haya! Mambo yakifikia hapo, ni Mwislamu wa aina gani atakayejifakhiri kuwa na Amiirul-mu'minin sampuli ya Yazid?

Mawahabi waliotoa karatasi zao na kumwita Yazid Amiirul-mu'minin bakhti yao hawakuwako zama za Ukhalifa wa Umar bin Abdulaziz. Wangekiona cha mtema kuni! Khalifa huyo, aliyekuwa kabila moja na Yazid, alimpiga mtu aliyemwita Yazid hivyo, viboko ishirini! Kama wataka kuyaona hayo, nawatizame uk. 69 wa Juzuu ya Tatu ya Shadharaatudh Dhahab.

Inshallah, katika karatasi yetu ijayo, tutaangalia aliyoyasema Bwana Mtume s.a.w.w. kuhusu mtu huyu aitwaye Yazid kabla ya kunukuu hukumu zilizotolewa na wanazuoni wa Kisunni juu yake.

ABDILAHI NASSIR
S.L.P. 84603
MOMBASA
22 Safar, 1424
25 Aprili, 2003
(Inaendelea)

8) 29 Swafar, 1424 2 Mei, 2003

Baada ya kuona sifa mbaya mbaya za Yazid zilizonukuliwa kwa baadhi ya wanazuoni wakubwa wakubwa wa Kisunni, hebu sasa tutizame alivyosema Mtume Muhammad s.a.w.w. katika Hadith zake, na jinsi wanazuoni wa Hadith wa Kisunni walivyozieleza.

Hadith ambazo nitazitaja humu leo ni zile zilizomo katika Sahih Bukhari peke yake. Kama wengi wetu tunavyojua, kitabu hicho -- kwa masunni na kwa mawahabi pia -- ndicho kitabu kilicho sahihi (kweli) mno baada ya Qur'ani Tukufu. Kwao wao, Hadith iliyotolewa humo huwa haina shaka!

Katika Kitaabul Fitan, mlango wa Qawlin Nabiyyi s.a.w.w. Hilaaku Ummatii Alaa Yaday Ughaylimatin Sufahaa, muna Hadith (kwa Kiingereza, ni Hadith Na. 180 iliyomo uk 147 wa Juzuu ya Tisia) isemayo: "Amr bin Yahya bin Said bin Amr bin Said amesema: 'Babu yangu amenipa habari kwa kusema: Nilikuwa nimekaa na Abuu Hurayra msikitini kwa Mtume s.a.w.w. Madina, tukiwa na Marwaan. Abuu Hurayra akasema, 'Nimemsikia mkweli na mwenye kuswadikiwa na Mwenyezi Mungu (yaani Bwana Mtume s.a.w.w.) akisema: Uangamifu wa umma wangu utakuwa mikononi mwa vijana wa Kikureshi. Marwaan akasema: 'Laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie vijana (hao).' Abuu Hurayra aksema: 'Lau ningelitaka kusema ni Banii fulani na Banii fulani ningelisema.' Nikawa ninatoka na babu yangu kwenda kwa Banii Marwaan pale walipoitawala Sham. Walipokuwa wakiwaona ni vijana wadogo, akitwambia: Huenda wale wakawa ni miongoni mwao. (Nasi) tukimwambia: Wewe unajua zaidi."

Kabla hatujanukuu ilivyoelezwa Hadith hiyo, ningependa wale wajuwao Kiingereza (wasiojua Kiarabu) wajue kwamba Hadith hiyo haikufasiriwa yote kwa ukamilifu katika hiyo nuskha ya Kiingereza. Kipande kikubwa, ambacho tumekichapisha kwa italiki katika tafsiri yetu ya Kiswahili hapo juu, hakikufasiriwa kwa Kiingereza -- sijui ni kwa mfasiri wake kughafilika au ni kwa kujighafilisha!

Hata hivyo, katika kuisherehe (kuifafanua) Hadith hiyo, Imam Ibn Hajar Al Asqalaani, katika uk. 10 wa Juzuu ya Kumi na Tatu ya kitabu chake kiitwacho Fat'hul Baari, ameitaja riwaya ya Ibn Abii Shayba isemayo "kwamba Abuu Hurayra alikuwa akenda sokoni na akisema: 'Ewe Mola! Usinidirikishe na mwaka wa sitini wala utawala wa
vijana.' " Halafu (yeye Ibn Hajar) akasema: "Na katika maneno haya muna ishara kuwa wa kwanza wa vijana hao alikuwa katika mwaka wa 60; na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Maana Yazid bin Muawiya alitawalishwa katika mwaka huo, na akabakia mpaka mwaka wa 64; akafa. Kisha akatawala mtoto wake, Muawiya, aliyekufa baada ya miezi (michache)."

Kwa hivyo, kwa mujibu wa Imam Ibn Hajar, miongoni mwa "vijana wa Kikureshi" ambao Bwana Mtume s.a.w.w. alitabiri kuwa umma wake utaangamia mikononi mwao, na ambao Abuu Hurayra alikiomba Mwenyezi Mungu asimkutanishe nao katika huo mwaka wa 60, ni Yazid. Jee, maneno ya Mtume s.a.w.w. yalianguka? Jee, baada ya mauaji aliyoyaamrisha Karbalaa na Madina na Makka, kama tulivyoona katika karatasi zetu mpaka sasa, umma wa Mtume Muhammad s.a.w.w. haukuangamia? Au hao waliouliwa walikuwa ni makafiri, si Waislamu? Hivyo basi, bado Yazid ni Amiirul-mu'minin?

Wala si kwamba Abuu Hurayra, pale alipotaja "Banii fulani na Banii fulani" katika Hadith tuliyoitaja hapo juu, alikuwa hawajui ni kina nani; la! Alikuwa akijua, lakini akiogopa kuwataja kwa majina. Na hilo liwazi tunapoiangalia tena Sahih Bukhari. Katika Kitaabul Ilm, Mlango wa Hifdhil Ilm muna Hadith (kwa Kiingereza ni Hadith Na. 121 iliyomo uk. 89 wa Juzuu ya Kwanza) isemayo: "Imepokewa kwa Abuu Hurayra akisema, 'Nimehifadhi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w.w. aina mbili za ilimu. Moja ya ilimu hiyo nimeitangaza. Lakini nyengine, lau ningeliitangaza ingelikatwa koo (yangu) hii.' "

Katika kuifafanua Hadith hiyo, katika uk. 216 wa Juzuu ya Kwanza ya Fat'hul Baari, Imam Ibn Hajar amesema: "Wanazuoni wamechukulia kuwa ilimu ambayo (Abuu Hurayra) hakuieneza ni ya zile Hadith ambazo ndani yake mumetajwa majina ya watawala waovu, na hali zao na zama zao. Abuu Hurayra alikuwa akiwataja kikuu tu baadhi yao, wala hakuwa akiwatasua kwa kuiogopea nafsi yake kwao; kama alipokuwa akisema, 'Najilinda kwa Mwenyezi Mungu na mwaka wa 60 na utawala wa vijana'; alikuwa akiashiria Ukhalifa wa Yazid bin Muawiya kwa sababu ulikuwa katika mwaka wa 60 BH."

Wala ufafanuzi huo haukutolewa na Imam Ibn Hajar peke yake. Hata Imam Shihaabuddin Ahmad Al Qastwalaani, katika sherehe yake ya Hadith hizo hizo, ametoa karibu ufafanuzi kama huo. Wale wajuwao Kiarabu, wakitaka kuyaona hayo, nawatizame uk. 374 wa Juzuu ya Kwanza na uk. 11 - 12 wa Juzuu ya Kumi na Tano ya Irshaadus Saari.

Kwa hivyo Abuu Hurayra hakumtaja Yazid kwa jina kwa kujiogopea nafsi yake, asije akakatwa koo; si kwamba alikuwa hajui. Kwa lugha nyengine, alifanya taqiyya!

Lakini kama Abuu Hurayra alifanya taqiyya, jee wenziwe pia walifanya hivyo? Hilo inshallah tutaliona katika karatasi yetu ijayo.

ABDILAHI NASSIR
S.L.P. 84603
MOMBASA
29 Safar, 1424
2 Mei, 2003
(Inaendelea)

9) 7 Rabiul Awal, 1424, 9 Mei, 2003

Katika karatasi yetu ya nane tuliona jinsi Bwana Mtume s.a.w.w. alivyotabiri kuwa umma wake utaangamizwa na "vijana wa Kikureshi", na jinsi Abuu Hurayra -- kwa kuiogopea nafsi yake -- alivyofanya taqiyya ya kutotaja vijana hao walikuwa ni kina nani, japokuwa alikuwa akiwajua! Pia tuliona vile wanazuoni walivyotasua kuwa wa kwanza wa vijana hao alikuwa ni Yazid bin Muawiya. Leo, inshallah, tutayasoma ya maimamu na mashekhe wengine ambao hawakuogopa kumtaja Yazid kwa jina, bali hata kumlaani!

Wa kwanza ni Imam Ahmad bin Hambal. Yeye, kama ilivyonukuliwa katika uk. 440 wa Juzuu ya Nne ya Miizaanul I'tidaal ya Imam Dhahabi, amesema: "Haifai kupokea Hadith kwake (Yazid)." Na huyo Imam Dhahabi, yeye mwenyewe katika ukurasa huo huo, amesema kuwa Yazid "ni mtu ambaye uadilifu wake una walakini. Haifai kupokea Hadith kwake." Haya! Ikiwa mtu mwenyewe haaminiwi kadri hiyo, afaa kuitwa Amiirul - mu'minin?

Wala Imam Hambal hakuzuia tu kupoea Hadith kwa Yazid, bali alimlaani kamwe kwa sababu ya kumuuwa Imam Hussein a.s., kama ilivyoelezwa katika
uk. 63 -- 64 wa Al-It'haaf Bihubbil Ashraaf.

Wa pili ni Sheikh Muhammad Abduh. Yeye, katika tafsiri yake ya Qur'ani Tukufu iitwayo Tafsiirul Manaar (uk. 367 -- 368 wa Juzuu ya Sita), baada ya kueleza jinsi Yazid alivyompinga Imam Hussein a.s., alisema: "Mwenyezi Mungu amshinde, na amshinde kila aliyemtetea miongoni mwa karaamiyya na nawaasib (wanaomchukia Imam Alii a.s.) ambao hawaachi kuendelea kupendelea kuabudu wafalme madhalimu katika kupinga kusimamishwa uadilifu na dini (ya Mwenyezi Mungu)."

Wa tatu ni Imam Shawkaani. Yeye, katika uk. 362 wa Juzuu ya Sabaa ya kitabu chake kiitwacho Naylul Awtwaar, baada ya kuwalaumu wanaomkosoa Imam Hussein a.s. kwa kumpinga Yazid, amemlaani Yazid na babake (Muawiya) kwa kusema "Mwenyezi Mungu awalaani!" Halafu aksema, kuhusu lawama hizo, "Ajabu iliyoje ya Mwenyezi Mungu, ya maneno hayo yanayoikausha damu na ambayo, kwa kuyasikia tu, majabali hupasuka!"

Wa nne ni Imam Taftaazaani, kama alivyonukuliwa katika uk. 12 wa Juzuu ya Kumi na Tano ya Irshaadus Saari, sherehe ya Sahih Bukhari. Imam huyo, baada ya kusema kuwa wanazuoni wameafikiana "kuruhusu kumlaani aliyemuuwa (Imam Hussein a.s.) au aliyeamrisha auwawe, au aliyeruhusu, au aliyeridhia"; na baada ya kueleza kuwa "ni jambo lililoenea kuwa Yazid aliridhia kuuwawa Hussein r.a. na kuitweza Nyumba ya Mtume s.a.w.w.", amesema: "Laana ya Mwenyezi Mungu imshukie yeye na answari wake na wasaidizi wake!"

Wa tano ni mtoto wake mwenyewe Yazid aliyempa jina la babake (Muawiya). Huyu alishika Ukhalifa baada ya babake (Yazid) kufa. Lakini yeye hakuendelea; baada ya siku 40 au, kwa kauli nyengine, baada ya miezi mitano alijiuzulu. Alipojiuzulu alipanda mimbari akatoa khutba. Katika khutba hiyo, miongoni mwa aliyoyasema, alitaja ugomvi uliotokea baina ya babu yake (Muawiya bin Abii Sufyaan) na "aliyekuwa bora kuliko yeye na wasiokuwa yeye (yaani Imam Alii a.s.)." Halafu akamtaja babake (Yazid) na "vitendo vyake viovu", na kwamba "hakuwa na sifa za kuwa Khalifa wa umma wa Muhammad (s.a.w.w.)"; akataja na "dhulma alizowafanyia watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w.w." Mwisho wa khutba yake alilia sana, na akawambia jamaa zake, Banii Umayya, kuwa hataweza kubeba dhambi zao. Kwa hivyo "shauri zenu! Uchukueni Ukhalifa huu mumpe mumtakaye. Mimi simo tena." Hayo yote yameelezwa katika uk. 301 wa Juzuu ya Pili ya Taariikhul Khamiis.

Haya!, Baada ya kuyasoma yote hayo (mbali mengi sana tuliyoyaacha) bado Yazid huyo angali Amiirul mu'minin? Hata baada ya mwanawe mwenyewe kusema kuwa hakuwa na sifa za kuwa hivyo? Nani anayemjua zaidi baba wa mtu? Mwanawe au watu kando? Majibu ninakuachia wewe ndugu msomaji.

Inshallah, katika karatasi yetu ijayo, tutaliangalia la mawahabi kuwazuia masunni wasiigize yafanywayo na mashia -- kama walivyosema katika karatasi yao tunayoijadili.

ABDILAHI NASSIR
S.L.P. 84603
MOMBASA
7 Rabiiul Awwal, 1424
9 Mei, 2003
(Inaendelea)

10) 14 Rabiiul Awwal, 1424, 16 Mei, 2003

Katika makala yao ambayo tumekuwa tukiyajadili katika mfululizo huu, mawahabi waliwalaumu maimamu wa kisunni wa Mombasa kwa kufanya mihadhara yao katika Msikiti wa Konzi katika siku kumi za kwanza za mwezi wa Muharram! Kwa nini? Kwa sababu, kwa mantiki ya kiwahabi, kwa kufanya hivyo maimamu wa kisunni wanawapoteza "wafuasi wa Sunna kwa kuwaiga hao hao MaShia"!

Kabla ya kulijibu neno lao hilo, ningependa wasomaji wetu waelewe mambo mawili muhimu. La kwanza ni kwamba, katika mihadhara yao hiyo, maimamu hao kwa kawaida hawazungumzii yanayozungumzwa na mashia katika majlisi zao za Muharram, bali ni kinyume chake kamwe! Kwa hivyo wanawapoteza vipi masunni, na wanawaiga vipi mashia?

La pili ni kwamba, kwa maneno hayo, masunni wasihadaike wakadhania kwamba mawahabi ni wenzao. Maana, kwa maneno yao na imani yao, masunni wasiozikubali itikadi za kiwahabi, na mashia, ni gora (doti) moja. Wote si waumini bali ni mushrikina ambao "ni halali (kuimwaga) damu yao na (kuwanyang'anya) mali yao hata kama wasema laa ilaaha illallaah, waswali, wafunga na wadai kuwa ni Waislamu"! Kwa lugha nyengine, sote (masunni na mashia), kwa mawahabi, tu makafiri! Hayo siwazulii bali yameelezwa wazi katika uk. 179 wa kitabu cha maisha ya Imam wao kiitwacho Muhammad bin Abdilwahhaab: Muswlihun Madhluum wa Muftaraa Alayh cha Ustadh Mas'ud An-Nadawii.

Sasa tuangalie ya "kuwaiga hao hao MaShia". Ni mwanzo leo mawahabi kufanya hivyo? Jawabu ni: La! Sio mwanzo, japokuwa hawa wetu wa Mombasa wamekuja na kisingizio cha kwamba mihadhara hiyo inayofanywa na maimamu wa kisunni, mbali na kuiga mashia, haikufanywa na Bwana Mtume s.a.w.w. Kwa hivyo, maadamu halikufanywa na Bwana Mtume s.a.w.w., halifai kufanywa!

Unapoyazingatia maneno yao hayo, kwa dhahiri, utadhania kwamba mawahabi wana ghera sana ya kulifuata kila lililofanywa na Bwana Mtume s.a.w.w., na kulipinga kila ambalo hakulifanya. Lakini kwa wale ambao wameusoma Uwahabi na kuujua, wanajua kwamba ukweli si hivyo bali ni kinyume chake! Wao hutumia ghera zao hizo kuficha chuki zao tu walizonazo dhidi ya waumini hata kama waumini hao watayafanya yaliyofanywa na Bwana Mtume s.a.w.w.!

Tuchukue mfano mmoja tu wa yaliyosemwa na Ibn Taymiyya. Huyu ni mwanachuoni wao aliyefariki dunia katika mwaka wa 728 BH, baada ya kuishi miaka 67. Mawazo yake yalimuathiri sana Muhammad bin Abdilwahhab ambaye, kwa kusaidiwa na ufalme na mali ya Mfalme Saud, ameweza zaidi kuyaeneza madhihabi yake kuliko Ibn Taymiyya mwenyewe. Yeye, Ibn Taymiyya, katika zama zake, hakufaulu kufanya hivyo kwa sababu alipingwa vikali na mashekhe wenzake waliofikia hadi hata ya kumkufarisha!

Katika uk. 143 wa Juzuu ya Pili ya kitabu chake kiitwacho Minhaajus Sunnah amesema kuwa inafaa "kuacha baadhi ya mambo ya sunna (mustahabbaat) yawapo ni alama yao (mashia)"! Moja kati ya sunna, ambazo wasio mashia huhimizwa waziache, ni kuvaa pete mkono wa kulia japokuwa hivyo ndivyo alivyokuwa akivaa Bwana Mtume s.a.w.w.! Kwa nini? Kwa sababu sunna hiyo inafuatwa sana na mashia!

Ewe ndugu yangu! Kama mawahabi wawaita ahlul bid'a wale watu wanaofanya ambayo hayakufanywa na Mtume s.a.w.w., sisi tuwaiteje wao wanaozuiya watu kuyafanya yaliyofanywa na Bwana Mtume s.a.w.w. kwa sababu tu yanafanywa na wasiowapenda (yaani mashia)? Baina ya mashia (wanaoifanya sunna ya Bwana Mtume s.a.w.w.) na mawahabi (wanaoizuiya) ni nani ahlus sunnah, na ni nani ahlul bid'a? Uamuzi ninakuachia wewe.

Kwa hivyo mawahabi wanapowazuia maimamu wa masunni wasiwaige mashia, mambo ni hayo. Pengine, hapa, tumalizie mfululizo wa makaratasi yetu haya kwa suali hii: Kama mashia, wanapomaliza haja zao, hujitwahirisha (huchamba) kwa mkono wa kushoto, ndio masunni wachambe kwa mkono wa kulia ili wasiwaige mashia? Jamani! Hawa mawahabi wanahukumu vipi mambo?

ABDILAHI NASSIR
S.L.P. 84603
MOMBASA
14 Rabiul Awwal, 1424
16 Mei, 2003
(Inaendelea)