read


Hotuba ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) Kuhusu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Hotuba Ya Mtume Mtukufu (S.A.W.W.) Kuhusu Mwezi Mtukufu Wa Ramadhani

Makala haya yametarjumiwa na: Amiraly M. H. Datoo.

Amenakili Sheikh As-Sadduq r.a. kutoka kwa Al Imam 'Ali ar-Ridha a.s. kutokea kwa Al Imam Musa al-Kadhim a.s. kutokea kwa Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kutokea kwa Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. kutokea Al Imam Zaynul 'Aabediin a.s. kutokea kwa Al Imam Hussein ibn ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kutokea Imam Amir Al-Muuminiin Al Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kutokea kwa Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w.:

Ya ayyuha-Naas (Enyi watu)! Kwa hakika Mwezi wa Allah swt umewafikieni pamoja na baraka, rehema na misamaha yake, kwani ni mwezi ulio bora kwa Allah swt, usiku na mchana wake ni bora kuliko usiku na mchana wowote mwingine, saa zake ndizo bora kabisa kuliko saa zote na ni mwezi ambamo Allah swt anakualikeni na kuwafanyeni katika watu waliokarimiwa, pumzi zenu katika Mwezi huu ni Tasbihi, na usingizi wenu humo ni ‘ibada, na amali zenu humo zinakubaliwa na Dua’a zenu humo zinajibiwa na hivyo mumwombe Allah swt kwa nia safi na iliyo kweli na moyo msafi ili awajaalieni tawfiqi ya kufunga saumu na usomaji wa Qur’ani Tukufu katika mwezi huu mtukufu. Kwa hakika yeyote atakayekosa msamehe wa Allah swt katika mwezi huu ulio Adhimu basi atakuwa ni mtu asiyebahatika.

Mkumbukeni njaa na kiu cha Siku ya Qiyamah mkiwa katika hali ya njaa na kiu katika mwezi huu mtukufu, na vile vile, mutoe sadaqa zenu kwa ajili ya mafukara na masikini miongoni mwenu, muwaheshimu walio wakubwa wenu, na kuwahurumia walio wadogo miongoni mwenu na muwajaze kwa huruma zenu.

Mzihifadhi ndimi zenu na muyaweke macho yenu chini kwa yale yote yasiyoruhusiwa kutazamwa na wala msiyasikie yale yote yasiyoruhusiwa kusikilizwa, muwawie vyema mayatima ili wanapokuwa watoto wenu mayatima, nao pia watendewe mema na mumwombe Allah swt msamaha wa madhambi yenu, na mnyoosheeni Allah swt mikono yenu kwake kwa ajili ya Dua’a katika nyakati za Sala kwani ndiyo iliyo saa bora kabisa ambamo Allah swt huwatazama wanaomwabudu kwa Rehema na hujibu anapoombwa na huitikia anapoitwa.

Ya ayyuha-Naas (Enyi watu)! Kwa hakika nafsi zenu zinategemea amali zenu na muzikomboe kwa istighfar zenu, migongo yenu imelemewa kwa uzito wa madhambi yenu na hivyo mupunguze uzito wenu kwa kurefusha sujuda zenu na mujue kuwa Allah swt ametamka kwa kula kiapo cha Ukuu Wake kwa kutowaadhibu wanaosali na wanaosujudu na kutowatishia moto Siku ya Qiyamah, ambamo watu watakuwa wamesimama mbele ya Mola wao.

Ya ayyuha-Naas (Enyi watu)! Miongoni mwenu atakayemfuturisha aliyefunga saumu katika funga za Mwezi huu Mtukufu basi ni sawa na kupata thawabu za kumpatia uhuru mtumwa mmoja na kupatiwa msamaha wa madhambi yaliyopita.”

Masahaba walisema: “Ewe Mtume Mtukufu s.a.w.w.! Si wote tulio na uwezo huo.” Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alijibu: “Jiepusheni na moto wa Jahannam hata kwa kulisha kipande cha tende au hata kwa kunywisha maji. Kwa hakika Allah swt hupendezewa na hulipa mema kwa atendaye hivyo hata kama hatakuwa na zaidi. ”

Ya ayyuha-Naas (Enyi watu)! Yeyote atakayezirekebisha tabia zake basi Allah swt atamfanyia wepesi upitishio wake siku ya Qiyamah juu ya Siraat ambapo miguu ya wengineo ikitetemeka, na yeyote yule atakayewafanyisha kazi kidogo wamfanyakazi wake siku hizi za funga, basi Allah swt pia atamfanyia wepesi hisabu yake Siku ya Qiyamah, na yeyote yule atakayeziepusha shari zake kwa watu, basi Allah swt atamwepusha na ghadhabu Zake, na yeyote atakayewakirimu mayatima basi Allah swt atamkirimu Siku ya Qiyamah na yeyote atakayewatendea mema ndugu na jamaa zake basi Allah swt atamjaalia Rehema Zake Siku ya Qiyamah.

Na yeyote atakayevunja uhusiano wake pamoja na jamaa na ndugu zake, basi Allah swt pia atauvunja uhusiano wake pamoja mtu huyo. Na atakayesali Sala za Sunnah katika mwezi huu Mtukufu, basi Allah swt atamwepusha na moto wa Jahannam na yeyote yule atakayetimiza Sala zake zilizo Wajib basi atalipwa usawa wa Sala sabini kuliko miezi mingine, na huyo atakuwa na uzito wa mizani kuliko watu wengine watakao kuwa na uzito hafifu wa mizani katika Siku hiyo, na yeyote yule atakayesoma hata Ayah moja ya Qur’ani Tukufu katika Mwezi huu Mtukufu, basi atapata thawabu za kuhitimu Qur’ani kamili, zaidi kuliko miezi mingine.

Ya ayyuha-Naas (Enyi watu)! Kwa hakika milango ya Jannat (Peponi) ipo wazi katika mwezi huu Mtukufu, hivyo mwombeni Allah swt kuwa milango hiyo isifungwe kwa ajili yenu, na vile vile milango ya Jahannam (Motoni) ipo imefungwa katika mwezi huu Mtukufu, hivyo mwombeni Allah swt kuwa milango hiyo isifunguliwe kwa ajili yenu. Na Mashetani wamefungwa kwa minyororo katika mwezi huu Mtukufu, na hivyo mumwombe Allah swt kuwa hao Mashetani wasiwasaliti ………!”

Ndugu msomaji, unaombwa kuwasomea Surah al-Fatihah na Sura al-Ikhlaas (Qul-Huwallahu Ahad …) mara tatu kwa ajili ya thawabu za marehemu wote