read

'Uislamu Umesema Kabla Yake
Mtungaji: Hadi Mudarrisi
Mfasiri: Hassan A. Mwalupa
*******
Makala hii inaeleza kuwa kuna mambo mengi yaliyotajwa katika Qur’ani na hadithi lakini sayansi imekuja kuyagundua baadaye na hii inawapasa waislamu walete fikra za kimaendeleo na kujitokeza katika nyanja mbalimbali na kufanya utafiti zaidi.

*******
Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, mwenye kurehemu.

Jaribio Na Akili

Je, Uislamu ni nadharia tupu kuhusu ulimwengu na maisha?

Kama tukizingatia maana ya nadharia kuwa ni dhanio (hypothesis) ambayo ukweli wake haukuhakikishwa kwa hoja thabiti, basi Uislamu sio nadharia.

Hii ni kwa sababu nadharia, kwa msingi huu, ni fikra maalumu anayobuni mtu au watu baada ya kutafakari au kufanya majaribio (experiments) juu ya kitu au vitu maalum.

Tunaposema kwamba Uislamu ni falsafa ya ulimwengu na maisha, tunakusudia kwamba Uislamu unavumbua uhakika wa matukio ya mwenendo na muundo wa ulimwengu ambao mtu hawezi kuujua ila baada ya kupita muda mrefu katika kufanya utafiti mkubwa.

Kwa mfano, Uislamu unaposema:

"Enyi mlioamini! Hakika ulevi na kamari na masanamu (ya kuabudiwa) na mishale (ya ramli) ni uchafu katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo ili mpate kufaulu;" (5:90)

hapo Uislamu hautoi nadharia kuhusu ulevi au kamari, bali unabainisha uhakika wa uchafu unaopatikana katika ulevi na kamari.

Lakini inawezekanaje kutoa hoja juu ya uhakika huu kufuatana na kanuni zote za Kiislamu, mfumo wake na desturi zake?

Kuna namna mbili za misingi ya maarifa (elimu):

(1) Maarifa ya kimajaribio; na
(2) Maarifa ya kiakili.

Elimu ya kwanza ya kimajaribio ni ile inayofahamika kutokana na majaribio ya vitu (maada) wakati ambapo elimu ya pili ya kiakili ni ile ambayo inatolewa dalili ya masuala ya kiakili bila ya kutegemea majaribio.

Kwa mfano, suala la kuwa maji yamefanyika kwa oksijeni na haidrojeni ni jambo la kimajaribio ambalo binadamu hakujua ila baada ya kufanya majaribio mengi juu ya maji yenyewe. Na suala la kwamba kila uvumbuzi hauna budi kuwa na mvumbuzi wake si suala la kiakili lisilohitaji kufanyiwa majaribio ya kimaada, kwani tunachukulia kuwa tunapoona ugunduzi wowote, basi yuko mgunduzi wake pia.

Kwa hiyo, haiwezekani kujulikana kitu kimoja kwa kutegemea elimu ya majaribio peke yake, bali tunaweza kusema kuwa matokeo ya dalili za majaribio yanapatikana kwa kuishia kwenye majaribio ya kiakili. Lau kusingekuwepo elimu ya akili, utafiti wa majaribio usingetoa matokeo yoyote yanayofaa.

Kwa mfano, suala la maji tulilolitaja linazingatiwa kuwa ni suala la majaribio tu, lakini kwa hakika ni suala la kiakili; kwa sababu hatuwezi kuamini kwamba kila maji yamefanyika kwa oksijeni na haidrojeni kwa kutegemea njia ya majaribio peke yake. Hatuwezi kufanya jaribio la kila aina ya maji na matone yake yote. Tunaweza kujaribu baadhi ya matone katika baadhi ya aina tofauti za maji, kisha tukaweka kanuni moja kuhusu maji yote kwa kutegemea kanuni ya kiakili kwamba: "Maji yote ni ya namna moja na kwamba jaribio la aina moja ya maji linatosha kutoa matokeo ya utungo wa matone yote ya aina hiyo ya maji." Hili ni jambo la kiakili ambalo haliwezi kutafitiwa kwa majaribio.

Kwa namna hii majaribio yanategemea dalili za akili katika kutoa matokeo yake kwa kiasi ambacho kama hayatotegemea akili, basi yatakuwa ni majaribio yasiyokamilika.

Kufuatana na uhakika huu, haijuzu kukataa jambo lolote kwa kuwa eti haliwezi kufanyiwa majaribio au haliwezi kupimwa kwa ala za kimaada. Jaribio si lengo ila ni njia ya kufikia kwenye lengo ambalo ni kujua suala au jambo hilo.

Kwa hivyo, tukilijua suala fulani kwa njia ya kiakili bila ya kutegemea jaribio lolote, basi hapana shaka imani yetu itakuwa na nguvu zaidi kuliko kama tukilijua kwa nija ya majaribio. Kwa sababu majaribio mara nyingine yanakosea, wakati ambapo masuala ya kiakili hayawezi kukosea.

Ikiwa jambo hilo ni sahihi kuhusiana na kila kitu, basi hapana budi kuwa ni sahihi kuhusiana na Uislamu, kwani masuala ya Kiislamu yanagawanyika katika mafungu mawili:

(1) Lile ambalo usahihi wake unathibiti kwa majaribio; na
(2) Lile ambalo usahihi wake unathibiti kwa akili.

Kwa mfano, uchafu (ubaya) wa damu umethibitishwa kwa majaribio, wakati ambapo uchafu wa damu ya mwanamke anapokuwa mwezini ni wa kimaanawi tu, haukufanyiwa jaribio lolote wala hakuna haja ya kufanyiwa jaribio kwa sababu ni suala lililo wazi kabisa kiakili, kama alivyobainisha Mwenyezi Mungu.

Kwa vyovyote vile, kwa kawaida lazima mtu ajue dalili za kiakili katika kila jambo moja peke yake. Vivyo hivyo, si lazima mtu kujua dalili zote za mambo au vitu vyote vingine ili kupata uhakika wake ulio thabiti, bali inatosha kupata msingi utakaothibitisha suala hilo kwa njia ya dalili za kiakili au kimajaribio.

Na hivyo ndivyo ilivyo katika masuala yote ya Kiislamu. Si lazima tujue kwa mapana dalili za maneno yote yaliyosema Uislamu ndipo tuamini, bali inatosha kujua kuwa hayo yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Kama vile ambavyo si lazima tujue kuwa dawa fulani itamponya au itamdhuru mgonjwa fulani kwa kutosheka na maelekezo ya daktari kuhusu kuitumia au kutoitumia dawa hiyo, vivyo hivyo, inatosha kuamini maneno ya Mwenyezi Mungu peke Yake.

Tukijua kwamba Uislamu ni dini iliyoshuka kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na tukijua kwamba Mwenyezi Mungu ni Muumba wa ulimwengu na uhai wote - kama vile dalili na hoja zote zinavyothibitisha - basi hatutolazimika baada ya hapo kutaka kujua kila dalili au sababu zilizoufanya Uislamu kuweka sheria fulani juu ya baadhi ya mambo au kuharamisha baadhi ya vitu. Kwa sababu kuamini kwetu kuwa Uislamu wenyewe unayaelewa matukio na mambo ya kimaisha na kibinadamu kunatosha kumfanya mtu aamini mambo mengine madogomadogo ambayo uhakika wake ni thabiti bila kuhitaji kujua kwa urefu.

Kwa hivyo, haijuzu kwetu kukataa msingi wowote katika misingi ya Uislamu, au mfumo wowote katika mifumo ya Kiislamu, au sheria yoyote katika sheria za Kiislamu, kwa hoja kwamba hatuijui falsafa ya msingi, mfumo au sheria hiyo. Ni lazima Mwislamu aukubali msingi wa Kiislamu baada ya kumthibitikia barabara kiakili, au pengine baada ya kufanyiwa jaribio la elimu ya kisasa. Hivyo, ataona kwamba Uislamu hauweki sheria juu ya kitu chochote ila kwa sababu kuna maslahi na faida, na wala haukatazi kitu ila kwa sababu kuna maslahi pia.

Ni kweli kwamba kila elimu au sayansi ya kisasa inapopiga hatua huvumbua ukweli wa sheria au misingi ya Kiislamu ambayo wameitaja Mitume na Maimamu kabla ya karne 14 zilizopita.

Lakini pamoja na hayo, haijuzu kwetu kusadiki kuwa elimu ya kisasa ndiyo kipimo cha kukubali au kukataa misingi ya Kiislamu na kanuni zake, kwani uvumbuzi huo mara nyingi huwa ni wa kukisia na kudhania tu, Yaani nadharia, ijapokuwa wenyewe wanaita ni sayansi wakati ambapo Uislamu ni tukio la uhakika, na ni wazi kwamba nadharia haiwezi kuwa ni kipimo kwa tukio la uhakika.

Na hii haimaanishi kuwa tunakataa yale yanayotolewa na elimu ya kisasa, kwa sababu ni kinyume na akili kwa Uislamu ambao unathamini elimu ya nadharia kukataa matokeo ya elimu. Kwa maana nyngine tunakusudia kusema kwamba jaribio si kipimo cha kuukataa au kuukubali Uislamu, kwa sababu jaribio huwa linakosea, wakati ambapo Uislamu umesimama juu ya misingi ya kielimu na ya kiakili, na haukubali shaka.

Kwa hivyo, tunapovumbua baadhi ya mambo madogomadogo ambayo yametolewa dalili za kimajaribio juu ya usahihi wake kufuatana na yaliyosema Uislamu, hatukusudii kusema kwamba kwa kuwa sayansi imethibitisha uhakika wa uliyoyasema Uislamu, hivyo Uislamu ni kweli, bali tunataka kusema kwamba Uislamu umetangulia kusema hayo kabla sayansi haikuvumbua.

Kwa kuwa elimu ya kisasa imevumbua maelfu ya mambo na vitu ambavyo vinathibitisha usahihi wa Uislamu na maarifa yake, hivyo, sisi hapa tutatosheka kutaja baadhi ya ushahidi wa usemi huu kwa ajili ya wapendao haki, uadilifu na ukweli.

1. Angahewa Na Mlima Qaaf!

Katika nusu ya pili ya karne ya ishirini, sayansi imevumbua angahewa (atmosphere), na kusema:

"Ni mfuniko mnene wenye ukubwa wa kilometa 96.5.”

"Umeuzunguka dunia (ardhi) kama bangili inavyouzunguka mkono.”

"Na mfuniko huo (wa angahewa) ni mchanganyiko wa gesi ambazo zimekaa katika tabaka maalum kwenye ardhi. Ndani yake hupatikana mchanganyiko wa hewa endelevu kutokana na mkondo wenye kupanda na kushuka. Mchanganyiko huo ni wa: Naitrojeni 78.09 %, oksijeni 20.95 %, agoni 0.93%, kabonidayoksaidi 0.93%, pamoja na kiasi kidogo cha gesi kama neoni, kriptoni, heliamu, haidrojeni, senoni, na mvuke, maji na mavumbi."

Faida za mfuniko huu (wa angahewa) zilizovumbuliwa na elimu ya kisasa ni kama zifuatazo:

(1) Unaikinga ardhi kutokana na vimondo (meteors) na vingine kama hivyo.
(2) Ndio unaoakisi mwanga wa jua juu ya ardhi na kuhifadhi hewa (isipotee). Kama si hewa tusingeona chochote isipokuwa giza tu!
(3) Unahifadhi uvutano wa dunia ili uweze kubakia mahali pake maalum, na kama si hivyo, basi dunia ingechambukachambuka kutokana na uvutano.
Hivi ndivyo sayansi inavyosema kuhusu angahewa. Je, Uislamu unasemaje?

Uislamu hauuiti mfuniko huo kama angahewa, bali umeupa jina jingine unaloitwa Jabal Qaaf yaani 'Mlima Qaaf'. Huenda kwa kuzingatia kuwa 'Qaaf’ maana yake ni kinga (ngao). Vilevile umeuita 'mlima' (jabal) pengine kwa kuzingatia ukubwa wa gimba yake.

Kwa kuzingatia umuhimu wa angahewa katika maisha ya binadamu, Qur'ani inaanza sura kwa kuapa kwa jina lake:

Qaaf Naapa kwa (hii) Qur’ani Tukufu." (50:1,2)

Imam Ja’far Sadiq a.s. amesema: "Qaaf ni 'mlima' unaozunguka dunia (ardhi), na tao (kuba) la mbingu linatokana na 'mlima' huo; na kwa 'mlima' huo Mwenyezi Mungu anaizuia dunia isiwayumbishe watu wake." (Ma'aanil Akhbaar)

Katika hadithi nyingine, Imam amesema:
"Qaaf ni ‘mlima' ulioifunika dunia, unatokana na zumaridi, mfuniko wake unatokana na mlima huo)." (Tafsiyr Nuuruth-Thaqalayn, jz.5, uk. 104, 105)

(Mlima huo umefananishwa na zumaridi kijani kwa sababu ya maada zinazofanya zumaridi, na huenda viasili vilivyo katika zumaridi vimo katika angahewa pia.)

Kwa hivyo, Qaaf ni 'mlima' unaoizunguka dunia; na ni lazima uwe hivyo kwa sababu zifuatazo:

(1) Kuwepo kwake ni kinga na hifadhi kwa dunia.
(2) Mfuniko (kuba) wa mbingu tunaouona, na vilevile mwanga wa jua unaoakisi usingepatikana kama si kuwepo 'mlima' (angahewa) huo, kwa sababu ndio unaowezesha kupatikana hewa ambayo kwayo huakisidi mwanga wa jua.

(3) Kuwepo kwake ni lazima kwa ajili ya kuendelea uhai, kwani kama si hivyo dunia ingeyumbayunmba na watu wake, kwa sababu dunia iko katikati ya uvutano wa jua na mwezi na sayari nyinginezo.

Hivyo ndivyo ulivyosema Uislamu neno lake la kweli kuhusu mfuniko (tao) wa mbingu - yaani angahewa (atmosphere) - kabla sayansi haikuvumbua katika nusu ya pili ya karne ya ishirini.

2. Mtu Kuzungumza Kutoka Mwezini!

Wakati binadamu aliposhuka mwezini kwa mara ya kwanza, watu waligawanyika makundi mawili:
a) Waislamu wenye mawazo mafupi walidhani kwamba jambo hilo ni kukiuka miiko ya dini, na wakatoa hoja kwamba ulimwengu ni milki ya Mwenyezi Mungu, hivyo, haiwezekani kwa mtu yeyote kuingilia milki Yake kwa namna yoyote ile.

Watu hao wamesahau kwamba Mwenyezi Mungu hajitakii mamlaka yoyote, kwani Yeye ni Mwenye kujitosheleza na kila kitu. Ameumba ulimwengu umilikiwe na binadamu, kama alivyobainisha hilo katika hadithi kudsi, aliposema:

"Ewe binadamu! Nimeviumba vitu kwa ajili yako, na nimekuumba wewe kwa ajili Yangu." (Kalimatul-Laah)

Wamesahau pia kwamba Mwenyezi Mungu ameeleza waziwazi kuwa mbingu na ardhi vimeumbwa kwa ajili ya watu, kama anavyosema katika Qur'ani Tukufu:

“Enyi jamii ya majini na watu! Kama mkiweza kupita kwenye kando za mbingu na ardhi, basi piteni! Hamtapita ila kwa uwezo (sultaan)." (55:33)

Sultaan ni uwezo na nguvu. Mambo ya ulimwengu hayako ovyoovyo tu, kiasi ambacho mtu anaweza kujifanyia vile anavyotaka tu! Bali ulimwengu umeumbwa kulingana na nguvu na kanuni zake mahsusi, hivyo, ni lazima tunufaike kutokana na kanuni zake maalum.

b) Walahidi (wasioamini Mungu) wengi walipofusha macho yao kwa safari ya Apollo 11, wakidhani kuwa kutua chombo hicho mwezini kulikuwa ni mwujiza ambao huenda ukawa muhimu zaidi kuliko miujiza ya Mitume, eti kwa sababu sayansi imehakikisha jambo ambalo halikuwa likiwaziwa na mtu yeyote!

Wamesahau kwamba Mitume wameleta miujiza ambayo waundaji wa Apollo 11 - 15 na wanasayansi wote wa dunia nzima hawawezi kuleta mfano wake.

Lakini umuhimu wa Mitume hauletwi na miujiza, isipokuwa unaletwa na lile linachofafanuliwa na miujiza hiyo - nalo ni kuwasiliana kwao na Yule aliyewaumba watu, ardhi na mwezi.

Vilevile walahidi hao wamesahau kwamba suala la kutua kwenye mwezi lilisemwa waziwazi na wale wenye kujua uhai kupitia njia ya Mwenyezi Mungu. Imam Ja’far Sadiq a.s. amesema:
"Miongoni mwa alama za mwisho wa dunia ni kuwa binadamu atazungumza kutoka kwenye mwezi" (al-Malaahim wal Fitan). Na jambo hilo limethibitishwa katika theluthi ya mwisho ya karne ya ishirini.

3. ‘Maji Ya Ngozi’ Na Sunna Yake Ya Kiislamu

Maadui wa Uislamu wanaitakidi kwamba Uislamu hauwezi kuingilia mambo ya maisha ya binadamu.

Kwa nini?
Wanajibu kwamba Uislamu hauendi sambamba na ulimwengu wa kisasa wa zama za anga, elektroni, sabuni na maikrobi (microbes)!

Kwa mfano, Uislamu unasema: Ni jambo linalopendwa (sunna) kunywa maji ya hodhi ambayo watu wanajioshea nayo, pamoja na kuwa huenda maji hayo yakawa na maikrobi wa hatari sana. (Sharaa’i ‘il-Islam cha Muhaqqiq Hilli).

Vilevile Uislamu unasema: Ni sunna kutia maji kwenye chombo kimoja ili watu kadhaa watie mikono yao humo, kisha uyanywe maji hayo kabla haijaoshwa mikono. Jambo hili litasaidia kuondoa maradhi.

Je, dini yenye kufundisha mambo kama haya inaweza kuwa na nafasi katika ulimwengu wa kisasa wa sabuni, poda, madawa ya Dettol na madawa mengine ya kuua vijidudu vya maradhi? Lakini utaona kwamba kuna watu wanaosema kwamba mafundisho kama hayo ya Kiislamu hayaambatani na maendeleo ya zama za Dettol, sabuni na maikrobi!

Mtu alikuwa akidhania kwamba kutiwa mikono mingi katika kitu kimoja kunaleta madhara. Kwa hivyo wakatafuta dawa za kinga na sabuni kwa ajili ya kuua maikrobi. Lakini baadaye wakaiacha rai hiyo baada ya kufanya majaribio ya muda mrefu na kuona kwamba Uislamu umesema kweli wakati uliposema:
"Chakula kizuri ni kile kinacholiwa na watu wengi, na kwamba kunywa maji kwenye chombo wanachooshea watu ni jambo linalotakikana.

Utabibu wa kisasa umegundua kuwa kiwiliwili cha mtu kinatoa kinga ya magonjwa kwa ukamilifu kabisa kama damu inavyotoa kinga kama hiyo wakati inapoingiliwa na maikrobi. Hata ngozi ya mgonjwa wa kisukari hutoa kinga ya maradhi hayo nje ya kiwiliwili chake, kiasi ambacho lau ataweka mkono wake katika chombo chenye maji, basi maji hayo yatakuwa na faida kuponesha magonjwa ikiwa atayatumia mwenyewe au hata mtu mwingine.

Kuna makala moja ya jarida la utabibu ulioandika haya: "Kiwiliwili cha mtu ni dawa bora inayomnufaisha mtu mwenyewe dhidi ya magonjwa!

"Hizi ndizo habari za elimu ya utabibu zilizotangazwa duniani. Uvumbuzi huo umetiliwa nguvu na utafiti wa Schafertsmann(?) wenye kujulikana kwa jina la sirumi (serum WW). Mwili wa binadamu unatoa majimaji ambayo hata kama yakichanganyika na maji safi bado yanakuwa ni kitulizo cha kuponesha magonjwa mbalimbali.

“Na hii ndiyo namna ya kutayarisha dawa hii ya ajabu ambayo imepewa jina la ‘maji ya ngozi’:

Weka maji safi katika chombo, kisha tumbukiza mkono wa mwanamume au mwanamke kwa muda wa dakika kati ya thelathini na arobaini. Inawezekana kuuosha mkono huo kabla ya kuuingiza kwenye maji, lakini usioshwe kwa dawa za kuuwa vijidudu.

"Mpaka hapa utakuwa umetimia utengenezaji wa dawa hii ya ajabu ambayo atatumia mgonjwa kwa kunywa au kwa kupigwa sindano. Kama ni kunywa itakuwa ni vijiko viwili vikubwa mara tano kwa siku; na kama ni sindano, basi itakuwa ni sentimetamraba mbili mara mbili kwa siku, lakini kabla ya kupiga sindano yatachemshwa katika mahali palipo wazi au kwenye baridi mpaka yabakie kiasi cha 1/50 ya kiasi chake cha asili.

"Inawezekana kwa mgonjwa mwenyewe kutayarisha dawa hii, kwani 'maji ya ngozi' yanayotokana na mgonjwa wa kisukari yanaponesha ugonjwa huo; vivyo hivyo, maji yanayotokana na mtu asiyekuwa na ugonjwa yanaponesha ugonjwa huo pia."

Makala hiyo inaendelea kuandika: "Maradhi yote ya ngozi yanaweza kuponeshwa na dawa ya ‘maji ya ngozi'. Dawa hii imerekodi ushindi mkubwa katika kuponesha maradhi ya vimeng'enya (enzymes) na upele katika mwili, hasa kwenye uso. Mpaka sasa siri ya dawa hii bado haijajulikana, isipokuwa daktari mmoja wa Kifaransa amesema kwamba ngozi hutoa dawa maalum na kwamba watu wenye desturi ya kubusana, miili yao hupata kinga ya magonjwa mbalimbali" (al-Aamiluun fin-Naft, JuIai 1971, na. 109).

Naam, hiyo ni fikra ya aina peke yake inayohimiza kufanya majaribio na utafiti wa uangalifu zaidi.

4. Jua Pia Linazunguka

Kwa muda mrefu watu walikuwa wakiitakidi nadharia ya Ptolemy kuhusu elimu ya falaki (astronomy). Nadharia yake iliziba kabisa njia za kufikiria juu ya ulimwengu, kwa sababu alikuwa akisema kwamba ulimwengu ni kama tufe kubwa lililotulia mahali maalum, na kwamba nyota na jua vinalizunguka tufe hilo ambalo ni dunia (earth).

Kwa hivyo, kulingana na fikra hii, dunia imetulia na haina mwendo wowote!

Baada ya uzoefu mrefu, binadamu akavumbua kwamba mambo yalikuwa kinyume kabisa na nadharia hiyo, kwamba dunia ndiyo inayolizunguka jua, na kwamba ulimwengu (universe) si dunia, jua na nyota peke yake, bali ni mkubwa zaidi ya hivyo, na kwamba hatuwezi kuvikisia hata kwa miaka mingi ya mwanga (light years).

Nadharia mpya ikachukua mahali pa nadharia ya zamani ya falaki ikisema kwamba jua ndilo lililotulia kabisa, na kwamba dunia na sayari nyingine za mfumo wa jua ndizo zinazolizunguka jua.

Nadharia hii nayo pia ikatolewa makosa baada ya kupatikana uzoefu mkubwa; na ikasema kwamba jua halikutulia, bali linazunguka katika njia yake isiyojulikana pamoja na sayari zake.

Lakini …

Je, uvumbuzi huu wa kisayansi ulio muhimu ambao umebadilisha fikra za watu wengi juu ya ulimwengu na maisha, ni matokeo na matunda ya karne ya ishirini?

Bila shaka, siyo!!!

Uislamu ambao tangu karne kumi na nne zilizopita umefichua uhakika wa kutua mtu kwenye mwezi, vivyo hivyo, umefichua uhakika wa jambo hili, kama unavyoeleza waziwazi katika Qur'ani Tukufu:
"Na jua linakwenda kituoni pake. Hicho ni kipimo cha Mwenye nguvu, Mwenye kujua." (36:38)

Kwa mujibu wa maarifa ya mwisho ya binadamu, jua - kama ulivyosema Uislamu - linazunguka katika anga (space) kwa mwendo wa maili 750 kwa dakika moja.

Jambo lililo muhimu hapa ni kuwa jua linazunguka kuelekea mahali maalum ambapo litaangamia pamoja na dunia, na hapo kutatokea Kiyama: "Hicho ni kipimo cha Mwenye nguvu, Mwenye kujua."

5. Tando Tatu Kwa Kijusi Kimoja!

"Kijusi (mtoto) hujikunja katika fuko (uterasi) la uzazi, na fuko hukaa katika tumbo."

Hivi ndivyo walivyokuwa wakiitakidi watu kuhusu binadamu - au ni sawa zaidi kusema - namna walivyokuwa wakijua kuhusu kijusi (mtoto anamokuwa tumboni). Nadharia zote kuhusu jambo hili linatokana na itikadi hiyo.

Lakini...

Lakini watu wote hawakuwa nyuma kiasi hiki, wale waliouamini Uislamu walikuwa wakijua kwamba mtoto (kijusi) anaishi ndani ya tando (mapazia) tatu, ingawaje walikuwa wakiona utando au ufuniko mmoja tu!

Waislamu walikuwa wakiitakidi hivyo kwa vile Qur'ani inasema waziwazi:

"(Mwenyezi Mungu) hukuumbeni matumboni mwa mama zenu - umbo baada ya umbo - katika viza vitatu." (39:6)

Watu wengine walikuwa wakiwachezea shere Waislamu kwa sababu ya fikra hiyo.

Zikapita siku hadi vyombo vya madaktari vilipofanya kazi ya kupasua mwili wa binadamu na kudhihirisha ukweli wa mambo, kwamba:

Kwa hakika kijusi hakiishi katika fuko moja tu, kwa sababu uterasi au fuko la uzazi lina viza au vifuniko (tando) vitatu: utando wa tumbo, utando wa kaboni na utando unaomfunika mtoto (au chupa ya uzazi). Lakini tando hizo hazionekani ila kwa uchunguzi wa kupasua, kwa sababu macho yanaona fuko moja tu!

6. Redio Na Vyombo Vya Kutarjumia

Imam Sadiq a.s. amesema:

"Utakuja wakati ambapo mtu aliyeko mashariki atamwona na kumsikia mtu aliyeko magharibi, na kila taifa litasikia kwa lugha yake."

"Na kwamba Waarabu watajitoa katika utawala wa kigeni, na watajitawala wenyewe kwa wenyewe, kisha watatoa hatamu zao."

"Na halitobaki tabaka lolote la watu isipokuwa litatawaliwa na watu wengine." (Bihaarul Anwaar, jz. 13, uk. 135,165)

Maneno haya machache ya Imam yanafafanua mambo manne yaliyotokea baada ya kupita zaidi ya miaka elfu moja:

Kwanza: Uvumbuzi wa redio na televisheni ambapo mtu wa mashariki anaweza kumwona na kumsikia aliyeko magharibi. Je, hatuko katika hali hiyo hivi sasa?

Pili: Kuvumbuliwa kwa vyombo vya kutafsiri ambavyo hutumiwa hivi sasa katika mikutano ya kimataifa, wakati ambapo vinamwezesha mtu mwenye kuhutubia, kuhutubia kwa lugha yake na wakati huohuo kila mtu akasikia tafsiri ya hotuba hiyo kwa lugha yake.

Tatu: Kujikomboa jamii za Kiarabu kutoka katika minyororo ya wakoloni kama hadithi inavyosema: "Waarabu watajitoa katika utawala wa kigeni na watajitawala wenyewe kwa wenyewe.

Na baada ya kujitoa katika utawala wa kidini na wa kimaadili wa wageni, watajitoa katika utumwa wao pia.

Nne: Kuenea utawala wa kikabila badala ya utawala wa kidini na wa kiumma mmoja katika ulimwengu wa sasa wa Kiarabu ni uthibitisho wa hadithi hii kwamba hakuna kikundi kimoja cha Waarabu kitakachobaki ila kitatawaliwa na kikundi kingine.

Hii ni mifano minne miongoni mwa mifano kadhaa ambayo Uislamu kabla na zaidi ya miaka elfu iliyopita umeelezea kutokea kwake katika ulimwengu wa kisasa.

Kwa kutoa mifano hiyo, hatukusudii kusema kwamba tutosheke na uvumbuzi wa kisayansi ambao umekwishatolewa utabiri au habari zake na dini yetu, na tuyaache mambo mengine yaliyosemwa na dini yetu ambayo bado hayakuvumbuliwa na sayansi.

Umma wa Kiislamu umerithi hazina kubwa ya fikra za kimaendeleo, na unapata msukumo kwa kuvumbuliwa hazina hiyo.

Kwa hivyo, ni wajibu kwetu kutenda juu ya msingi wa siasa ya kujitokeza mbele sisi wenyewe badala ya kubaki katika hali ya kutendewa au radiamali.

Hadi al-Mudarrisi
Dubai, Shaaban 25, 1391 AH