read

Mkufu wa Ajabu

Mji wa Madina ulikuwa ukiwaka kwa joto kali baada ya adhuhuri. Jua lilikuwa kali na ardhi ilikuwa ikiunguza. Ni watu wachache tu ndio waliokuwa wakitoka kwenye kivuli cha nyumba na kwenda kwenye jua jingi wakati huo. Mji ulikuwa mtupu na kwa nadra kiliweza kuonekana kivuli cha mpita njia juu ya ardhi.

Hata hivyo, mji wa Madina ulikuwa ni mwanga wa pekee wa matumaini ya mzee. Alipoingia katika mji, alisimama chini ya kivuli kidogo cha nyumba ya udongo. Akavuta pumzi ndefu kuonyesha kwamba amefurahi na amepata utulivu. Akaparigusa jasho la kipaji chake kwa mkono wa kanzu yake iliyochafuka, na akasema moyoni:

"Namshukuru Mwenyezi Mungu! Hapa ni Madina. Hapa ni mji wa Mtume. Nikimwomba Mtume Mtukufu uchofu wangu wote utalipika. Yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Yeye ni tegemeo la watu. Hakuna mtu yeyote aliyemsikia Mtume akisema 'Hapana!' Hakumkatalia mtu yeyote. Inatosha tu uende msikitini na ukomeshe uchofu, njaa na ufukara huu. Basi mbona umesimama, mzee? Hapa mpaka msikitini si mbali."

Mzee aliwahi kuja Madina kabla yake, hivyo, alikuwa akivijua vichochoro na mitaa ya mji.

Kile kilichokuwa kikimwumiza zaidi kilikuwa jeraha na malengelenge ya miguu. Vitu alivyokuwa navyo aliviuza ili anunue kipande cha mkate, na akawa hana viatu kwa ajili ya safari yake ya masafa marefu katika joto. Hakuwa na njia, kwani ilimbidi kwa vyovyote vile asafiri mpaka Madina. Hivyo, akaikata nguo yake vipandevipande kufunga miguu yake. Akabakiwa na jeraha, malengelenge na uchofu kutokana na kwenda kwa miguu.

Vizuri. Hapa ni msikitini na wakati wa sala ya alasiri haukupita sana. Ni lazima Mtume Mtukufu awemo msikitini wakati huu.

Akapangusa uso wake ulioungua kwa jua na ndevu zake nyeupe zilizochafuka na akaingia msikitini.

Sala ya alasiri ilikuwa imekwishamalizika na Mtume Mtukufu alikuwa amekaa kwenye mihrabu akizungumza na wafuasi wake.

"Sura nzuri ioje ya Muhammad! Utulivu uoje uliokaa kwenye sura ya Mtume! Ikiwa kwa kumwona yeye kunamtoa mtu uchofu wake, itakuwaje ikiwa ataondoka mahali pake na kuniuliza hali yangu mimi mzee nisiyejulikana na niliyevaa nguo mbovumbovu?"

Mtume Mtukufu alipoona uso wa mgeni mzee aliyechoka akaondoka nafasi yake, akaitikia salamu yake kwa furaha, akamkumbatia na kumkalisha karibu naye.

Ammar Yasir, Jabir Ansari, Bilal Habashi na masahaba wengine wakampa mkono na wakamkaribisha kwa furaha.

Mzee alikuwa amepata taabu sana kwa kadiri kwamba aliona bora kwanza aeleze taabu yake kabla ya kukaa.

"Mwenyezi Mungu asimjaaIie mtu yeyote awe na dhiki ugenini. Mimi katika mji wangu ninaishi maisha ya heshima, lakini katika safari hii nimefikiwa na jambo Iililonifanya nipoteze kila nilichokuwa nacho. Sasa nina njaa! Si viatu, wala nguo, wala masurufu! Nimeweza kwa taabu nyingi kujifikisha hapa ili uniokoe katika hali hii."

Mtume mwenyewe alikuwa na njaa. Nguo aliyoivaa ilikuwa ndiyo nguo yake ya pekee, na nyumbani hapakuwepo kitu chochote cha kuweza kumsaidia mzee. Lakini hakuwa na desturi ya kusema "Hapana!" Hakuna mtu yeyote aliyerejea mikono mitupu kutoka kwake, na haifai mzee huyo avunjike moyo.

Tabasamu ya kufurahisha ya Mtume Mtukufu ilikunjua uso wa mzee.

"Mimi sina kitu sasa hivi, lakini nitakupeleka mahali ambapo nina hakika hutarejea mkono mtupu. Nyumba ya binti yangu Fatima ipo hapa karibu. Fatima ni kipande cha mwili wangu. Yeye ni mtu anayependwa na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, naye pia humpenda Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Yeye anapendelea zaidi matakwa na maridhawa ya Mola na Mtume Wake kuliko yake. Uongofu, ufanisi, kheri na baraka hupatikana nyumbani kwake siku zote. Ondoka ndugu yangu! Nenda kwa Fatima ili ufarijiwe dhiki yako. Bilal, atakuongoza mpaka nyumbani kwa Fatima."

Mzee na Bilal wakaondoka. Nyumba ya Fatima haikuwa mbali. Nyumba ya Fatima ilikuwa ubavuni mwa nyumba ya Mtume. Mzee akasimama pembeni mwa mlango na akatoa salamu kwa sauti kubwa:

"Salaamun 'alaykum, enyi AhIi Bait wa Mtume!"

Binti Mtukufu wa Mtume Muhammad (s.a.w.) akaitikia kutoka ndani:

"Wa'alaykumus salaam warahmatullahi wabarakatuh! Ni nani na una kazi gani?"

Mzee akasema kwa upole na unyenyekevu:

"Mimi ni mzee wa Kiarabu. Naona njaa, sina nguo na maskini. Nimekwenda kwa baba yako mtukufu, Mtume wa Mwenyezi Mungu, kumwomba msaada, naye amenipeleka kwako."

Fatima hakuwa mtu wa kumrejesha maskini kwake bila ya kumpa ehochote. Fatima alikuwa mfano wa uchaji na kujitolea. Fatima alikuwa kipenzi bora kabisa wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Lakini afanye nini? Siku tatu zimepita hakuwa na kitu cha kula yeye na familia yake! Ni siku tatu tangu njaa iingie katika nyumba ya Fatima! Familia hiyo wamepitisha siku tatu kwa kunywa maji peke yake. Lakini Fatima hakusita wala hakufikiri. Tandiko dogo lililokaliwa na Hasan na Husayn angeweza kupewa maskini.

Tandiko Ienyewe lilikuwa la ngozi ya kondoo ambalo Hasan na Husayn walikuwa wakilikalia na kulilalia! Fatima alilikunja na kumpa mzee na kumwomba radhi:

"Natumai Mwenyezi Mungu atakupa bora kuliko hili."

Lakini mzee akakataa kulipokea!

"Ewe Binti wa Mtume! Mimi nilifanye nini hilo? Mimi nina njaa, sina nguo wala sina matumizi ya safari."

Fatima aliduwaa. Akatafutatafuta katika nyumba yake ndogo apate kitu kingine. Mara akakumbuka mkufu aliopewa zawadi na binti wa Hamza ambaye ni binti wa ami yake. Akauchukua na kumpa mzee na kumwambia:

"Uuze mkufu huu. Natumai Mwenyezi Mungu atakuondolea shida yako kwa pesa utakayopata."

Mzee akauchukua mkufu na akaomba dua, kisha akaenda kwa Mtume Mtukufu. Mtume Mtukufu alipomsikia mzee akimhadithia kisa chenyewe, akatokwa na machozi na akasema:

"Hapana shaka mushkili wako utaondoka, kwa sababu mkufu huu umetunzwa na mwanamke ambaye ni fakhari wa wanawake wote ulimwenguni."

Ammar Yasir akamsogelea Mtume Mtukufu. Wakati wote huo alikuwa amekaa akitazama tu. Alionekana alikuwa hana raha. Binti wa Mtume ametoa rasilimali yake yote na yeye....Hapana! Hakuweza kustahamili.

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Unaniruhusu niununue mkufu huu?"

Mtume Mtukufu akatokwa na macho ya furaha, akacheka na kusema:

"Ndiyo, ewe Ammar! Yeyote atakayeununua mkufu huu atasalimika na moto wa Jahannam."

Ammar akamtazama mzee na kumwuliza: "Mkufu wako unauza kiasi gani?"

Mzee akajibu:

"Nahitaji kiasi cha pesa kuweza kununua chakula na nguo na kutumia safarini mpaka nifike katika mji wangu. Mkufu nauuza kwa kiasi hicho!"

Ammar akamtazama kwa huruma mzee aliyechoka, kisha akamwambia:

"Mbali na uliyoyasema, mimi ninakupa dinari ishirini za dhahabu na dirhamu mia mbili za fedha badala ya mkufu huo."

Macho ya mzee yaling'ara kwa furaha:

"Wewe ni mtu karimu mno!"

Ammar akatazama chini kwa kuona haya.

Akasema:

"Thamani ya mkufu uliovaliwa na binti wa Mtume Mtukufu ni zaidi mno kuliko haya. Lakini hivi sasa sina zaidi kuliko haya."

Mzee akainua mikono yake kuomba dua:

"Ewe Mola! Mbariki binti wa Mtume neema ambayo hakuwahi mtu yeyote kuiona au kuisikia."

Ammar Yasir akamchukua mzee kwake, akapokea mkufu kutoka kwake na akampa yale aliyomwahidi, kisha mzee akaenda zake.

Ammar akatia manukato na marashi katika mkufu unukie. Kisha akauweka kwenye kitambaa kizuri chenye thamani na kukifunga. Akamwita mtumwa wake Saham. Saham alikuwa mtumwa mtiifu na mwenye adabu ambaye alimpata katika vita vya Khaybar.

"Njoo!" Chukua mkufu huu na mkabidhi Mtume Mtukufu! Kisha wewe mwenyewe utatumika kwa Mtume."

Saham akauchukua mkufu na akampa Mtume. Mtume Mtukufu akamwombea dua Ammar lakini hakuupokea mkufu. Akasema:

"Mpe salamu zangu binti yangu Fatima. Mpe mkufu na mwambie kwamba wewe utakuwa chini ya amri yake."

Fatima Zahra akaupokea mkufu kwa mshangao mkubwa, na akamwambia Saham:

"Wewe uko huru katika njia ya Mwenyezi Mungu! Unaweza kwenda popote unapotaka!"

Saham akacheka na kusema:

"Nashangazwa na baraka ya mkufu huu! Umemshibisha mwenye njaa; umemvisha asiye na nguo; umemkidhia haja ya maskini; umemwacha huru mtumwa; na mwisho wake umerejea kwa mwenyewe! Kwa kweli nyumba hii imejaa kheri na baraka."

Mtume Muhammad (s.a.w.) amesema:

"Na kuhusu binti yangu Fatima, kwa hakika yeye ni bibi wa wanawake wa ulimwengu tangu wa mwanzo hadi wa mwisho. Yeye ni kipande cha mwili wangu. Yeye ni nuru ya macho yangu. Yeye ni tunda la moyo wangu. Yeye ni roho ya mwili wangu. Yeye ni hurulaini mwanadamu. Anaposimama kwenye mihrabu mbele ya Mola wake Mwenyezi Mtukufu, huwaangazia malaika wa mbinguni nuru yake kama nyota zinavyowaangazia watu wa ardhini nuru zake. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu huwaambia malaika: 'Enyi malaika Wangu! Mtazameni mja Wangu Fatima, bibi wa waja Wangu, amesimama mbele Yangu kuniabudu. Viungo vyake vinatetemeka kwa hofu Yangu, hali ya kuwa ananiabudu kwa moyo wake wote. Nakufanyeni nyinyi kuwa ni mashahidi Wangu kwamba nimewasalimisha wafuasi wake kutokana na Moto."'

(Amali, Sheikh Saduuq, uk. 99-100)