read

Uharamisho Wa Kamari Katika Islam
Makala haya yamekusanywa na kutarjumiwa na:
Amiraly M.H. Datoo (PO Box 838 Bukoba, Tanzania)

Kitabu hiki kinazungumzia uharamisho wa kamari katika Islam kwa kuangalia Quran na hadith. Pia kinaongelea sababu za kamari kuharamishwa katika Islam na athari zake kwenye maisha ya mwanadamu na jamii kwa ujumla.

Maneno Mawili

Ninamshukuru Allah swt pamoja na Mtume Mtukufu s.a.w.w. na Ahli - Bayt Toharifu a.s. kwa kunijaalia neema hii ya kuweza kukitarjumu kijitabu hiki juu ya maudhui haya ya kamari ili kuweza kuwafaidisha wanaadamu wenzetu ili nao waweze kujiokoa na janga hili kubwa linaloangamiza watu pamoja na famili zao zikiteseka kizazi baada ya kizazi.

Mimi binafsi nimewaona wajukuu ambao mpaka leo wanateseka kwa ajili ya madhambi ya mababu zao. Vile vile hapa mjini kwetu nilikuta watu wenye mapesa wakiongoza katika makundi yao ya kucheza kamari kwa mapesa, yaani Waislamu ndio waliokuwa wakiendesha madanguro hayo. Kwa hakika nilijaribu kutoa makala juu ya uharamisho wa kamari, lakini niliyokumbana nayo yananitosha,na wala sina haja kuyaelezea hapa. Ndipo hapo nilipoona umuhimu wa kukitayarisha kijitabu hiki juu ya uovu wa kamari.

Makusudi yangu ni kutaka kuwasaidia na kuwaelimisha watu juu ya uovu huo wa kamari.

Ni mategemeo yangu kuwa maudhui haya yatatufaidisha na kutuongoza katika njia njema yenye kujenga maisha yetu na ya jamii nzima kwa ujumla.

Amiraly M.H.Datoo
P.O.Box 838
Bukoba - Tanzania
2 Septemba 1995

*********************************

Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema:-

"Katika hivyo mna madhara makubwa na (baadhi ya) manufaakwa (baadhi ya) watu.Lakini madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake." (Al-Baqarah 2:219)

Kamari ni mojawapo ya starehe iliyo hatari mno ambayo imekuwapo miongoni mwa watu katika karne nyingi zilizopita na ambayo imezaa maovu mengi mno katika jamii ya wanaadamu

Katika zama zetu hizi pia,kamari imeshamiri mno kiasi kwamba inatumiwa na watu kwa kisingizio cha kutuliza moyo na kufurahisha roho na huku kikiwa ni kiangamizo kikubwa mno katika zama hizi hata kuliko hapo kabla. Na jamii yetu hii imeangamizwa na kuwindwa na starehe hizi zenye maangamizo.

Katika baadhi za nchi,kamari na vyombo vyake vinatumiwa katika uchumi wao kwani wanatengeza vyombo hivyo kwa ajili ya kuviuza au kuendesha shughuli hizo au wanafaidika kwa kutoza kodi kubwa, na ndiyo maana wamevipatia umuhimu mkubwa mno.Kwa hivyo,tabaka nyingi wanajipatia mapato na uchumi wao kwa mambo hayo na papo hapo kuzipatia serikali zao mapato makubwa.

Katika baadhi ya nchi la Ulaya na Marekani kumezuka idara kubwa kubwa za kuchezea kamari. Matajiri wakubwa wakubwa kutoka sehemu zote za ulimwenguni wapo wanavutiwa kwenda huko kucheza kamari. Hivyo wenye kumiliki Idara hizo,wanavyo vipato vikubwa mno kupita kiasi na humo sehemu fulani huwa inakwenda katika hazina ya serikali zao.

Ubovu wa kamari kiuchumi umekuwa umetahadharishwa na wanakanuni wa Kiislamu kiasi cha miaka elfu moja mia nne (1400) iliyopita na vile vile imetahadharishwa katika Qurani Tukufu. Lakini kwa kuwa madhara yake ni mengi mno kuliko faida zake, ndiyo sababu iliyoifanya ikaharamishwa ili Waislamu wasije wakadanganyika kwa faida chache za vitu, huku wakaangamia na kupoteza mali yao yote na hata kujipatia hasara ya kiroho.

Serikali zote zinaelewa vyema kabisa maovu yote yanayotokana na michezo ya kamari (pata - potea) lakini haziko tayari kukabiliana na hatari ya kukosa kipato kinachotokana na michezo hiyo na hivyo kamwe hawataweza kufanya jitihada za kukomesha michezo hiyo.

Huko Uingereza, katika mwaka 1853 kulikatazwa kamari, lakini pamoja na hayo, bado kulikuwapo majumba makubwa kumi na nane ya kuchezea kamari kwa ajili ya matajiri. Huko Marekani, mwaka 1855 na Ujerumani mwaka 1882 pia kulikatazwa michezo ya kamari ambapo kanuni za Islamu uharamisho wa kucheza michezo yote ya kamari umekuwepo miaka maelfu kabla ya nchi hizo kutoa hukumu kama hizo.

Kwa hivi sasa, huko Marekani na Ulaya, yapo majumba makubwa ya kudumu ya kuchezea kamari ambapo usiku na mchana maelfu ya watu watokao mbali na karibu hufika pamoja na masanduku yaliyojaa dola za Kimarekani kwa ajili ya kucheza kamari - michezo ya pata potea.

Gazeti moja linaandika juu ya Los Vegas ambapo ndipo makazi maarufu kwa kamari kuwa:

"Wale wanakamari wanakuja huku, idadi yao haijulikani kwa usahihi, lakini inakadiriwa wanakamari zaidi ya elfu arobaini huwapo usiku na mchana. Katika makazi hayo ya kamari hapachezwi na mtu mmoja, bali ni maelfu ya watu wanaocheza kamari za aina nyingi............"

Katika mjihuu ipo hotel moja kubwa maarufu ijulikanayo kama 'Sahra Hotel.' Humo kuna jukwaa moja mahsusi la kuchezea kamari ambamo kuna vyombo vya kutumia umeme kwa ajili ya kamari ambavyo vimekuwa vimezungukwa na matajiri wenye kuchezea mamilioni ya dola. Katika vyombo hivyo huwapo vijihela fulani ambavyo hununuliwa kwa thamani ya dola kutika kwa wahusika wa hapo, na huvitumbukiza ndani ya mashine kwa kutegemea kupata mamia au maelfu ya dola na kwa kutumia nguvu zote huisukuma kwa mbele usukani wake. Na kwa kuwa mtu huwa hana hisia za kuishiwa na dola zake, huendelea kwa vishindo katika michezo hiyo.

Ni dhahiri kuwa wenye kuyamiliki majumba hayo ya kamari wanapata faida kubwa, hivyo daima wao watapinga hatua zote za kutaka kuyafunga majumba hayo ya uovu. Nao wapo tayari kuwaangamiza na vile vile kuwatia mahabusu wale wote wanaofanya harakati za kutaka kuwafahamisha na kuwaonya watu juu ya ubaya wa kamarina michezo yote inayohusiana nayo. Kwa kweli hawa watu ni hatari mno. Ni sawa na wale wafanyao biashara ya mihadarati katika nchi za Latin Amerika ambao huvuruga kila kitu zikiwemo hatua za serikali. Watu hao lazima wajue kuwa wao sio adui zetu bali pia ni adui wa Allah swt pamoja na Mtume Mtukufu s.a.w.w. na ubinadamu kwa ujumla.

Sisi tunayaita majumba hayo kuwa ni makazi ya 'fisq na fujur' kwa sababu katika makazi haya hutokea maovu ya kila aina yenye kuleta maafa makubwa.

Katika magezeti tuyasomayo, huwa tunapatiwa habari kama hizo zenye maafa na maagamizo kama hayo. Habari mojawapo iliyopatikana ni kama ifuatayo hapo chini:

"Monte Carlo-Italia - Mtu mmoja wa Argentina alicheza kamari kwa masaa 19 na kupoteza dola arobaini elfu. Wakati jumba la kamari lilipofungwa, alikwenda zake msituni na kujiua kwa kukipasua kichwa chake, amejiangamiza na kupoteza maisha yake........."

Idara mojawapo ya Gaylep juu ya maafa yatokanayo na michezo ya kamari, imeeleza kuwa idadi imekuwa ikiongezeka katika mauaji ya kujiua wenyewe wanakamari. Katika mwaka 1961 idadi ya wacheza kujiua ilizidi. Idara mojawapo ya Marekani imeeleza kuwa mcheza kamari mmoja huwa ameshiriki asilimia thelathini (30%) ya makosa.

Daktari mmoja wa Marekani amefanya uchunguzi kwa miaka kumi na sita, na hatimaye akagundua kuwa katika Marekani peke yake, kila mwaka zaidi ya wanakamari elfu mbili huuawa. Daktari huyu pia amethibitisha kuwa wakati wa kucheza kamari, moyo wa mwanakamari huenda kwa kasi mara mbili yakawaida na baadhi ya wanakamari, hudunda mara mia moja na mara nyingine utamwona mwanakamari akidondoka chini kwa ghafla au huzeeka miaka kumi kabla ya uzee wake au hufariki miaka kumi au kumi na tano kabla ya kifo chake cha kawaida.

Kamari inayo ubaya mmoja mkubwa sana katika mtizamo wa jamii na kinafsi ambao umeweza kuzaa maovu makubwa mno. Ubaya huo ni uadui na kisasi utokeao miongoni mwa watu kwa sababu ya michezo ya namna hiyo.

Kamari huwajazia washiriki mioyo ya bughudha na kisasi. Huangamiza urafiki, mapenzi na udugu. Hufanya mtu awe daima na uchu wa kulipiza kisasi na ghadhabu.

Katika Qurani Tukufu twaambiwa:

"Hakika Sheitani anataka kukitilieni uadui na bughudha baina yenu kwa ajili ya ulevi na kamari.........."(Al-Maidah, 5:91)

Ni dhahiri kuwa mcheza kamari anayeshindwa na kupoteza fedha zake, huhamaki na kughadhabika kwa kumwona mwenzake akitumbukiza fedha hizo zote mfukoni mwake huku akicheka kwa furaha ya ushindi wake. Hivyo hasira na ghadhabu hizo huja wakati mmoja zikatokeza na kusababisha maafa makubwa.

Ni jambo la kawaida kwa mtu kughadhabika kwani fedha hizo alizipata kwa kutokwa na jasho, akizipoteza kwa mtu ambaye ameketi naye bila hata ya kutaabika.

Jambo jingine ni kwamba mcheza kamari anaposhindwa katika michezo yake ya pata-potea huhangaika mno hasa kwa kupoteza usingizi wake na yeye huacha kuzingatia kazi zake azifanyazo na hukalia michezo ya kamari akiwa anadhani kuwa ataweza kushinda dhidi ya mpinzani wake ili aweze kuutuliza moyo wake.

Gazeti mojawapo limeandika:

"Katika mji mmoja, mwanakamari mmoja alimchinja vibaya sana mpinzani wake kwa kisu. Alisema kuwa alimwua mpinzani wake kwa sababu yeye alimlazimisha mpinzani wake aendelee kucheza naye, baada ya kushindwa, lakini mpinzani alikataa kata kata na kuondoka. "Basi mimi nilikasirika na kumfuata hadi niamuua........."

Katika kuuendeleza mchezo wa kamari, mchezaji anaponogewa na mchezo, basi yeye huweza kuviweka vitu vyake vyote alivyonavyo rehani katika mchezo wa kamari, na hata huweza kuipoteza heshima yake kwa kumweka mkewe ashindaniwe katika mchezo wa kamari na vile vile huweza kuiweka nyumba yake au shamba lake. Hatimaye huondoka akiwa amekwisha filisiwa mali yake yote.

Kabla ya kuja kwa Dini ya Islamu na Shariah, watu wa zama za ujahilliyya walikuwa wakicheza kamari za namna mbalimbali. Mcheza kamari alikuwa akitoa fedha zake na milki yake, baadaye alikuwa akitoa nyumba yake na vyote vile alivyokuwa navyo. Alipokuwa akishindwa, alikuwa akimweka mkewe ashindaniwe katika michezo yake na alikuwa akiinuka na kumkabidhi mpinzani wake mkewe kwa fakhari zote.

As Sasiq a.s. ameeleza:

"Makoreishi walikuwa wakiwatumia wake zao na mali zao katika michezo ya pata-potea na kuvishindania. Allah Subahanahu wa Ta'ala aliharamisha michezo hiyo nakuwakataza watu wasicheze michezo ya kamari............."

Inawezekana labda jambo hili watu wengi waliliona ni la ajabu mno baada ya mtu kufikia katika hatua ya kuipoteza heshima yake pamoja na mke wake katika michezo ya kamari. Lakini katika dunia yetu hii yenye maendeleo ya utamaduni, tunaziona nchi zinazodai kuwa ndizo zenye utamaduni na ustaarabu kuliko nyingine ndimo tunamosikia na kuyaona hayo yakitokea.

Kwa mujibu waripoti, tuyaangalie yafuatayo:

"Mexico-French agency-Novemba 25-Mwenye kurekodi Jaa-Orchestra za televisheni ya Mexico, alikuwa mpenda michezo ya pokari na usiku uliotanguliwa aliandaa nyumbani kwake michezo ya kamari na kuwaalika wachezaji mashuhuri. Katika michezo hiyo, alishindea na kupoteza mali yake yote pamoja na nyumba yake hiyo walimokuwa wakichezea kamari. Yeye alikileta kitu kimoja chenye thamani kwake kilichokuwa kimebakia nacho ni mwanamke wake!

Kwa masikitiko makubwa sana, baada ya kushindwa mchezo wa kamari, mke wake alikataa kabisa kuchukuliwa na mtu asiye mume wake.Hapo mume wake alimlazimisha mke huku akimpiga vibaya mno.Kwa sababu ya vipigo alivyopigwa, masikini mwanamke huyo amelazwa katika hospitali. Na hakuna matumaini ya kupona........"

Tendo lolote lile linalomfanya mtu adhalilishwe na kudharauliwa na linaloweza kuzaa maovu na maafa, haliwezi kamwe kukubaliwa kiakili au kimantiki na daima litapingwa.

Kwa kupitia Quran na mtume s.a.w.w. zimeharamishwa aina zote za kamari kwa Waislamu na wanadamu wote kwa ujumla.Vile vile imeharamisha vyombo vitumikavyo kwa kuvitengeneza au kuviuza na kuvinunua. Mapato yatokanayo na kuchezwa kwa michezo ya kamari na pata-potea pia yameharamishwa katika Islamu na kuwakataza Waislamu wasizitumie mali hizo.

Ar-Ridha a.s. amesema kuhusiana na hayo:

"Allah swt ameharamisha aina zote za kamari na kuamuru Waislamu wajiepushe nayo. Amenajisisha kamari na kusema kuwa ni tendo la Sheitani na amewatahadharisha wajiepushe na michezo ya satranj (chess) na miraba mingineyo pia. Kamari na michezo ya miraba na aina nyingine zote zimefanywa kuwa mbaya kabisa hata kuliko mchezo wa satranj (chess)............"

Al-Bakir a.s. amesema:

"Wakati Aya tukufu ya Qurani (al-Maidah: 90) ilipoteremka, basi watu walimuuliza Mtume s.a.w.w. 'maisar' ni kutu gani? (kitu kilicho haramishwa na Allah swt na kukiita tendo la sheitani) alisema kuwa kazi yoyote ile ambamo kamari au kitu chochote kile chenye kushinda au kushindwa, hata kama kutatumiwa alama ya mifupa ya vidole au alama zake katika michezo ya kamari, imeharamishwa."

Islamu imekuwa daima ikitaka kuirekebisha na kuitakasa na hatimaye kuiongoza jamii ya Waislamu katika tabia na hali njema kabisa. Lakini ni jambo la kuhuzunisha sana kuona kuwa maadui wa Islam wameweza kuwahadaa watu wenye ujuzi kidogo katika maovu haya. vile vile ni bahati mbaya kabisa kuona kuwa baadhi yetu wametengeneza na kutayarisha majumba yetu yawe ni mahala pa kuchezea kamari na hata wengine kuyakodisha majumba kwa ajili hiyo.

Michezo ya kamari imekuwa ikipendwa na watu katika hali mbalimbali. Wengine wakiipenda kwa juu juu tu wakati wengine wakiichukulia maanani. Wanaipenda tabia hii mbovu kwa moyo wao. Wanataka kuiga tabia za Magharibi na wanataka kujijumuisha katika utamaduni wao wakidhani kuwa wataweza kuwa maarufu miongoni mwa watu wa Magharibi. Je hawaoni kuwa huko Ulaya na Marekani wao pia nao wanataabika kwa maovu ya kamari na Pombe? Je hawawajui wanaocheza kamari na vile wanavyochinjana, kuiba na kujiua na kufanya maovu ya aina zote yatokeayo kwao? Je si wao wanaendelea kutunga sheria za kuwapinga vijana chini ya miaka kumi na mbili wasiingie katika vilabu vya pombe na kamari?

Gazeti la Teheran litolewalo kila wiki 'Ittilaat' Na 1521 lilieleza juu ya uchezaji wa kamari huko Ulaya ambapo ilisema kuwa "raisi wa wacheza kamari ajiua."

"Tajiri mashuhuri wa Ujerumani na Mfalme wa wanakamari wa nchi hiyo, amejiua wiki hii kutokana na kudaiwa mamilioni ya Deustch Mark za Ujerumani na Cassino mojawapo. Tajiri huyu ajulikanaye kwa jina la Rulof Ladder, alisema miaka mingi kabla ya kujiua na kabla hajawa tajiri kuwa: 'Muwe na yakini kuwa mimi nitajiua iwapo kipato changu kitapungua na kufikia chini ya Mark elfu kumi kwa mwezi..........."

Na masikini huyo ikafikia hali mbaya kama hiyo ya kupteza utajiri wake wote katika michezo ya kamari na hatimaye akajiua!

Baada ya kumalizika vita vikuu vya dunia. Rulof Lodder alikuwa hana chochote hapo Ujerumani, lakini baadaye alianza biashara na katika kipindi kifupi, aliweza kupata utajiri. Katika mapatano mojawapo aliweza kupata faida ya mamilioni ya Mark na kuziweka katika Masoko ya Fedha (stock exchange) na hivyo aliweza kujipatia utajiri mkubwa sana.

Lakini Rulof alikuwa akipendelea sana kucheza michezo ya kamari, hususan mchezo wa Rulet. Kila usiku alikuwa akienda katika majumba mashuhuri ya kamari duniani na jambo la kuvutia ni kwamba, daima alikuwa akishinda katika michezo hiyo. Msaidizi wake mmoja alisema kuwa yeye alikuwa amekusanya sehemu kubwa ya utajiri wake kutokana na mchezo huo. Daima alikuwa akishinda kiasi kikubwa cha kuzidi Mark laki moja na hii ndiyo sababu iliyomfanya ajulikane kama Mfalme wa wacheza kamari katika majumba yote ya kamari. Yeye alipokuwa akiingia katika jumba lolote la kamari, mwenye jumba hilo alikuwa akikusanya vitu vyake vyote na kufanya hesabu kwani walijua kuwa wao watavipoteza vyote mbele ya Rulof katika kamari.

Hadi miaka miwili iliyopita, yeye alishindwa mara nne tu katika michezo yote ya Kamari. Hadi hapo jana, kiasi alichoshindwa katika michezo hiyo haikuzidi Mark laki hamsini. Lakini katika kipindi cha miaka miwili amekuwa akishindwa kila mara. Na katika Masoko ya fedha (stock exchange) amekuwa akipata kiwango kidogo cha faida. Amekuwa akipoteza faida hiyo kila siku hata kufikia mara mbili au mara tatu yake. Hivyo majumba yote ya kamari yakaonekana kuwa yamemgeuzia uso wa bahati bwana Rulof. Yeye amekuwa akibadilisha majumba ya kamari kwa matumaini ya kufanikiwa mahali fulani, lakini amekuwa daima akishindwa na kupata hasara kubwa. Hatimaye alikwenda zake huko Monte Carlo,lakini na huko pia amekuwa akishindwa, kwa kiasi cha Mark laki themanini.

Pole pole furaha na starehe za Rulof zilipungua kidogo kidogo kwani alitaabika mno kwa sababu za kushindwa katika michezo yake ya kamari usiku na mchana na hivyo alikuwa hawezi kumudu shughuli zake za mchana katika Masoko ya fedha. Hivyo mapato yake yakawa yanazidi kudidimia huku akipoteza fedha nyingi katika michezo ya kamari. Katika muda wa mwezi mmoja,Rulof alikuwa amebakiza majumba machache aliyokuwa akimiliki. Na hayo pia aliyauza na kuweza kupata kiasi kizuri cha fedha. Alikuwa akiwaambia marafiki zake: "Kwa kiasi cha fedha nilizonazo, mimi nitaweza kurudisha mali na utajiri wangu wote nilioupoteza katika kamari."

Rulof alikwenda Hamburg na kucheza kamari katika majumba mashuhuri na baadaye alikwenda hadi Monte Carlo, lakini kote huku alishindwa michezo yote na akapoteza yale yote aliyokuwa nayo, na badala yake akawa amebakia akidaiwa mamilioni ya Mark za Ujerumani. Hivyo kufilisika kukamfanya asiwe na hamu na chochote humu duniani.

Katika hali hiyo, alikwenda katika majumba ya kamari, lakini hakuweza kucheza kamwe kwani alikuwa fukara kabisa. Hatimaye alikwenda katika kijumba chake kidogo mjini Kolon na humo akavila vidonge vya usingizi na vidonge vinginevyo kwa wingi kwa kutaka kujiua. Maiti yake iligunduliwa baada ya saa ishirini na nne baada ya kujiua."

Mfano Wenye Fundisho

(Katika Iran) "Kijana mmoja ajiua katika Cassino mojawapo baada ya kupoteza Tumaini laki nne na themanini elfu. (Gazeti la Firdousi Na. 998)

Hii ni mifano ya wacheza kamari ambao wanajipatia na kuukusanya utajiri wao baada ya jitihada zao na ambao hatimaye huja kujiingiza katika uchezaji wa kamari. Hivyo hao hujipotezea raha na starehe za kimwili pamoja na kiroho, wao hujaribu kutafuta kila njia na hila ili waweze kujiepusha na balaa waliyojitafutia na lakini hujikuta hawana njia nyingineyo isipokuwa ni kujiua tu.

Inawezekana baadhi ya watu wanafikiria kuwa vioja vyote hivyo vya wacheza kamari hutendwa na wale watu wenye utajiri mkubwa tu.Lakini tunaposoma magazeti yachapishwayo kwetu, twaona kuwa maovu kama hayo pia hutendwa hata petu na iwe wazi kwa wale wote watakaojiingiza katika uchezaji wa kamari basi hata nao pia watakumbana nayo, hivyo wayasubiri yatakayowapata!

Je hatutaweza kumshukuru Allah swt kwani ametubainishia wazi wazi kwa kupitia Mtume wake Mtukufu s.a.w.w. kuwa:

"Hakika sheitani anataka kututilieni uadui na bughudha baina yenu kwa ajili ya ulevi na kamari......" (Al-Maidah, 5:91)"

Ar-Ridha a.s. amesema:

"Khawatim, arba-ashara (ni vyombo ambavyo vilikuwa vikitumiwa kwa kuchezea kamari) na vyombo vyote vile vitumiwavyo katika kuchezea kamari, ni lazima kila mtu ajiepushe navyo, hata kwa jauzi, lauzi, na vile vile alama za mifupa ya vidole, ambavyo aghalabu hutumiwa na watoto kwa kuchezea."

Hapa pana ulazima wa kuelezea juu ya sura mbalimbali za michezo ya kamari na vile zilivyo hukumu za Islamu kuhusiana na kamari na wachezaji wake.

Qurani kwa maelezo na dalili imeelezea kuwa kamari ni haramu kabisa katika sura yoyote ile. Qurani Tukufu inatoa sababu na kufafanua kamari, faida zake, hasara zake na kutoa ishara juu ya maovu yatokanayo na hayo. Na utukufu huo upo juu ya misingi ya faida zake unapolinganisha na wa maovu na hasara zake.

Kwa kuwa watu wengi wanacheza kamari kwa ajili ya kujifurahisha au kupoteza muda wao, au kwa ajili ya kujipatia fedha na mali, ndiyo maana Qurani Tukufu inaelezea kwa kuzitaja faida zake kidogo na kuwatanabahisha watu wasijiingize katika mtego wa uchezaji wa kamari na hatimaye kuangamia, wakati Qurani yenyewe inamtakia kila mtu kila la kheri ili aishi maisha marefu ya raha na siha njema.

Si jambo la busara mtu kujitafutia balaa kubwa kama tulizozitaja kwa ajili ya kutaka faida kidogo ya mali. Vile vile wachezaji wa kamari watambue kuwa wanapojipotezea faida za kimali,kiroho na kijamii na vile vile kuharibu siha na tabia zao njema.

Qurani Tukufu penginepo inatuambia kuwa michezo ya kamari ni sawa na matendo ya Sheitani. Rejea Aya ya 90/91 ya Sura al-Maidah.

Vilevile katika aya zinginezo za Qurani imeelezwa kuwa kamari ni utangamano na uadui,hisisa za kisasa na kadhalika kumdhalilisha mchezaji na huvunja uhusiano wa mtu pamoja na Allah swt na hujipotezea furaha ya kiroho. Rejea Aya 90/91 ya Sura al-Maidah.

Katika Islam michezo ya kamari ni ile michezo ambamo kuna sharti la kushinda au kushindwa na huchezewa na watu wawili au zaidi kwa masharti ya kwamba iwapo mmoja atashindwa basi atawalipa fedha au mali kiasi fulani kwa wenzake walioshinda. Aina hizi za kamari zimeharamishwa kabisa katika Islam na mafuqahaa wameelezea kuwa kuiheshimu Shariah hii ya Islam ni faradhi ya kila mmoja wetu.

Sura ya pili ya uchezaji wa kamari ni mfano wa utumiaji wa karata au vibao vya satranji kwa madhumuni ya kutuliza nyoyo zao au kwa ajili ya kuupoteza muda wao na humo huwezekana wasitiliane masharti ya kulipiana fedha au mali yoyote ile. Aina hii ya michezo pia imeharamishwa kwa mujibu wa Fatwa za Maulamaa wa Kiislamu.

Sura ya tatu ni kule kutotumia kwa vitu vya kamari lakini kunakuwapo kwa sharti la kupata-pote. Mfano kusema kule,iwapo timu fulani ya mpira ikishinda au kushindwa basi mimi nitakulipa fedha kiasi fulani ,na mwenzako naye pia akakujibu vivyo hivyo.Hatimaye aliyebahatika kwa kushinda timu yake basi hupatiwa alichoahidiwa. Je,tumeyasahau yale tuliyokuwa tukiyasikia na kusoma magazetini juu ya mabishano kama hayo ya kamari kuhusu michezo ya mpira baina ya timu moja na timu nyingine,na yale yaliyokuwa yakitokea hadi wengine kupoteza fedha,mali,majumba na hata wanawake zao? Je,si hayo hayo yanayozungumzwa na Islam kuhusu maovu ya kamari?

Wakati nikitayarisha makala haya,nilijiwa na rafiki yangu kazini mwangu kwa kuniuliza maana ya mchezo uitwao football-pool,kwani yeye akiwa hapa Bukoba mjini amepokea barua moja kutoka Nigeria ikimwomba awekeane sharti la ushindani la fedha juu ya timu za mpira wa miguu za Uingereza ambazo zipo karibu kuanza mchuano yao. Jee,hii si kamari mojawapo ? Mkazi wa Nigeria anamtafuta Mtanzania ili kushiundana naye,Loh ! Yakimataifa hiyo.

Basi msomaji ujue kuwa hivyo pia ni haramu mbele ya mafuqahaa wa Kiislamu na ambapo kwa wasio Waislamu,kwao wanayaona ni mambo ya kawaida tu.

Kuna sababu mbili zivutiazo kuitazama kamari katika Islam (i) kwa sababu kamari ni haramu yenyewe na katika Islam imehesabiwa kuwa ni dhambi (ii) kwa sababu faida ya fedha iliyopatikana na kamari ni haramu kwamujibu wa Sharia za Islam, fedha hizo au kitu hicho alichokipata mtu aliyeshinda kamwe hawezi kuvimiliki na wala hana haki ya kukitunza na hivyo inambidi kuvirjesha kwa mmilikaji wa awali.

Vile vile michezo yetu ya bahati nasibu ya kununua tiketi pia ni mojawapo ya michezo ya kamari. Hivyo mafuqahaa wanatukataza kabisa kushiriki katika ununuzi wa tiketi hizo kwani fedha hizo ni kwa ajili ya michezo tu. Iwapo mtu atapenda kushiriki katika michezo ya kuchangisha fedha kwa ajili ya miradi fulani ya kusaidia au kuleta maendeleo,kwa njia ya kutoa msaada,basi itambidi atoe mchango na wala si kutaka kushinda zawadi ya fedha au kitu,ama sivyo hiyo pia itakuwa ni kamari.

Hivyo chunga fedha zako zisitumike katika kamari kwa hali yoyote ile ! Jasho lako la halali litumike katika njia halali tu.

Vita Vya Kimsingi

Ili kutaka kuing'oa mizizini hii balaa kubwa ya kamari,Islam haikuiharamisha tu bali hata kutangaza vita vya kuvinunua,kuviuza na hata mtu kuviweka.

Upo uwezekano wa baadhi ya watu kutuuliza iwapo michezo ya ubao Satranji na mengineyo kama hiyo, itachezwa bila ya malipo, kutawezekanaje kuwa haramu ambapo siku hizi hutumiwa kwa ajili ya kuchangamsha akili na vile vile imepatiwa nafasi katika idara za elimu?

Basi sisi tunaweza kuwajibu watu kama hao hivi:

(i) Michezo kama hiyo haikosi maovu na hatari kama tulivyokwisha yaona na wala haikuweza kuthibitika kinyume na hayo. Vile vile mabingwa na wasomi wote pia wanasadikisha ukweli kuhusu maovu hayo.

(ii) Uislam imetangaza vita vikali dhidi ya kamari kwa kutaka kuing'oa toka mizizini mwake hata kama itakuwa ni michezo ya kamari bila ya kutumika fedha au mali vyote ni haramu.Vile vile kununua na kuuza au kununua vifaa vya kamari, au kuvitengeneza pia kumeharamishwa vikali.Pia tusikaribie kabisa chochote kila kitumikacho au kitushawishicho katika kukaribia kamari au michezo yake. Hivyo hata marafiki wetu kwa njia yeyote wanaocheza kamari au wanaohusika tuwaache!

Ni lazima kuitangaza vita thabiti dhidi ya ufisadi wowote ule na hatimaye hata kuung'oa mizizi yake, kwa sababu iwapo vifaa na vyombo vya kuchezea kamari vitakuwa vikitengeneza bila ya upingamizi, na iwapo tutakuwa tukiviweka vitu hivyo majumbani na madukani mwetu au popote pale bila ya upinzani wowote, basi mwanzoni tutakuwa tukifurahia kuwa navyo, kwani tutastarehe na kuufanya wakati wetu uende vizuri. Lakini hapo baadaye kuna hatari kubwa ya kujitokeza balaa kubwa ya kamari na michezo yake na labda sisi tukaibuka kuwa mabingwa wa michezo hiyo ya kamari.

Leo hii iwapo utakwenda madukani basi utawaona wafanya biashara wanauza 'gum' (ubani wa kutafuna) zitokanazo nchi za Ulaya na Magharibi ambazo ndani yake kuna picha au karata zenye sura za wachezaji muziki mashuhuri duniani. Hivyo watoto hukimbilia kununua hiyo gum ili kuweza kukusanya mapicha hayo au karata hizo.

Karata hizo zipo ndogo kiasi cha kuingia katika mifuko ya mtu au mikebe ya hisabati ya watoto waendapo mashuleni. Athari mbaya juu ya watoto hawa ni kwamba wao wanakuja kuwajua vyema wanamuziki na disco humu ulimwenguni na kuzivuruga akili zako kutaka kuingia mitindo yao na ufisadi wao, vile vile utawaona watoto hao wakicheza karata - kamari hata mashuleni au jioni wanapokuwa wametoka mashuleni.

Sasa je uuzaji wa vitu kama hivi vya gum, pipi na vinginevyo vinashirikiana katika kuueneza ufisadi kama huu unaruhusiwa katika Islamu na je, kipato chake ni halali? Magharibi inataka kuzivuruga akili zetu na utamaduni wetu pamoja na watoto wetu. Tujitahadhari kabla hatujapotoka!

Na hii ndiyo sababu Islamu imeharamisha vifaa vyote vya kamari na imejaribu sana kutaka kung'oa hizi fitina kutoka mizizi yake na kwa hakika watu wote wale wenye imani thabiti juu ya Islamu (si kwa Mwislamu kwa jina tu), basi hao kamwe hawataweza kushiriki katika dhambi kubwa zisizosameheka na vile vile watakuwa daima wakijiweka mbali na michezo yote ile ya kamari hata kama itakuwa ni michezo ya bahati nasibu au kushindana bila ya kutoa fedha kama tulivyokwisha soma hapo mbeleni.

As-Sadiq a.s. amesema:

"Kumtolea salaam mcheza kamari ni dhambi na vile vile kusimama karibu na mkeka wa wacheza kamari kwa kuutazama mchezo wa kamari na kuona uso wa mcheza kamari, basi vyote hivyo vina dhambi sawa na yule amtoleae salaamu mcheza kamari. Hafla na makusanyiko hayo ni mojawapo ya hafla iliyoharamishwa kwa Sheria za Islamu na washiriki wake wanawajibika kupatiwa adhabu na ghadhabu za Allah swt na hivyo inawabidi waisubiri."

Alitokea mtu mmoja kutoka Basra akamuuliza:

"Abul Hassan ameelezea juu ya kamari na satranj (chess) kwa ubalagha sana wakati alipoulizwa na mtu mmoja wa Basra kuwa yeye huwa anashiriki kaitika hafla za michezo ya Satranj (chess) lakini yeye huwa hachezi bali huwa ni mtazamaji tu, alijibiwa kuwa anao uhusiano gani pamoja na faida gani na ile hafla ambazo hazitazamwi na Allah swt kwa Rehema zake na ambazo husubiriwa kwa ghadhabu na adhabu za Allah swt?"

As-Sadiq a.s. amesema:

"Uuzaji wa Satranj (chess) ni haramu, utumiaji wa mapato yatokanayo na hayo ni haramu, kuviweka ni kukosa imani, uchezaji wake ni shirk, kumtolea salaamu mcheza Satranj ni dhambi na kumfundisha mtu mwingine ni maangamizo na mwenye kufanya maangamizo ni mwenye dhambi kubwa kabisa."

Moja ya sababu za kumfanya mtu acheze kamari, ni kule kutaka kuuiga utamaduni wa Magharibi. huo ni ugonjwa mkubwa ambao umewafanya wengine wajaribu kuiga Umagharibi na hivyo hujikuta wametumbukia katika balaa kubwa ya uchezaji wa kamari na hata tabia ya kunywa pombe na kuvuta bangi au utumiaji wa madawa ya kulevya na tabia mbaya mbaya za uasherati na kukosa aibu na heshima. Hali zote kama hizi tumeona zikishamiri mno hata hapa kwetu katika sura mbalimbali.

Kwa hayo, wazee wetu hulia machozi ya damu kuona hali kama hiyo imetokezea, lakini hao wacheza kamari na wapotofu hujiona kuwa wao ndio watu walioendelea na kuwa wapo bega kwa bega pamoja na wanamagharibi pamoja na utamaduni wao. Aidha huona kwamba huo msafara wa wacheza kamari hauwaachi. Lakini ni lazima kuwa wao watambue kuwa hawajaendelea chochote bali wamejitumbukiza katika laana mojawapo kubwa mno! Akupoteza fahamu, akili, uume na kueneza ugonjwa wa Aids na ni miongoni mwa matokeo ya hali hiyo.

Kwa hakika watu wakitaka kuingiza Umagharibi, lazima inawabidi waigize elimu, ufundi na taknolojia ya viwanda huko Magharibi ili waweze kuleta maendeleo yao kwa jamii nzima na wala si kutaka kuiponza na kuiangamiza jamii nzima. Kwa hayo mema, maisha yao yatakuwa yenye maana.

Tujikumbushe Hadithi moja ya Mtume Mtukufu s.a.w.w. isemaye: "Mbora wa watu ni yule ambaye anawafaa watu wengineo." Sasa je sisi ni bora ya watu au dhalili?

Na maendeleo ya kamari ni ya ajabu sana, kwani zamani wacheza kamari walikuwa ni wanaume peke yao ambao walikuwa wakiketi mezani mwao wakicheza kamari mbalimbali na kurudi majumbani mwao hapo asubuhi wakiwa wamechoka. Lakini siku hizi, hata wanawake pia wamejaa katika majumba ya kuchezea kamari kwani wao pia wamekwisha ambukizwa uovu huo.

Vile vile wasichana wenye umri mdogo hutumiwa kuwavutia wacheza kamari wakati wao wanapotoa huduma kwao. Vijana hao huvaa nguo fupi kabisa hadi kuonyesha mavazi yao ya ndani (jaribu kufika katika Cassino yoyote iliyo karibu nawe, Dsm au Nairobi au Kampala). Kwa kweli hawa wanawake wanadai kuwa haya ni maendeleo yao na wanaweza kuthibitisha kuwa wapo sawa na wanaume hivyo wapo bega kwa bega pamoja nao. Lakini wajue kuwa wao wapo katika hali ya upotofu!

Sasa inambidi kila mtu ajiepushe na kuwaepusha jamaa na marafiki kutoka katika moto huu ili wasiangamie na kuteketea na babala yake wajielekeze katika hukumu za Dini. Aidha tusiwe na uhusiano wowote na wacheza kamari, wala sisi na wenzetu tusishiriki katika hafla zozote za wacheza kamari, isipokuwa tujiepushe na vitu vyote vinavyoweza kutuingiza na kutushirikisha katika balaa hii kubwa. Tukifanya hivyo basi Allah swt atatazama kwa mtazamo wenye rehema na baraka ama sivyo tusubiri maangamizo na adhabu zake!

Bila shaka, huu msiba wa kamari lazima ukabiliwe kama vile unapokuta balaa la ugonjwa. Vita madhubuti na yenye kutumiwa mbinu mbali mbali lazima vitangazwe dhidi ya kamari ili itokomezwe kabisa.

Wakati kunapozuka ugonjwa hatari wa kuambukiza (kama ugonjwa wa tauni au mwingineo) katika nchi yoyote ile basi Wizara ya afya inatoa maelezo na maonyo juu ya hatari na athari za magonjwa hayo kwa raia na hatua za kujikinga na magonjwa hayo. Na hufuatilia pia na pengine inapostahili huweka sehemu hiyo chini ya karantini na watu wa sehemu zingine. Hususan wale waliobainika kupatwa na magonjwa hayo. Hao nguo zao pia huchomwa moto iwapo itahitajika kwa ajili ya usalama wa wengine. Wakati mwingine inabidi kuchoma moto hata kijiji kizima baada ya kuwatoa watu wake au mahala penye ugonjwa. Hatua zote hizo zinatumiwa kwa ajili ya kuzuia ugonjwa huo usienee katika sehemu nyingine na kuleta balaa zaidi ya kuangamia.

Loh! Yote hayo yanaweza kutekelezwa kwa ajili ya ugonjwa wa mwili wa mwanadamu. Lakini kunahitajika vile vile hatua kama hizi na zaidi dhidi ya wacheza kamari na kufanya kampeni ya kuwaelimisha na kuwafahamisha watu juu ya athari na hatari za kamari na vile maovu yatokanayo na michezo hiyo katika jamii zetu kwa sababu ya kamari. Sehemu na majumba yanayotumiwa na wacheza kamari yafungwe na hao wacheza kamari washughulishwe katika kazi mbali mbali zenye kuleta maendeleo kwa jamii nzima.

Vijana na watoto wakatazwe kabisa kucheza hiyo michezo na vile vile wasishirikiane pamoja na wala wasiwe na uhusiano wowote pamoja na wacheza kamari. Watu wenye elimu ya Dini na dunia, wenye busara lazima wakutane na watu hawa wanao cheza kamari na wajaribu sana kwa kuwafanya waache kucheza michezo hiyo iliyolaaniwa ili Rehema na Baraka za Allah swt ziwafikie wao pia na hivyo uovu huu unaweza kung'olewa toka mizizini mwake na kutupiliwa mbali.

Hapo jamii yetu itakuwa safi na watoto wetu watakuwa wema wenye adabu na nia ya kutaka kuitunza yao ya baadaye. Kwa hivyo inatubidi vile vile kufuatilia mienendo na tabia ya watoto wetu-kila wakifanyacho na kule waendako!