read

Maadili Ya Tabasamu (Imamu Musa Al-Kadhim, a.s.)

********
Kitabu hiki kinaeleza maisha ya Imam Musa Al-Kadhim, ambaye ni mmoja wa  Maimamu watokanao na Nyumba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na namna alivyotimiza jukumu lake ya kuongoza jamii.

***********

Shukrani

Kitabu hiki kiliandikwa kwa lugha ya Urdu na Mtukufu Saiyadul Ulama Maulana Sayyid Ali Naqi Saheb, Mujtahid wa Chuo Kikuu cha Lucknow, Uhindi.

Kimetafisirwa kwa lugha ya Kiingereza na Sayyid Hashim Raza Rizvi, B.A., B.T., Yadgar-e-Husaini, H.S. School; Allahabad, Uhindi, na kutolewa na Imamia Mission, Lucknow, U.P., Uhindi.

Kimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahiii kutoka hiyo tafsiri ya Kiingereza na Marehemu Bwana L.W. Hamisi Kitumboy (aliyekuwa Muballighi - Mkaguzi, wetu) na kikachekiwa na kusahihishwa na Mwalimu Dhikiri (Zakir Ali) U.M. Kiondo, Edita wa "Sauti ya Bilal".

Utangulizi

Ulimwengu unaugua kwa ajili ya mashirika ya vitisho. Ili kujiambatanisha na misingi ya ukweli na kuzitii kanuni za akili katika hail zo zote zile ziwazo, huonekana kuwa ni nguvu inayopita uwezo wa mwanadamu. Kujifunza maisha ya wale viongozi wa wanaadamu kama walivyowajibikiwa kukabiliana na upinzani mkali sana wa nguvu ya mabaya, katika njia yao ya kutimiza jukumu na imani yao, hakika kutakuwa na faida sana kwetu. Maimamu watokanao na Nyumba ya Mtukufu Mtume [s] walitupa mifano hiyo na maisha ya lmamu Musa Kadhim [a] ni mfano mmojawapo.

Jina Na Nasaba Yake

Jina lake lilikuwa Musa bin Jaafar. "Kun'yat" (jina la watoto ni Abul Hasan, jina lake la heshima ni Al-Kadhim. Hivyo jina lake kamili ni imamu Musa Al-Kadhim. Baba yake ni Imamu Jaafar As-Sadiq aliyetokana na Mtukufu Mtume [s] kupina kwa lmamu Husayn [a]. Mama yake alikuwa Bibi Hamidah Khatun kutoka Berber (nchini Somalia).

Kuzaliwa Kwake

Imamu Musa Kadhim [a] alizaliwa mnamo tarehe 7 Safar (Mfunguo Tano) mnamo mwaka 128 Hijiriya. Wakati huo baba yake, Imamu Jaafar As-Sadiq [a] alikuwa akiutumia barabara wasaa waliopewa na watawala wa wakati huo kwa kuutangaza Uislamu wa Kweli na kwa kuizimishia kiu ya wale waliokuwa wakiitafuta elimu ya kidini. Ingawa Imamu Jaafar As-Sadiq [a] alikuwa tayari keshapata watoto wawili wakati huo, kuzaliwa kwa mtoto huyu (Imamu Musa [a]) kuliipa jamii hiyo furaha kuu kwa kuwa mtoto huyu aliandikiwa kuwa na saba katika nyororo ya warithi wa Mtukufu Mtume [s].

Kulelewa Kwake Na Maisha Yake Ya Awali

Imamu [a] alipitisha miaka ishirini ya maisha yake chini ya malezi ya baba yake. Zawadi ya nguvu ya kiroho itokayo kwa Mwenyezi Mungu na mazingira aliyokuwemo baba yake (aliyekuwa na kazi kubwa ya kuyatangazia mafundisho ya Mtukufu Mtume [s] hata wafuasi wao wakaitwa kwa jina lake la "Millat Jaafariyah" vilimpa mjukuu huyu mdogo wa Mtukufu Mtume [s] sura ya kuvutia mbele ya watu wote kiasi ambacho licha tu ya kuchaguliwa kwake kuwa Imamu baada ya baba yake, alijulikana pia kwa matendo yake mema ya kibinafsi.

Uimamu Wake

Mnamo mwaka wa 148 Hijiriya Imamu Jaafar As -Sadiq [a] alifariki na Imamu Musa Kadhim [a] akawa mlinzi wa Dhamana Takatiafu ya Ukhalifa. Wakati huo milki ya Bani Abbas ilikuwa ikitawaliwa na mfalme Mansur Dawaniqi, mtawala katili sana na aliyehusika sana na mauwaji ya wana wengi wa Mtukufu Mtume [s] na ambaye wakati huo, tayari mara nyingi keshafanya hila za kutaka kumuuwa lmamu Jaafar As-Sadiq [a] na mwishowe akamtilia sumu na akafa. Hivyo Imamu Ja'afar As-Sadiq [a] alitegemea kuwa watawala wa wakati ule hawatamruhusu mwanawe aishi kwa amani. Hivyo aliunda kamati ya watu watano kulinda mali yake baada ya kufa kwake. Wa kwanza wao alikuwa ni mfalme Mansur mwenyewe, wengine ni Mabwana Muhammad bin Sulaiman, gavana wa Madina, Abdallah Aftah kaka yake Imamu Musa AI-Kadhim [a], yeye Imamu Musa Kadhim [a] mwenyewe na mama yake Bibi Hamidah Khatun.

Mfalme Mansur aliposikia habari za kifo cha Imamu Jaafar As-Sadiq [a], alisema mara tatu "Inna LiIlah" (maneno anayoyasema Mwislamu asikiapo hadari za kifo cha mtu) na kisha akasema, "Sasa ni nani aliyebaki ili kulijaza pengo lililoachwa na Jaafar?" Kisha alimwandikia barua gavana wa Madina aone kama Imamu Jaafar As-Sadiq [a], alimteua mtu ye yote yule kuwa mlinzi wa usia wake baada yake Gavana alijibu kuwa yeye mfalme, mwenyewe alikuwa mmoja wa wanakamati watano. Habari hizi zilimnyamazisha Mansur na akazama kufikiria na alipoibuka akasema, "Basi watu hawa hawawezi kuon­dolewa". Baada ya hapo Mansur aliishi miaka kumi lakini hakuweka kizuizi cho chote kwa lmamu katika kuutangaza Uislamu wa kweli. Mfalme Mansur alikuwa akijishughulisha na usimamizi wa ujenzi wa mji wa Baghdad na alimaliza kazi hiyo mnamo mwaka 157 Hijiriya, mwaka mmoja tu kabla ya kifo chake.

Siku Ya Shida

Mfalme Mansur alifariki mnamo mwaka 158 Hijiriya na mwanawe Mahdi akatawala badala yake. Hapo mwanzoni yeye naye alitulia na hakufanya jambo lo lote lile lenye kuvunja hadhi ya Imamu [a]. Lakini mara moja “silica” za ukoo wa Bani Abbas za kuwasumbua watoto wa Mtukufu Mtume [s] zilipanda na mnamo mwaka 164 Hijiriya alipokuja Hijaz ili kuhiji, alimchukuwa Imamu [a] na kwenda naye Baghdad na kumfunga. Imamu [a] aliwekwa jela kwa muda wa mwaka mmoja na baada ya hapo alifunguliwa na kuruhusiwa arudi Madina. Alipofariki mfalme Mahdi, nduguye Hadi alitawala mnamo mwaka 169 Hijiriya na akatawala kwa muda wa miezi kumi na mitatu. Baada ya hapo ulifuatia utawala wa Harun AI-Rashid uliokuwa muda ambao Imamu [a] hakuweza kuishi kwa amani.

Tabia Yake

Yeye alikuwa mmoja wa watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume [s] na alikuwa na sifa zile zile za maadili na maisha matakatifu vitu vilivyokuwa vikizitofautisha roho hizi takatifu na watu wengine. Ni kweli kuwa baadhi yao wanaonekana kuwa walikuwa wakijulikana kwa sifa fulani fulani. Inaonyesha kuwa sifa aliyojulikana nayo sana lmamu Musa Kadhim [a] ni uvumilivu na usamehevu mwingi sana kiasi ambacho aliitwa "Al-Kadhim” (Mwenye kuvunja ghadhabu). Hajapata kuonekana akimkasirikia mtu ye yote yule. Kila mara alikuwa akitabasamu hata alipokuwa katika hali ngumu sana. Mmoja wa magavana wa Madina ilimsumbua sana kiasi cha kumtukana Imamu [a] lakini aliwaambia watu wake wasimrudishie jibu Ia matusi hayo. Wakati matusi hayo yalipokithiri sana kiasi cha kutoweza kuvumilika na kila mara wale wanafunzi wake walikuwa wakilalamika kwa Imamu [a] kuhusu matusi hayo, aliwaambia kuwa yeye mwenyewe atalishughulikia jambo hilo. Baada ya wafuasi wake kuzituliza hasira zao, lmamu [a] alikwenda nyumbani kwa gavana huyo kwa adabu nzuri sana kiasi ambacho gavana huyo alisikitika kwa yale yote aliyoyatenda hapo nyuma na akaomba msamaha kwa lmamu [a]. Kisha Imamu [a] alirudi kwa watu wake na akawauliza njia nzuri ya kulikabili tatizo hilo; kama ni ile aliyoitumia yeye au ile waliyotaka kuitumia. Mara moja wote walikubali kuwa ile njia aliyoitumia Imamu [a] ilikuwa nzuri zaidi. Hivyo aliuthibitisha ukweli wa hadithi ya mhenga wake, Hadhrat Ali bin Abi Talib [a] isemayo "Mshinde adui wako kwa kumtendea mema", hadi leo bado inapatikana katika kitabu cha hotuba na hadithi zake kiitwacho "Nahj-ul-Balaghah" hakika matendo ya namna hii huwafanya maadui wayakubali. Ndio maana Hadhrat Ali bin Abi Talib [a] ameongezea kutoa ushauri wake akisema, "Lakini katu usiitumie njia hii isio ya kijeuri unapojibizana na mtu asiye na uwezo wa kuikubali; kwa maana ufanyapo hivyo utauzidisha ujeuri wake."

Kwa hakika uwezo wa ndani wa kuweza kujua wakati wa kutumia njia isiyo ya kijeuri ni nadra kabisa; kama ulivyokuwa uwezo wa kipekee wa Maimamu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume [s].

Kila kulipotokea kutokuwa na tabia kama hizi kwa upande wa maadui, ambazo kufuatana na ubora wa Maimamu zingelihitaji kupingwa, kila mara alipendelea kuwatendea mema. Kwa hakika jambo hili halikuweza hata kidogo kuwafanya wazue hila ya kuigeukia tabia yao ya kawaida ya kijeuri. Kama vile Hadhrat Ali bin Abi Talib [a] alivyomtendea mema Abd-ur-Rahman ibn Muljim ambaye baadaye atakuwa muuwaji wake, Imamu Musa Kadhim [a] alimfanyia mema Muhammad bin Ismail ambaye baadaye alikuwa zana ya kifo cha Imamu [a]. Hata alipokuwa akisafiri kwenda Baghdad kulalamika mbele ya baraza la mfalme dhidi ya Imamu [a], Imamu [a] mwenye alimpa fedha.

Muda aliokuwa Imamu [a] akiishi ulikuwa mbaya sana kwa kuutangazia Uisiamu wa Kweli. Hakuweza kuwasiliana na wapenzi wa elimu na hakuweza kufanya kazi kama alivyofanya Imamu Jaafar As Sadiq [a]. Aliishi maisha ya kujitenga na ni tabia zake nzuri tuzilizoweza kuwaongoza wanaadamu kwenye mafundisho ya Mtukufu Mtume [s] na Dhuria wake [a].

Alikuwa akikaa kimya katika vikao vyake na marafiki zake na a hakuzungumza ila mtu anapozungumza naye. Vivyo marafiki na maadui wote kwa pamoja waliukubali ubroa wa kichwa na moyo wake. Na kuhusu ibada yake kwa Mwenyezi Mungu, na sala zake za usiku, alijulikana kuwa yu "Abd Salih" (Mja Msalihina).

Ukarimu na upole wake pia vilifahamiwa sana. Alikuwa na kawaida ya kuwasaidia maskini wa mjini Madina kwa siri.

Kila asubuhi baada ya sala na ibada zote alimsujudia Mwenyezi Mungu na hakuinua kichwa chake hadi adhuhuri. Alikuwa akisoma Qur'ani Tukufu kwa sauti ya kuvutia sana. Alikuwa akilia alipokuwa akisoma Qur'ani na wasikilizaji nao pia walilia.

Utawala Wa Harun Al-Rashid

Mnamo mwaka 170 Hijiriya Harun Al-Rashid alitawazwa baada ya Mfalme Hadi. Harun alikuwa na mifano yote ya wafalme wa Bani Abbas machoni pake. Baba yake Mansur alikuwa adui mkubwa wa Imamu Jaafar As-Sadiq [a] na Hadi aliona kuwa ilikuwa kwa ajili ya akili yake ya kibusara aliyoijenga Imamu Jaafar As-Sadiq [a] na ni kujiam­batanisha na misingi ya akili hiyo, kulikomzuia asimuuwe mrithi wa Imamu Jaafar As-Sadiq [a]. (Hakika ule ujenzi wa mji wa Baghdad pia ulikuwa sababu ya kutofanya hivyo).

Sasa hakuna cho chote cha kumzuia Harun asiitimize azma hiyo. Sasa baba yake keshakufa. Wazo la kwanza kumjia lilikuwa kujiondolea fikara iliyodumu sana akilini mwa watu wa ukoo wa Bani Abbas ya kuwa Senta ya Madina iliwapa urahisi watu wabaya kufanya matendo yao maovu. Lakini matatizo ya ndani ya serikali na kule kukaa kimya na maisha ya kujitenga ya Imamu [a] vilimzuia Harun kuchukua hatua ya kidhahiri dhidi ya senta ya Madina.

Wakati huo huo masaibu ya Bwana Yahya bin Abdallah bin Hasan yalitukia ba Bwana alifungwa kikatili na kisha aliuawa bila ya aibu yo yote baada ya kuahidiwa usalama wa maisha yake. Ingawa Imamu [a] hakuhusika na matendo ya Yahya asijiingize katika mambo ya watawala, uadui uliokuwepo tangu zamani kwa watu wa Myumba ya Mtukufu Mtume [s] katika nyoyo za watu wa ukoo wa Bani Abbas ulipanda kwa sababu tu ya matendo ya Yahyo na Imamu [a] alitulia tu kutokana na matokeo ya mienendo ya Bani Abbas. Yahya bin Khalid Barmaki, waziri mkuu alizua shitaka dhidi ya Bwana Jaafar, mwalimu wa mwana mkubwa wa mfalme Harun aitwaye Amin kuwa bwana huyo alikuwa mfuasi wa Imamu [a]. Shitaka hili lilihusika na Bwana Jaafar kidhahiri lakini vile vile lilihusika na mambo ya Imamu [a] mwenyewe kisirisiri.

Mara moja Harun alidhamiria kumsumbua Imamu [a]. Harun aliwahi kwenda Maka kuhiji na Imamu [a] alikwenda huko kwa kusudio hilo hilo katika mwaka huo huo. Harun alijionea mwenyewe heshima aliyokuwanayo lmamu [a] mbele ya Waislamu na uadui wake kwa watu wa Nyumba ya Mtume [s] wa tangu wahenga wake ulimpanda hadi moyoni mwake na ulitiwa nguvu na upinzani wa Muhammad bin Ismaili.

Bwana Ismaili alikwua mwana mkubwa wa Imamu Jaafar As-Sadiq [a] na hivyo watu walifikiria kuwa ndiye atakayekuwa mrithi (atakayekuwa Imamu wa saba), lakini Bwana Ismaili alifariki wakati wa uhai wa Imamu Jaafar As-Sadiq [a] na wazo hili lilithibitishwa kwamba si Ia kweli, lakini vivyo baadhi ya watu walifikiria kuwa haki ya kumrithia Imamu Jaafar Sadiq [a] ni lazima ibakie katika kizazi cha Ismaili. Hawakuukubali Uimamu wa Imamu Musa Kadhim [a] na hadi leo iko madhehebu ya Isma'iliyah yenye imani hii.

Hivyo Bwana Muhammad mwana wa Bwana Ismaili alikuwa na sababu ya kuwa na fikara tofauti na zile za Imamu [a]. Lakini kwa vile wafuasi wake walikuwa wachache mno na hawakuwa watu mashuhuri walijiambatanisha na Imamu [a] na hawakutoa upinzani wa kiwaziwazi.

Harun, akiifikiria hali hiyo, alimwita Yahya Barmaki na kumtaka ushauri wake baada ya kumuambai kuwa alimtaka yeye Yahya ateuwe watu wafaao kutoka miongoni mwa kizazi cha Bwana Abu TaIib wamuelezee mambo yote kuhusu lmamu [a]. Yahya ambaye yeye mwenyewe hakuwa hata kidogo nyuma ya Harun katika uadui kwa watu wa Nyumba ya Bibi Fatima [a], alimtaja Muhammad bin Ismaili kuwa mtu afaaye zaidi kuelezea zaidi kuhusu Imamu [a]. Hivyo mara moja barua iliandikwa kwa Muhammad ambaye alifikiria kuwa kuitwa kwenye mji mkuu wa mfalme lilikuwa jambo la bahati sana kwake kwa kuidumisha shabaha yake ya mafanikio ya kidunia. Lakini hakuwa na fedha za kutosha kwa gharama za safari ya kwenda Baghdad. Hata hivyo alipokuwa hana uhusiano mzuri na Imamu [a] wa kumfanya athubutu kumwendea na kumuomba msaada, aliijua vizuri tabia ya Imamu [a] kiasi cha kutoweza kukatishwa tamaa na mambo hayo. Alimwendea Imamu [a]. Imamu [a] aliielewa vizuri asili na shabaha ya kuendelea Baghdad, lakini ili kujifanya kuwa haijui sababu hiyo, alimuuliza sababu inayomfanya aende mjini huko.

Muhammad alitaja hali ya kiuchumi aliyokuwa nayo na kwamba alikuwa akienda mjini huko kuijaribu bahati yake. Imamu [a] akamwambia, "Haina haja ya kwenda huko, nakuahidi kukufanyia mtayarisho ya kukulipia madeni yako yote na kukupatia mahitaji yako". Lakini Muhammad hakuweza kuiacha nia yake ya kwenda Bagh­dad. Alipokuwa akiondoka alimwambia Imamu [a] “Tafadhali nipe mwongozo fulani kuhusu tabia yangu inavyopasika kuwa huko." Imamu [a] hakulijibu swali hill. Lakini Muhammad alipomshikilia kufanya hivyo, Imamu [a] alisema, "Usishiriki katika mauwaji yangu, na kuwafanya wanangu kuwa yatima". Muhammad alionyesha kushangazwa na maneno hayo na aliendelea kumshikilia Imamu [a] ampe ushauri wa kweli. Imamu [a] alikataa kusema jambo lo lote lile jingine. Alipokuwa akiondoka, Imamu [a] alimpa dinar 450 na dirham 1500 kwa ajili ya gharama ya safari yake. Matokeo ya safari hii ni kama yalivyotazamiwa na Imamu [a].

Muhammad alifika Baghdad akiwa mgeni wa Yahya Barmaki, Waziri Mkuu ambaye alifuatana naye kwenda kwenye baraza Ia mfalme Harun. Alipewa heshima kubwa. Katika mazungumzo, Harun alimuuliza kuhusu habari za Madina. Muhammad alitoa habari mbaya zaidi za hali ilivyokuwa mjini humo na akasema, “Sijapata kuona wafalme wawili katika milki moja". Alipoombwa kueleza vizuri alisema, "Kama hivi unavyotawala hapa Baghdad, ndivyo alivyo Musa Kadhim huko Madina. Anapokea kodi kutoka sehemu mbali mbali za milki hii na yu mpinzani wako mkubwa.”

Haya ndio mambo Yahya aliyomletea Muhammad ayasema. Harun alichukizwa sana kuyasikia mambo haya. Alimpa Muhammad dinar 10,000 lakini Mwenyezi Mungu hakumuandikia kujinufaisha kwa fedha hii. Usiku huo huo alipatwa na maumivu ya koo na akafariki asubuhi yake. Harun aliomba arudishiwe pesa hizo na zilirudishwa. Lakini aliyaamini yale yote aliyoyasema Mumammad. Na aliamua amwuwe Imamu [a].

Hivyo mnamo mwaka 179 Hijiriya alikwenda tena Maka na alikwenda Madina kutoka hapo. Baada ya siku moja au mbili alituma watu kwenda kumtia kizuizini Imamu [a]. Walipofika nyumbani kwake walimkuta kenda kulizuru kaburi la Mtume Muhammad [s]. Bila ya kujali utakatifu wa Kuba tukufu Ia Mtume [s] walimtia kizuizini Imamu [a] hali ya kuwa yu katika Sala na wakampeleka kwa Harun. Huu ni mfano mwingine wa utovu wa heshima na staha kwa kum­bukumbu za Mtukufu Mtume [s], kutokuwa na fikara za kiutu na fikara za Waislamu wa aina ya pekee wa Madina waliomuacha huyu.

Wito Wa Mwenyezi Mungu

Mtu wa mwisho kuchaguliwa na Harun kwa kazi ni Sindi bin Shahid. Mtu huyu ndiye aliyekuwa na moyo mgumu zaidi na asiyekuwa na huruma hata kidogo. Hivyo Imamu [a] alifungwa na akafariki mnamo tarehe 25 Rajab mwaka 183 Hijiriya akiwa na umri wa miaka hamsini na mitano. Ukatili wa mfalme haukuishia hapo Mwili wa marehemu Imamu [a] ulipelekwa kaburini kwa maneno ya matusi makali.

Watu fulani waliamka na kuichukua maiti hiyo na kwenda kuizika mahali paitwapo siku hizi Kadhimain (Iraq) kwa heshima zote za kimazishi.

Nyongeza Baadhi Ya Hadithi Za Imamu Musa Kadhim [A]

1. Imamu [a] alikuwa kila mara akisema, "Nimeiona elimu katika watu wanne. Wa kwanza ni yule amjuaye Mwenyezi Mungu wake. Wa pili ni yule anayetambua kile Mwenyezi Mungu alichomtendea. Wa tatu ni yule ajuaye kile Mwenyezi Mungu anachotegemea kukipata kutoka kwake. Wa nne ni yule ajuaye kile kitakachomtenga na kumuondolea Imani yake.

2. Imamu [a] alikuwa na kawaida ya kuomba dua akisema, "Ewe Mwenyezi Mungu, ninao maadui wengi wambao upanga wao umekuwa butu kwangu na ambao sumu yao kali imepoteza ukali wake kwangu. Ewe Mwenyezi Mungu, Jicho lako lililo Angafu daima katu halinisahau. Kila nilipojiona mnyonge katika kuzikabili taabu na nilipojiona dhaifu mbele ya mahitaji na matakwa (vitu) vinavyo nisonga songa, (Wewe) Uliniondolea shida hizo kwa Uwezo Wako. Na yote haya nilifanikiwa kuyapata kwa msaada wako, na juhudi zangu zilizo dhaifu na nguvu yangu ndogo havikuwa na kazi yo yote katika mafanikio yangu hayo. Umemfanya adui wangu kuangukia (yeye mwenyewe) ndani ya shimo alilonichimbia. Umemshinda katika hila zake mbaya na umemwondolea utukufu wote katika ulimwengu huu na kesho huko Akhera. Hivyo sifa zote Zakustahiki Wewe, Ewe Mwenyezi Mungu.”

Mjukuu wa Mtukufu Mtume [s] akifanyiwa haya hawakuweza hata kuonyesha kutoridhika kwao. lmamu [a] alikamatwa mnamo tarehe 20 Shawwal (Mfunguo Mosi), mwaka 179 Hijiriya.

Ikiwa tahadhari muhimu sana dhidi ya jaribio lo lote la kumtambua Imamu wa wakati ule, Harun alichukua ngamia wawili waliofungiwa minyororo na katika mmoja wao alimkalisha Imamu [a] na kumwacha mwingine bila ya mtu. Kisha aliwapeleka Basra mmoja mmoja huku wakisindikizwa na kundi kubwa la watu. Shabaha yake ilikuwa ni kuwatatanisha watu wasielewe ni wapi alipo lmamu [a] au atakapofungiwa.

Jambo hili lilikuwa kitisho kikubwa kwa jamii ya Imamu [a], kunyang'anywa kiongozi wao wakati alipokuwa safarini na kujulishwa kuwa alichukuliwa akiwa mfungwa. Kwa hakika Imamu [a] aliathiriwa sana na mambo aliyotendewa lakini subira zake za kimyakimya zilizishinda taabu zote.

Alipelekwa Basra (Iraq) kwa kupitia njia ndefu zaidi iliyochukua muda wa mwezi mzima na siku kumi na saba. Mnamo tarehe 7 Dhul-Hijja (Mfunguo Tatu) mwaka 179 Hijiriya aliwasili Basra ambako aliwekwa kizuizini kwa muda wa mwaka mzima. Wakati huo gavana wa Basra alikuwa Bwana Isa mwana wa ami yake mfalme Harun. Isa alizijali amri za mfalme kuhusu kifungo cha Imamu [a], lakini baadaye alianza kuzifikiria sababu za kifungo cha Imamu [a]. Mara moja aligun­dua kuwa alikuwa ishara ya uchamungu.

Alimuelezea Harun mawazo yake. Jambo hili lilimfanya adhaniwe mabaya na Harun. Hivyo alimuondoa Imamu [a] Basra na kumleta Baghdad na kumfunga huko chini ya ulinzi wa Bwana Fazl bin Rabi. Baadaye alihisi kuwa Fazl nae alimpendelea Imamu [a]. Hapo akamchaguwa Yahya Barmaki kufanya kazi hiyo. Hiyo ndiyo nguvu ya tabia za Imamu [a] kwamba iliwabidi wafalme waovu wa ukoo wa Bani Ab­bas kubadili walinzi wa jela alimofungiwa mrithi atokanaye na Ukoo wa Mtukufu Mtume [s] na walifanya hivyo kila mara. Vile vile inaonyesha kuwa Harun alitambua moyoni mwake kuwa lmamu [a] angeliweza kuwavutia walinzi wa gereza kama alivyofanya.

3. Kuhusu Umoja wa Mwenyezi Mungu, Imamu [a] alisema:
"Mwenyezi Mungu wetu, Aliyetukuka Zaidi na wa juu zaidi ni Mmoja tu, Yu mwenye kujitosheleza katika Ukamilifu wake Hana mwana wa Kumrithi. Hakuzaa ye yote yule wa kushiriki naye katika Ufalme wake. Hana mke wala dhuria ye yote. Wala hana mshauri. Yu Mwenye kuishi na hadhoofiki. Yu mwenye Nguvu zote ambaye Nguvu Yake haishindwi. Yu Mbora zaidi asiyekuwa na dosari yo yote. Yu Mmoja wa Kimawazo Ambaye hana pupa. Yu Wa Milele, Ambaye Kuwepo kwake kwa milele hakuingiliwi na kitu cho chote kile... Yu wa milele na Asiyekufa. Yu Asili (muumba) wa viumbe vyote na hashindwi. Yu mwenye kumiliki utajiri usiomalizika. Yu mwenye Utukufu usiofifia. Yu mjuzi wa yote ambaye hakuna kiwezacho kujificha kutoka katika Jicho lake lenye kuonuyote. Yu Mwadilifu mno na hairuhusu dhuluma itoroke. Yu Mkarimu asiyekataa kutoa Baraka Zake. Akili (za mwanadamu) haziwezi kuielewa barabara maana halisi ya Dhati yake. Wala fikara (za mwanadamu) haziwezi kumsawiri barabara. Maeneo hayawezi kumuweka. Nafasi haiwezi kuiwekea mipaka Dhati Yake. Kuona kwa macho yetu hakuwezi Kumfikia Naye Anakushikilia kuona kwetu. Yu Mwema na Mjuzi wa Yote. Hakuna cho chote kile kifananacho Naye. Yu Mwenye kusikia na kuona yote. Hakuna kikundi cha watu watatu kinacho zungumza mahali fulani ila Yu wa nne wao. Na wanapokuwepo watu watano Yu wa sita wao. Yu pamoja na (viumbe) wote, yu pamoja na wachache na yu pamoja na wengi. Yu wa Awali kabisa Aliyekuwepo kabla ya vyote. Yu wa Milele na vitu vyote vitakapokoma kuwepo, Yeye Atakuwepo. Yu Asiyeingiliwa na Muda na cho chote kile kiwacho ni kiumbe (chake) na usanii Wake. Ametukuka zaidi kiasi cha kutostahili kusifiwa kwa sifa za viumbe (Vyake)."