read

Hadithi fupi ya Amru bin Jumuuh na vita ya Uhud.

Dua Iliyokubaliwa

Mtungaji : Ustadh Shahid Murtadha Mutahhari

Mtarjumi : S. Muhammad Ridha Shushtary

Mchoraji : Sadiq Sanduqi

Mchapishaji
Islamic Thought Foundation
No. 5 Takhti Sq., Shahid Beheshti Ave.
P O Box 14155-3899
Tehran, Islamic Republic of Iran

Kimetolewa wavuni na timu ya
Ahlul Bayt Digital Islamic Library Project

_____________________________________________________________________

"Ewe Mola! Usinirejeshe nyumbani kwangu!"

Haya ni maneno aliyoyasikia Hind, mke wa Amru bin Jumuuh, kutoka kwa mume wake alipokuwa akiondoka nyumbani baada ya kujiandaa kwa silaha kwenda kushiriki katika vita vya Uhud. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Amru bin Jumuuh kushiriki katika jihadi pamoja na Waislamu wengine. Hajawahi kabla yake kupigana vita kwa sababu alikuwa na kilema cha mguu ambao ulikuwa ukichechemea sana. Kufuatana na hukumu wazi wazi ya Qur'ani Tukufu, jihadi si wajibu kwa kipofu, kiwete na mgonjwa. Ingawa yeye mwenyewe hajawahi kushiriki katika jihadi, lakini alikuwa na wanawe wanne kama simba ambao daima walikuwa pamoja na Mtume Muhammad (SAW) katika medani za vita.

Hakuna mtu aliyefikiria kwamba Amru, juu ya kuwa na udhuru wake na baada ya kuwapeleka wanawe wanne katika jihadi, angetaka yeye mwenyewe awe miongoni mwa askari wa Kiislamu.

Jamaa zake waliposikia juu ya uamuzi wake, wakamwendea kutaka kumshawishi abadilishe uamuzi wake.
"Kwanza kabisa, kwa mujibu wa sheria, wewe umesamehewa usipigane jihadi. Pili, una watoto wanne mashujaa ambao wamekwenda pamoja na Mtume Mtukufu vitani. Kwa hivyo, hakuna haja yo yote ya kujiunga katika jeshi."

Amru akasema: "Kwa hoja hiyo hiyo kwamba wanangu wanatamani kupata ufanisi wa kudumu na Pepo ya milele, nami vivyo hivyo natamani. Ajabu! Wao wende kupata mafanikio ya kuuawa shahidi na mimi nikae nyumbani pamoja nanyi!? La! Hayumkiniki kabisa!"

Jamaa zake Amru hawakumwacha kumshawishi, bali daima kila mmoja wao alikuwa akienda kwake kutaka kuubadilisha uamuzi wake.

Mwishowe, Amru kwa kutaka kuwanyamazisha jamaa zake, akamwendea Mtume Mtukufu na kumwambia: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Jamaa zangu wanataka kunifunga nyumbani ili nisiweze kushiriki katika vita vya kupigana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba nina tamaa ya kuingia Peponi kwa mguu huu huu uliolemaa."

Mtume Mtukufu akasema: "Ewe Amru! Wewe una udhuru wa kisheria. Mwenyezi Mungu amekusamehe, na jihadi si wajibu kwako."

Amru akasema: "Mimi naelewa hilo, lakini nina tamaa ya kupata huo ufanisi mkubwa licha ya jihadi kutokuwa wajibu kwangu."

Mtume Mtukufu akawambia jamaa zake: "Msimzuie. Mwache aende vitani. Ilivyokuwa ana tamaa ya kufa shahidi, huenda Mwenyezi Mungu atambariki."

Mandhari ya hamasa kubwa kabisa katika vita vya Uhud ilikuwa ni mapigano ya Amru bin Jumuuh, ambaye licha ya kuwa na mguu uliolemaa, alikuwa akihujumu katikati ya jeshi la adui huku akipiga kelele: "Natamani Pepo."

Mwanawe mmoja alikuwa nyuma yake. Watu wawili hao walipigana kwa ushujaa mkubwa mpaka wote wakauwa shahidi.

Baada ya kumalizika vita, mabibi wengi wa Madina wakatoka nje ya mji kutaka kujua matokeo ya vita, hasa baada ya kufika habari za kutisha mjini Madina. Miongoni mwa mabibi hao alikuwepo Aisha, mke wa Mtume Mtukufu.

Baada ya kutoka nje ya mji kidogo, Aisha alimwona Hind (mke wa Amru bin Jumuuh) alivuta hatamu ya ngamia aliyekuwa amebeba maiti watatu juu ya mgongo wake huku akielekea Madina.

Aisha akamwuliza: "Kuna habari gani?"

Hind akajibu: 'Alhamdulillah! Mtume yu salama. Madamu yeye yu salama, sisi hatuna majonzi yo yote. Habari nyingine ni kwamba Mwenyezi Mungu amewaangamiza makafiri hali wakiwa wamejawa na hasira."

Aisha akamwuliza: "Ni nani maiti hawa?"

Hind akajibu: "Maiti hawa ni kakangu, mwanangu na mume wangu."

Aisha akamwuliza: "Unawachukuwa wapi?"

Hind akajibu: "Ninawachukua Madina kuwazika."

Baada ya kusema hayo, Hind akavuta hatamu ya ngamia kuelekea Madina, lakini ngamia alifanya matata kwenda na mwisho akakaa chini.

Aisha akasema: "Mzigo wa ngamia ni mzito, hawezi kuubeba."

Hind akasema: "Si hivyo. Ngamia wetu ana nguvu sana. Kwa kawaida hubeba sawa na mizigo ya ngamia wawili. Ni lazima kuna sababu nyingine." Baada ya kusema hayo, akavuta tena hatamu upande wa Madina, lakini ngamia akagoma tena. Alipomgeuza upande wa Uhud, ngamia akaanza kwenda kwa haraka.

Hind akaona ni mambo ya ajabu. Mnyama hakuwa tayari kwenda upande wa Madina lakini alikazana alipoelekezwa upande wa Uhud. Akawaza moyoni: "Labda kuna siri katika jambo hili."

Hind akavuta hatamu ya ngamia aliyebeba maiti na akarejea moja kwa moja kwa Mtume Mtukufu katika Uhud.

Akamwambia: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Kuna kisa cha ajabu hapa. Nimembebesha ngamia huyu maiti hawa ili niwachukue Madina kuwazika. Nilipovuta hatamu kuelekea Madina, ngamia amekataa kutii, lakini nilipomwelekeza Uhud, akaanza kwenda kwa haraka. Kwa nini?"

Mtume Mtukufu akasema: "Je, mume wako alisema kitu alipokuwa akija Uhud?"

Hind akasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Alipoondoka nyumbani, nilimsikia akisema: "Ewe Mola! Usinirejeshe nyumbani kwangu!"

Mtume Mtukufu akasema: "Basi hii ndiyo sababu yenyewe. Dua ya dhati ya shahidi huyu imekubaliwa. Mwenyezi Mungu hataki maiti huyu arejeshwe Madina. Miongoni mwenu Waansari (wasaidizi wa Mtume) kuna wale ambao wakiomba cho chote kwa Mwenyezi Mungu na wakaapa, Mwenyezi Mungu huzikubalia dua zao. Mume wako Amru bin Jumuuh ni miongoni mwao."

Kwa shauri la Mtume Mtukufu, maiti watatu hao wakazikwa hapo hapo Uhud. Kisha Mtume Mtukufu akamwambia Hind: "Watu watatu hawa watakuwa pamoja Peponi."

Hind alisisimishwa sana na tukio hilo, na akamwambia Mtume Mtukufu huku akitetemeka: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Niombee Mwenyezi Mungu nami pia niwe pamoja nao."