read

Pamoja Na Mitume Katika Njia Ya Mashaka
Mtungaji: Sayyid Muhammad Taqi Mudarrisi
Mfasiri: Hassan A Mwalupa

*******

Kitabu hiki kidogo kina elezea Visa vya Mitume, vilivyo nukuliwa kutoka Qur’ani na Historia. Visa hivi vinaelezea namna gani Mitume walipata misukosuko wakati wana fikisha Ujumbe wa Allah swt.
Na vivyo hivyo katika nyakati zozote, atakaye fanya kazi ya kuutetea Uislamu na itikadi za Waislamu atajikuta yuko peke yake na hana msaidizi. Basi visa hivi vitampa nishati na vitamzidishia azma na subira ya kuenedelea na kazi yake.

*****

Utangulizi Wa Mchapishaji

Mpenzi msomaji!
Assalaamu alaykum wa rahmatullahi wa barakaatuh!

Je, imetokea siku moja kuwa na shaka na ukahisi upweke katika njia ya haki kwa sababu ya uchache wa wafuasi wake?

Je, umejikuta siku moja uko peke yako katika uwanja wa mapambano?

Je, umewahi kuzunguka huku na huko ukimtafuta mtu atakayekusaidia kutatua matatizo ya maisha na njia yake ngumu?

Je, umewahi siku moja kuhitajia akiba ya chakula kwa ajili ya safari ya maisha ya mashaka?

Je, yamekutokea yote hayo?

Sitangoja jibu kutoka kwako! Kwani jibu la watu wote litakuwa moja tu, nalo ni: “Ndiyo. Mambo hayo yote yametufika.”

Ndugu yangu Mwislamu! Hakika hukuwa peke yako katika njia iliyokupwekesha; wametangulia katika njia hiyo Mitume watukufu, wanaharakati na wanamapinduzi wa mwanzoni.

Hakika hukuwa peke yako katika uwanja wa mapambano uliosimama kuutetea Uislamu na itikadi za Waislamu, bali walitangulia mawalii na watu wema katika uwanja huohuo na mahali hapohapo ambapo ulisimama kwa lengo hilohilo na matumaini hayohayo uliyokuwa nayo. Basi njia ni moja kufuatana na malengo na matumaini yake.

Kwa hivyo, hukuwa peke yako.

Pengine umekuwa peke yako katika wakati wako ambao ulifuata njia hiyo, lakini hukuwa peke yako katika nyakati zote ambazo amefaradhia Mwenyezi Mungu kukata mbuga ya maisha yenye miiba. Mitume watukufu, maimamu wema, wanaitikadi (wenye kubeba ujumbe) wa mwanzoni na mashahidi watukufu, kila mmoja wao ameingia katika majaribio hayo magumu ya kiitikadi, akayakabili na kuyavumilia kwa msimamo thabiti. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu akamlipa malipo yake bila ya kupungua chochote.

Basi makusudio yetu tunapokwenda katika njia yenye kudumu ya hao waliotutangulia ni kuwafuata na kuchukua mwanga wa taa yao na azma, subira na msimamo wao.

Ewe ndugu yangu Mwislamu! Hakika kitabu hiki kitakuonyesha visa vya Mitume na Manabii jinsi walivyopambana na mashaka na matatizo ya maisha na jinsi usafi wao ulivyozidi na ukatoa johari ambazo zinadhihirisha hakika yao safi isiyokuwa na vumbi.

Vilevile kitabu hiki kinaonyesha kwamba kila mashaka ya njia ya Manabii yalivyozidi ndivyo azma na uthabiti wa njia yao ya haki ulivyozidi. Mafanikio hayo yanatokana na kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na kuhakikisha malengo yao ya kiitikadi.

Visa vya Mitume vilivyotajwa katika kitabu hiki vimenukuliwa kutoka Qur’ani Tukufu na vitabu vya kihistoria na vya kiitikadi. Kwa hakika fikra za kitabu hiki na darasa zake zinawezekana kuzingatiwa kuwa ni mwanga utakaotuongoza kushika njia ya kujenga hadhi ya mwislamu kufuatana na maoni ya Qur’ani.

Hakika uzoefu wao ni mali waliyoturithisha ili tugharamie mahitaji yote katika njia ya kiitikadi. Kuirudisha hadhi ya Kiislamu katika tukio la maisha huhesabiwa katika mambo muhimu zaidi ya wanaofanyia kazi Uislamu leo. Kwa hivyo, halipatikani hilo ila kwa kupatikana kiigizo chema, nacho ni Mitume.

Kutokana na umuhimu na haja kubwa ya kitabu hiki, Jumuia ya Udugu wa Kiislamu imekichapisha tena kitabu hiki kama ni mojawapo ya kazi zake za kiutamaduni na kimaarifa.

Chapa ya kwanza ya kitabu hiki (kwa kugha ya Kiarabu) kilichapishwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, lakini pamoja na kupita muda huo mrefu bado kitabu hiki kinatoa pumzi ya uhai. Kwa nini kisiwe hivyo ilhali mishipa yake imeambatana na mishipa ya historia ya kiitikadi iliyo hai?

Mtungaji wa kitabu hiki ni mwanachuoni mtukufu Sayyid Muhammad Taqi al-Mudarrisi ambaye ameingia katika nyanja mbalimbali za kazi za Kiislamu kama vile kujenga shule na vyuo vya kidini vya kisasa. Vilevile amejiendeleza katika kutunga vitabu vya darasa na utafiti wa Kiislamu pamoja na huduma nyinginezo za Kiislamu ambazo anaendelea kuzitoa katika Umma wa Kiislamu. Kitabu hiki chenye fasaha ni miongoni mwa natija zake za mwanzoni, na amekiandika akiwa na umri wa miaka ishirini.

Ifuatayo ni orodha ya vitabu vyake vya darasa vilivyokwisha chapishwa ambavyo vinajadili kwa mapana katika fani mbalimbali za Kiislamu:

1) Fikra za Kiislamu: Mwelekeo wa Kisasa

2) Mantiki ya Kiislamu: Misingi na Njia Zake

3) Amali za Kiislamu: Asili na Malengo Yake

4) Jamii ya Kiislamu: Asili na Malengo Yake

5) Historia ya Kiislamu

6) Ufufuo wa Kiislamu

7) Fiqihi ya Kiislamu

8) Mijadala katika Qur’ani Tukufu

9) Tafsiri ya Qur’ani. Mwongozo katika Qur’ani.

Kuna vitabu kadhaa vya Kiislamu na mamia ya kaseti za Mihadhara yake ambayo anaendelea kutoa. Vyote ni katika lugha ya asili ya Kiarabu.

Mchapishaji wa kitabu hiki ni Maktab as-Sayyid al-Mudarrisi ambayo ni taasisi ya utamaduni wa Kiislamu yenye lengo la kueneza fikra za Kiislamu miongoni mwa wana wa Umma wa kiislamu na kuingiza roho ya udugu wa Kiislamu. Jumuia hii inafanya kazi nyingi za Kiislamu.

Mwishowe, tunapenda kuwakumbusha ndugu zetu mambo mawili:

1) Kitabu hiki kinatoa zingatio, faida na kielelezo, kwa kuwa Mitume ni kiigizo chetu.

2) Saidia kueneza kitabu hiki kwa upana zaidi, kisome, kisha mpe rafiki yako afaidike.

Tunakuombea mafanikio mema na kabuli njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Maktab as-Sayyid al-Mudarrisi

Utangulizi Wa Mtungaji

Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mtukufu, na rehema na amani zimshukie Mtume Wake Muhammad (saww), Nabii wa Mwisho, na juu ya kizazi chake kitakatifu.

Hakika Umma wa Kiislamu umeshindwa kabisa, na kushindwa huko kunafuatia machungu na mateso; kisha ukosefu mkubwa katika pande mbili: upande wa kimaada (kidunia) na upande wa kimaanawi (kiroho). Kukosekana upande wa kimaanawi ni sababu ya kukosekana upande wa kimaada, kwani umaada sio nguvu inayojileta yenyewe kwa mtu na kuweza kubaki au kuondoka wakati wowote, bali ni natija ya kazi ya mtu na mapato ya juhudi yake. Mtu hafanyi bidii ila baada ya kujua maana ya juhudi yake.

Kwa hivyo, kukosekana umaanawi katika Umma wa Kiislamu ndiko ambako kunapasa kuupiga vita na kuupigania ili urudi utukufu na ushindi na Umma uishi katika neema baada ya kuwa katika adhabu. Hatuwezi kuupiga vita ukosefu huu bila ya kueneza mwamko sahihi wa Kiislamu kwa kutafsiri Qur'ani, kueneza maarifa yake. kuelezea maisha ya mashujaa wa Kiislamu, n.k.

Kitabu hiki kidogo ni jaribio dogo katika kutimiza lengo hili, kwani tumenakili mifano michache ya visa vya Mitume.

Kilele Cha Utukufu

Hakika Mitume (amani iwe juu yao) wamekumbana na matatizo mengi na wamepita katika njia ya miiba (mashaka) kuelekea kwenye utukufu wa kitu hadi wakafika kwenye kilele cha ukamilifu na utukufu. Wakawa ni watu wa ngazi za juu kwa kufikia kwenye kilele cha ubinadamu.

Kwa hivyo, wao walijua njia, wakaongoka na wakajua malengo ya njia hizo na wakalingania watu na kuwaongoza wale waliopotea kwenye lile walilolijua. Waliwafungulia watu njia ambazo zilikuwa hazijulikani kwa kuwa walikuwa wenyeji katika mambo hayo na walikuwa na nguvu na uwezo kutokana na bahari yao ya
elimu, upole na sifa zao za uvumilivu na uthabiti.

Hatuwezi kuvipima vipawa vyao vinavyoshindania kheri, utiifu na utukufu. Hatuwezi kuvipima kwa vipawa vyetu. Nguvu yao ya uwezo, udhibiti wao wa nafsi, matamanio, dunia na udanganyifu wake, na kuvumilia kwao misiba, ni muujiza wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe Vyake.

Kwa hakika, Mitume wametuachia athari nyingi na mazingatio mengi ambazo ndizo zinazotusaidia. Wao ndio waliotufundisha namna ya kuvumbua vitu visivyojulikana na kutosalimu amri mbele ya vitu hivyo. Wametufundisha namna ya kupambana na kuyashinda matamanio, kuwa na msimamo mzuri katika kuyakabili matamanio na kuwa na azma imara. Lau tusingefuata ushauri wao tusingekuwa watu kama tulivyo. Lau tungekubali ujinga tangu siku ya kwanza na kutawaliwa na matamanio, tungejikuta tumo katika pango la ushenzi na tungelikuwa kama wanyama tu!

Ni lazima tulizingatie na tufaidike kutokana na ibra au mafunzo ya mambo yetu muhimu ya kidini na kidunia. Mazingatio hayo hayawezi kutekelezwa bila ya sisi wenyewe kutaka kuelekea na hayawezi kutuhimiza bila ya sisi wenyewe kujihimiza. Mfano wake ni kama umeme unaotoa mwangaza wakati ule tunapotaka utoe mwangaza.

Mazingatio haya huunda nguvu, uwezo na azma katika harakati, huimarisha kazi na hutakasa utiifu; na kila mmoja katika misimamo hiyo mitukufu ya kiutu hutukuza athari zake katika maisha na hutoa matumaini makubwa kwa maazimio yake. Haya ndiyo mapinduzi ya hakika ambayo kipimo cha utukufu wake yanaonekana katika malengo yake.

1. Vipi Tutazingatia?

Vipi tutazingatia visa vya Mitume na Manabii? Vipi tutaweza kuilinganisha historia ya zamani na matatizo yetu ya sasa? Hakika swali hili linataka jibu pana.

Hakika mtu ana tabia ya kuogopa vitu asivyovijua na hujihadhari na upotofu. Kwa hivyo, hujiepusha na mambo yasiyojulikana.

Mitume wameondoa tatizo hili katika maisha ya kiutu kwa kujiingiza katika mambo yasiyojulikana, na huko ni kwa kuomba msaada wa Mwenyezi Mungu.

Wameweza kumthibitishia mtu kwamba utafiti wa mambo yasiyojulikana ndiyo njia ya pekee ya maendeleo katika maisha; kisha wakamfundisha mtu ushujaa katika kazi hii tukufu kukabiliana na kitu kisichojulikana.

Mitume wamewashajaisha watu kuvunja vikwazo vya matamanio ambavyo vimemzunguka mtu kila upande mpaka kumfanya mnyonge kabisa ilhali Mwenyezi Mungu amemuumba mtukufu. Unyonge ni udhalilifu mfano wa kuni zinazomchoma.

Ikiwa ni hivyo, basi ni juu yetu kujifunza mwenendo wao uliojaa jihadi iliyoimarika na bidii ya amali (utendaji) katika njia ya kujikomboa kifikra na kumpeleka mtu kwenye kheri.

Hebu tuangalie mambo haya mawili matukufu ambayo ni ushujaa na ujasiri katika kuyapetuka mambo yasiyojulikana, na ushujaa katika kuondoa vikwazo vya matamanio.

2. Kiigizo Kizuri

Tumesema kuwa maisha ya Mitume ni kiigizo cha mambo ya kheri walivoyafanya, kuyafundisha, kuyawekea mpaka mambo ya shari na kuthibitisha bidii ya jihadi na harakati za kudumu.

Kwa hivyo, tunajifunza kutoka kwao mambo haya:

1. Namna ya kujikomboa kutokana na shari na washari. Vilevile namna ya kujikomboa kutoka katika makucha ya mataghuti (madhalimu) na wanyonyaji wa nchi.

2. Namna ya kuvumilia udhalilifu, unyonge, uduni, mateso, adhabu na machukivu ili tusikwame katika shabaha yetu wala zisidhoofike nishati zetu.

3. Namna ya kuendelea daima katika jihadi na mapambano dhidi ya adui wetu. Ijapokuwa natija yake itachelewa, lakini ni lazima tuendeleze mapambano hata kama mauti yatatufikia njiani na kuwaigiza walioendeleza harakati zao kwa bidii mpaka wakapata yale waliyoyatamani kabla ya kufikia mwisho.

4. Namna ya kumnyenyekea Mwenyezi Mungu kwa moyo safi bila ya kutegemea malipo au shukrani kutoka kwa viumbe.

5. Namna ya kutatua maelfu ya matatizo yaliyozidi ambayo yanatungoja/yanatuongoza katika harakati zifanywazo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na ambayo Mitume wameyapatia ufumbuzi wake kamili.

3. Sababu za Kijinga

Kuna baadhi ya watu wanaopendelea uvivu, wanaostahabu udhaifu na kupendelea kungojangoja bila ya kufanya bidii yoyote. Husema: “Hakika harakati huleta matatizo", au husema: “Hatuna uwezo wa kufanya kazi fulani za kiharakati." Wakijibiwa: "Mbona Mitume waliweza kuwa na harakati licha ya matatizo waliyokuwa nayo?" Husema "Mitume walikuwa wakipata msaada wa wahyi (ufunuo) na wakilindwa kwa nguvu za Kiungu. Isitoshe, wameumbwa wakiwa na ujuzi, hekima, usafi, uwerevu na mengineyo ambayo yaliwaandalia njia na kuwawekea msingi mzuri; kisha wao walikuwa na miujiza iliyowaandaa kwa tablighi na kuhami nafsi zao na za wasaidizi wao."

Ninawaambia watu hawa: "Ukweli ni kuwa sababu hizi haziwezi kukuteteeni, enyi wavivu! Wenyewe mnasema kinagaubaga kuwa hamwezi kuwa na harakati, hivi ni kwa sababu mnadharau na ni wazembe."

Bila shaka sababu hizi zinaweza kuwapa faida wale walio tayari kupiga mbizi katika mawimbi makubwa ya bahari. Kwa hivyo, si Mitume peke yao ndio wenye kulindwa na kusaidiwa, bali yeyote yule mwenye kufanya kazi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hupata taufiki na msaada Wake. Qur'ani inasema:

''Mkimsaidia Mwenyezi Mungu atakusaidieni na ataithibitisha miguu (hatua) yenu.” (47:7)

Uzoefu umeonyesha kwamba mwenye kuwa na harakati kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hana budi kupata nusura kutoka Kwake.

Vivyo hivyo, vipawa vyao (Mitume) wameviweka wazi katika vitendo vyao, maneno yao, visa vyao na utukufu wao wamevibakisha kwetu kama ni hazina safi ambayo tunaweza kutoa kiasi tunachotaka na tunachohitajia. Qur'ani inasema:

“Hakika katika visa vyao kuna mazingatio kwa wenye akili.” (12:111)

Kuna mifano mingi katika Qur'ani ya uzoefu katika maisha ya Mitume na maadili yao. Vivyo hivyo, katika vitabu vya sira kuna hekima nyingi zilizotolewa na Mitume katika karne nyingi zilizopita.

Madai ya baadhi ya watu kwamba Mitume walikuwa na miujiza ni sawa, lakini ukweli ni kuwa Mitume hawakuutumia uwezo huu ila kwa nadra sana. Mara nyingi walijadiliana na watu kwa dalili za kiakili, na walipoanza kuwalingania watu walikuwa wakifukuzwa na kuadhibiwa wao pamoja na masahaba zao. Lau wangelikuwa wakitegemea miujiza ya kujikinga, basi kazi yao ingekuwa nyepesi sana na wala wasingeadhibiwa.

Kwa hivyo, miujiza ilikuwa ni kwa ajili ya kubainisha Utume wao na hoja ya Mwenyezi Mungu kwa watu ili katika siku ya Kiyama watu wasidai na kusema: "Ewe Mola wetu! Sisi tumemkanusha mtu aliyetaka kututawala na kuchukua milki zetu."

Mitume hawakuzitatua kazi nyinginezo kwa kutumia miujiza, bali kwa kufuata maumbile ya Mwenyezi Mungu anayowaumbia viumbe Vyake na neno Lake wakati alipokadiria kila kitu kwa mujibu wa sababu zake. Wao ni kama watu wengine - hula. huenda sokoni, hufanya tablighi, na hujitahidi kufuata mwendo wa watu wa kawaida. Tukiangalia mfano mmoja tu utatosha kutupa dalili dhahiri ya hoja hiyo.

4. Njia ya Mashaka

Mitume (amani iwe juu yao) wamekumbana na mashaka (miiba) katika mwendo wao wa kuwaongoza watu kwenye njia ya uongofu. Ni watu wachache sana miongoni mwa wanaofanya kazi za daawa (tablighi) wanaopata mashaka kama hayo. Hakika Mitume wamepata shida na misukosuko mingi sana, matusi na tuhuma. Lakini wao walitegemea nguzo ya haki mbele ya batili, mwanga mbele ya giza na ukweli mbele ya hadaa na vitimbi. Wakathibiti katika hali hiyo kama jabali mbele ya kimbunga, na walikwenda katika njia hiyo ngumu ya mashaka kwa mwendo wa kasi bila ya kuogopa wala kujali masumbuko yaliyokuwa yakiwangoja njiani.

Tunathibitisha hapa visa vichache vya Mitume hao ambavyo vinaonyesha msimamo wao thabiti katika njia ya daawa (tablighi), visa ambavyo vina mazingatio na ukumbusho kwa waumini.

Tutadondoa hapa visa vya maisha yao yaliyojaa jiihadi na mapambano na tunataraji kwamba wasomaji watagundua njia yao pana ya kufuata jihadi yao tukufu ili iwe ni somo kwao. Jambo hili ni wajibu kwa kila binadamu mwema kulifanya mbele ya ubatilifu na watu wake. Wasomaji wazingatie kwamba lau wangechukua nafasi ya Mitume na wangeitakidi itikadi yao, je. wangefanya nini mbele ya ubatilifu unaotawala? Hebu tuchukulie kwamba hii ni zama za Mitume na watu ndio haohao na matatizo ndiyo hayohayo, nasi tunataka kutenda kama walivyotenda wao ili kuiga mifano yao.

Visa Vya Jihadi Ndefu

1. Nabii Idris (as)

Kuna watu wengine ambao wanapotiwa hima na tamaa, na wanapo danganywa na makusudio yao, mara huanza kufanya bidii na kutafuta kila njia ili wapate matamanio na makusudio haya. Kuna wengine ambao kazi yao ni vitimbi, hila na wizi, na wengine kazi yao ni kutafuta utawala na uongozi wa kuhukumu watu na miji. Watu hao hujitahidi kwa kila njia ili kufikia malengo yao. Hakika watu wa aina hii ni waovu sana, kwa sababu wameharibika na wanawaharibu wengine, wamepotea na wanawapoteza wengine. Hao ndio viongozi waovu wanaowaongoza watu kwenye Moto.

Mfano mmojawapo wa aina ya watu tuliyowataja alikuwa dhalimu mmoja aliyeishi katika zama za Nabii Idris (as) ambaye aliwamiliki watu na kuwafanya watumishi wanyonge wanaomtumikia kwa kila analolitaka na kulitamani. Ikiwa mmoja wao alionyesha upinzani wowote basi alikuwa akimtesa kwa adhabu mbaya sana. Siku moja alipokua akitembea njiani aliona shamba zuri lenye rutuba lililokuwa ni mali ya mja mwema wa Mwenyezi Mungu ambaye alikuwa akijipatia maisha ya ukoo wake kwa kulimia ardhi hiyo. Mfalme dhalimu alivutiwa sana na shamba hilo, na alipouliza ni la nani, akaambiwa kuwa ni la mpinzani mmoja fulani. Akataka kulinunua, lakini yule mtu akakataa kwa kumjibu "Ardhi hii wanahitaji zaidi ukoo wangu kuliko wewe."

Mfalme akarudi nyumbani kwake akiwa amekasirika. Akamhadithia mkewe habari hiyo. Mkewe akamwambia: "Usikasirike, ikiwa unashindwa kumwua kwa kukosa sababu, mimi nitafanya mpango."

Mwanamke yule akawaita watu na kuwaamrisha washuhudie kwamba mtu fulani ni mpinzani wa dini ya mfalme. Kwa hivyo, mfalme akapata sababu. Akamwua yule mja mwema na akachukua ardhi na kuwafukuza wajane na mayatima wake.

Mwenyezi Mungu akakasirika kwa kitendo hicho. Akampa wahyi (ufunuo) Nabii Idris (as) kuwa aende kwa mfalme. Akamwendea mfalme na ujumbe wa Mwenyezi Mungu unaosema:
"Hivi umeridhia kumwua mja Wangu muumini na kuitia ufakiri familia yake ili uchukue ardhi yake? Naapa kwa Utukufu Wangu, nitakutesa nitaondoa ufalme wako, nitauharibu mji wako na nitawalisha mbwa nyama ya mke wako."

Mfalme aliposikia maneno hayo kutoka kwa Nabii Idris (as), akamwambia: "Toka, ewe Idris nisije nikakuua." Mkewe akamwambia: "Isikufadhaishe ujumbe wa Mungu wa Idris. Mimi nitatuma watu wakamwue, hivyo, utabatilika ujumbe wa Mungu wake." Mfalme akamwamrisha mkewe atekeleze njama hiyo.

Akatuma watu arobaini wakamwue Nabii mwaminifu. Nabii Idris (as) akakimbia mwituni na akawa akiishi humo na kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa tahadhari.

Baada ya muda, mfalme taghuti akafa. Mke wake akafa pia, na mwili wake ukawa chakula cha mbwa. Mji wake ukaharibika kama alivyoahidi Mwenyezi Mungu kupitia ulimi wa Nabii Idris (as).

Akatawala dhalimu mwingine na akawa kama yule wa kwanza kwa ushenzi na kiburi. Ikapita miaka ishirini baada ya kuondoka Nabii Idris (as) na mvua haikunyesha. Hali ya watu ikawa mbaya sana na wakawa wanatafuta chakula kutoka katika miji jirani.

Kisha watu wa mji ule wakakusanyika kumwomba Mwenyezi Mungu awaepushe na balaa iliyowasibu. Wakajua kuwa hakuna wa kutegemewa isipokuwa Mwenyezi Mungu. Wakanaza kutubia na wakafikiri namna ya kumwabudu Mungu. Je, wangeweza kumtii Mwenyezi Mungu bila ya kuongozwa?

Mwenyezi Mungu akamleta Nabii Idris (as) kutoka mahali pake alipokuwa akimwabudu. Nabii Idris (as) akawaombea mvua, ikanyesha sana mpaka ikakaribia kuwagharikisha.

Pamoja na mwujiza huo, Nabii Idris (as) alikuwa ni mtu wa pekee aliyeweza kuandika na kushona nguo, na vilevile alikuwa ni mwenye maarifa ya ujuzi wa hesabu na nyota.

2. Mzee wa Mitume

Baada ya Nabii Idris (as) kurejea kwa Mola wake, watu wakaanza kuzusha mambo mapya (bid'a) katika dini, wakahitalifiana kwa tofauti kubwa na wakayarudia mambo yao ya zamani. Kikundi kidogo tu cha watu ndicho kilichoshikamana na mafunzo ya Nabii Idris (as), na kufuata kama alivyoagizia. Wakabaki juu ya njia hiyo ambayo ilikataliwa na watu wengi.
Katika kizazi cha Nabii Idris (as) alikuwepo mtu mmoja akiitwa Nuh. Alikuwa mrefu na mwenye fikra nyingi. Alijiweka mbali na watu kwenye majabali, alikuwa akila mimea ya ardhi tu na akimwabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake.

Alipofikia umri wa miaka arobaini ambapo maandalizi ya uongozi unapokamilika na msimamo anaoutaka Mwenyezi Mungu unapothibitika, alijiwa na Jibril (as) na kumwuliza:

"Kwa nini umejitenga na watu?" Akamjibu:
"Kwa sababu watu wangu hawamjui Mwenyezi Mungu, na kama wakinijua mimi wataniua." Jibril akamwambia: "Kama ukipewa nguvu utaweza kuwakabili?" Akajibu: "Hivyo ndivyo ninavyotaka."

Kwa hivyo, Jibril (as) akampa ujumbe wa Mola Wake na akamwamrisha aeneze mwito wa Mwenyezi Mungu. Akaondoka Nabii Nuh (as) kwa furaha kuelekea kwa jamii ya watu wake. Akawakuta wamejikusanya kwenye masanamu ambayo hayadhuru wala hayanufaishi chochote, na hayasikii wala hayaoni. Watu walikuwa wametawaliwa na upotevu wakawa viziwi na vipofu, hawasikii haki yoyote wala hawana uongofu wowote.

Nabii Nuh (as) akawaendea haraka akiwa na fimbo yake nyeupe ya miujiza ikiwa ndiyo msaidizi wake. Akasimama mbele yao kuwalingania. Akawa kama kimondo kilichoshuka juu ya upotevu wao au kama mwangaza ulioangaza kwenye giza. Akawaambia: "Laa ilaaha illallaah! - Hapana Mungu apasaye kuabudiwa ila Allah!" Hilo likawa ni tamko lililotoka katika moyo wa kishujaa uliojaa imani, mategemeo na utulivu. Watu wakaathirika na tamko hilo na masanamu yao yakatikisika.

Wakasema madhalimu: ''Ni nani huyo?"

Akasema Nabii Nuh (as): "Ni mimi mja wa Mwenyezi Mungu; amenituma kwenu kuwa Mtume wenu."

Madhalimu hao wakaanza kumwadhibu baada ya kumkanusha Mola wake na kuukadhibisha Utume wake. Lakini Nabii Nuh (as) akaendelea kuwalingania, nao pia wakaendelea kumkanusha na kumkadhibisha. Ilikuwa ni kawaida kwake kwenda katika hafla na mikutano yao akiwalingania dini, lakini watu walikuwa wakigeuka huku na huko na wengine wakiziba masikio yao ili wasisikie mwito wa haki. Watu walikuwa wakishikwa na mori kipumbavu. Walikuwa wakimwadhibu sana Mtume wao mpaka akizimia. Baada ya kuzimia, ami yake alikuwa akija kumchukua nyumbani kwake kumwuguza. Mara nyingine alikuwa akizimia kwa muda wa siku tatu mfululizo bila ya kuzinduka na anapozinduka alikuwa akiwaombea kwa kusema:
"Ewe Mola wangu! Waongoze watu wangu kwani hakika wao hawajui."

Umri wa Nabii Nuh (as) ukazidi na upotevu wa watu wake ukazidi pia. Akasubiri Nuh kwa subira kubwa lakini utaghuti wao na kiburi chao cha kukataa haki kikazidi pia.

Miaka mingi ikapita na watu hao wakabaki katika hali hiyo hiyo. Kizazi kimoja kikaondoka na kingine kikaja, lakini kila kimoja kiliendelea kumkadhibisha na kuukadhibisha Utume wake.

Karne moja baada ya pili zikapita lakini kaumu ya Nuh ikaendelea na ukafiri na inadi yao. Ilikuwa kwamba mtu akijiona amezeeka na anakaribia kufa, basi humchukua mtoto wake kwa Nabii Nuh (as) na kumwambia: "Ewe mwanangu! Nitakapokufa usisikilize maneno ya mwendawazimu huyu."

Katika misukosuko hii, Nabii Nuh (as) aliishi muda mrefu uliofikia miaka 950 akiwalingania watu wake, na katika muda huo ni watu wachache wapatao 80 tu ndio waliomwamini!

Kikundi kimoja cha waumini kilikuwa kikiadhibiwa pamoja naye lakini kilikuwa na subira ndogo, hivyo wakamwomba Nabii Nuh (as) awaombee makafiri iwateremkee balaa. Wakati huo miaka 300 ilikuwa imekwishapita tangu alipoanza kuwalingania watu. Akakusudia kuwaombea balaa makafiri, mara akajiwa na malaika 12,000 ambao ni miongoni mwa malaika watukufu. Wakamwambia Nabii Nuh (as): “Tunakuomba usiwaombee balaa watu wako." Akasema Nabii Nuh (as): "Ninawapa muda mwingine wa miaka 300."

Ilipofika miaka 600, hakukuwepo hata mmoja aliyemwamini. Akakusudia kuwaombea balaa. Malaika wakamjia tena na wakamtaka asiwaombee balaa. Nabii Nuh (as) akaongeza muda mwingine wa miaka 300.

Ilipotimia miaka 900, akakusudia kuwaombea balaa. Mwenyezi Mungu akamteremshia wahyi akisema:

"Hataamini yeyote katika watu wako isipokuwa yule aliyekwisha amini.” (11:36)

Akasema Nabii Nuh (as):

“Ewe Mola wangu! Usimwache juu ya ardhi mkazi yeyote katika makafiri.” (71:26)

Mwenyezi Mungu akaitikia dua yake. Ikaja tufani kubwa, yakamiminika maji kutoka mbinguni na zikabubujika chemchemi kutoka ardhini mpaka majabali yakafunikwa kwa maji. Watu wote wakaangamia isipokuwa wale walioingia katika safina ambayo ilikuwa ikikata mawimbi makubwa kama jabali. Safina ilisheheni jozi moja ya kila aina ya viumbe.

Kisha Mwenyezi Mungu akaamrisha ardhi imeze maji yake na mbingu iache kunyesha, na ikapitishwa amri ya kuangamizwa makafiri. Safina ikatua kwenye mlima mmoja ikiwa na watu 80 tu waliomwamini Nabii Nuh (as).

Kisa hiki cha Nabii Nuh mtukufu ni mwujiza mmoja miongoni mwa miujiza michache katika historia. Ingawa Nabii Nuh (as) alijitahidi kuwalingania watu wake kwa muda wa miaka 950 aliokaa nao, lakini waliendelea na upinzani wao na hawakuzidi chochote isipokuwa ukafiri na ulahidi. Hivyo, adhabu iliwashukia ambayo iliwataabisha na kuwaangamiza wote bila ya kumhurumia au kumwacha mtu yeyote.

3. Uthabiti na Jihadi ya Nabii Ibrahim

Aliposhuka Nabii Nuh (as) kutoka katika safina yake kwa salama pamoja na waumini aliokuwa nao, hapo tena watoto wake na wafuasi wakaimarisha nchi, naye akamshukuru Mwenyezi Mungu na kuridhika.

Miaka 50 baada ya gharika, Nabil Nuh (as) akafariki dunia. Umma wake ukaanza kuzidi kwa kuzaliana kizazi baada ya kizazi. Lakini baadaye watu wakaanza kuhitalifiana. Kuna wale ambao walishikilia imara imani kwa kushikamana na mafunzo ya Nabii Nuh (as), na wengine wakapotea kwa kufuata matamanio yao, na kwa kuacha kumwabudu Mwenyezi Mungu na kufanya mambo maovu.

Kizazi cha Nabii Nuh (as) kikagawanyika kati ya waumini ambao walikuwa katika kizazi cha Sam na ndicho kizazi kilichotoa mitume na mawasii, na wengine makafiri ambao walikuwa kizazi cha Hami na Kanaan na wengineo.

Mambo yakaendelea vivyo hivyo huku Mwenyezi Mungu akipeleka manabii katika baadhi ya vijiji. Wengine wakaongoka na wengine wakapotea, wakaangamizwa na kuadhibiwa.

Hatimaye, Mwenyezi Mungu akampeleka Mtume Mtukufu Ibrahim (as) kwa watu wote. Nabii Ibrahim (as) akawalingania watu wamwabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake, akayavunja masanamu na akaamrisha mema na kukataza maovu.

Katika zama zake alikuwepo mfalme dhalimu akijulikana kwa jina la Namrud bin Kanaan ambaye alimiliki nchi akaueneza ufalme wake kwa vitimbi na hadaa. Namrud alikuwa na waziri aitwaye Azar ambaye alikuwa mnajimu na kuhani na mwenye hadhi kubwa sana mbele ya mfalme.

Katika unajimu wake akaona kuwa atatokeza mtu mkubwa ambaye atauangusha ufalme na kuleta dini mpya. Akampasha mfalme habari hiyo, naye mfalme akafadhaika. Kisha Azar akamwambia kuwa bado hajazaliwa mtu huyo. Mfalme akaogopa kidogo na akasema: "Tutawatenga wanawake na waume zao ili asizaliwe huyu mtoto, na wale wenye mimba tutawaangalia atakayezaa mtoto wa kiume tutamwua." Kisha mfalme akauliza: "Atazaliwa wapi motto huyo?" Azar akamjibu: "Katika mji huuhuu."

Namrud akatoa amri. Watumishi wake wakaanza ufisadi wao katika mji kwa kuwadhalilisha watu, kumtenganisha mtu na mkewe, kuwaua watoto wa kiume na kuwasaliza wanawake. Hali hiyo ikaendelea na huku mji ukiwa umejaa misukosuko na vikwazo.

Naam. Namrud alitaka hivyo na Mwenyezi Mungu akataka vingine. Namrud akajaribu kufanya dawa aliyoitaka kwa kutumia uwezo wake na nguvu yake, lakini uwezo wa ghaibu (usioonekana) ukapitisha lile lililolitaka. Kwa hivyo, uwezo wa Namrud ukashindwa, na akazaliwa Ibrahim kwa kificho katika pango la jabali. Ibrahim akakua haraka haraka mpaka akawa kijana. Baada ya kufariki baba yake muumini, Tarikh, akalelewa na ami yake kafiri, Azar, aliyekuwa waziri wa mfalme. Ibrahim akawa anaishi katika kitovu cha ukafiri, makao ya nguvu za kidhalimu, chimbuko la uovu wote na shimo la uchafu na maradhi yote, katika nyumba ya ami yake ambaye alikuwa na uwezo na sauti katika mji.

Azar alimpenda sana Ibrahim kuliko watoto wake aliowazaa, kwa vile alivyoona utukufu wake ushujaa, tabia nzuri, ukweli na vitendo safi.

Azar alikuwa akitengeneza masanamu katika jumba la mfalme na yanapokuwa mengi huwapa watoto wake wakauze barabarani na wachukue faida inayopatikana katika biashara hiyo.

Ibrahim alipokua, Azar akamtaka ashiriki katika kuuza masanamu ili apate fedha za kuongezea matumizi yake ya maisha. Ibrahim ambayo moyo wake haujawahi kuingia doa la ukafiri wala kuingia shaka, akapata fursa ya kutekeleza ujumbe wake mzito, wakati ambapo mji ulikuwa umejaa dhuluma, wafuasi madhalimu na makafiri wenye kuitakidi nguvu ya mfalme jabari.

Kwa sababu hii, Nabii Ibrahim (as) akaanza kuwazindua watu na kutoa wito kabla ya kumkabili mfalme.

Akaanza kuyafunga kamba za shingoni yale masanamu na kuyaburura huku akiwalingania watu akisema: "Ni nani anayetaka kununua kitu kisichofaa wala kunufaisha?" Kisha anayatosa katika maji machafu kwa ajili ya kuyadharau na kuwafahamisha watu kuwa hayana uwezo wowote.

Hiyo ndiyo hatua ya kwanza aliyoifanya kwa miungu ya uwongo na lilikuwa pigo la nguvu lililowapofusha wenye kughafilika. Kisha akawa anafikiria viumbe wale waliodanganywa na matamanio yao wakaabudu asiyekuwa Mungu. Baadhi yao wakiabudu masanamu ya kuchonga na wengine wakielekea kwenye sayari kama vile Zuhura, mwezi au jua wakiviabudu na kuviomba msaada.

Nabii Ibrahim (as) akawa anawahoji kwa hoja za kiakili kwa kuithibitisha haki, kuibatilisha batili na kuwaongoza watu kwenye njia iliyonyooka. Akawa nao mpaka ilipotokeza Zuhura. akapiga kelele akisema: "Huyu ndiye mola wangu!" Akangoja mpaka ilipotua, akasema:
"Sipendi wanaopotea." Kisha alipoangalia mbinguni akaona mwezi umetokeza upande wa mashariki kama mashua ya fedha inayotembea katika bahari ya nuru. Akasema: "Huyu ndiye mola wangu. Huyu ni mkubwa." Alisema haya kulinganisha ukubwa na nguvu ili kudhihirisha ujinga wao. Mwezi ulipotua na kupotea, akasema:

"Asiponiongoza Mola wangu, bila shake nitakuwa miongoni mwa watu wapotevu."

Zikapita saa, mara akaona jua linachomoza. Akasema. "Huyu ndiye mola wangu. Huyu mkubwa zaidi." Akakaa pamoja na wale wajinga wanaoabudu jua, akasubiri mpaka lilipotua jua akasema: 'Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayoyashirikisha. Kwa hakika, mimi nimeuelekeza uso wangu kwa Yule aliyeziumba mbingu na ardhi, kwa kujihalisisha. Mimi si miongoni mwa washirikina." (6:77-79)

Kwa njia hii hoja zake zilishinda na ikatoweka batili ya watu wake na upotevu wao. Nabii Ibrahim (as) akashinda katika vita vya kifikra na akawashinda washirikina.

Nabii Ibrahim (as) hakutosheka na hatua hizi mbili katika kuwaongoza watu kwenye njia ya haki, bali alifikiria njia nyingine itakayovunja ibada ya masanamu na itakayowapeleka watu kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu. Mfalme alizizuia fikra za watu zisipanuke na badala yake akizifanya finyu.

Hivyo, huwa ni vigumu kuleta mapinduzi hasa ya kiitikadi na kiibada kwa jamii hiyo. Nabii Ibrahim (as) alingojea muda mrefu mpaka ilipofika siku ya sikukuu ya washirikina, wakatoka kwenda jangwani wakicheza na kusherehekea, na kuziacha tupu nyumba zao.

Namrud pamoja na watu wake wakaelekea jangwani. Watu wakamjia Nabii Ibrahim (as) na wakamtaka aende nao kwenye sikukuu yao, lakini akakataa kwa kujitia ni mgonjwa.

Mji ulipobaki mtupu, akaanza mbinu yake. Akaenda katika nyumba yao ya ibada yenye miungu iliyoganda isiyoona chochote wala kujua lolote akiwa amechukua sururu. Alipofikia kwenye jiwe lililochongwa ambalo linahukumu mimea na roho, akasimama mbele yake. Akaliwekea kila sanamu chakula na kuliambia: "Kula na useme!" Akalipiga kila sanamu kwa sururu na kulivunja vipandevipande. Akafanya hivyo moja baada ya jingine mpaka likabaki sanamu kubwa ambalo akaliwekea sururu kwenye shingo yake. Kisha akarudi akisubiri mambo yatakavyokuwa.

Mfalme aliporudi na watu wake, mara wakaona masanamu yamevunjikavunjika, siyo katika hali waliyoyaacha. Wakasema: "Ni nani aliyeifanyia hivi miungu yetu?" Baadhi yao wakasema:

"Tumemsikia kijana mmoja akiwataja waungu wetu kwa ubaya. Jina lake ni Ibrahim."

Wakamleta Nabii Ibrahim (as) katika hadhara ya watu. Namrud akamwuliza: "Ni nani aliyewafanyia hivi miungu wetu?'' Nabii Ibrahim (as) akajibu huku akiwachezea shere na moyo wake ukiwa imara. "Aliyefanya hivyo ni huyo mkubwa wao." Akaashiria lile sanamu kubwa alilolitundikia sururu shingoni mwake. Akasema "Mwulizeni ikiwa anaweza kutamka." Tamko hili likatoa cheche za moto zilizochoma batili na kumwangazia mtu mwangaza na kumwelekeza kwenye akili yake na umbile lake aliloumbwa. Qur’an inasema:

“Basi wakajirudi nafsi zao na wakasema ‘Hakika nyinyi mlikuwa madhalimu.’ Kisha wakainamisha vichwa vyao, (wakasema:)”Hakika umekwishajua kwamba hawa hawasemi.’ Akasema: Je, mnaabudu badala ya Mwenyezi Mungu (miungu) isiyokufaeni chochote wala kukudhuru? Kefule yenu na hivyo mnavyoviabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu. Je, hamfikiri?’ Wakasema: ‘Mteketezeni kwa moto na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo.’” (21:64-68)

Washirikina wakakoka moto waliokusanyia kuni kwa muda mrefu. Wakafikiria kuwa hiyo ni adhabu yake na iwe ni fundisho kwa yule atakayefuata njia nyingine isiyokuwa ya mfalme. Mvuke wa moto ilikuwa mkali kwa kadiri kwamba ungeweza kumchoma ndege aliyepita juu umbali wa farsakh moja yaani kilometa nane.

Namrud akakaa juu ya jumba lake kubwa. Nabii Ibrahim (as) akaletwa mbele ya watu. Wakafikiria namna ya kumtupa motoni kwa vile hawakuweza kuukaribia moto kutokana na ukali wake. Kwa kufuata maelekezo ya Iblisi, wakatengeneza panda kubwa na wakamweka juu yake. Nabii Ibrahim (as) akakaa imara, hakusikitika wala hakujuta kwa aliyoyafanya, bali lilimfurahisha hilo kwa kuyakinisha kuwa hiyo ndiyo njia ya pekee ya kutekeleza lengo lake.

Azar, ami yake, akaja na kumkuta Nabii Ibrahim (as) amewekwa kwenye panda bila ya kuwa na wasiwasi wowote. Akampiga makofi na kumwambia: "Wacha mambo yako hayo." Nabii Ibrahim (as) akakataa kuuacha msimamo wake wa haki.

Panda ikavutwa na Nabii Mtukufu akarushwa katika moto. Malaika akamija na kumwuliza kama anataka haja yoyote kwake. Akasema:
"Ninaye Mola Ambaye hivi sasa anajua hali yangu."

Alipoukaribia moto, Mwenyezi Mungu aliuambia: "Ewe moto kuwa baridi na salama juu ya Ibrahim." (21:69)

Mara moto ukageuka kuwa bustani kijani na Nabii Ibrahim (as) akiwa amekaa kwenye kitandiko akizungumza na Jibril (as).

Namrud akawa anaangalia mandhari ile kwa mbali. Akapata mfadhaiko kwa kushindwa kwa vitendo vyake, akawa anasema. "Mwenye kutaka kujichukulia Mola na achukue mfano wa Ibrahim."

Nabii Ibrahim (as) akatoka motoni na Namrud akawa hana la kusema. Lakini hata hivyo aliendelea na ukafiri wake na kumfukuza Nabii Ibrahim (as). Nabii Ibrahim (as) akayakabili yote hayo kwa moyo imara na thabiti, na hakuacha kusema kuwa Namrud alikuwa kwenye upotofu na kwamba yeye na watu wake wamechukiwa na Mola Mtukufu.

Huu ni muhtasari wa historia ya maisha ya Nabi Ibrahim (as) ambayo imejaa jihadi.

4. Nabii Musa (as)

Karne baada karne zikapita, kizazi baada ya kizazi vikazaliwa, ulimwengu ukaharibika na kurekebika, na watu wengine wakaamini na wengine wakakufuru. Mwenyezi Mungu akawatuma Mitume mmoja baada ya mwingine, na umma ukaendelea na ukafiri na kumkataa Mungu isipokuwa wachache tu. Dola ya Qibtiya ndiyo ikawa yenye maendeleo katika historia ya binadamu. Katika Misri walikuwepo wafalme waliokuwa wakiitwa mafirauni ambao walitawala watu na kumiliki miji na kukawa na ufisadi mwingi.

Alikuwepo Firauni mmoja, jina lake Walid bin Musawab ambaye aliwatawala watu na akadai kwamba ni mungu. Alikuwa akiwafanyia watu vile alivyotaka kwa madai kwamba yeye ndiye aliyewaumba, aliyewaruzuku na kuwamiliki.

Katika dola hiyo ya Qibtiya, kulikuwepo kundi moja la Wana wa Israili (Bani Israil) waliobaki Misri ambao ni wana wa Nabii Ya’qub. Walikuwa ni watu wanyonge, jeshi lao halikuwa na nguvu na walikuwa wakipingana na mafirauni.

Mafirauni walikuwa wakiwakandamiza kufanya kazi ngumu na kuwalipa malipo madogo au kuwapa kazi duni; na walikuwa wakiwachukulia kama ni wanyama walioumbwa kwa ajili yao.

Wana wa Israil walikuwa wakingojea kutimia ahadi ambayo ilikuwa ikipokewa kutoka kizazi baada ya kingine kwamba angedhihiri baina yao mtu mmoja ambaye atapambana na Firauni na kumshinda. Kila wakati ulivyozidi kupita ndivyo walivyoendelea kumngoja kwa hamu.

Kwa muda mrefu wakamngoja, lakini ahadi yao haikutimia mpaka wakakaribia kukata tamaa. Utawala wa Qibtiya ukazidisha dhuluma ya kinyama kwa kuwachinja watoto wao wa kiume na kuwabakiza watoto wa kike, ili watakapokua wawafanye vijakazi na watumishi wao.

Hatimaye, Mwenyezi Mungu akampeleka Nabii Musa (as) kuwa Mtume wao. Kuzaliwa kwake kulikuwa ni kwa kificho na matatizo kama kuzaliwa kwa Nabii Ibrahim (as). Musa akakua katika malezi ya Firauni na akafanywa kama mtoto wake kwa vile hakuwa na mtoto atakayerithi kiti chake. Akawa anaitwa Musa bin Firauni na alikuwa akitembea katika jumba la mfalme vile alivyopenda.

Siku moja Mwisraili moja aligombana na Mqibti mmoja. Musa akamsaidia Mwisraili na akampiga ngumi Mqibti ambaye akaanguka chini na kufa.

Mkasa huo ukawashtua Waqibti, wakawa wanataka fidia kwa mtu wao. Waliwatilia shaka Wana wa Israili, lakini hawakumjua aliyeua, na wakawa wakimtafuta huku na huko.

Kesho yake, Musa alipokuwa akitembea njiani akamwona yule Mwisraili aliyemsaidia akigombana na Mqibti mwingine. Musa akataka kumsaidia yule Mwisraili, akamkaribia ili amshike Mqibti. Yule Mwisraili akadhania kuwa Musa anataka kumshika yeye. Akapiga kelele huku watu wakimsikia akisema: "Unataka kuniua, ewe Musa kama ulivyoua jana." Watu wakajua kwamba Musa ndiye aliyeua.

Firauni akajua kuwa kijana aliyemlea amekuwa adui wake sasa, kwa sababu ameungana na jamaa zake Waisraili kwa kuwasaidia na kutumia nguvu zake kwa ajili ya wanyonge.

Kwa hivyo, Firauni akakasirika na akawa anahofia ufalme wake. Akaamrisha auawe. Ili kuiokoa nafsi yake, Musa akakimbia kutoka Misri kuelekea Madain ambapo hapakuwa chini ya mamlaka ya Firauni. Akakaa huko na akaoa binti ya Nabii Shuayb (as).

Baada ya hapo, Musa akaamua kurudi Misri. Alipofika Mlima Sinai, Mwenyezi Mungu akamtuma na ujumbe wa dini mpya. Akampa azma, uthabiti na miujiza, na akampa ndugu yake Harun kuwa msaidizi wake.

Wakenda kwenye baraza la Firauni, mtawala taghuti, hali ya kuwa wao ni wanyonge wasiokuwa na kitu. Wakataka kumzungumzia mambo aliyoyachukia kwamba aikufurishe nafsi yake na amwamini Mungu, aondoe madai yake ya uwongo ya uungu na amwabudu Mungu Aliye Mmoja. Manabii Musa na Harun (as) walitaka kufanya jihadi hiyo bila ya kuwa na jeshi, mali au msaada wowote isipokuwa walimtegemea Mwenyezi Mungu tu.

Nabii Musa (as) akaanza kusema: "Mimi ni Mjumbe wa Mola wa viumbe vyote." Firauni akasema:

"Basi lete muujiza ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli." (7:104-106)

Akatupa fimbo yake iliyokuwa na ncha mbili, mara ikageuka nyoka. Firauni akaiangalia akaona inatoa ndimi za moto. Akaogopa na kuanza kupiga kelele: "Ewe Musa! Ichukue." Akaichukua na ikageuka fimbo. Firauni akarudi kwenye upotevu wake, akasema: "Hakika hawa wawili ni wachawi." Akataka shauri la watu wake na wasaidizi wake jinsi ya kufanya na hali wamekuja na hoja na dalili za ushindi.

Wakamshauri wamfunge Nabii Musa (as) pamoja na nduguye, kisha wawakusanye wachawi watakaoshindana kwa uchawi na watamshinda, na ndipo itakapokuwa rahisi kuwahukumu. Firauni akawafiki rai hiyo. Wahubiri wawili watukufu wakafungwa pamoja na wachawi wengine wa Kiisraili.

Akatuma katika miji na vitongoji aletwe kila mchawi na kila anayejifundisha uchawi katika vijana wa Kiisraili.

Wachawi na watu wengi wakakusanyika katika siku ya sikukuu. Wakaja ili washangilie ushindi wa wachawi na wawafanyie vitimbi Nabii Musa (as) na Nabii Harun (as) pamoja na watu wao na wathibitishe ibada ya Firauni na watu wake.

Wachawi wakatupa kamba na fimbo zao na zikageuka nyoka wakizunguka huku na huko. Ukawa ni uchawi mkubwa uliowapumbaza watu. Wakawafuata wachawi na hadhi kubwa.

Nabii Musa (as) akatupa fimbo yake, mara ikegeuka nyoka anayokwenda mbiombio, akawameza nyoka wao wote na kuwaogopesha wachawi, Firauni na Hamana, na huku wafuasi wao wakiwa wanashuhudia.

Watu wakaanza kukimbia kiasi ambacho walikuwa wengi kutokana na msongamano wa kukimbizana. Firauni akaanguka na kuzirai. Kisha Nabii Musa (as) akamchukua nyoka na akarudia kuwa fimbo kama kwanza. Fimbo na kamba zilizokuwa nyoka mbele ya watu zote zikamezwa kama vile hakukuwako na kitu chochote.

Wachawi wakashindwa na wakasujudu na kusema: Tumemwamini Mola wa Harun na Musa.” Wachawi na Wana wa Israili wote pamoja na kikundi cha Waqibta wakamwamini Nabii Musa (as). Lakini Firauni ambaye hakutaka haki wala mwangaza alibaki katika batili na giza.

Firauni akaona kwamba batili inategemea nguvu isiyokuwa na hoja yoyote wala dalili yoyote, hivyo akaamua kuwaadhibu wachawi. Akawaambia: “Kwa nini mmemwamini kabla sijawapa idhini? Hakika huyo ni mkubwa wenu ambaye amewafundisha.” Kisha akawatesa vibaya kwa kuikata mikono na miguu yao na akawasulubu kwenye shina la mtende. Akawafanya kuwa ni mazingatio na ono kwa anayefikiria kuipinga itikadi ya Firauni au atakayedhihirisha kumfuata Manabii Musa na Harun (as).

Firauni mkatili alikuwa akimwadhibu kila aliyemwamini Nabii Musa na nduguye. Mateso yote hayo hayakupunguza kitu katika azma ya Nabii Musa (as) wala hayakudhoofisha nguvu ya matakwa, ukakamavu na uthibiti wake, bali akaendelea kutangaza upinzani wake dhidi ya Firauni kwa uwazi kabisa, kuongoza kundi lililomwamini kwenye kheri na kuwakinga kiasi alivyoweza na kumtaka Firauni kuwaachia wafungwa wao.

Ingawa Firauni na waziri wake Hamana na askari wao waliendelea na ukafiri na upinzani wao dhidi ya Nabii Musa (as), lakini pamoja na yote hayo Nabii Musa (as) alibaki katika matumaini yake ya kuwaongoza watu wake kwenye haki. Akaendelea kuwalingania katika imani kwa amri ya Mwenyezi Mungu na akawadhihirishia miujiza ya damu, chawa, nzige, tufani, vyura na mengineyo, lakini halikumzidishia hilo Firauni isipokuwa upinzani na ukafiri.

Nabii Musa (as) akapigana jihadi dhidi ya Firauni na watu wake mpaka Mwenyezi Mungu akawaangamiza katika Mto Naili. Baada ya hapo akapigana na Wana wa Israili waasi ambao upinzani wao dhidi ya haki unaendelea hadi hivi leo.

5. Nabii Isa bin Maryam (as)

Ni utukufu usiokuwa na mpaka ambao lau tungetaka kuuelezea kwa matamko tusingefaulu.

Ni mapinduzi yenye kudumu ambayo hayalinganishwi na mapinduzi ya nchi yoyote au maendeleo yoyote, bali ni mapinduzi yaliyo kusanya itikadi, amali (harakati) na haki.

Huo ni utukufu tunaouona katika maisha ya Nabii Isa bin Maryam (as) (Yesu Kristo) aliyefanya mapinduzi ya vikwazo vyote na ufisadi, na akaendeleza jihadi katika uhai wake na akaendeleza vita vya damu mpaka akashinda na ukathibiti ushindi mpaka Siku ya Kiyama.

Maryam binti Imran (as) alikuwa bibi mwema na mwenye utukufu ambaye alikuwa mfano katika historia ya wanawake. Mama yake aliweka nadhiri kumweka wakfu aliyemo tumboni mwake ili kuitumikia dini. Alipomzaa Maryam (as), akasema: "Mola wangu nimemzaa mwanamke!"

Kisha akamweka katika nyumba takatifu (Baytul Muqaddas); na Maryam (as) akawa akisali, akifunga na kuabudu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, akiwa mbali na watu.

Maryam (as) akabaki katika mihrabu kwa muda wa miaka kadhaa katika malezi ya Nabii Zakariya (as). Kisha akachukuwa mimba kwa idhini ya Mwenyezi Mungu bila ya kuguswa na mwanamume yeyote, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoweza kuumba kiumbe bila ya kutanguliwa na kitu chochote au mfano wowote.

Ulipomjia uchungu wa kuzaa, akajitenga na jamaa zake, akaenda mahali upande wa mashariki mwa msikiti penye shina la mtende ambapo akamzaa Masihi ambaye alikuwa mfano bora na msimamo wa kiutu. Kisha akarudi kwa jamaa zake akiwa amembeba. Jamaa zake wakamfokea Maryam: "Umemtoa wapi huyu? Baba yako hakuwa mtu mbaya wala mama yako hakuwa mzinifu!" Akawaashiria mtoto aliyezaliwa, wakasema: "Tutazungumza vipi na mtoto mchanga aliye kitandani?"

Walikuwa wakimdhania dhana mbaya bibi huyu mtakatifu, naye akawa hasemi kwa kutekeleza saumu yake ya kutozungumza. Mara mtoto akaanza kuzungumza, akisema: "Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, amenipa kitabu na amenifanya Mtume." Nabii Isa (as) akaziba midomo yao.

Masihi Isa (as) akakua na akawalingania watu kwa sala na saumu na kuwa na tabia nzuri na kuiacha dunia na kuifuata Akhera ambayo ni maisha bora yenye kudumu. Watu wakawa wanampinga kama ilivyokuwa kwa Mitume wengine.

Masihi Isa (as) alikuwa imara kuwaongoza wafuasi wake. Wakawa wanasafiri mashariki na magharibi wakiwahubiria watu na kuwalingania kusimama dhidi ya wafalme na ujeuri wao, ambao walikuwa wamezama katika matamanio ya kidunia.

Hakika adhabu kali wanayoipata Mitume kutoka kwa makafiri inatokana na ukosefu wa imani ya watu wao na kuendelea kwao na upinzani juu ya kuwa Mitume wao walikuwa wakiwaonyesha dalili na ushahidi waziwazi.

Nabii Isa (as) alidhihirisha miujiza yake kwa kuwaponesha vipofu na wenye ukoma na kuwafufua watu wakawa wakitoka makaburini mwao wakisema na kujua mambo. Habari hizo zikaenea kwa watu wengi na wakawa wanawapeleka wagonjwa kwake. Kipofu mmoja alikuwa haoni tangu kuzaliwa kwake, Nabii Isa (as) anampangusa kwa mkono wake mtukufu mara anaanza kuona. Wagonjwa ambao waganga walishindwa kuwatibu waliletwa kwake, naye akawaponesha bila ya dawa yoyote. Mtu mmoja alifiwa na mpenzi wake, akamwendea Nabii Isa (as), naye akamfufua kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Akamfanya ndege kutokana na udongo, na miujiza mingine kadhaa. Lakini pamoja na miujiza yote hiyo, makafiri waliendelea kumwudhi, kumtukana na kumtoa maanani. Mara nyingine walimtuhumu na kumpiga magumi pamoja na kuwaudhi wafuasi na wasaidizi wake.
Wakaendelea na upinzani huo mpaka wakafikiria kumwua kwa kudhani kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuizima nuru ya haki. Njama yao ya kumwua ikashindwa, na Mwenyezi Mungu akampaza na wakamwua mtu aliyefananishwa na Nabii Isa (as).

Muhtasari Wa Visa vya Jihadi

1. Mwenyezi Mungu alimtuma Nabii Salih (as) akiwa na umri wa miaka 16. Alibaki miongoni mwa watu wake kwa muda wa miaka 120, lakini hawakuitika mwito wake. Hakika yeye aliwalingania watu wake kwa miaka 104.

2. Nabii Ibrahim (as) alikuwa peke yake kuulingania umma kumpwekesha Mwenyezi Mungu wakati giza lilipotanda katika historia ya ulimwengu, na alibaki miongoni mwa watu wake miaka kadhaa, lakini hakuna mtu yeyote aliyemwamini.

3. Nabii Lut (as) alitumwa Madain katika ardhi ya Sham. Akawahubiria watu, lakini hakukuwazidisha chochote isipokuwa ukafiri na ukanaji; hata mkewe ambaye alikuwa mshiriki katika maisha yake, alikuwa akishirikiana na makafiri.

4. Nabii Yusuf bin Ya'qub (as) alipigana jihadi na nafsi kama mwamba mbele ya bahari. Alizungukwa na matatizo katika maisha yake yote akiwa ndani ya kisima, pamoja na msafara, katika nyumba ya Aziz, katika jela na mbele ya mfalme. Alipokuwa kifungoni alimwomba Mwenyezi Mungu pekee bila kujali kuwa alikuwa mfungwa aliye mbali na kwao.

5. Nabii Ayyub (as) alipewa mtihani na Mola wake kwa kuisha mali yake, kufiwa na watoto wake na kupata maradhi katika viungo vyake vyote isipokuwa akili tu! Iblisi akawahadaa watu wake, wakamfukuza na kumweka mbali na mji. Akashukuru na kusubiri mpaka kapona.

6. Mwenyezi Mungu alimtuma Nabii Shuayb (as). Wakamkanusha na wakaukanusha Utume wake: wakamfukuza katika mji na wakawaua wasaidizi wake. Akawalingania tu mpaka ikawakuta adhabu.

7. Nabii Khidhr (as) alikimbia kutoka nyumbani mwa baba yake ambaye alikuwa mfalme. Akaukimbia ufalme akaenda kumwabudu Mwenyezi Mungu na kuwalingania watu kumwabudu Yeye tu.

8. Nabii Daniel (as) alibaki katika shimo la kisima miaka kadhaa akinywa maji yake na kunywa maziwa ya simba ambaye alitiwa ndani pamoja naye. Chakula choa kilikuwa udongo wa kisima.

9. Nabii Yunus bin Mata (as) alitumwa kwa watu wake akiwa na umri wa miaka 30 akawa anawalingania kwenye imani kwa muda wa miaka 33. Hawakumwamini isipokuwa watu wawili tu!

10. Mwenyezi Mungu akamtuma Mtume wa Kihabeshi (Kiethiopia) ambaye aliwalingania watu wake kwa Mwenyezi Mungu, lakini wakamkadhibisha, wakampiga vita na wakamchimbia handaki na kumchoma humo pamoja na wafuasi wake.

Mpaka hapa tunamaliza muhtasari huu wa historia ya Mitume na Manabii mashujaa, na masaibu waliyoyapata katika njia yao ya mashaka kuelekea kwenye uongofu.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa taufiki na tunamwomba atufanikishe kufuata njia ya Mitume na kuongoka kwa mwendo wao. Hakika Yeye Ndiye Mwenye kutoa taufiki.

Muhammad Taqi al-Mudarrisi
Karbala - Iraq
1385/6 Hijria
1965 Miladia

Kwa jina ya Allah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

1. Hakika waumini wote ni ndugu.
2. Jumuia ya Udugu wa Kiislamu ni taasisi ya utamaduni yenye malengo yafuatayo:

a) Kueneza fikra na utamaduni wa Kiislamu kwa mapana zaidi.
b) Kustawisha mfungamano wa kindugu na mapenzi kati ya Waislamu.
c) Kusaidiana na taasisi na jumuia zote za Kiislamu na za kibinadamu.
d) Kutoa mchango katika kutatua matatizo ya Kiislamu ili kuusaidia Umma wa leo na kutoa maoni halisi ya Kiislamu.

Kwa hivyo, tunawaomba ndugu wote wa Kiislamu wana wa Umma huu, kusaidiana na kushirikiana nasi katika kutekeleza malengo hayo matukufu.

Mnaweza kutuandikia kwa anwani hii:

Maktab As-Sayyid Almudarrisi
P.O Box 14155-5717
Tehran
Islamic Republic of Iran