read

Hivi Kweli Mashia Wanaweza Kuwa Na Qur’an Yao?

Bismihi Ta ‘Ala

Kuna baadhi ya watu hudai na kujaribu kuonyesha kuwa Mashia wanayo Qur’an yao tofauti na hii ambayo sote tumeizoea.

Watu wa aina hiyo, ilikuwa ni jambo la busara kwao kuangalia baadhi ya aya ambazo Mwenyeezi Mungu anasema kuwa hakuna binadamu awezaye kuleta mfano wa Qur’an mfano (2:23-24) na nyinginezo (10:38, 11:13, 17:88):

وَإِنْ كُنْتُمْ فِي رَيْبٍ مِمَّا نَزَّلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِنْ مِثْلِهِ وَادْعُوا شُهَدَاءَكُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {23}

فَإِنْ لَمْ تَفْعَلُوا وَلَنْ تَفْعَلُوا فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ۖ أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ {24}

“Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia mja wetu basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli.” 2:23

“Na mkitofanya na wala hamtofanya kamwebasi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe walio andaliwa hao wanao kanusha” 2:24

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ ۖ قُلْ فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِثْلِهِ وَادْعُوا مَنِ اسْتَطَعْتُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {38}

“Je! Ndiyo wanasema ameizua? Sema: Hebu leteni sura moja mfano wake na muwaite (kukusaidieni) muwawezao, isipo kuwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnasema kweli.” 10:38

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ ۖ قُلْ فَأْتُوا بِعَشْرِ سُوَرٍ مِثْلِهِ مُفْتَرَيَاتٍ وَادْعُوا مَنِ اسْتَطَعْتُمْ مِنْ دُونِ اللَّهِ إِنْ كُنْتُمْ صَادِقِينَ {13}

“Au wanasema: Ameizua? Sema: Basi leteni sura kumi zilizo zuliwa mfano wa hii, na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli” 11:13

قُلْ لَئِنِ اجْتَمَعَتِ الْإِنْسُ وَالْجِنُّ عَلَىٰ أَنْ يَأْتُوا بِمِثْلِ هَٰذَا الْقُرْآنِ لَا يَأْتُونَ بِمِثْلِهِ وَلَوْ كَانَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ ظَهِيرًا {88}

“Sema: Wangeli kusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur’ani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao.”17:88

Kwa kuwa Allah kasema kuwa hakuna binadamu awezaye kuleta mfano wa Quran; na Mashia ni wanadamu (kama wengine), kwa hiyo hawana uwezo wa kuzua Qur’an nyingine; na kwa maana hiyo hawana Qur’an nyingine zaidi ya hii iliyopo inayofahamika na kila Muislamu.

Na ikiwa italazimishwa kuwa Ipo , italazimika kukubali kuwa Allah ni muongo (Mwenyezi Mungu apishe mbali hilo, kwani ametakasika na kila aibu,) kwa kusema binadamu hawezi kuleta mfano wa Qur’an ilhali binaadamu (Mashia) wameileta. Na Allah ametakasika na kusema uongo; bali ni nani awezaye kuwa mkweli zaidi kuliko yeye?

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَنُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۖ وَعْدَ اللَّهِ حَقًّا ۚ وَمَنْ أَصْدَقُ مِنَ اللَّهِ قِيلًا {122}

“Na wale walio amini na wakatenda mema, tutawaingiza katika Bustani zipitayo mito kati yake. Watadumu humo milele. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo kweli. Na nani mkweli zaidi kwa usemi kuliko Mwenyezi Mungu. 4:122

Zaidi ya hapo mashia wenyewe wanaitakidi ( wanaamini kuwa hii Qur’an ( tuijuwayo wote) ndio (Qur’an) aliyokuja nayo Mtume Muhammad (s.a.w.), haikuzidi wala kupungua. Kwani Mwenyezi Mungu mwenyewe kaahidi kuihifadhi na ziada, upungufu na mabadiliko.

Na ikiwa hilo pia litapingwa kwa kudai kuwa wao wanafanya Taqiyyah ( yaani kuficha unachokiamini na kusema usichokiamini kwa kuhofia madhara yawezayo kukupata) ambayo wasio mashia huichukulia kama ni unafiki; basi ifahamike kuwa Taqiyyah, inaweza kuficha imani na wala haiwezi kuficha kitabu kilichopo tokea wakati huo ( wa mwanzo wa Ushia) hadi sasa bila kuweza yeyote miongoni mwa wasio mashia kukiona kitabu hicho.

Na, ikiwa, hata tukijaalia kuwa kipo na chaweza kupatikana na kuonekana na kila mtu, pia kitabu hicho hakiwezi kuwa ni Qur’an au mfano wake kwani Mwenyeezi Mungu ambaye ni mkweli kisha sema kuwa hakuna uwezekano wa kupatikana Qur’an nyingine ( ya pili).

Na kwa sababu hiyo, mashia hawatakuwa na chochote cha kutuhumiwa kuhusu kumiliki Qur’an yao.

Na ikiwa itasemwa kuwa Qur’an hiyo waliyonayo si kama hii ya Waislamu, bali ni Qur’an yao ya kikafiri (kama wanavyodai baadhi ya watu kuwa mashia ni makafiri), basi kitabu hicho hakitafaa kuitwa ni Qur’an kwani Qur’an ni kwa ajili ya ( na ni kitabu cha) Waislamu pekee.

Kwa hiyo, kwa hoja hiyo mashia watakuwa hawana Qur’an nyingine.

Na fikra ya kuwachukulia mashia kuwa ni makafiri inashangaza sana na inapingana na hali halisi na ukweli wa mambo ulivyo duniani (kuwahusu mashia), kwani kigezo tosha cha kuthibitisha kuwa wao si makafiri ni kule kuruhusiwa kwao kwenda kuhiji sehemu ya watu ambao ndio wanadai ukafiri wao.

Je kafiri anaruhusiwa kuingia kuhiji Makka na kuzuru ( Madinah)? Ikiwa haruhusiwi, mbona mashia wanaruhusiwa?

Na kwa kuwa wanaruhusiwa, basi huo ni uthibitisho kuwa wao si makafiri.

Kwa kifupi; mashia hawana Qur’an yao, kwani hawana uwezo wa kuileta Qur’an ambayo ingekuwa ya kwao. Kwa hiyo tuhuma hizo hazina maana wala msingi. Na lengo lake ni kujaribu kuvunja umoja wa waislamu ili wadhoofike na wapate kushindwa na adui yao kafri ambaye ndiye aliye nyuma ya propaganda hizo.

Was-salaam
Ndugu yenu Jamali A. Kasole.