read

Kitabu hiki kiitwacho Bwana Abu Tallb [a] madhulumu wa historia ni tarjuma ya juzuu ya 7 na 8 ya kitabu mashuhuri kiitwacho AI-Ghadiir cha Allamah al-Amini na ambacho kinazungumzia hali ya maisha ya Bwana Abu Talib [a] ambaye ni baba mzazi wa Amir al-Mu'miniinKitabu hiki kiitwacho Bwana Abu Tallb [a] Imam Ali ibn Abi Talib [a].

Maneno Machache

Bismilahir Rahmanir Rahiim
Alhamdu li waliyyihi was-Salaatu-ala Nabiyyihi wa Aalihil Aimmati wa Awliyail Ummah.

Kitabu hiki kiitwacho Bwana Abu Tallb [a] madhulumu wa historia ni tarjuma ya juzuu ya 7 na 8 ya kitabu mashuhuri kiitwacho AI-Ghadiir cha Allamah al-Amini na ambacho kinazungumzia hali ya maisha ya Bwana Abu Talib [a] ambaye ni baba mzazi wa Amir al-Mu'miniin Imam Ali ibn Abi Talib [a]. Kama vile zilivyofanywa kazi zigine za utafiti basi mtunzi wa kitabu hiki cha Al-Ghadiir ametimiza wajibu wake pia.

Katika lugha nyingi sana kumeandikwa kwa uchache sana kuhusu Bwana Abu Talib [a] na hayo machache yaliyoandikwa kuna mambo mengi mno yenye kutatanisha ndani yake. Mazungumzo makubwa sana katika maisha yake ni kule kuangalia na kutafakari Bwana Abu Talib [a] amefanya mambo gani na ameyafanyaje mambo hayo katika umri wake huo kwa mujibu wa ushahidi wa kihistoria ambayo machache yake yamo katika kitabu hiki-tunaona kuwa Bwana Abu Talib [a] wakati wake mwingi ameutumikia Uislamu na vile vile katika kumhifadhi na kumnusuru Mtume [s].

Katika hali hii yeye ameweza kuvumilia hasira na ukali wa chuki za kabila lake la Maquraish kiasi cha yeye na hao wachache walipokuwa wametolewa nje ya mji wakakaa katika Shayb-i-Abu Talib na wakastahimili matatizo na dhiki zote na wakaweza kufanya subira ya hali ya juu. Kwa hakika ni kwamba wakati huo ndio uliokuwa wa harakati na mikakati mipya ya mapinduzi ya Kiislam ambayo yalikuwa yakitekelezwa na Mtume [s]. Kwa hakika Shayb-i-Abu Talib kisa chake hicho kinaonyesha wazi uhalifu uliokuwa ukifanywa na Maquraish kisiasa kiuchumi na kimaisha na kijamii vilevile cihidi ya Mtume [s] na watu wake.

Katika hali ngumu kabisa kama hizi na zinginezo tulizonazo katika historia Bwana Abu Talib kwa nyakati mbalimbali ameweza kujitolea yeye mwenyewe kumnusuru na kumlinda Mtume [s] na vile vile amewaamrisha wanawe Ali [a] na Jaafer [a] wawe daima wakijitolea kwa ajili ya kumnusuru na kumwokoa Mtume [s]. Kwa mukhtasari kabisa tunaona kuwa maisha yake yote alikuwa ameshajitolea katika kuunusuru na kueneza Uislamu na kumwokoa na kumkinga Mtume [s] kwa sababu tu yeye alikuwa amekwishaongoka na kupata hidaya ya Islam.

Yeye wakati wa mwisho wa pumzi yake alikuwa akiwasisitiza na kuwahimiza watoto na jamaa zake wawe daima mbele katika kumnusuru na kumkinga na kumuunga mkono Mtume Muhammad [s] katika kueneza Uislamu. Na vile vile kwa kifo chake (ambacho kilikuwa baada ya kifo cha Bi Khadijat-il-Kubra) Mtume [s] alikuwa amehuzunika mno kiasi kwamba alikuwa ameutangaza mwaka huo kuwa ni aamul huzun yaani mwaka wa huzuni kubwa.

Kwa kupata mwangaza huo bado tunaona katika vitabu vingine vya kihistoria vya madhehebu mengine yakiwa yanamtaja Bwana Abu Talib kuwa ni mushrik na kuthubutu kumsema kuwa ni kafiri. Kwa hakika tuhuma kama hizi katika historia ni njama kubwa sana zilizofanywa na wamejaaribu hao waliotoa tuhuma hizo kuthibitisha tuhuma zao kwa aya za Qurani tukufu na hadithi za Mtume [s].

Kama tutakavyoweza kuona vyema madhumuni makubwa ya hawa watoao tuhuma kwa kusema Bwana Abu Talib ni mushrik na kafiri huku wakimchukulia yeye kuwa ni mtu mmoja wa kawaida lakini siri ya malengo yao ni kule kuthibitisha kuwa baba yake Imam Ali ibn Abi Talib [a] alikuwa ni mushriki na kafiri ili waweze kumvunja nguvu Imam Ali [a]. Ni dhahiri kuwa ni jambo ambalo tunalielewa kuwa iwapo baba atapata pigo basi shida hiyo kubwa itamfikia na kumwathiri mtoto wake katika maisha na nyadhifa zake. Lakini kama tulivyokwisha kuona kuwa malengo yao sio Bwana Abu Talib mwenyewe bali wao wanataka kumdhoofisha na kumvunja nguvu Imam Ali [a] kuwa baba yake alikuwa hana imani na alikuwa mushriki na kafiri ili kwamba Imam Ali [a] hali na maisha yake yawe na dosari kubwa.

Vyote tulivyokwisha kuvisoma hapo juu, usahihi wake au uwazi wake unakuwa pale wakati tunapoona kuwa historia hii hii na waandishi hawa hawa na wanonakili riwaya hawa hawa ambao wanatoa uamuzi kama huo kuhusu Abu Talib [a] - wanakaa kimya kuhusu wazazi wao waliokuwa wakija daima mbele ya Imam Ali [a] katika maisha yao - wao daima wamekuwa wakiyeyuka mbele ya nuru ya Imam Ali [a] kwa kutoweza kustahimili nuru hiyo.

Tunaona kuwa waandishi hawa hawa na wanaoripoti riwaya hizi ndio wanaoandika fadhila zake lakini tunashangaa kuona pamoja na kuandika sifa na fadhila na daraja zake makabila yao na watu wao wanashindwa kupambanua upotofu huu ulivyo ndipo hapo tunaona kuwa Allamah Amin amefanya utafiti wa hali ya juu usio na kifani na ameweza kuchambua historia kwa undani kabisa pamoja na matukio na riwaya na ametupatia matunda mazuri mno ya kazi yake ambayo imejibu na imeweza kuondoa tuhuma zote dhidi ya Bwana Abu Talib [a] kuwa yeye alikuwa ni mushrik na kafiri. Bwana Amini ameweka uwanja wazi kama tutakavyoweza kushuhudia wenyewe kuwa Bwana Abu Talib kamwe hakuwa mushrik wala kafiri.

Hata hivyo inabidi kitabu kijiarifishe chenyewe hivyo sisi tunayafupisha mazungumzo haya ili msomaji aweze aweze kujibwaga katika uwanja wa utafiti ili kufikia majibu na kuwapima viongozi wanaotoa tuhuma dhidi ya Bwana Abu Talib [a].

Amiraly M.H. Datoo
P.O. Box 838,
BUKOBA - Tanzania (E. Africa)
23 Ramadhan 1417 A.H.
2 Februari 1997

Habari za Mtunzi kwa Mukhtasari:Allama Al-Amini

(Mtunzi wa kitabu cha Al-Ghadiir)

Allamah Sheikh Abdul Hussain (Amini) -- mtoto wa Sheikh Ahmad na mjukuu wa Sheikh Najaf Ali Mulaqqab Amin Shar'a. Jina Ia Amini limetokana na mababu zake. Allamah Amini alizaliwa katika nyumba ya wazee waliobobea katika ilimu na Dini mjini Tabriz (Iran) mnamo mwaka 1320 A.H. Kwa kuwa baba yake alikuwa ni mtu ambaye amesoma sana hivyo maisha yake yakawa katika fani hii ya kujipatia ilimu na maarifa ya Dini na nyanja zinginezo za fani hii. Ilithibitika kuwa Al-Amini alikuwa ni mwenye akili na maarifa ya aina yake - alikuwa na upeo mkubwa wa kuhifadhi ilimu na mwenye nguvu.

Alijipata ilimu ya mwanzo kutoka kwa wazazi wake na baadaye alijiunga katika chuo ambacho hadi leo ni mashuhuri huko mjini Tabriz. Katika chuo hicho alijifunza misingi ya awali ya Fiqh na Usuul kutoka kwa ma-Ulamaa wafuatao: Ayatullah Sayyid Muhammad ibn Abdul Karim Musawi, Araf Maulana Ayatullah Sayyid Murtadha ibn Muhammad Husseini Khusrushahi, Ayatullah Sheikh Hussein ibn Abd Ali Tutunchi na Allamah Sheikh Mirza Ali Asghar Maliki.

Kauli na Mashairi ya Bwana Abu Talib [a]

Bwana Abu Talib [a] zimfikie salaamu za Allah (s.w.t). Ninawadondosheeni majauhari yake kutoka Hadith, historia na Vitabu vya sira.

Bwana Abu Talib [a] alitunga mashairi katika kumsifu mfalme Najjashi wa Ethiopia ambaye katika mashairi yake anamsifu vile mfalme huyo alivyowapokea, kuwakirimu na kuwanusuru Waislamu ambao walikuwa wamesafiri kutoka Makkah kwenda Uhabeshi. Kama vile anavyotuelezea:

(1) Watu wema na wakuu wanaelewa kuwa Muhammad ni waziri wa Musa na Masihi Ibun Maryam.

Ametujia na mwongozo mfano wa ule walio kuja nao hao wawili, kila mmoja aongoza kwa amri ya Mungu na amenifadhika.

Kwa kuwa wao wote wanatuonyesha njia atakavyo Allah (s.w.t). Wao wanafanya uhusiano na watu wote. Na ninyi (Wakristo) mnasoma katika vitabu vyenu kuhusu (Mtume Muhammad [s]) taarifa na sifa zake, hivyo sivyo visa vya uongo, bali ni habari zilizo za kweli.

Ewe Najjashi wewe ni mtu mmoja ambaye wakati baadhi ya watu wa Ummah wa Mtume Muhammad [s], wamerudi wakitoa sifa na kukutaarufisha na wala hawakuwa na mambo mengine isipokuwa ukarimu wako.1

Katika Qasida nyingineyo, Bwana Abu Talib [a] anasema:

"Katika kipindi hiki cha ushindi na kunusuru waambie wa Ghalib, Lui na Tiim kuwa (dhidi ya Muhammad) ni harakati zao zisizo na matunda, sisi Bani Hashim ni panga za Mwenyezi Mungu na sisi ndio wenye Ukuu na fadhila juu ya makabila mengine.

Je hamujui kuwa kuvunja uhusiano - ni dhambi kubwa sana, kuwa ni upumbavu na ujinga mkubwa sana, je nyie hamuelewi kuwa mwanadamu ataweza kufungukiwa na busara alizojaliwa na Mwenyezi Mungu zilizo dhahiri na batini? Musadanganyike kwa kuona kuwa mna neema za kidunia zitadumu mutambue wazi kuwa hivi si vitu vya kudumu milele bali ni vyenye kuangamia.

Isiwe kwamba ndoto hii iwasumbuayo kuwa kumuudhi Mtume Muhammad [s] ukawachukua katika maangamizo na wala isiwe ikawa nyie ndie mukawa ndiyo miguu ya wale Watu wapotofu.

Malengo na matakwa yenu yalikuwa ni kwamba huyu Muhammad [s] mumuue, na kwamba ndoto yenu hii imekuwa ikiwasumbua na isiyofua dafu. Nyie mmezani kuwa sisi Bani Hashim tutakupatieni Muhammad [s] na tutakapokuja mbele yenu hatutaweza na wala hatutaweza kumtetea wala kumhami.

Mtambueni wazi kuwa huyu ni mmoja wa mitume wa Allah (s.w.t.) ambaye anayeteremshiwa Aya zake Allah (s.w.t.) na yeyote yule atakayemjibu hapana basi huyo mtu daima atakuwa katika majuto na atakuwa akijiuma meno yake.

Hebu tazameni mjionee wenyewe, asili na kwa unasaba Hashemi ndiyo wanaomzunguka Muhammad ambao wanawaangaamiza na kuwafukuza wale wote wanaotaka kumdhuru Muhammad.2

Katika sahifah mojawapo ambayo hapo mbeleni Bwana Abu Talib [a] analielezea shairi lake hivi:

"Mimi chochote kile nikisemacho kwa lazima kabila Ia Lui na khususan tawi Ia kabila hili - Bani Kaab!

Je nyinyi hamutambui kuwa sisi tunamtukuza Muhammad kama vile alivyokuwa ametukuzwa Musa kwa sababu tunajua kuwa huyu ni Mtume Atakayeteremshiwa kitabu na Aya takatifu za Mwenyezi Mungu na kwamba mapenzi yake yapo katika mioyo ya watu wote.

Haijuzu kamwe kumfanyia uadui mtu kama huyu ambaye amechaguliwa kuwa rafiki wa Mwenyezi Mungu.

Tahadhari yenu! Tahadhari yenu! Jitahadharini sana musiingie katika makaburi yenu ambamo mutakapoulizwa kuhusu madhambi yenu na mema yenu kwani wakati huo utakuwa ni mgumu mno.

Isitokee kwamba ninyi mukausahaulisha ujamaa, udugu na uhusiano wetu bora uliokuwapo na mukaingia kwa kutumbukia katika mashimo ya wale walioasi na madhalimu.

Basi mimi kwa kula kiapo cha nyumba ya Mwenyezi Mungu ninasema kuwa sisi kamwe hatutamsalimisha Muhammad mbele ya maadui wake hata kama itatubidi sisi tukabiliane na kupambana na vile vile tustahimili magumu na misiba ya kila aina.

Je sisi si watoto wa Hashim ambaye daima alikuwa akitupatia silaha na kututayarisha kwa ajili ya vita na kuwausia watoto wake daima wawe washupavu na hodari?

Na hii ndiyo sababu moja kubwa kabisa kamwe hatujahisi na wala hatuhisi na hatutahisi magumu ya vita na kwa sababu hiyo kubwa sisi kamwe hatutarudi nyuma kutokea uwanja wa vita.

Sisi daima tuko imara na thabiti katika shida na misiba yote na wala kamwe hatupigi makelele badala yake sisi tunakuwa tukijiimarisha na kuwa madhubuti zaidi katika vita vyetu ambavyo hata mahodari katika nyanja hizi nao wanashindwa na kufa nguvu.3

Katika baadhi ya mashairi yake yapo yafuatayo:

Ni jambo la kusikitisha kuwa nyota ya mwisho wa usiku imenitia katika mabano ya huzuni, ingawaje nyota ya matumaini bado haijazama.

Nyota hii ya huzuni imenishtua wakati macho mengi yalikuwa yamefungwa na wale waliokuwa macho wamekuwa mashughuli katika kuhadithiana visa.

Kisa hiki kinaelezea ndoto zile za kuteseka cha wale ambao wanataka kumghilibu Muhammad, ili waweze kumfanyia dhuluma. Lakini mtu ambaye hawezi kujimudu kwa kuzidi kwake basi mtu huyu mwenyewe anatumbukia katika dhuluma mojawapo.

Wao kwa hasira na juhudi zao na kwa matendo yao maovu wameanza kuongozwa na hizi ndoto mbaya zenye kuangamiza na kuleta majuto hapo mbeleni.

Wao wanategemea kuwa sisi tutafanya kazi moja kubwa - yaani tutamsalimisha Muhammad mikononi mwao, ingawaje kazi hii haitawezekana kamwe bila ya kutumika kwa mapanga, mishale na mikuki yaani bila kutokea kwa vita, haiwezekani.

Wao wanadhani kuwa sisi bila ya kutumia mapanga yetu katika vita tutakubali kumsalimisha Mtume Muhammad [s] ili mapanga yao yajae damu huku sisi tukiwia radhi.

Basi wale Bani Fahr wakae kwa tahadhari bado hawajazisikia sauti zao kuuliwa ambayo yatakuwa yamejaa kwa masikitiko na masiba na shida mbali mbali. Fikirieni vyema kabisa kuwa mazungumzo yetu haya ni yenye faida kubwa kwa upande wenu na wala isije ikatokea kuwa nasaha zetu hizi zikipuuzwa zikafungua milango ya vita moja kwa moja.4

Katika shairi mojawapo akiongea na Mtume Muhammad [s], Bwana Abu Talib [a] anasema:

"Kwa kiapo cha Allah (s.w.t)! Kutokana na wingi wa majeshi yenu na nguvu zenu, kamwe kamwe hamutaweza kutughilibu. Hivyo munaweza kuvitumikia tu hadi pale vinapokuwa na roho kabla ya kuuawa.

Kwa hivyo ni nasaha zangu kuwa (Ewe Mtume Muhammad [s]) tangaza Da'awa yako dhahiri kwa sababu humo hakuna jambo la aibu wala upotofu.

Jitihada na Zahma za Bwana Abu Talib [A] kwa Ajili ya Mtume Muhammad [S]

Salaam zimfikie kiongozi wa Makkah Bwana Abu Talib [a] kwa sababu yeye amemsaidia Mtume Muhammad [s] kwa kila hali kwa kumhifadhi na vile vile kwa jitihada zake katika kuinusuru dini ya Islam na kuyaweka maisha na kwa kuwaita na kuwalingania katika dini ya Islam katika hali ya hatari na misukosuko mbalimbali kuanzia pale Mtume Muhammad [s] alipoutangaza utume wake na kwa jitihada zote na harakati zote tunazozijua na zote zile tutakazozisoma humu kitabuni na kusikia kutoka kwa wanazuoni wengine zinatuthibitishia wazi kuwa yeye alikuwa ni Mwislamu halisi na mwenye imani kamili na alikuwa ni mtu ambaye anayo imani kamili juu ya Mtume Muhammad [s] ndivyo yanavyodhihirisha matendo na jitihada zake.

Kwa imani yake hii kwa Allah (s.w.t.) na utiifu wake kwa Mtume Muhammad [s] Inshaalah itakuwa dhahiri na bayana siku ya Qiyamah, hata hivyo sisi hapa tunajaribu kwa mukhtasari na uwezo wetu mdogo kuwaleteeni machache kuhusu vile alivyokuwa ameisimamia dini ya Islam kwa ushupavu na umadhubuti na jitihada zake zote katika kuinusuru na kuieneleza dini ya Islam kwa hali na mali.

Safari ya Sham

lbn Is-haq anasema: Bwana Abu Talib [a] alikuwa akienda pamoja na msafara wa wafanya biashara kuelekea Sham (Syria). Wafanya biashara hao walijitayarisha wakiwa na shehena yao ya lazima na walijiandaa kuondoka na mara akatokea Mtume Muhammad [s] na akashika hatamu (kamba) ya ngamia na akasema:
"Ewe Baba yangu! Je mimi unaniacha mikononi mwa nani, ukiondoka? Wakati unatambua kuwa mimi sina baba ambaye atanisaidia na wala sina mama atakayenipa mapenzi yake?"

Kwa kusikia haya Bwana Abu Talib [a] alipitiwa na hali tofauti, na baada ya kujimudu akasema: "Kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu! Mimi nitamchukua huyu pia kwa sababu siwezi kamwe kutengana naye na wala yeye kamwe hawezi kutengana nami! Hivyo Mtume Muhammad [s] akaweza kwenda pamoja na msafara wa Bwana Abu Talib [a] kuelekea Sham.

Pole pole msafara huo ulielekea na kufika katika mji wa Basra ambao ulikuwa chini ya himaya ya Sham. Njiani humo msafara ukipitia katika kanisa moja ambamo kulikuwa na Padri mmoja akiitwa Buhaira ambaye alikuwa mwenye ilimu sana na alikuwa akiwahudumia wasafiri wa Kikristo huko. Naye alikuwa akiwapatia Wakristo ilimu ya dini yao kutoka katika kitabu alichokuwa amekipata katika urithi wake.

Ingawaje misafara mingi kama hiyo ilikuwa imekwishampitia huyo Buhaira, yeye kamwe hakuizingatia misafara hiyo wala hakuwa akizungumza nao hadi ulipofika mwaka huo wakati msafara huo kutoka Makkah ulipofika hapo karibu naye. Msafara huo ulipokaribia na Kanisa hilo, waliweza kufunga mahema yao na kufanya kituo hicho chao cha mapumziko. Kwa sababu hii imetokana na yeye kuona kutokea katika kanisa lake nuru iliyokuwa ikiteremka kutoka mbinguni ikiwa katika sura ya wingu ambalo lilikuwa likienda pamoja na msafara huo kwa sababu alikuwamo mtu katika msafara huo akikingwa na miale ya jua hata pale msafara huo ulipokuwa umepumzika chini ya mti. Na aliweza kuona vile vile matawi ya mti huo yakiinama kutoa heshima. Na mtu huyo alikuwa ndiye Mtume Muhammad [s].

Buhaira aliyaona hayo yote na kutoka nje ya kanisa na kuwaamrisha watu wake waanze kufanya matayarisho kwa ajili ya kuwakirimu wasafiri hao na wakati vyakula vilipokuwa tayari aliwatumia ujumbe ufuatao:

"Enyi kundi la Maqureishi! Mimi nimewatayarishieni vyakula na ninataka ninyi nyote wakubwa kwa wadogo, watumwa na wote walio huru - mje katika karamu yangu hii."

Mtu mmoja kutoka msafara huo akaenda kumwuliza Buhaira ni hoja gani iliyomfanya yeye kuwakirimu leo kwani daima wamekuwa wakipita hapo bila hata ya kuwajali!

Buhaira alijibu: "Ndiyo! leo nimeona dalili tofauti kabisa na kwa sababu hiyo mimi niwe mkirimu wenu usiku huu mtakapokuwa katika kituo chenu hicho. Mimi nimewatayarishieni vyakula ili mje mle na kupumzika vyema katika kituo hiki karibu yetu."

Hivyo watu wote waliokuwa katika msafara huo walikwenda kwake isipokuwa Mtume Muhammad [s] kwa sababu ya udogo wa umri wake, walimwacha kituoni humo akiwa pamoja na mizigo ya wasafiri. Buhaira alipowatupia macho yake hakuona ishara yoyote ile makhususi na hivyo aliwauliza iwapo kuna mtu yeyote kati yao ambaye hajafika hapo.

Wao walimjibu: "Wale wote waliokuwa, wakistahiki kuja wamefika hapa isipokuwa yupo kijana mmoja ambaye ana umri mdogo.. tumemwacha kituoni pamoja na mizigo yetu."

Buhaira akawaambia: "Haiwezekani kumwacha mtu yeyote ila aje ashiriki pamoja nasi katika karamu hii."

Mmoja miongoni mwa Maqureishi akasema: "Kwa kiapo cha Lat na Uzza!5 Leo lazima kunajambo la ajabu!"

Je sasa hi kweli itawezekana kwetu sisi kumtenga Mtume Muhammad [s] kwa kutoshiriki katika karamu hii na mara akainuka na kaenda kwa Mtume Muhammed [s] akambeba na kumleta miongoni mwao ili ashiriki katika karamu hiyo. Buhaira alipomtupia tu jicho kijana huyo alishangaa kwa sababu ubashiri na dalili zote alizokuwa akizijua za kuja kwa Mtume aliziona katika kijana huyo (Mtume Muhammad [s]) na hivyo alikuwa akijaribu kuzipeleleza na kujaribu kuthibitisha kwa kila ubashiri na dalili alizokuwa akizijua. Wakati huu wasafiri wote walikuwa wamekwisha kula na kurejea katika kituo chao kwa mapumziko. Buheira aliinuka na kumwendea Mtume Muhammad [s] na akamwambia:

"Ewe mwana! Kwa kiapo cha Lat na Uzza' kuwa kile nitakachokuuliza utanijibu kwa usahihi". Mtume Muhammad [s] alimwambia: "Kamwe usiniulize kwa viapo vya Lat na Uzza'.

Buhaira akasema: "Vyema basi ninakupa viapo vya Mwenyezi Mungu."

Hapo ndipo Mtume Muhammad [s] alisema: "Tafadhali uliza kile utakacho."

Hapo Buhaira alianza kumwuliza mambo mengi ambayo alikuwa ameyasikia na kuyajua kuhusu mambo yatakayotokea hapo siku za usoni. Ndipo Mtume Muhammad [s] alipoendelea na hoja zake alizoziuliza. Majibu ya Mtume Muhammad [s] yalikuwa kwa mujibu wa dalili alizokuwa akizijua Buhaira kuhusu Mtume atakayekuja. Baadaye Buhaira alilitazama bega la Mtume Muhammad [s] kama vile alivyokuwa akijua yeye na akauona muhuri wa Utume.

Kwa tukio hili Bwana Abu Talib [a] amelizungumzia hivi katika mashairi yake.

Kwa hakika mwana wa Amina, Mtume Muhammad [s] katika macho yangu anao daraja kubwa sana hata kuliko watoto wangu! Na wakati ngamia wangu walipokuwa wakiondoka kwa safari yeye aliwashika hatamu na hapo uadilifu wangu ukajaa vile alivyokuwa yeye mwenye kuwasaidia na kuwanusuru wengi mno na mimi nilipomwita aje miongoni mwa watu atembee na azunguke wakati msafara wa kwenda mbali ulipokuwa tayari kwenda mbali. Hapo mji wake ameuacha mbali mno kiasi kwamba wakajikuta wamefika Basra. Huko yeye akakutana na Padri Buhaira aliyekuwa akimsubiri kwa hamu ya muda mrefu.

Yeye alimwelezea kuhusu Mtume Muhammad [s] dalili za kweli na aliomba wale wote wenye husuda wasimkaribie kamwe.

Wakati kikundi kimoja cha Mayahudi walipoona kuwa Mtume Muhammad [s] alipokuwa akienda kulikuwa na wingu likimfuata juu yake basi wakakutana na kuafikiana kuwa wamuuwe Mtuume Muhammad [s]. Lakini Buhaira alijitolea kifua wazi na aliweza kuwazuia Mayahudi hao wasiweze kumuuwa Mtume Muhammad [s].

Na kwa ajili ya suala hili Bwana Abu Talib [a] amesema mashairi yafuatayo:

Je mimi nilipokuwa nimenuia moyoni mwangu kuhusu safari yangu ya kuelekea Sham, je wewe hukuiona hali yangu ilivyokuwa?

Kwa hakika safari hii ilikuwa ya lazima kutengana, utengano ambao wazazi wanavyouhisi ulivyo mgumu utengano huo ulikuwa na Mtume Muhammad [s] wakati ambao mimi nilikuwa nimejitayarisha kwenda Sham. Lakini nilijikaza na kuondoka na kumtakia kila la kheri hadi nitakaporejea na yeye kwa huzuni na hofu alikuwa akilia na ngamia walikuwa baina yetu wawili.

Na Mtume Muhammad [s] ndiye aliyekuwa ameshika kamba ya ngamia.

Mimi nilimkumbuka sana baba yake na niliangua kilio kwani daima nilikuwa nikimlilia.

Bwana Abu Talib [a] aliendelea kuelezea kuwa mimi nilimruhusu Mtume Muhammad [s] aje pamoja nasi katika msafara huu."

Bwana Abu Talib [a] anaongezea katika mashairi yake hivi.

Sisi tulipewa makaribisho mazuri sana na huduma nzuri kabisa hapo Basra na tulijiwa na Buhaira ambaye alitupatia kila aina ya huduma na alituambia kuwa tuwalete watu wetu wote katika karamu aliyokuwa ametuandalia bila ya kukosa hata mmoja wetu.

Sisi tulimwambia kuwa sisi sote watu wazima tulikuwa tumefika isipokuwa kijana mmoja mdogo ndiye tuliyekuwa tumemwacha hapo nyuma ambaye ni yatima pia. Lakini Buhaira alimwita kijana huyo mdogo.

Alituambia kuwa kulikuwapo na vyakula vingi mno hivyo haikuwapasa kumwacha nyuma kijana huyo na kama wasingemleta huyo kijana mbele yake kushiriki katika karamu hiyo hasi asingewaheshimu kamwe. Na Buhaira alipomwona Mtume Muhammad [s] akija kuelekea nyumba yake huku akiwa amefuatwa na wingu juu yake, hapo ndipo Buhaira alipojitupa chini huku akisujudu na kwa mapenzi mno alimkumbatia Mtume Muhammad [s]6

Bwana Abu Talib [A] Aomba Mvua kwa Wasila wa Mtume [S]

Jalhama ibn Urfatah anasema: Wakati mmoja mimi nilifika Makkah ambapo wakazi wake walikuwa katika mpito wa kipindi shadidi cha ukame na njaa kali.

Maquraish wakasema: "Ewe Abu Talib chemchemi zote zimekauka na wakazi wote wa mji wameathirika mno kwa ukame pamoja na njaa hii kali. Hivyo twendeni sote tukusanyike ili tuombe kwa Mwenyezi Mungu atuondolee balaa hii kubwa iliyotukumba.

Hapo tukamwoona Bwana Abu Talib [a] anatoka nje huku akiwa amemshika mkono kijana mmoj, mtoto huyo ni Mtume Muhammad [s] aliyeonekana akiwa kama jua ilivyo nyuma ya wingu jeusi. Pamoja na Mtume Muhammad [s] kulikuwapo na watoto wengi. Bwana Abu Talib [a] alimwinua Mtume Muhammad [s] juu na kumwegemesha juu ya kuta za Al-Kaaba na wakati bado huyo kijana akiwa yungali katika mikono ya Bwana Abu Talib [a], aliomba dua ya kupata mvua.

Ingawaje wakati huo kulikuwa hakuna mawingu ya mvua hapo angani ikaonekana kuwa mawingu yameanza kukusanyika kutoka sehemu mbalimbali na muda si mrefu mvua ilianza kunyesha mito, mabwawa, mashamba na makonde yote yalijaa maji kwa kiasi kilichohitajika na hivyo maisha neema yakarudia kama kawaida. Kwa tukio hili Bwana Abu Talib[a] aliyasema mashairi yafuatayo:

Mtume Muhammad [s] ni mtukufu kiasi kwamba mawingu yanapoona uso wake yanajawa kwa maji ya kunyesha mvua yeye huyu, yatima atawanusuru mayatima na atakuwa mlezi wa wajane na wanaukoo wa Hashim ambao wanakuwa na misiba na shida basi watakuwa wakisaidiwa na wakifarijiwa na huyu. Nao wataishi maisha ya neema. Huyu Mtume Muhammad [s] ni mizini ya uadilifu kwamba hatadhulumiwa mtu yeyote hata kwa kiasi cha punje ndogo

Huyu atakuwa na ilimu na maarifa kiasi kwamba watu hawatakuwa na uwezo wa kupima ilimu na fahamu zake.7

Mambo haya yanadhihiri wazi kabisa kuwa Bwana Abu Talib [a] alikuwa akielewa vyema kabisa wadhifa na daraja Mtume Muhammad [s] na utume wake na alikuwa na imani kamili juu ya maswala haya. Tumeona tukio moja muhimu kabisa kuwa huko Makkah kulikuwa na ukame na njaa ya hatari kabisa kwa hivyo kulipopita kipindi cha miaka miwili mfululizo bila ya kunyesha mvua basi Bwana Abdul Muttalib alimwamrisha mtoto wake Bwana Abu Talib [a] kuwa amchukue Mtume Muhammad [s] na kumviringisha katika nguo kwani wakati huo Mtume Muhammad [s] alikuwa yungali mtoto mchanga kabisa na baadaye Bwana Abdul Muttalib alielekea al-Kaaba tukufu na alimwinua juu Mtume Muhammad [s] huku akisema:

"Ewe Mwenyezi Mungu! Kwa ajili ya mtoto huyu aliye mkononi mwangu (na alirejea senteso hii kwa mara tatu na akaendelea kusema) "Ewe mwenyezi Mungu! Kwa ajili ya mtoto huyu tunaomba utunyeshee mvua moja kwa moja. Na kulikuwa hakujapita muda watu wakaanza kuona mawingu ya kunyesha mvua ambayo ilinyesha kwa wingi kiasi kwamba watu walianza kuingiwa na hofu ya kuporomoka kwa Masjid al-Haram kwa mafuriko.8

Wakati huo Bwana Abu Talib [a] alisoma Qasida hii.

Mtume Muhammad [s] ni mtukufu kiasi kwamba mawingu yanapoona uso wake yanajawa kwa maji ya kunyesha mvua yeye huyu, yatima atawanusuru mayatima na atakuwa mlezi wa wajane.

Hivyo Bwana Abdul Muttalib kwa kuomba dua ya mvua kumwomba Mwenyezi Mungu kwa wasila wa Mtume Muhammad [s] na vile vile Bwana Abu Talib [a] naye pia kuomba mvua kwa wasila wa Mtume Muhammad [s] wakati mtume akiwa bado kijana. Hivyo matukio haya mawili yanatuthibitishia kuwa wazee hawa wawili walikuwa wakijua utukufu na kuwa Mtume Muhammad [s] ataleta dini ya haki yenye kuwaita watu katika kumuabudu mmoja tu hivyo wao walikuwa na imani kamili juu ya Mtume Muhammad [s].

Hivyo matukio haya mawili ya kihistoria yanaonyesha waziwazi vile yakithibitsha imani zao kamili juu ya Tawhidi na Utume. Hivyo vinatutosheleza sisi matukio haya mawili kuona na kuamini, wazee hawa wawili Bwana Abdul Muttalib na Bwana Abu Talib [a] walivyokuwa na imani kamili juu ya Tawhid, Utume, na Mtume Muhammad [s].

Bwana Abu Talib [A] na Uzawa wa Imam Ali [A]

Jaabir ibn Abdullah anasema:
Mimi nilimwuliza Mtume Muhammad [s] kuhusu kuzaliwa kwa Imam Ali [a] na Mtume Muhammad [s] aliniambia: "Bila shaka, ewe Jaabir! umeniuliza kuhusu yule anayezaliwa ambaye ni mtu bora kabisa ambaye ni sawa na Masihi ibn Maryam. Allah (s.w.t.) ameniumba mimi na Ali [a] kwa nuru moja i.e. mimi kwa nuru ya Ali na Ali kwa nuru yangu. Na sote tulikuwa pamoja hadi ukafika wakati mimi nikapitia tumbo Ia mama yangu Amina na Ali [a] akapitia katika tumbo la mama yake Fatema binti Asad ndio kuzaliwa kwake.

Katika zama zile kulikuwa na Mubiram bin Daayab bin Ishkebani ambaye alikuwa ni mcha mungu mmoja ambaye kwa muda wa miaka mia mbili na sabini alikuwa akifanya ibada ya Mwenyezi Mungu tu bila hata ya siku moja kumwomba mola wake ombi lolote. Ikatokea kwamba Allah (s.w.t) akamtuma Bwana Abu Talib [a] aende kwa huyo mcha mungu. Mcha mungu huyo alipomwona Bwana Abu Talib [a] amemjia basi akainuka kutoka nafasini mwake na akaubusu uso wake na kumkalisha karibu nae.

Hapo ndipo alipomwuliza Bwana Abu Talib [a] kuwa yeye ni nani?" Bwana Abu Talib [a] akajibu: "Mimi ninao uhusiano na Tahama". Mcha mungu huyo alimwuliza "Tahama anatokana na kabila gani?" Bwana Abu Talib [a] akamjibu: "Mimi ninatokana na ukoo wa Bani Hashim." Kwa kuyasikia hayo, mchamungu huyo aliinuka kutoka nafasini mwake na kwa mora nyingine tena aliubusu uso wake na akasema: "Ewe Bwana! Mwenyezi Mungu amenibashiria habari Fulani." Hapo Bwana Abu Talib [a] kwa shauku ya kutaka kujua akamwambia "Je ubashiri huo ni upi, naomba uniambie." Mchamungu huyo alianza kumwambia: "Katika kizazi chako atazaliwa mtoto mmoja ambaye atakuwa ndiye walii wa Mwenyezi Mungu

Wakati ulipofika usiku wa kuzaliwa kwa Imam Ali [a] usiku huo ulikuwa wa kung'ara mno, basi Bwana Abu Talib [a] alionekana akitoka nje huku akisema kwa furaha mno kuwa amezaliwa walii wa Mwenyezi Mungu katika al-Kaaba tukufu. Usiku huo ukapita na siku ya pili ikafuata mnamo wakati wa mchana Bwana Abu Talib [a] alingia katika al-Kaaba tukufu huku akiyasema mashairi yafuatayo:

"Ewe Mola kiangamize kiza hiki, Ewe Mola wa kuleta nuru ya mwezi tunaomba utudhihirishie amri yako iwe dhahiri kwetu.

Tunaomba ubashiri wako katika kumpatia jina huyu mtoto.

Baada ya hapo Mtume Muhammad [s] akasema: "Wakati huo nikasikia sauti moja kutoka mbinguni ikisema:

"Enyi watu wa ukoo wa Mtume Muhammad [s] mpenzi mmebahatiwa kumpata mtoto mpenzi na mtoharifu, jina lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni Ali ambalo limetokana na jina lake Mwenyezi Mungu la A'ala.9

Bwana Abu Talib [A] na Habari za Utume

Hambali faqihi, Ibrahim bin Ali bin Muhammad bin Danwiri anaandika kisa kimoja kirefu sana katika kitabu chake Nihayaat-ul-Talib kwa kumnakili Taus bin Abbas, kuwa:

Mtume Muhammad [s] alimwambia Bwana Abbas (r.a.) (i.e. ndugu wa baba yake) kuwa:

"Mwenyezi Mungu amenibashiria Utume, Unabii pamoja na risala Tukufu na ameniamrisha nitangaze wazi wazi mahubiri na Da'awa, Naomba kujua rai yako?"

Bwana Abbas (r.a.) akasema: "Ewe kipenzi cha ndugu yangu! Wewe unaelewa waziwazi kuwa Maquraish wanahusuda mno na ukoo wako. Kwa hakika kila usemacho kwa hakika kama itatokea kuwa hivyo hivyo basi kunaweza kutokea machafuko makubwa kabisa ya kuangamizana. Wao watatulenga sote kwa pamoja katika kutuangamiza na watatung'oa kutoka mizizi yetu na kututupilia mbali. Wewe tuache katika hali hii tulivyo na hivyo uache harakati zako hizo. Hata hivyo ni ushauri wangu kuwa umwendee baba yako mkubwa, Bwana Abu Talib [a] kwa sababu yeye ndiye kaka yetu mkubwa kuliko sisi sote. Usikie na ushauri wake unasemaje. Yeye atakusudia na vile vile hatakuacha peke yako wala hatakusalimisha kwa maadui zako.

Baada ya hapo Mtume Muhammad [s] pamoja na baba yake mdogo Bwana Abbas (r.a.) walikwenda kwa Bwana Abu Talib [a] na Bwana Abu Talib [a] alipowaona hao wawili wakija, akawaambia "Kwa hakika leo kunajambo muhimu sana, je ni swala gani lililowaleteni kwangu mimi wakati huu?" Bwana Abbas (r.a) akamwambia Bwana Abu Talib [a] mazungumzo yote yaliyotokea baina yake na Mtume Muhammad [s] na kwa kuyasikia hayo Bwana Abu Talib [a] alimtazama Mtume Muhammad [s] na akasema:

"Ewe mtoto wa ndugu yangu! Inuka na tangaza kile ulichoamrishwa na Mwenyezi Mungu bila ya woga au kusita kwa sababu wewe ni mtu mwema na hodari na wewe unatokana na nyumba moja tukufu na madhubuti kabisa na ya viongozi. Nakula kiapo cha Mwenyezi Mungu, hakuna hata ulimi mmoja ambao utakaokuletea shida wewe ila utakabiliwa kwa ulimi mkali na wenye kuzikata hizo zote na mapanga makali yatavurumishwa.

Kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu! Makabila ya Waarabu watakuwa watiifu kwako kama vile wanyama watoto wanapokuwa watiifu na wanyenyekevu kwa wale wawanyweshao maziwa. Uhakika huu ni kwamba mtukufu baba yangu Bwana Abdul Muttalib alikuwa daima akikisoma kitabu na kuniambia: "Bila shaka atatokezea Mtume katika kizazi changu. Ni matumaini yangu kuwa niwe hai katika zama za Mtume huyo na niletee imani dini yake huo ni usia wangu kwa watoto wangu wote wale watakaokuwa hai katika zama hizo za mtume huyo waikubalie dini yake.10

Allamah Amini anasema:

Ndugu wasomaji ninyi mmejionea kwa roho tulivu vile Bwana Abu Talib [a] anamnakili baba yake Abdul Muttalib. Yeye anampa nguvu na hima na moyo Mtume Muhammad [s] autangaze utume wake na kufanya Da'awa na alitukuze jina Ia Mwenyezi Mungu na kulifikisha kwa watu wote. Yeye vile vile anakubali na kuamini uhakika huu uliodhahiri kuwa Mtume Muhammad [s] ndiye mtume aliyebashiriwa katika vitabu vya mitume iliyotangulia na kwamba Waarabu watajisalimisha mbele ya utume wake na kuleta imani juu ya dini yake.

Ndugu msomaji, jee kweli unaweza kuamini na hata kuthubutu kusema kuwa Bwana Abu Talib [a] akiwa anayajua yote hayo kuhusu mtume na utume wake na vile ilivyokuwa imebashiriwa katika vitabu vitukufu vya mitume iliyomtangulia bado akawa mushrik na kafiri? Yeye awaambie watu wote waje kumsikia Mtume Muhammad [s] juu ya Da'awa ya dini ya Kiislamu wakati huo huo yeye akajiepusha na maneno ya Mtume Muhammad [s] akabakia kafiri?

Kwa hakika kufuatana na mambo yalivyo bayana mtu yeyote atakayethubutu kusema kuwa Bwana Abu Talib [a] alikuwa ni mushriki au kafiri basi mtu kama huyo ni mnafiki na muongo na tumwelewe waziwazi kuwa mtu huyo anazo tuhuma na mawazo ya kishetani ambayo hayatamfikisha popote ila katika shimo la upotofu na maangamizo.

Hizo ndiyo njama za Mawahabi kutaka kumdhalilisha Bwana Abu Talib [a] kwa sababu ni baba yake Imam Ali [a].

Kupotea Kwa Mtume Muhammad[s]

Maquraish wote walikusanyika katika ijitimai, mkutano mkubwa huko nyumbani kwa Bwana Abu Talib [a] kuhusu da'awa ya Mtume Muhammad [s]. Wao wote kwa pamoja walianza kudhihirisha chuki, hasira na vitisho vya dhidi ya Mtume Muhammad [s]. Waliinuka kwa hasira na ghadhabu na walijawa na mawazo ya kulipiza kisasi; "Sasa sisi sote kwa pamoja tuinuke kutoka hapa na tuondoke zetu na tuendelee kuabudu miungu yetu kama vile tulivyokuwa tukiabudu hapo awali. Bila shaka katika tablighi hii kuna maslahi yao." 11

 • 1. Mustadrak Hakim, J. 2, uk. 623 kwa kutokea Ibn Is-haq
 • 2. Ibn Abi Hadid, Juz. 3, Uk. 313
 • 3. Sirah Ibn Hisham, J. 1, UK. 373; Sharh Nahjul Balagha Ibn Abi al-Hadid, J. 3, uk. 313; Bulugh-al-Arab, J. 1, uk. 325; Khazana-al-adab li-Baghdadi, J. 1, uk. 261; Rawdh-al Anaf, J. 1, uk. 220; Tarikh lbn Kathiir, J. 3, uk. 87; Isni al-Matalib, uk. 6-13; Talabat al-Talib, uk. 10
 • 4. Sharh Najul Balagha, lbn Abi Al-Hadid, J. 3, uk. 3312.
 • 5. Lat na Uzza' ni majina ya miungu iliyokuwa ikiabudiwa kabla ya kuja kwa Uslamu.
 • 6. Diwan Abu Talib [a], J. 4, uk. 33-35; Tarikh Ibn Asakir, J. 1, uk. 269-272; Riwdha-al-Anaf, J.1, uk. 120.
 • 7. Qastalani, Sharh Bukhari, j. 2, uk. 327; Mawahib li-diniyya, j. 1, uk. 48; Khasais al-Kubra, j. 1, uk. 86-124; Sharh Bihujjatil mahafil, j.1, uk. 119; Siira Halabiyyah, j. 1, uk. 125; Wahlan, Surat an- Nabawiyyah, j. 1, uk. 87; Talabat al-Talib, uk. 42; Taarikh ibn Asakir.
 • 8. Shahristani, Milal wa Nihal, maelezo sura ya 3, uk. 225
 • 9. Kanji Sahafi, Kifayat al-Talib, uk. 260
 • 10. Sayyid bin Tausi: taraif, uk. 85; Abul Hasan Shariff: Dhiya al-Aalamiin
 • 11. Al-Qur'an, Sura Saad Aya 6